Jinsi Kikwete alivyopiku washindani wake – 008

Viongozi na watawala walio safi, wema, wenye nia na matendo mema, hawawezi kuogopa kuhojiwa. Hawatumii nguvu za dola kutisha au kuumiza wanasiasa, wanahabari, wachambuzi, vyama vya kiraia, wasomi, na watu wengine wote wanaokosoa kauli na utendaji wao.
Wanapoanza kuzuia watu kukusanyika; wanapoanza kuzuia watu kuhoji; wanapoanza kughilibu vyombo vya habari ili viwape sifa bandia; wanapoanza kufungia au kufuta magazeti yanayowakosoa; ujue kuna uchafu au udhaifu mahali fulani, na wanataka kuufunika kwa mabavu.
Katika utawala wa kidemokrasia, viongozi waadilifu hutawala kwa hoja, ushawishi, na uwazi. Vitisho ni rungu la mafisadi wanaotaka waonekane waadilifu. Utawala wa kidemokrasia katika enzi hizi hauwezi kuruhusu uadilifu na vitisho vikae katika meza moja.
Rais Benjamin Mkapa aliingia madarakani katika wakati mgumu kisiasa. Upinzani wa kisiasa ulikuwa unaanza, na haukuwa umejipanga vizuri kimfumo, lakini ulikuwa mkali. Alisifiwa na waliomnadi, huku akitiliwa shaka na waliompinga.
Hata hivyo, mwanzoni, aliaminisha wengi kuwa ana chembe chembe za uadilifu. Kwa kauli zake, alionekana kuchukia rushwa. Kwanza, alitangaza hadharani mali zake; idadi ya nyumba alizonazo na akaunti zake za benki.
Hata hivyo, alipokuwa madarakani, hakupenda waliomkosoa. Mara chache, alilumbana nao. Waandishi waliong’ng’ania kuandika kasoro za serikali walipachikwa jina la “waandishi uchwara.” Alidhani kwamba ubabe ungeweza kumsaidia kusogeza siku. Bahati mbaya, baadhi ya wasaidizi wake ndio walikuwa wanaonesha “matobo” na “matundu” katika serikali yake. Waliommaliza zaidi ni wale waliowahi kushindana naye, au waliokuwa watia nia wa urais kupitia CCM.
Washindani wake ndani ya CCM walifanikiwa kujenga taswira hasi ya utawala wa Rais Mkapa na Waziri Mkuu Frederick Sumaye, kiasi kwamba muda wake wa kuondoka madarakani ulipowadia, hakuwa na wengi waliokuwa wanamshabikia na kumtetea. Walihakikisha hata jitihada zake za kuweka mrithi aliyemtaka zinashindikana. Katika mkutano mkuu wa CCM uliomteua Jakaya Kikwete kuwa mgombea urais, Rais Mkapa alijilazimisha tu kuimba “tuna imani na Kikwete…” lakini waliokuwa karibu naye walijua kuwa moyoni hakuwa na imani naye.
Ajabu ni kwamba, alitangaza mali zake wakati anaingia madarakani, lakini wakati anaondoka hakututangazia kiasi cha mali alichokuwa amechuma akiwa Ikulu. Hakutaka wananchi wampime kama naye alikuwa ameathiriwa na ukwasi au “ukapa.”
Ilijulikana baadaye kwamba alipokuwa Ikulu, alitumia ofisi hiyo na kodi za wananchi kuanzisha biashara kadhaa. Ndipo tukajua kwamba alijenga “mahekalu” mapya, tukajua pia aliwahi kuwa mmoja wa wamiliki wa mgodi wa Kiwira; tukajua alivyoidhinisha fedha za EPA (Akaunti ya Madeni ya Nje) zitolewe Benki Kuu, jambo ambalo lilithibitika kuwa lilikuwa la kifisadi; tukajua alivyoshirikiana na mkewe kuanzisha kampuni ya ANBEN wakitumia anuani ya Ikulu, na mengine mengi.
Wale wale ambao yeye aliwaita “waandishi uchwara” ndio waliibua ufisadi wa rais mstaafu aliyeingia madarakani akiitwa “Mr. Clean.” Kumbe ndiyo sababu iliyokuwa inamfanya afokee wakosoaji.
Katika hali tofauti, serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete ilianza kwa jeuri ya ushindi wa kishindo (zaidi ya asilimia 80). Ilijivunia mapenzi ya umma kwa rais mpya. Kama John Magufuli anavyojinadi kwa kaulimbiu ya “Hapa Kazi Tu,” Kikwete alijitapa kwa kauli mbiu ya ANGUKA (ari mpya, nguvu mpya, kasi mpya).
Lakini, licha ya sifa ambazo Rais Kikwete alipewa na vyombo vya habari, dalili za serikali yake kushindwa zilionekana mapema. Ni wazi, umma ulitaka rais asiyefanana na Mkapa. Ukampata. Wananchi walikuwa na imani naye, lakini rais mwenyewe hakuwa anajiamini. Kuna dalili zilizotokea mwanzoni na mwishoni wa kampeni zake, ambazo zilihitaji tafsiri ya wasomi, wachambuzi, na watabiri.
Kwa mfano, kabla ya wagombea urais wa vyama vyote kuanza kampeni mikoani, uliandaliwa mdahalo wa kukutanisha wagombea wote ili wajinadi mbele ya umma. Ulipaswa kurushwa moja kwa moja kwenye televisheni, kuwapa wananchi wengi fursa ya kulinganisha haki wa sera zao, kuwahoji maswali, kupima uelewa na uwezo wao.
Wengine walikubali kushiriki mdahalo. Kikwete alikataa. Sababu alizotoa, kupitia kwa washauri wake, ni kwamba alikuwa ameshaanza kampeni mikoani. Kikwete na washauri wake waligoma hata kupangiwa tarehe nyingine kwa ajili ya mdahalo.
Kitendo cha Kikwete kugomea mdahalo kiliibua maswali. Anaogopa nini? Anaficha nini? Mbona mwaka 1995 CCM walikuwa na kimbelembele cha mdahalo na mgombea wao alifanya vizuri? Huyu wa sasa hajiamini?
Hata hivyo, tukiondoa udhaifu huu wa kukwepa mdahalo, Kikwete alikuwa mgombea mwenye nguvu kuliko wote kimkakati na kimtandao. Alijua wengine waliokuwa wanamshabikia hawakujua udhaifu wake, na hakutaka wamjue kupitia kwenye mdahalo huo. Hakwenda. Mdahalo ulifutwa.
Kwa wadadisi wa mambo, hii ilikuwa hofu ya kushindwa. Ilikuwa dalili kwamba kuna mambo mazito anayoficha. Ama hakuwa tayari au hakuwa na uwezo wa kuyatetea katika mdahalo.
Ikaja ishara nyingine, mwishoni mwa kampeni, siku ya moja kabla ya uchaguzi. CCM iliandaa mkutano mkubwa katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. Baada ya shamrashamra na hotuba za utangulizi kutoka kwa viongozi kadhaa waandamizi, ikafika zamu ya mgombea urais kuhutubia.
Akiwa ameanza kuhutubia, alizidiwa ghafla, akaanguka jukwaani. Kizaazaa kikatawala. Wakubwa wakahamanika. Mgombea akakimbizwa hospitalini. Kampeni zikafungwa kwa simanzi. Baada ya muda, Kikwete akapata nafuu, akaitiwa waandishi wa habari nyumbani kwake ili kuwajulisha kuwa yu mzima.
Yeye na wapambe wake waliwasihi waandishi wasitangaze habari ya kuanguka jukwaani ili “wasimharibie.” Walipanga mkakati huo huku wakitambua kuwa wakati Kikwete anaanguka, wananchi walikuwepo, na vyombo vya habari vilikuwa vinarusha matangazo moja kwa moja.
Na kwa hali ya kawaida, hiyo ndiyo ilikuwa habari kubwa kitaifa. Mgombea kuanguka jukwaani si jambo la kawaida, si dogo. Baadhi ya wapiga picha walikabidhi mikanda ya picha kwa timu ya Kikwete ili kuwakikishia kwamba haziwezi kutumika. Wengine walinyang’anywa kamera. Mmoja tu, Deus Mhagale, ndiye alifanikiwa kuficha picha yake, ikatumika katika gazeti la Mwananchi la kesho yake. Lakini, kwa sababu ya kutumika picha hiyo, wanamtandao na mashabiki wa Kikwete walimshambulia kwa vitisho na maneno makali.

Tukio hilo liliibua maswali. Kwanini mgombea urais ameanguka jukwaani? Anaumwa? Amewahi kuanguka popote kwa mtindo huu? Alikuja mkutanoni bila kujiandaa? Ni njaa? Ni woga? Ni uchovu? Ni kutojiamini? Ni ushirikina? Ni nini? Ilikuja kujulikana baada ya miaka miwili kwamba aliwahi kuanguka akiwa katika shughuli kadhaa za kiserikali, wakati mwingine nje ya nchi, lakini haikuwahi kuripotiwa. Lakini sababu ambayo yeye na wapambe wake walitoa mbele ya waandishi wa habari siku alipoanguka jukwaani ni kwamba alikuwa na uchovu wa mfungo!
Lakini kuanguka kwa mgombea hakukuwa ishara njema. Kulileta hisia za afya mbovu, wasiwasi, na hofu ya kushindwa. Kwa wengine, ilikuwa dalili ya anguko la serikali yake mbele ya safari. Hata hivyo, licha ya yote hayo, serikali ya awamu ya nne, chini ya Rais Kikwete, ilianza kazi kwa sifa, kishindo, na mbwembwe; na haikuwa tayari kukosolewa.
Hali hii haikuanza ghafla. Iliandaliwa mapema, wakati wa mchakato wa kuwania uteuzi ndani ya chama, na wakati wa kampeni baada ya kuteuliwa. Njia mbalimbali zilitumika. Makundi ya vijana yalipangwa na kusambazwa kila wilaya, kujadili na kuzungumzia umahiri wa Kikwete. Viongozi wa dini wenye ushawishi waliwekwa karibu, kama marafiki ambao wangetumika wakati wa mahitaji.
Wafanyabiashara wakubwa na wa kati waliwekwa karibu, na kuahidiwa nafuu baada ya serikali kuingia madarakani. Baadhi ya wahariri wenye ushawishi na wamiliki wa vyombo vya habari waliwekwa karibu, kwa “zawadi,” ahadi, au urafiki ambao ungetumika kudhibiti ukosoaji.
Zaidi ya hayo, kwa kutambua kuwa si wahariri au wamiliki wote wangeingizwa kirahisi katika mkumbo huu wa urafiki wenye shaka, aliandaliwa mtu, akapewa fungu la hela, akaagizwa kufuatilia magazeti yenye “habari mbaya” za Kikwete, ama zisiandikwe, au akishindwa kuzizuia, zikaandikwa, aweke utaratibu wa kununua magazeti yote asubuhi kwenye vituo muhimu nchi nzima, yasiingie sokoni.
Na wakati wakihakikisha “habari mbaya” za Kikwete haziandikwi, wao walifanya bidii kutambua nani anapanga kugombea urais; na walipomtambua waliweka vijana wa kumchimbachimba na kumchokonoa ili wapate habari mbaya zake, ziandikwe magazetini. Haikuwa lazima ziwe mbaya kweli, ilimradi ziliwekwa katika mrengo wa ubaya, na kuwasaidia kuonesha au kujenga taswira hasi ya mshindani wao mbele ya umma, kuwa si mwadilifu wala mzalendo.
Miongoni mwa waathirika wakuu wa fitina hizi ni Iddi Simba, aliyekuwa waziri wa viwanda; John Malecela, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CCM; Profesa Mark Mwandosya, aliyekuwa waziri wa uchukuzi; Frederick Sumaye, aliyekuwa waziri mkuu; na Dk. Salim Ahmed Salim, mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere.
Kwa kutokujua uzito wa fitina walizopigwa, na sababu kuu ya kuibuliwa kwa “kashfa” zao, wengi wao walidharau propaganda mbaya dhidi yao. Walipokuwa wamechafuka na kunuka kila kona, wakajitokeza kutoa utetezi, wananchi hawakuwa tayari kusikiliza hoja zao, kwa kuwa picha iliyokuwa imechorwa kwenye vichwa vya Watanzania ilikuwa hasi.
Vibali vya sukari vilinyausha uwaziri wa Iddi Simba. Kashfa ya TTCL iliondoa uadilifu wa Prof. Mwandosya. Mashamba ya Kibaigwa, mkopo wa milioni 50 za PPF, na ziara ya wafanyabiashara Marekani na Ulaya viliondoa usafi wa Sumaye. Malecela alizushiwa kubadili dini na kuitwa Jumanne ili apate fedha za Waarabu. Dk. Salim alizushiwa kushiriki mauji ya Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar; akaitwa Mwarabu, asiyeweza kuwa na uzalendo kwa Tanzania.
Fitina na propaganda zilisaidia kunyamazisha wengine na kubeba mmoja. Tukapata serikali iliyotokana na ushabiki na zomeazomea. Hata baada ya Kikwete kukaa madarakani kwa miaka 10 na kuondoka, baadhi ya vidonda hivi bado ni vibichi.
Huu ulikuwa msingi wa utawala uliotumia vitisho na ghiliba kuumiza wengine na kufaidisha wengine. Ndiyo maana siku Sumaye alipochukua fomu ya kuwania urais ndani ya CCM mwaka 2005, aliwaambia waandishi wa habari: “Mgombea anayetumia kalamu kuumiza wenzake wakati anatafuta uongozi, akishaupata atatumia risasi kuumiza wanaomkosoa.”
Nilikumbuka mneno ya Sumaye siku Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage walipovamiwa na kushambuliwa kwa mapanga na tindikali katika jitihada za serikali kuzima sauti ya gazeti la MwanaHALISI. Niliyakumbuka Dk. Stephen Ulimboka alipotekwa na kuteswa vibaya. Niliyakumbuka pia Absalom Kibanda alipovamiwa na kuteswa.
Haya yalikuwa maandalizi ya uongozi usio tayari kukosolewa. Yalikuwa maandalizi yaliyojiandaa kufurahia sifa za kweli na za bandia. Ulikuwa uongozi wa watu wawili wasiokosolewa – rais na waziri mkuu. Kwa takribani miaka miwili ya kwanza, vyombo vya habari “viliruhusiwa” kukosoa mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, na maofisa kadhaa katika serikali yake. Lilikuwa “kosa” kukosoa rais au waziri mkuu.
Ni waandishi na wahariri wachache tu waliojitoa mhanga kukosoa kauli, vitendo au mwelekeo wa uongozi wa rais au waziri mkuu. Walikuwa wamejitengenezea, na wametengenezewa, ngome ya kutoguswa. Waliogopwa. Walidekezwa. Walitukuzwa. Na kwa jinsi hiyo, waliharibiwa.
Baadhi yetu tuliojitokeza kukosoa utawala wa Kikwete, tulishambuliwa na kutishwa kwa njia mbalimbali. Tukaambiwa tutarogwa, tutauawa, na kadhalika. Kwa hiyo, haikuwa ajabu kwamba waandishi waligeuka mashabiki wa Kikwete badala ya kufanya kazi yao ya uandishi wa habari. Jamii ilibaki inatushangaa jinsi “tulivyolala kitanda kimoja na serikali.”
Ndiyo maana mchora katuni Gado (Robert Mwampembwa) wa gazeti moja la Kenya, alichora katuni ya waandishi wa habari wa Tanzania wakiwa Ikulu wanalamba miguu ya Rais Kikwete, wengine wanashangilia, badala ya kumuuliza maswali. Ingawa serikali na baadhi ya waandishi walimshambulia mchora katuni huyo kwa maneno makali, ukweli ulibaki pale pale, kwamba Kikwete alisahaulisha baadhi ya waaandishi wa habari kazi yao, nao wakaridhika.
Baadhi ya wasomaji walikuwa waoga wa kusoma tulichoandika, kuliko hata sisi tulioandika. Baadaye, baadhi ya waandishi wakaondokewa na woga. Na kadiri siku zilivyoenda, niligundua kuwa wapo wanaoandika mambo mazito kuliko hata ya makala zangu.
Kwa hiyo, si Rais Magufuli pekee ambaye ameanza uongozi wa serikali kwa kuchukia kukosolewa. Hata Kikwete hakuwa tayari kukosolewa, bali alilazimishwa na wakati, na hali halisi. Ukali wa hoja za waliomkosoa magazetini ndio ulisindikiza bunge na jamii kukosoa serikali serikali kwa nguvu zaidi, hata kuiangusha katika sakata la Richmond, kampuni ya kufua umeme iliyoleta magumashi yaliyosababisha waziri mkuu kujiuzulu, na baraza la mawaziri kuvunjika.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mpasuko wa serikali ya Kikwete, na upenyo uliozaa ombwe la uongozi ambalo baadaye lilisababisha matatizo makubwa ambayo tumekuwa tunayajadili kwa miaka zaidi ya 10 sasa.
Mpasuko huo na ombwe hilo vilisababisha mtikisiko wa kisiasa katika CCM, serikali, na taifa zima. Mpasuko huo ndio ulilazimisha vigogo wa CCM kuanza kuhujumiana na kutuhumiana ufisadi – wakiimba wimbo uliotungwa na Chadema.
Mpasuko huo ndio ulimdhoofisha, na baadaye kumwimarisha Lowassa ndani na nje ya CCM. Edward Lowassa huyu tunayemuona, asingekuwa hapo alipo bila ugomvi, vita, chuki, na mpasuko uliotokana na jitihada za wakosoaji wa serikali ya Kikwete. Naamini kwamba leo, Lowassa anapotazama nyuma alikotoka, anajuta kwa jinsi alivyoshiriki kuasisi mfumo mbovu wa kisiasa uliochangia kudumaza demokrasia katika taifa hili.
Tumshukuru Mungu kwamba ajali kadhaa za kisiasa zilimfikisha Lowassa katika hali ya kuwa miongoni mwa wananchi wanaopigania demokrasia tuliyonyimwa kwa muda mrefu. Ni bahati kwamba baadaye alilazimishwa kupata fursa ya kuona makosa ya mfumo wake wa huko nyuma, naye akaanza jitihada za kusahihisha makosa hayo.

Like
14

Leave a Comment

Your email address will not be published.