KIJIJI alikozaliwa, kukukulia na kuanza kusomea Dk. Philip Isidori Nzabhayanga Mpango, hakina mawasiliano ya simu, radio wala barabara zinazopitika wakati wa mvua.
Dk Mpango ndiye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Ni mzaliwa wa Kijiji cha Kasumo, Kata ya Kajana, Wilaya ya Buhingwe , Mkoa wa Kigoma.
SAUTI KUBWA imetembelea katika kijiji hicho na kubaini kuwepo kwa changamto nyingi ambazo zinazorotesha ustawi wa eneo na wakazi wake wengi wakikumbatiwa na “umasikini wa kutupa.”
Wananchi wengi wameonekana kuvaa nguo zilizochaka, kuchanika na wengine wakitembea bila viatu wala kandambili.
SAUTI KUBWA ambayo imeweka kambi katika kampeni za kumpata mbunge wa Jimbo la Buhigwe, limeshuhudia watu kadhaa wenye simu za mkono, wengi wakiwa na “vitochi” wakijazana eneo moja liitwalo Mlimani, wakienda kupata mawimbi ya mawasiliano.
Jimbo hilo kwa sasa halina mbunge baada ya Dk. Mpango kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amechukua nafasi ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa sasa, baada ya kufariki kwa Rais John Magufuli. Magufuli alifariki dunia Machi 17, mwaka huu.
Kijiji cha Kasumo, ni miongoni mwa vijiji ambavyo vinapakana na Burundi. Watu wake wengi – wa mpakani, wamekuwa wakihusiana na wenzao wa nchi hiyo jirani; inadaiwa watu wengi wa maene hayo wanamuingiliano wa kidugu.
Wakazi wa Kijiji cha Kasumo ni wakulima wa mihogo, maharagwe na mahindi kwa kiasi kidogo. Kata ya Kajana, pamoja na changamoto hizo za miundombinu, ina zahanati zinazofanya kazi na kuwa na wahudumu wa afya wanaoonekana “kutosha.”
Jana kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyefika kijijini hapo kufanya kampeni za mgombea wa chama chake, Garula Tandtse, aliwaeleza wananchi kwamba suluhisho la matatizo yao ni kumchagua mgombea wa chama chake.
Zitto alisema ikiwa wananchi hao wanahitaji maendeleo ya kweli, watayapata kupitia kwa Tandtse ambaye amekuwa “kijana wao” na kamwe hatawaangusha kwa kutoonekana kwa wapigakura wake.