Kesi ya Mbowe: Shahidi wa 13 asema alifungua kesi kwa “hearsay”

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo tarehe 8 Februari 2022.

Shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka Mkaguzi wa Polisi Tumaini Swila ameendelea kuhojiwa na mawakili wa utetezi. Wakili Fredrick Kihwelo ameuliza jumla ya maswali 76 na Peter Kibatala ameuliza jumla ya maswali 323. Amejibu hoja tisa (9) za Mawakili wa Serikali na kutoa hoja saba (7). Shahidi amejibu jumla ya maswali 376 yakiwamo yale ya Kihwelo. Jumla ya maswali ambayo alijibu ‘SIFAHAMU’ ni 20, ‘SIWEZI KUJIBU’ ni 7, ‘SIWZI KUONGELEA HAPA’ ni matano (5), ‘HAPANA’ ni 20 na ‘NDIYO’ yako 33.

Jaji ameshaingia mahakamani tayari kuendelea na kesi. Sasa ni saa 3:48 asubuhi.

Kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamuhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe inatajwa.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Ikupendeze Mheshimiwa Jaji mimi naitwa Robert Kidando na nipo pamoja na wakili

 1. Pius Hilla
 2. Abdallah Chavula
 3. Jenitreza Kitali
 4. Nassoro Katuga
 5. Esther Martin
 6. Ignasi Mwinuka na
 7. Tulimanywa Majige

Peter KIBATALA: Mheshimiwa Jaji ikupendeza naitwa Peter Kibatala. Nipo na wakili

 1. Sisty Aloyce
 2. Iddi Msawanga
 3. Maria Mushi
 4. Hadija Aron
 5. Lusako Mwaiseke
 6. Fredrick Kihwelo KIBATALA: Wakili Nashon Nkungu amepata emergency kidogo lakini yupo karibu sana kufika.

JAJI: Kabla hatujaendelea wasiliana naye tujue yupo wapi.

KIBATALA: Sawa Mheshimiwa Jaji.

(Peter Kibatala anatoka ndani ya chumba cha mahakama kwenda kupiga simu).

(Mahakama inasubiri kidogo na ukimya umetawalia).

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba sasa nimtambulishe Wakili Nashon Nkungu. Samahani sana amechelewa kwa sababu ya usafiri.

(Jaji anaita washitakiwa wote wanne. Na wanaitika kuwa wapo mahakamani).

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, shauri limekuja kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa. Tupo tayari kuendelea.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji nasi pia tupo tayari kuendelea.

JAJI: Shahidi nakukumbusha ulikuwa chini ya kiapo, na utaendelea kuwa chini ya kiapo.

JAJI: Nakualika Wakili Fredrick Kihwelo
KIHWELO: Shahidi salama?

SHAHIDI: Salama.

KIHWELO: Kwa mujibu wa ushahidi wako ulisema ulipeleka simu nane.

SHAHIDI: Sahihi.

KIHWELO: Nakukumbusha namba za simu ulizotaja hapa Mahakamani (ambazo ni) 0719-933 386 na 0784-779 944.

SHAHIDI: Sahihi.

KIHWELO: Shahidi ukienda dukani kununua simu, je, ndani kunakuwa na line?

SHAHIDI: Hapana.

KIHWELO: Kwa hiyo simu na line ni vitu viwili tofauti?

SHAHIDI: Sahihi.

KIHWELO: Mwambie Mheshimiwa Jaji zilikiwa simu nane ambazo ziliwasilishwa Mahakamani kama vielelezo, na kama line za simu nane ziliwasilishwa kama vielelezo.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIHWELO: Mkumbushe Mheshimiwa Jaji ni vielelezo namba ngapi, hizo line nane.

SHAHIDI: Line za simu zipo ndani ya simu zenyewe.

KIHWELO: Tumeshakubaliana kuwa line na simu ni vitu viwili tofauti. Sasa nataka kujua line nane ni kielelezo namba ngapi.

SHAHIDI: Hapana. Ziliwasilishwa simu tu. Line zipo ndani.

KIHWELO: Unajua kuwa IMEI namba haionyeshi line bali umiliki wa simu?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Unafahamu kuwa namna pekee ya kuonyesha umiliki wa line ni kuleta namba IMCI?

SHAHIDI: Siyo sahihi.

KIHWELO: Unafahamu kwamba namba ya IMCI ni tofauti na namba za simu?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIHWELO: Unaweza kumwambia Mheshimiwa Jaji kwamba mmeleta namba za IMCI za line hapa Mahakamani?

SHAHIDI: Siwezi kulijibia hilo.

KIHWELO: Kwenye maelezo yako ulisema mwezi Januari 2020 ulipata uhamisho wa muda kwenda Makao Makuu Ndogo Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi pia kuwa mwezi Agosti 2021 ulirudi katika kituo chako cha kazi Temeke?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Uhamishoni wako ulikuwa wa muda gani?

SHAHIDI: Muda wa mwaka mmoja.

KIHWELO: Unaweza kumwambia Mheshimiwa Jaji suala la uhamisho ni mchakato au tukio?

SHAHIDI: Ni taratibu za kazi.

KIHWELO: Twende kwenye taratibu za kazi. Wakati wa mahojiano yako uliaambia Mahakama hii kuwa wakati wa uhamisho ulipitia taratibu mbalimbali?

SHAHIDI: Ndiyo. Nilieleza.

KIHWELO: Shahidi nitakuwa sahihi nikisema dalili zote zinasema kwamba uhamisho wako ulikuwa wa kimkakati na ulihusu shauri hili?

SHAHIDI: Si kweli.

KIHWELO: Wakati wa mahojiano ulisema taarifa za ,atendo y akihalifu zilipokelewa na DCI Robert Boaz?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Na vitendo hivyo vilikuwa vinahusu uchomaji masoko?

SHAHIDI: Ndiyo. Na matukio mengine.

KIHWELO: Ilikuwa kukata miti barabarani?

SHAHIDI: Ndiyo. Na matukio mengine.

KIHWELO: Na maandamano?

SHAHIDI: Ndiyo. Na matukio mengine.

KIHWELO: Katika orodha hiyo niliyotaja kuna ugaidi?

SHAHIDI: Ndiyo. Upo.

KIHWELO: Ulisema kuna viongozi walitaka kudhuriwa. Je, unaweza kumkumbusha Mheshimiwa Jaji majina ya hao viongozi?

SHAHIDI: Lengai Ole Sabaya.

KIHWELO: Mtaje mwingine.

SHAHIDI: Mwingine simfahamu.

KIHWELO: Kwa hiyo ulikuwa unaandika usichokifahamu?

SHAHIDI: Namjua huyo.

KIHWELO: Mtuhumiwa wa kwanza hadi wa nne waliandaa vipi maandamano?

SHAHIDI: Wanajua watuhumiwa.

KIHWELO: Wewe unafahamu vipi kwamba walipanga maandamano?

SHAHIDI: Wanajua watuhumiwa.

KIHWELO: Kwani maandamano ni kosa?

SHAHIDI: Siyo kosa kama ulifuata sheria.

KIHWELO: Kwani walikuwa wameshaandamana au walikuwa wanapanga?

SHAHIDI: Walikuwa wanapanga.

KIHWELO: Ulijuaje kama hawataomba kibali?

SHAHIDI: Hilo siwezi kulijibu.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba tarehe 18 Julai 2020 ulifungua jalada la kesi ya kula njama za kutenda matendo ya ugaidi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba maelekezo hayo ulipewa na ACP Kingai?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba mtu mmoja anaweza kuamua ufunguliwe kosa la namna gani?

SHAHIDI: Siyo sahihi.

KIHWELO: Wakati unaelekezwa na Ramadhan Kingai kufungua shauri hili ulikuwa umepewa jukumu la kuwa mshauri wake?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Kwani alikuambia fungua shauri hili au mlijadiliana kwamba kwa mujibu wa ushahidi huu tufungue shauri hilo?

SHAHIDI: Alinielekeza.

KIHWELO: Kwani alikuambia amejadiliana na nani kwamba wameona inafaa kosa la ugaidi lifunguliwe?

SHAHIDI: Hakuniambia.

KIHWELO: Kwa hiyo ni sahihi kwamba Ramadhan Kingai ndiye aliyetaka shauri hilo lifunguliwe?

SHAHIDI: Siwezi Kujibu hilo.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba wewe ndiyo ulipokea simu kutoka kwa DC Goodluck zilizotoka Moshi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Unaweza kuieleza Mahakama taratibu za makabidhiano?

SHAHIDI: Alinikabidhi zikiwa zimeandikwa PF145 nikaenda kuzihifadhi katika kabati la chuma.

KIHWELO: Ni sahihi pia kuwa Ramadhan Kingai alimwamuru DC Goodluck akukabidhi simu za Khalfani Bwire?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIHWELO: Ni kweli pia simu za Luteni Dennis Urio ulikabidhiwa kwa hati ya makabidhiano?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Na hati ya makabidhiano hiyo ipo Mahakamani hapa?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi pia unawasilisha Mahakamani hati ya makabidhiano ya simu za Khalfani Bwire?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Kwa mujibu wa maelezo yako, ulipokea taarifa za uchunguzi wa simu kutoka kwa Inspekta Innocent Ndowo.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Na ulipokea taarifa hiyo kwa kusaini kitabu cha makabidhiano.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Unaweza kumwambia Mheshimiwa Jaji ikiwa umekiwasilisha Mahakamani hapa kitabu hicho.

SHAHIDI: Sijawasilisha.

KIHWELO: Ni sahihi pia ulipokea simu nane kutoka kwa Inspekta Innocent Ndowo?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni kweli pia unawasilisha hati ya makabidhiano baina yako na Inspekta Innocent Ndowo?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Kwa mujibu wa maelezo yako unasema kuwa Mheshimiwa Freeman Mbowe alikuwa akiwawezesha watuhumiwa kwa fedha na huduma mbalimbali.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Tuambie huduma mbalimbali ni zipi?

SHAHIDI: Mtuhumiwa Freeman Mbowe ndiye aliyekuwa anawasafirisha, kuwapatia malazi huko walipokuwa wanafika Moshi.

KIHWELO: Katika maelezo yako unasema kuwa uchunguzi wa cyber unaonyesha Mheshimiwa Freeman Mbowe alikuwa anawaelekeza watuhumiwa nini cha kufanya. Je, ni wapi tutaona hayo maelekezo?

SHAHIDI: Kwenye maelezo ya onyo ya mshitakiwa.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba jina la Mheshimiwa Mbowe halikuandikwa katika jalada la kesi kwa sababu kama mngeandika angejua?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Na kama angejua angesitisha mipango hiyo?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIHWELO: Kwani shahidi mtu akiwa anataka kutenda uhalifu, halafu akasitisha kuna tatizo?

SHAHIDI: Hakuna. Ila angeweza kubadili njia ya kutenda uhalifu.

KIHWELO: Kwani Mheshimiwa Mbowe ana mtoto Polisi?

SHAHIDI: Hapana.

KIHWELO: Kwani ana ndugu Jeshi la Polisi?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIHWELO: Mwambie Mheshimiwa Jaji ni kwa namna gani taarifa zingemfikia Mheshimiwa Mbowe.

SHAHIDI: Kwa kubadilishana taarifa siyo kwamba watavujisha.

KIHWELO: Kwani shahidi ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kuficha majina ya watuhumiwa?

SHAHIDI: Ndiyo. Ni kawaida.

KIHWELO: Ni matukio gani mengine ambayo Jeshi la Polisi wanaficha majina ya watuhumiwa?

SHAHIDI: Siwezi kuongelea hapa.

KIHWELO: Ila umesema ni kawaida yenu.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIHWELO: Ulisema unafanya kazi Kitengo X?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIHWELO: Kwani shahidi kuna makosa mengine makubwa ambayo unaona ni hatarishi kuyasema hapa?

SHAHIDI: Yapo.

KIHWELO: Tuambie ni mambo yapi zaidi ya haya wanayoshtakiwa.

SHAHIDI: Siwezi kuyasema hapa.

KIHWELO: Mwambie Mheshimiwa Jaji basi kama hutaki kutuambia sisi.

SHAHIDI: Siwezi kusema hapa.

KIHWELO: Ulisema kwamba baada ya Kingai kukupigia mkutane Polisi Central, ulisema hukuwaona watuhumiwa. Ni sahihi?

SHAHIDI: Ni sahihi, ila nilijua wapo Central.

KIHWELO: Shahidi, katika jalada ambalo jina limefichwa, nani alikuwa mtuhumiwa?

SHAHIDI: Freeman Aikael Mbowe.

KIHWELO: Jina lake lilikuwepo kwenye jalada?

SHAHIDI: Hapana. Ila mtuhumiwa ni Mbowe.

KIHWELO: Katika maelezo yako ya ushahidi wako, unasema watuhumiwa wamekiri makosa yao?

SHAHIDI: Ni sahihi. Baada ya kusoma maelezo yao.

KIHWELO: Na ulipowapelekea karatasi nane, walikukatalia kuwa ile michoro na maandishi siyo ya kwetu?

SHAHIDI: Ni sahihi. Walikataa.

KIHWELO: Mtu aliyekiri anawezaje kukataa wakati wa sampuli?

SHAHIDI: Inategemea.

KIHWELO: Kwa hiyo katika maandishi yao walikiri au walikataa?

SHAHIDI: Mshitakiwa wa kwanza alikataa, lakini baada ya sampuri zake kwenda kwa mchunguzi majibu yakawa ni yeye.

KIHWELO: Asante Mheshimiwa Jaji. Ya kwangu ni hayo tu.

(Anasimama Peter Kibatala).

KIBATALA: Shahidi tumeshawahi kukutana mimi na wewe kwa mara ya kwanza au tumeshawahi kufanya kazi pamoja?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Hakuna zoezi lolote la kisheria tulifanya na wewe? Siyo kwenye hii kesi, kuhusiana na uchukuaji wa vielelezo?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Wacha tuendelee. Shahidi unakumbuka wakati unazungumzia kuhusu kidaftari nilisimama kwamba mnafanya zoezi siyo la umuhimu sana? Baadaye tukaambiwa tuache muendelee?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kwenye process ya kukusanya data na sample, zilikuwa processed na baadaye zikaenda kwa expert?

SHAHIDI: Siyo mimi. Kidaftari kilikamatwa na mtu mwingine.

KIBATALA: Ni kweli kwamba sampuli za mwandiko ulizochukua ndiyo zilipelekwa kwa ajili ya uchunguzi?

SHAHIDI: Ni kweli mimi ndiye niliyechukua sampuli.

KIBATALA: Ulichukua sampuli kwa maelekezo ya Musa Nankaa au maelekezo ya Ramadhan Kingai?

SHAHIDI: Kwa maelekezo ya Ramadhan Kingai.

KIBATALA: Unafahamu kazi ya kuchukua sampuli ni kazi ya kisayansi?

SHAHIDI: Ndiyo nafahamu.

KIBATALA: Wewe umesomea mchakato wa uchukuaji sampuli?

SHAHIDI: Nimesomea.

KIBATALA: Wapi?

SHAHIDI: Katika chuo cha taaluma ya Polisi Dar es Salaam.

KIBATALA: Kozi inaitwaje?

SHAHIDI: Device ID Course.

KIBATALA: Ilikuwa module au ilikuwa ni Main Component.

SHAHIDI: Mimi siyo mchunguzi.

KIBATALA: Ndiyo swali langu hapo sasa. Wewe ni mtaalamu?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Mimi nimesomea mambo ya Account for Lawyers ila siwezi kujiita mhasibu. Je, wewe ni mtaalamu?

SHAHIDI: Siyo mtaalamu ila nimesomea.

KIHWELO: Unajua maana ya Exemplar?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIHWELO: Unafahamu maana ya Requested Writing Sample au Requests Exemplar?

SHAHIDI: Fafanua hapo.

KIHWELO: Nifafanue nini wakati hizo ni terms za kisayansi?

SHAHIDI: Sifahamu.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, sisi tunaona ni haki shahidi akiomba ufafanuzi, shahidi apewe ufafanuzi. Tunaona ni haki.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji hakuna shida. Mbeleni akitaka nimfafanulie nitafanya.

KIBATALA: Wewe kwa kuwa unasema kwamba umefundishwa namna ya kuchukua sample, je unafahamu kwamba ikitokea ubishani juu ya saini yangu, moja ya njia mojawapo ni kuniambia nilete nyaraka zingine zenye sahihi yangu hiyo ndiyo inaitwa Requested Exemplar?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Wakati unachukua sampuli kwa Khalfani Bwire, ulikuwa unafahamu hilo?

SHAHIDI: Nilikuwa nafahamu.

KIBATALA: Lakini nyiye mlichukua Requested Sample?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama ulimwambia kwamba pamoja na sampuli zile nane mlichukua nyaraka zingine za Khalfani Bwire.

SHAHIDI: Nilisema.

KIBATALA: Mlichukua nini? Kitambulisho?

SHAHIDI: Notebook.

KIBATALA: Kingai alikuwa anajua kuhusu hiyo notebook?

SHAHIDI: Nataka kufafanua.

KIBATALA: Sitaki ufafanuzi. Jibu swali.

SHAHIDI: Alikuwa hafahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba hiyo notebook ni mali ya mtuhumiwa?

SHAHIDI: Siyo mali ya mtuhumiwa.

KIBATALA: Hiyo notebook alikamatwa nayo nyumbani au ulimkuta nayo kituoni?

SHAHIDI: Ninachofahamu ni kwamba waliichukua nyumbani kwa Khalfani Bwire.

KIBATALA: Na nani alikukabidhi?

SHAHIDI: Sajenti Johnson.

KIBATALA: Nikienda katika maelezo ya Sajenti Johnson nitaona kama alikukabidhi notebook?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Na mlikabidhiana kwa utaratibu upi?

SHAHIDI: Wa kipolisi.

KIBATALA: Na hiyo nyaraka ambayo mlikabidhiana hiyo diary ni muhimu sana kama mtaleta hiyo nyaraka.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji, tutumie neno notebook kuepuka confusion.

KIBATALA: Sawa, I apologize, tutumie nano notebook. Ni nyaraka gani ulionyesha hapa Mahakamani kwamba mlikabidhiana?

SHAHIDI: Sijaonyesha Mahakamani.

KIBATALA: Wakati unamkabidhi mtaalamu wa maandishi hiyo notebook ulimkabidhi kienyeji au kwa maandishi ya kipolisi?

SHAHIDI: Kwa maandishi.

KIBATALA: Maandishi yapi? Mwambie Mheshimiwa Jaji.

SHAHIDI: Barua na dispatch book.

KIBATALA: Umetoa hapa Mahakamani hiyo dispatch?

SHAHIDI: Sijaonyesha.

KIBATALA: Umetoa Mahakamani hiyo barua?

SHAHIDI: Sijaonyesha.

KIBATALA: Turudi tena katika sampuli. Je, unafahamu kwamba unapochukua sampuli unatakiwa uchukue sampuli katika mazingira ambayo ni strictly controlled environment?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Je, hayo mazingira uliyoyachukulia hizo sampuli ni strictly controlled environment?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Unafahamu kwamba ili ku- create controlled environment ulitakiwa umpeleke sehemu nyingine?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Wewe ulifanya hivyo?

SHAHIDI: Ndiyo. Nilimhamisha kutoka kituoni kwenda Jengo la RCO.

KIBATALA: Majengo ya pale tunayafahamu wote. Je zinafika mita 100?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Unafahamu kwamba mwandiko wa mtu unaweza kubadilika kutokana na other factors kama psychology?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba ukichukua mwandiko wa mtu ambaye amefiwa na mzazi unaweza kuwa tofauti?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba mtu akipigwa na kufungwa pingu mwandiko unakuwa tofauti?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unawafahamu waandishi wa sayansi ya uchukuaji wa maandishi?

SHAHIDI: Simfahamu yoyote.

KIBATALA: Unamfahamu mwandishi wa Sayansi ya Uchukuaji wa maandishi anaitwa Garry Breath?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Garry Breath anashauri kuwa unapochukua sampuli za maandishi za mtuhumiwa lazima pawe na mtu mwingine kushuhudia.

SHAHIDI: Ndiyo lakini siyo lazima.

KIBATALA: Kwani wewe na Garry Breath nani mtaalamu wa Sayansi ya Uchukuaji wa maandishi?

SHAHIDI: Mimi.

KIBATALA: Kwani wewe una certificate hata ya sayansi ya uchukuaji wa maandishi?

SHAHIDI: Sina.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Garry Breath ni daktari wa Sayansi ya Uchukuaji wa maandishi anatumiwa mpaka na FBI mbali na kuandika vitabu?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Wewe ulichukua sampuli ngapi kutoka kwa Bwire?

SHAHIDI: Nane.

KIBATALA: Unafahamu kwamba inatakiwa uwe na sampuli siyo chini ya 15?

SHAHIDI: Siyo Kweli.

KIBATALA: Kwani wewe umepata wapi kuwa sampuli unatakiwa uchukue nane?

SHAHIDI: Nilifundishwa chuoni.

KIBATALA: Unafahamu kwamba katika sayansi ya uchukuaji wa maandishi unashauriwa uchukue Upper Case na Lower Case?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Ufahamu kwamba unatakiwa uchukue alphabet, punctuation mark, na namba?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Sasa si ndiyo Upper Case na Lower Case?

SHAHIDI: Nilikuwa sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba sayansi ya uchukuaji wa maandishi inaendana na sayansi ya INC Dating?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Wala hufahamu kwamba INC Dating ni sayansi ya uchukuaji wa maandishi, ilikujia umri wa wino tangu maandishi yaandikwe?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba kwetu sisi ni muhimu kujua kama michoro Khalfani Bwire alichora kabla ya kukutana na Urio na Mbowe?

SHAHIDI: Kwangu siyo muhimu.

KIBATALA: Kwani kama Bwire alichora hiyo michoro kabla ya kukutana na Mbowe na Urio, je, itahusiana na kesi hii?

SHAHIDI: Inategemea.

KIBATALA: Inategemea nini?

SHAHIDI: Unachokisema.

KIBATALA: Kwani kama Bwire alichora hiyo michoro kabla ya kukutana na Mbowe na Urio, je, itahusiana na kesi hii?

SHAHIDI: Siwezi kujibu.

KIBATALA: Unaposema huwezi kujibu ni kwamba hutaki au hujui?

SHAHIDI: Basi rudia swali.

KIBATALA: Kama Bwire alichora hiyo michoro tarehe 5 Mei 2020, je, kidaftari hicho kitakuwa na umuhimu katika hii Kesi?

SHAHIDI: Hakitakuwa na umuhimu.

KIBATALA: Shahidi na bado unasisitiza kwamba kwako umuhimu ilikuwa siyo kimechorwa lini au kimechorwa na nani?

SHAHIDI: Umuhimu ilikuwa kujua kimechorwa na nani.

KIBATALA: Je, unafahamu maana ya Confirmation Bias?

SHAHIDI: Fafanua.

KIBATALA: Ni hali ya mtu kufanya upelelezi akiwa na dhana yake kichwani, ili kuthibitisha anachokiwaza yeye. Sasa unafahamu?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Huoni kwamba inawezekana kilichorwa siku za nyuma?

SHAHIDI: Kama kingekuwa na nia njema asingekataa.

KIBATALA: Unafahamu kwenye sayansi ya upelelezi maana ya Tool Elevation?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Ni hali ambayo unachungulia dirishani au mlangoni, kisha unakuja kusema umeona kuna TV na unaacha kusema vingine ulivyoviona kama vile kabati, meza na redio.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji! Mheshimiwa Jaji! Kama shahidi amesema kwamba hafahamu kuhusu Tool Elevation, sasa ni vizuri kabla hajauliza swali ahakikishe shahidi kaelewa.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji nimepokea maombi ya hisani. Nitafanya.

KIBATALA: Je, shahidi unafahamu kwamba katika sayansi ya uchunguzi na upelelezi wamekatazwa kufanya Tool Elevation?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Shahidi nimesikia unasema kwamba katika shauri hili mlalamikaji ni DCI.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Lakini huyo DCI ni bosi wa Ramadhan Kingai, bosi wa Inspekta Ndowo, bosi wa Inspekta Mahita, bosi wa Inspekta Swila, bosi wa Jumanne Malangahe, bosi wa DC Goodluck, bosi wa Koplo Hafidh, bosi wa Sajenti Nuru, ambao wote ndio wapelelezi na ndio mashahidi.

SHAHIDI: Ni sahihi, lakini kuna vitengo tofauti.

KIBATALA: Kwani hao wa vitengo tofauti hawapo chini ya DCI?

SHAHIDI: Ni bosi wao.

KIBATALA: Wakati huo Deputy DCI alikuwa nani?

SHAHIDI: Alikuwa Charles Kenyela.

KIBATALA: Ni sahihi sasa DCI kama yeye alikuwa ndiye mlalamikaji, asingemwachia Deputy DCI apeleleze?

SHAHIDI: Si kweli.

KIBATALA: Je, RPC akiwa anakutuhumu wewe, anaruhusiwa kukupeleleza?

SHAHIDI: Hairuhusiwi.

KIBATALA: Kwanini hairuhusiwi?

SHAHIDI: Ni utaratibu tu wa kazi.

KIBATALA: Order iliyotoka kwa DCI unaweza kui- challenge?

SHAHIDI: Inategemea.

KIBATALA: DCI alikupigia simu ufungue jalada la ugaidi. Unaweza kumbishia?

SHAHIDI: Kama lipo sahihi nafungua.

KIBATALA: Kwani wewe wakati unapewa taarifa ufungue jalada la kesi ya ugaidi, ulikuwa na material gani mbele yako?

SHAHIDI: Uwepo wa taarifa.

KIBATALA: Kwani hiyo taarifa ulipokea wewe?

SHAHIDI: Alipokea Afande Boazi.

KIBATALA: Mpaka wakati huo ulikuwa umeomgea na Luteni Urio au ilikuwa bado?

SHAHIDI: Ilikuwa bado.

KIBATALA: Kwa hiyo wewe ulifungua sababu ya hearsay?

SHAHIDI: Taarifa zilikuwepo.

KIBATALA: Tunataka kujua kama ulipokea amri au ulifanya kazi kama Independent Detective. Je, wakati unafungua faili ulikuwa umeshamhoji na kuandika maelezo ya Afande Boazi?

SHAHIDI: Ilikuwa bado.

KIBATALA: Tunakubaliana kuwa wakati wanaongea Urio na mlalamikaji Afande Boazi wewe hukuwepo.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Na wewe bado unasisitiza kwamba ulikuwa na material wakati unafungua jalada la kesi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Unafahamu maana ya hearsay?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Ni sahihi kwamba wewe ulifanyia kazi hearsay?

SHAHIDI: Ni hearsay?

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji naomba kwenda washroom (kujisaidia).

(Shahidi anarejea Mahakamani).

KIBATALA: Shahidi tuliishia pale kwamba yale uliyofungulia kesi ni hearsay.

KIBATALA: Je, aliyekuwa in charge wa upelelezi wa kesi hii yote alikuwa huyo huyo Robert Boaz? Je, maelekezo na taarifa zote kuhusu upelelezi yalikuwa yanatoka kwa Robert Boaz?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Je, mtu huyo hana maslahi binafsi?

SHAHIDI: Hana maslahi binafsi.

KIBATALA: Unafahamu maslahi binafsi na viashiria vyake?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Na hapa huvioni?

SHAHIDI: Sivioni.

KIBATALA: Pride, integrity, dignity ya DCI inajadiliwa katika kesi hii.

SHAHIDI: Kinachojadiliwa hapa ni kesi.

KIBATALA: Kwani nani alipokea taarifa akaona kwamba hapa kuna kosa la ugaidi?

SHAHIDI: DCI Robert Boaz.

KIBATALA: Unaona hakuna maslahi binafsi?

SHAHIDI: Hakuna.

KIBATALA: Wewe ulifungua jalada siku ya tarehe 18 Julai 2020?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni kweli kwamba ulifungua jalada bila kuwa na maelezo ya Robert Boaz?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Uliona maelezo ya Robert Boaz tarehe 13 Agosti 2020 kuwa ameandika chini ya kifungu cha 3(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai?

SHAHIDI: Naomba kuona … Ndiyo.

KIBATALA: Unafahamu kwa mujibu wa sheria, askari anayepokea taarifa kwa mdomo au kwa maandishi anatakiwa arekodi kwa maandishi haraka sana?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Je, unataka kuniambia kuwa unaweza kupokea taarifa kwa mtoa taarifa, unaweza kufungua faili la kesi bila kuwa na maelezo ya mlalamikaji?

SHAHIDI: Kama anayefungua kesi ni raia lazima uchukue maelezo, ila kama kwa Polisi maelezo siyo lazima.

KIBATALA: Ni Kifungu gani kinachofanya hiyo tofauti?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Nikupatie PGO utaweza kuona?

SHAHIDI: Sawa. Naomba.

KIBATALA: Tafuta sehemu inayosema kwamba taarifa hii urekodi mapema sana na taarifa fulani siyo lazima.

SHAHIDI: Nimekuambia sikumbuki.

KIBATALA: Take time. Nimekuombea PGO hapo.

(Shahidi anaipekua PGO).

SHAHIDI: Kwenye PGO sioni.

KIBATALA: Sasa nakuonyesha kile kifungu cha 10(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

(Shahidi amesogezewa laptop baada ya mawakili wa Serikali kuihakiki hiyo laptop).

(Shahidi anasoma. Jaji anamtazama).

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama unafahamu maana hicho kifungu.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji sasa nini maana yake.

SHAHIDI: Kwamba askari Polisi ambaye anapokea taarifa, ataandika maelezo ya mtoa taarifa yeyote.

KIBATALA: Sheria imeweka utofauti?

SHAHIDI: Haijaweka.

KIBATALA: Haya. Taja sasa mwongozo ambao unakuruhusu kutoandika maelezo ya mlalamikaji kama ni polisi.

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Sasa mbona ulisema kuna mwongozo? Lengo lako lilikuwa nini?

(Shahidi anakaa kimyaa).

KIBATALA: Haya. Nisionekane naku- harrass. Je, maelezo ya Robert Boaz uliandika lini?

SHAHIDI: Tarehe 13 Oktoba 2020.

KIBATALA: Ni baada ya miezi mingapi?

SHAHIDI: Miezi mitatu.

KIBATALA: Bado mnataka tusione kuwa kesi ni ya kutunga?

KIBATALA: Haya maelezo ya mtoa taarifa umeandika lini?

SHAHIDI: Tarehe 11 Agosti 2020.

KIBATALA: Muda gani umepita?

SHAHIDI: Wiki mbili.

KIBATALA: Kutoka tarehe 18 Julai 2020 mpaka tarehe 11 Agosti 2020 ni wiki mbili?

SHAHIDI: Ni wiki tatu.

KIBATALA: Kwa hiyo tangu ufungue faili hata maelezo ya mtoa taarifa ulichukua baada ya wiki tatu, kwanini tusiamini mlimkamata Luten Dennis Urio mkampiga baada ya kutajwa na Adamoo kisha mkampa ‘dili’ la kuwa shahidi?

SHAHIDI: Si kweli.

KIBATALA: Ulisema kwamba ulifungua P.E file?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Je, faili la P.E ulilipa kosa gani?

SHAHIDI: Lile jalada ni jalada la uchunguzi.

(Wasikilizaji wote mahakamani wako kimyaa wakimtazama shahidi kwa mshangao).

KIBATALA: Ukimaliza kuongea mambo yako jibu swali langu Jalada la P.E. Uliandika kosa au halikuwa na kosa?

SHAHIDI: Jalada la P.E halikuwa limeandikwa kosa.

KIBATALA: Wewe tarehe 14 Kwamba Robert Boaz amekutana na Dennis Urio umeitoa wapi?

SHAHIDI: Nilipata kwenye kikaratasi alichonipa Kingai.

KIBATALA: Kwa hiyo Kingai ndiye kakuambia? Maana Kingai alikuwa katika kikao cha Robert Boaz na Urio.

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Kwanini sasa Robert Boaz katika maelezo yake hakuna sehemu aliyoitaja tarehe 14?,Angalia maelezo hayo hapo.

SHAHIDI: Hakutaja.

(Shahidi anaonekana kubabaika huku akitafuta tarehe kwenye maelezo ya Boaz).

KIBATALA: Tafuta kwa Kingai kama alitaja hiyo tarehe 14.

SHAHIDI: Hajataja.

KIBATALA: Kingai aliandika lini maelezo yake?

SHAHIDI: Tarehe 28 Juni 2021.

KIBATALA: Nikisema hiyo tarehe 14 mmebuni baada ya sisi kumuhoji Luteni Dennis Urio?

SHAHIDI: Si kweli. Mimi ndiye nilifungua faili.

KIBATALA: Kipi ulichokifanya wewe kama mpelelezi mpaka tarehe 18 Julai 2020 mpaka ukapandisha status ya faili?

SHAHIDI: Kingai alinielekeza nifanye hivyo.

KIBATALA: Kwa hiyo hakuna ulichofanya wewe cha kupandisha status ya faili zaidi ya Kingai?

SHAHIDI: Ndiyo. Ilikuwa ni maelezo ya Kingai.

KIBATALA: Kwa hiyo mpaka unapandisha status ya faili kutoka kwa Kingai ulikuwa unawajua hao akina Khalfani Bwire?

SHAHIDI: Hapana. Nilikuwa siwafahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba Urio na wenzake kwa mara ya kwanza walikutana tarehe 20 Julai 2020?

SHAHIDI: Ndiyo nafahamu lakini palikuwa na mawasiliano.

KIBATALA: Ilikuwa ni personal knowledge au mambo ya hearsay?

SHAHIDI: Ilikuwa ni hearsay.

KIBATALA: Na kama siyo hearsay tuambie hapa Dennis Urio aliongea kwa mara ya kwanza na Bwire au Lijenje?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Umeshawahi kuona mawasiliano ya Khalfani Bwire na Moses Lijenje?

SHAHIDI: Kupitia maelezo ya onyo.

KIBATALA: Kwa maana hiyo unamwambia Mheshimiwa Jaji kwamba mawasiliano ya Urio, Bwire na Lijenje ni maelezo ya onyo?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Nini kilisababisha ukapandisha hadhi ya faili?

SHAHIDI: Niliambiwa na Kingai nifanye hivyo.

KIBATALA: Ulisema kwamba mojawapo ya sababu ya kutoweka jina la Mbowe mlikuwa mnaogopa leakage. Je, wakati mnafungua faili Kingai aliwaambia kuwa kuna tuhuma za ugaidi?

SHAHIDI: Hapana

KIBATALA: Nani kati yenu aliyeamua kuwa kuna tuhuma za ugaidi? Ni wewe au Kingai?

SHAHIDI: Siyo mimi.

KIBATALA: Ni lini baada ya kufungua, uli- form professional opinion zako ukaona kwamba hapa kuna tuhuma za ugaidi?

SHAHIDI: Baada ya kumuhoji Luteni Dennis Urio.

KIBATALA: Unasema kwamba wewe ulikuwa katika Kitengo X. Je, ulimwambia Jaji kwamba wewe na Kingai mlikaa ofisi gani?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Mimi nikisema hukusema, je, utakaa?

SHAHIDI: Sikumbuki.

SHAHIDI: Tarehe 27 Julai 2020 nilipokea faili kutoka kwa DCI nikampigia simu kwamba jalada hili mimi na wewe tumepangiwa, na mimi ni msaidizi wako.

KIBATALA: Je, ni protocol ya kawaida faili kutoka kwa junior officer kwenda kwa superior wako?

SHAHIDI: Ni jambo la kawaida.

KIBATALA: Tarehe ngapi ambayo mliamua kuwa msiweke jina la Freeman Mbowe katika faili?

SHAHIDI: Tarehe 18 Julai.

KIBATALA: Je, kwenye jalada la P.E jina la Mbowe lilikuwepo?

SHAHIDI: Lilikuwepo.

KIBATALA: Wakati huo Dennis Urio alikuwa anafahamu tayari kwamba Mbowe ni mtuhumiwa?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba Dennis Urio alikuwa anaishi wapi wakati huo?

SHAHIDI: Morogoro.

KIBATALA: Je, Dennis Urio ana kiapo cha Jeshi la Polisi?

SHAHIDI: Hapana, lakini ni askari wa JWTZ.

KIBATALA: Je, Dennis Urio mlimwapisha asitoke siri?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba Dennis Urio alikutana na Moses Lijenje na Khalfani Bwire akawaambia mnaenda kwa Freeman Mbowe (na) akiwashawishi mambo ya uhalifu mniambie?

SHAHIDI: Mimi sikupata nafasi kuongea naye.

KIBATALA: Je, unaona dhana yako ya usiri bado upo wakati Kingai tayari ameshaongea na watu zaidi?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba katika kikosi cha Ramadhan Kingai, gari yao ilikuwa na dereva wa cheo cha chini anaitwa Azizi?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba watuhumiwa walikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi Moshi?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwamba watuhumiwa walienda Kituo cha Polisi Mbweni? Je, bado kuna sababu ya usiri?

SHAHIDI: Watuhumiwa walikuwa wameshakamatwa.

KIBATALA: Freeman Mbowe alikuwa amekamatwa?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Sasa ni Mbowe mpumbavu kiasi gani kiasi magaidi wake wamekamatwa halafu yeye awe mtaani?

SHAHIDI: Jukumu letu lilikuwa kuzuia uhalifu usitendeke.

KIBATALA: Unafahamu tofauti ya kulipua vituo vya mafuta na kuchoma kituo cha mafuta?

SHAHIDI: Ni mambo mawili tofauti.

KIBATALA: Wewe ulikuwa na maelezo ya mashahidi ya washitakiwa, kwamba kosa lilikuwa ni kulipua vituo vya mafuta na kuchoma masoko.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Lakini Robert Boaz anasema kwamba ilikuwa ni kuchoma vituo vya mafuta.

SHAHIDI: Lakini haibadilishi kitu.

KIBATALA: Haibadilishi kitu wakati umeshasema ni mambo mawili tofauti?

KIBATALA: Na Kingai na Dennis Urio wanasema kulipua vituo vya mafuta. Je, mpaka hapo kuna sehemu mtu kazumgumzia kuchoma moto masoko?

SHAHIDI: Hakuna sehemu ambayo wamesema watachoma masoko.

KIBATALA: Sasa wewe taarifa ya kuchoma moto masoko ulitoa wapi?

SHAHIDI: Ni terminology tu.

KIBATALA: Mwanzoni si umesema kwamba ni tofauti? Ila sasa hivi ni terminology tu?

KIBATALA: Haya. Kwa Jumanne Malangahe anasema kuchoma moto vituo vya mafuta na kulipua mikusanyiko ya watu.

SHAHIDI: Tuone.

KIBATALA: Soma hapa.

(Shahidi anasoma).

SHAHIDI: “Kuchoma vituo vya kuuzia mafuta na kulipua mikusanyiko ya watu.”

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama Jumanne anasema kulipua masoko.

SHAHIDI: Hakuna sehemu imeandikwa kulipua masoko.

KIBATALA: Katika ushahidi wako unasema moja ya sources zako ….

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, tulikuwa tunajadiliana na wenzangu hapa, lakini kuanzia pale alipoenda kwa Boaz, Urio na sasa kwa shahidi mwenyewe … Sisi kwa shahidi mwenyewe hatuna tatizo,Mahakama inakuwa sehemu ngumu sababu wale wengine wameshatoa ushahidi wao … Kama wanataka kuingiza maelezo yale, ilitakiwa iwe kwa wale mashahidi. Kwa mujibu wa kifungu 164 cha Sheria ya Ushahidi kimeweka masharti. Sisi tunaona kwamba kile kinachoingia katika ushahidi, kinaingia kinyume na utaratibu.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, kwa heshima na taadhima, wao wenyewe walikuwa wanazungumzia kidaftari ambacho hakipo mahakamani … Inaweza kuwa na usawa. Pili kama hakusimama wakati huo, basi kuna Estoppel. Hawezi kuja sasa kuomba Mahakama ifute ushahidi kwa kazi ambayo hatujaisaidia. Tatu ni kwamba nauliza kutokana na majibu ya shahidi mwenyewe.

KIBATALA: Labda kama nitauliza maswali ambayo hayapo. Hii ni cross examination Mheshimiwa Jaji. Ni hayo tu.

JAJI: Wakati wakili anauliza maswali kuhusu eneo hilo shahidi aliomba aruhusiwe kurejea, ili aweze kujibu. Kwa namna ambavyo ameuliza, ameuliza akiwa anarejea, na shahidi amejibu maswali hayo kwa namna ambavyo alikuwa anarejeshwa na upande wa utetezi. Ni kweli nyaraka hazipo katika kumbukumbu za Mahakama. Katika Mazingira hayo Mahakama inaona kwa namna hiyo maswali ambayo yameulizwa na kujibia hayawezi kuondolewa. Mahakama inaelekeza wakili aendelee kuuliza maswali. NATOA AMRI.

(Mawakili wa pande zote mbili wanakubaliana na uamuzi Jaji kwa kusimama na kuinama kidogo).

KIBATALA: Katika maelezo yako umeona kuwa hakuna kulipua mikusanyiko ya watu?

SHAHIDI: Ni sahihi. Kwenye maelezo siwezi kuandika kila kitu.

KIBATALA: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba kwenye maelezo huwezi kuandika kila kitu?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Katika maelezo yako hakuna tarehe 14 Julai 2020 kama sehemu ya kufanya majukumu yako.

SHAHIDI: Ni kweli hakuna.

KIBATALA: Ni kweli shahidi statement yako umerekodiwa mapema sana kuliko ushahidi wa leo hapo kizimbani.

SHAHIDI: Ni kweli.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, ni saa saba kasoro, naomba kutoa hoja tuhairishe. Nikirudi tuweze kuendelea na maswali ya shahidi.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji hatuna pingamizi.

JAJI: Natoa ahirisho mpaka saa 7:45.

Jaji anatoka Mahakamani

Mahakama imerejea.

Jaji amerejea Mahakamani. Muda ni saa 8:27

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, quorum yetu ipo vile vile na tupo tayari kuendelea.

Peter KIBATALA: Mheshimiwa Jaji na mimi sijaarifiwa formally kwamba kuna Mtu kaondoka. Kuna kuchelewa tu kwa baadhi yetu. Kwa hiyo tupo tayari kuendelea.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, kwa hisani ya Mahakama na faida ya shahidi, naomba nikumbushwe jibu letu la mwisho.

JAJI: Kabla ya kufungua jalada.

KIBATALA: Shahidi nakuonyesha maelezo yako hapa baada ya kufungua jalada.

(Shahidi anasoma maelezo aliyopewa asome).

SHAHIDI: “Baada ya kufungua jalada hilo Afande DCI Robert Boaz alinitaka mimi kuwa mpelelezi wa shauri hilo. Baada ya kupewa jukumu hilo nilianza kuandika maelezo mbalimbali yakiwemo ya Dennis Urio.”

KIBATALA: Je, katika maelezo hayo uliyoyasoma, kuna mahala popote panapoonyesha wewe ulikuwa msaidizi wa Kingai au Kingai kushirikiana na wewe?

SHAHIDI: Huko sijaandika.

KIBATALA: Unaendelea kwa kusema kuwa baada ya hapo uliendelea na hatua mbalimbali ikiwemo kupeleka silaha aina ya pistol A5340 na risasi tatu ambapo nilichukua na kurudisha kwa Sajenti Nuru kwa kutumia Exhibit Register namba 19/2020?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Hii Exhibit Register ni mnyororo wa kipolisi kwa ajili ya kutunza kielelezo?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kwa hiyo kama tukitaka kuangalia makabidhiano ya wewe na Sajenti Nuru tutaona kwenye Exhibit Register?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Katika kuonyesha kama ulipokea kutoka kwa Sajenti Nuru wewe ulisaini na yeye akaweka particulars zake?

SHAHIDI: Niliandika majina na yeye akaandika majina.

KIBATALA: Hata tarehe na muda pia tutaona huko?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ulitoa kama kielelezo Exhibit Register 19/2020 hapa Mahakamani?

SHAHIDI: Sijatoa.

KIBATALA: Ili kuondoa mashaka, Exhibit Register tunayozungumzia ni hii ambayo inazungumzia bastola ambayo umeitambua hapa Mahakamani?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Kwanini hujaileta?

SHAHIDI: Sikuongozwa kuileta.

KIBATALA: Na hii Exhibit Register ni ya muhimu au siyo ya muhimu?

SHAHIDI: Ni ya muhimu.

KIBATALA: Kwa vyote vyote hakuna mahala ambapo umeitambua ile bastola kwa maneno CZ 100 Caliber kutoka mdomoni kwako?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Ni kwa sababu ile bastola ilikamatwa mahala fulani, ikafika kwa Sajenti Nuru kupitia kwa DC Goodluck, ile bastola ya Luger A5340 ulitambua kutoka kwenye mlolongo huo?

SHAHIDI: Pamoja na kuiangalia silaha yenyewe.

KIBATALA: Zile risasi pia unafahamu kwamba kila risasi moja ina vitambulisho vyake ikiwemo calibre?

SHAHIDI: Ndiyo nafahamu.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji nimeomba wanipatie bastola na risasi zake.

KIBATALA: Bwana Sebastien Madembwe ambaye ni Registar (Mrajisi) wa Silaha, je, katika barua yako kwenda kwake ulitaja zile taarifa za ziada za CZ 100 Calibre?

SHAHIDI: Haikuonyesha.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kuwa kama mtu atakuwa anaichunguza kwa nje hiyo bastola ataona maandishi ya CZ 100 Caliber.

SHAHIDI: Nimeshaikagua.

KIBATALA: Je, kuna mahala popote umeona maandishi ya CZ 100 Caliber?

SHAHIDI: Ndiyo. Yapo.

KIBATALA: Na wewe unasema ulipokabidhiwa bastola hiyo uliikagua?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ulipokagua hayo maandishi uliyaona au hukuyaona?

SHAHIDI: Niliyaona.

KIBATALA: Vipi kuhusu katika maelezo yako? Uliyataja hayo maneno?

SHAHIDI: Sikuyataja.

KIBATALA: Wakati unamkabidhi Sajenti Nuru ulimtajia au hukumtajia?

SHAHIDI: Sikumtajia.

KIBATALA: Je, anaruhusiwa kuongeza taarifa za ziada?

SHAHIDI: Ndiyo. Anaruhusiwa.

KIBATALA: Hii silaha alikabidhiwa Sajenti Nuru na DC Goodluck, na wewe ukaichukua na kurudisha kwa hati.Swali ni je, entry inatakiwa iwe kama ambavyo mlikabidhiana au kutofautiana?

SHAHIDI: Inaweza kutofautiana.

KIBATALA: Je, hayo maneno ya CZ 100 Caliber ni sehemu ya utambulisho au mapambo?

SHAHIDI: Ni sehemu ya utambulisho.

KIBATALA: Kwa ruhusa ya Mahakama nakuonyesha kielelezo namba P5 na P4.

(Kibatala anamwonyesha shahidi vielelezo).

KIBATALA: Hiyo ni live catridge. Je, chini yake kuna namba za caliber au hakuna?

SHAHIDI: Zipo.

KIBATALA: Msomee Mheshimiwa Jaji tafadhali.

SHAHIDI: Ni 9mm.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji samahani! Ninachojua katika risasi ni palikuwa na live ammunition. Yeye anatumia live catridge.

KIBATALA: Shahidi wacha tutumie neno la kaka yangu la live ammunition. Soma tena.

SHAHIDI: 9mm.

KIBATALA: Wakati wa ushahidi wako ulieleza description yake hiyo live ammunition kuwa ni 9mm?

SHAHIDI: Sikueleza.

KIBATALA: Katika maelezo yako ulizungumzia suala la kutoa kwa ballistic ukamkabidhi Sajenti Nuru?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji tunaomba wakili mwenzetu Peter Kibatala, alikuwa anaulizia kuhusu kupeleka kwa Mrajisi, as opposed kwa uchunguzi wa mlipuko.

KIBATALA: Wacha nirudie swali Mheshimiwa Jaji.

KIBATALA: Shahidi umeandika maelezo?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Je, ulirekodi tukio la makabidhiano ya bunduki na risasi baina yako wewe na Sajenti Nuru. Je, hiyo risasi ambayo ipo hai ulitaja?

SHAHIDI: Sikutaja.

KIBATALA: Unaweza kufahamu kwanini waliotengeneza hiyo risasi waliandika kwa sababu gani?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kuwa maana yake ni nini.

SHAHIDI: Ni risasi zinazotumika na bastola.

KIBATALA: Sawa. Nakupa sasa na kielelezo namba P5. Tafadhali na zenyewe ziangalie katika kitako. Anza ya kwanza. Je, ina maandishi tambulishi au haina?

SHAHIDI: Sioni vizuri.

KIBATALA: Yapo au hayapo?

SHAHIDI: Kuna maandishi.

KIBATALA: Na unakumbuka upo chini ya kiapo?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kwamba wewe huoni hapo neno 9mm Luger PMP? Kama huoni nikuombee umuonyeshe Jaji. Kwa sababu chini ya uangalizi wake wewe ndiye uliapishwa.

SHAHIDI: Nimeyaona.

KIBATALA: Yanafanana au yanatofautiana na maneno yaliyopo katika kielelezo P4?

SHAHIDI: Ni tofauti.

KIBATALA: Maneno PMP katika hiyo live ammunition yanafanana?

SHAHIDI: Yanatofautiana.

KIBATALA: Maneno Luger yanafanana?

SHAHIDI: Kwa maneno hayo zinatofautiana.

KIBATALA: Wewe ndiye uliyemkabidhi Sajenti Nuru. Je, ulifafanua kwa Mheshimiwa Jaji?

SHAHIDI: Sikufafanua.

KIBATALA: Unafahamu kwamba sisi tunatakiwa kulinganisha hizo risasi ili tujue kama kweli zilikamatwa kwa Adamoo au zilikuwa planted?

SHAHIDI: Siyo muhimu kwa upande wa risasi.

KIBATALA: Nenda kwenye hilo ganda la risasi.

SHAHIDI: Kinachoonekana hapa ni 9mm, mengine hayasomeki.

KIBATALA: Kwa ushahidi wako huoni maneno GEKO hapa?

SHAHIDI: Maneno yapo ila siwezi kuyasoma.

KIBATALA: Ngoja Jaji aandike kwamba maneno yapo ila siwezi kuyasoma.

KIBATALA: Hizo spent ammunition mbili zinafanama au zinatofautiana?

SHAHIDI: Zinatofautiana.

KIBATALA: Ulifafanua tofauti hiyo ya muhimu kwetu?

SHAHIDI: Sikufafanua.

KIBATALA: Katika conclusions zako unasema ushahidi mwingine ni watuhumiwa hao watatu kukutwa na silaha na risasi tatu, jambo linaloonyesha kweli walikuwa wanapanga uhalifu?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sehemu gani ambayo tutaona kuna tofauti?

SHAHIDI: Kwenye maelezo yangu utaona.

KIBATALA: Unakumbuka shahidi awali nilikuuliza duty yako unapokutana na Eliminative Evidence unatakiwa kuitambua?

SHAHIDI: Fafanua.

KIBATALA: Unatakiwa uende katika upelelezi ukiwa unaenda na majibu yako.

SHAHIDI: Nakumbuka.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji ni waapi tutaona ukishughulika na tofauti hizo.

SHAHIDI: Tofauti haiondoi dhana ya kwamba walikamatwa na silaha.

KIBATALA: Jibu swali langu.

SHAHIDI: Sikueleza.

KIBATALA: Jana ulimtaja Koplo Charles kumpa simu nane.

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kwa ufahamu wako wewe mtu muhimu katika kuonyesha Chain of Custody na kupokea simu zako, je, katika kesi hii kwa ufahamu ametajwa kama shahidi?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: …Niliuliza Exhibit Register 251/2021.

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Je, hiyo Exhibit Register ilikuwa mnajaza kama mapambo au zoezi la kisheria?

SHAHIDI: Ni zoezi la kisheria.

KIBATALA: Na ni Exhibit Register hiyo 251/2021 ndiyo ambayo tutaona kwamba Koplo Charles alipokea kutoka kwako simu?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Umetoa hapa Mahakamani kama kielelezo?

SHAHIDI: Sijaitoa.

KIBATALA: Ni katikati Exhibit Register hiyo ndiyo tungeona description ya kila simu Techno, Bundy, Samsung?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sahihi pia katika Exhibit Register 251 /2021 tungeona pia Description_ ya each individual card?

SHAHIDI: Inategemea.

KIBATALA: Mliandika katika Exhibit Register hiyo zile CID namba?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kumbe ni nyaraka moja ya muhimu sana?

KIBATALA: Je, ripoti ya uchunguzi, pamoja na Extraction Report mliandika katika Exhibit Register?

SHAHIDI: Hiyo sikukabidhi.

KIBATALA: Na je, ulimwambia Jaji kwamba kwanini hukuleta Mahakamani?

SHAHIDI: Sikumwambia.

KIBATALA: Je, hii Exhibit Register ni ya muhimu au siyo muhimu?

SHAHIDI: Ni ya muhimu katika utunzaji wa vielelezo.

KIBATALA: Katika ushahidi wako unasema kwamba mtuhumiwa Freeman Mbowe ndiye aliyeanzisha mchakato wa kuwatafuta makomandoo wa zamani? Je, ni kwa uthibitisho upi?

SHAHIDI: Ni Luteni Dennis Urio ndiyo alisema hivyo.

KIBATALA: Unakubaliana na mimi kwamba ili tupime hili lazima tuangalie ushahidi wa Dennis Urio na tuupime?

SHAHIDI: Na kwa kuwakamata wale watuhumiwa wanne.

KIBATALA: Kwani uliwakamata wewe?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji. Naomba shahidi apewe muda wa kujibu, maana anajibu hili anaulizwa hili.

KIBATALA: Wewe ulifanya nini zaidi ya maneno ya Dennis Urio?

SHAHIDI: Niliweza kufanya uchunguzi nikagundua kuwa Freeman Mbowe … nikapeleka faili ngazi ya juu.

SHAHIDI: Na mashahidi kama Justine Kaaya ambapo alisema katika ushahidi wake kuwa mtuhumiwa Freeman Mbowe alikuwa anamtaka taarifa bila yeye kujua ni za nini.

KIBATALA: Kama nimeelewa vizuri ni, transactions za Mbowe na Urio, maelezo ya Urio na Kaaya.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Tuanze na Justine Elia Kaaya. Si alikuwa mshitakiwa katika hii kesi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Alipokamatwa unafahamu kwamba aliyeandikwa maelezo yake ni Jumanne?

SHAHIDI: Siyo sahihi.

KIBATALA: Aliandikwa maelezo ya onyo na nani?

SHAHIDI: Sijui lakini ni huko huko Arusha.

KIBATALA: Lakini maelezo ya Kaaya uliyaona?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji maelezo ya Justine Kaaya yapo wapi ili tuweze kuyalinganisha katika yale ya onyo na yale ya ushahidi.

SHAHIDI: Hayapo Mahakamani.

KIBATALA: Alichokiandika Justin Elia Kaaya kinafanana au kinatofautiana na maelezo ambayo ameandika mara ya mwisho?

SHAHIDI: Hayawezi kufanana, ila yale mambo ya msingi yanafanana.

KIBATALA: Na hamkuona umuhimu wa kuyaleta ili tuone aliachiwa kwa ahadi ya kuwa shahidi au aliachiwa kwa sababu upelelezi umekamilika?

SHAHIDI: Hatukuona umuhimu.

KIBATALA: Kama maelezo ya Kaaya yangekuwapo Mahakamani kama kielelezo, tungepata nafasi ya kuyalinganisha au tusingepata?

SHAHIDI: Hakuna hiyo nafasi ya kuyaleta.

KIBATALA: Narudia tena. Kama maelezo ya Kaaya yangekuwapo Mahakamani kama kielelezo, tungepata nafasi ya kuyalinganisha au tusingepata?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, hilo swali halipo. Kaaya siyo mshitakiwa. Ni shahidi. Sasa maelezo yake yangetoka wapi?

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, ukinielekeza nitaenda pengine, ila swali langu halijajibiwa.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji! Mheshimiwa Jaji! Wakili anauliza kitu ambacho shahidi ameshasema kuwa hakurekodi yeye maelezo ya Kaaya. Hakuna namna yoyote kwenye procedure au Sheria ambayo wangeweza kuyaleta.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, hakuna hoja hapo. Ni maoni yake binafsi tu. Ndiyo maana hajataja sheria wala kesi ambbayo ameitumia.

JAJI: Nimesikia hoja ambayo upande wa Mashitaka wameleta. Ni kweli unasema kwamba wakili anauliza swali kuhusu mtu ambaye ni shahidi ambaye alikuwa mshitakiwa. Ni wazi kwamba maelezo yake ya onyo hakuna namna ambayo yangeweza kuja Mahakamani. Kwa sababu wakili ameuliza kwa haki ya mteja wake, wakili yupo kwenye cross examination. Mahakama inaona kwamba itaona mbeleni kama yatakuwa na back up, na itafanya maamuzi yake. Mahakama inaona kwa maana hiyo wakili aendelee kuuliza maswali. NATOA AMRI.

(Mawakili wa pande zote mbili wanakubaliana na uamuzi Jaji kwa kusimama na kuinama kidogo).

KIBATALA: Kaaya aliyasema katika maelezo ya tarehe 30 Julai 2021 wewe kama mpelelezi uli- verify vipi maelezo ya Kaaya?

SHAHIDI: Kupitia maelezo ya onyo washitakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu.

KIBATALA: Maelezo ya mshitakiwa wa kwanza hayapo Mahakamani. Ila kwa ushahidi wako ni kwamba nikiomba maelezo ya Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya nitaona wanasema walikaa kikao na Kaaya?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naomba kielelezo namba P1 (Maelezo ya onyo ya Adam Kasekwa).

(Kibatala anapatiwa kielelezo).

KIBATALA: Asante.

KIBATALA: Shahidi nimepewa maelezo ya onyo ya Adam Kasekwa. Nitafutie mstari unaosema kwamba palikuwa na kikao kilichofanyika Adamoo, Ling’wenya, Bwire na pengine Mbowe.

SHAHIDI: Nimeona.

KIBATALA: Soma kwa sauti.

SHAHIDI: “Mnamo tarehe 1 Agosti 2020 saa 11 alfajiri alituita na kutuonyesha picha ya Lengai Ole Sabaya.”

KIBATALA: Swali langu umesema kwenye maelezo yako umesema kwamba nikisoma hapo kwenye maelezo ya Adamoo anakiri alikaa kikao na Justine Elia Kaaya.

SHAHIDI: Hicho kikao ndiyo walikaa.

KIBATALA: Nataka unisomee majina.

SHAHIDI: Mie ndiyo nimeshasoma sasa (anamnyoshea Kibatala karatasi achukue).

KIBATALA: Sasa huo ni ujeuri. Naona hutaki tena tuendelee kuulizana maswali kirafiki.

SHAHIDI: Hakuna majina yao humu.

KIBATALA: Sasa je? Kaaya katajwa humo?

SHAHIDI: Hajatajwa.

KIBATALA: Ling’wenya katajwa?

SHAHIDI: Hajatajwa.

KIBATALA: Bwire likuwepo?

SHAHIDI: Nimeona hapa tarehe 25 Agosti 2020 kwamba walikutana.

KIBATALA: Sasa tarehe 1 Agosti 2020 ndiyo tarehe 25 Agosti 2020?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Sasa je, na hapo Kaaya katajwa?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Mahala pengine ambapo ulisema kwamba ulipata taarifa hizo ni maelezo ya Ling’wenya?

SHAHIDI: Sahihi.

KIBATALA: Haya. Chukua maelezo ya Mohammed Ling’wenya umitafutie mahala ambapo Ling’wenya amekiri kwamba alikaa kikao yeye, Adamoo, Mbowe na Kaaya, hata kama na Bwire pia ni sawa tu.

SHAHIDI: Baada ya Khalfani Bwire kwenda kumuona Mbowe waliongea kwa muda kisha Bwire akatuita, kwamba yeye anayetusumbua ni Sabaya, inabidi apewe discipline.

KIBATALA: Hapo kuna mahala Kaaya anatajwa?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Wewe umesema kwamba moja ya viashiria vyako ni maelezo ya kukiri ya haya washitakiwa hawa wawili. Sasa alichokuambia Kaaya ndiyo maelezo ya hawa wawili kukiri?

SHAHIDI: Nishajibu.

KIBATALA: Ni mpango upi ambao Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya walikuwa wanatekeleza pale Rau Madukani?

SHAHIDI: Walikuwa hawatekelezi.

KIBATALA: Ulisoma maelezo ya onyo la Mohammed Ling’wenya?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Alisema nini juu ya uwepo wake Rau Madukani?

SHAHIDI: Naomba nikumbushwe.

KIBATALA: Naomba kielelezo namba 13. Soma Ling’wenya anasema Rau Madukani ni kwa nani yake.

SHAHIDI: “Nasema niliporudi Moshi Mjini, tukiendelea kuchunguza maeneo mengine, wakati huo hatukufikia Aishi Hotelini, bali kwa dada yangu anayeishi Rau Madukani.”

KIBATALA: Sasa ni kweli kilichowapelekea Rau Madukani ni kwa sababu ndipo walipofikia na kwa sababu kuna dada yake anaitwa Athima Kibibi.

SHAHIDI: Ni sahihi ila hawakukamatiwa kwa dada yake.

KIBATALA: Kuna mahala ambapo anasema kwamba walikamatwa wakiwa kwenye maandalizi?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Kwani ukisoma huko juu walipokwenda kufanya surveillance ni Arusha au Rau Madukani?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Halafu ukiwa unajibu ongeza sauti wateja wangu wasikie.

KIBATALA: Wewe kama mpelelezi, Justine Kaaya aliwahi kukuambia kwamba alipoombwa taarifa za kuhusu Sabaya alienda kuripoti kwa mbunge wake?

SHAHIDI: Hakunieleza.

KIBATALA: Je, aliwahi kukuambia kama aliripoti mahala popote kabla ya kukamatwa?

SHAHIDI: Hakuwahi kunieleza.

KIBATALA: Katika maelezo ya Justine Kaaya aliwahi kukuambia katika interaction zake alikuwa anafanyia kwenye Land Cruiser ya Mbowe?

SHAHIDI: Hajawahi kuniambia.

KIBATALA: Wewe kama mpelelezi hukuona umuhimu wa kurekodi identity ya hilo gari?

SHAHIDI: Sikuona umuhimu.

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji naomba kwenda WASHROOM!!

(Shahidi karejea).

KIBATALA: Kama identity ya hiyo Land Cruiser uliona siyo ya muhimu, kama halikuwa kitu cha muhimu mbona uliandika katika maelezo yake ya tarehe 30 Julai 2021?

SHAHIDI: Kuweka niliona ndiyo muhimu ila kufuatilia ndiyo sikuona umuhimu.

KIBATALA: Ni sahihi sasa haya aliyokuja kuyasema kuhusu Freeman Mbowe aliyasema baada ya kuachiwa baada ya kutoka kwenye kesi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sahihi baada ya kuandika maelezo haya ndiyo alipewa vifaa vyake ikiwemo pesa (dola)?

SHAHIDI: Hapana. Alipewa kabla.

KIBATALA: Wewe kama mpelelezi, mmoja wa watekelezaji wa mpango wa kumdhuru Sabaya, Moses Lijenje na bosi wake Bwana Mbowe Master Mind yupo nje, je mlimtaarifu Sabaya au mamlaka yake ya uteuzi ili waongeze ulinzi?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Mliwafahamisha mamlaka wengine kama TISS?

SHAHIDI: Haikuwa jukumu langu.

KIBATALA: Unafahamu alikuambia viongozi wako?

SHAHIDI: Hawakuniambia.

KIBATALA: Wewe kama mpelelezi uliwahi kushauri?

SHAHIDI: Sikuwahi.

KIBATALA: Ni sahihi uliposoma statement hizo mbili hasa ya Ling’wenya kwamba Sabaya anamsumbua katika uchaguzi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sahihi pia katika maelezo ya Mohammed Ling’wenya kwamba ampigie Sabaya ili kumtia discipline ili asiendelee kung’oa bendera?

SHAHIDI: Naomba nijikumbushe.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, naomba kielelezo namba P13.

SHAHIDI: Yapo hayo ila siyo kushusha bendera.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama kuna sehemu yoyote lengo la Mbowe lilikuwa kuzua taharuki.

SHAHIDI: Hakuna.

KIBATALA: Unafahamu kwamba kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga, Mkuu wa Wilaya Fatma Kimaro alishambuliwa na watu wakapelekwa Mahakamani? Je, unakumbuka hilo tukio?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Haya! Soma na maelezo ya Adamoo.

(Shahidi anapewa maelezo ya Adamoo na anaanza kusoma).

SHAHIDI: “Kuanzia usiku wa tarehe 25 Julai 2020 tulikaa watu watano, mimi, Ling’wenya, Khalfani, na Freeman Mbowe pamoja na mtu mwingine anayeitwa Kakobe mlinzi wa Freeman Mbowe.”

(Shahidi anaendelea kusoma).

KIBATALA: Kwa hiyo ni sahihi kuwa motive ya kikao hicho hata kama kweli walikataa, lengo la Mbowe la kumdhuru Sabaya ilikuwa sababu Sabaya anavuruga wapiga kura wake?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sahihi kwenye paragraph hiyo hiyo lengo la kumdhuru Sabaya ni kwa sababu Sabaya amefanya hujuma na bendera nyingi zimeshushwa?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Ni sahihi pia hata kama kweli kikao kilikaa, lengo la Mbowe anasema raia wametishiwa?

SHAHIDI: Ni kweli.

KIBATALA: Pia ni kwa sababu Mbowe anasema Sabaya alikuwa na mpango wa kuiba kura?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Kuna mahala Mbowe anasema lengo la kumdhuru Sabaya ni kuzua taharuki? Kwenye maelezo ya Adamoo yanasema kuwa walipanga kumdhuru kwa kumpiga spray ya sumu?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Je, mbinu hizo mbili za maelezo ya Adamoo na Ling’wenya vinafanana?

SHAHIDI: Havifanani.

KIBATALA: Kwa kuwa havifanani, je, uliwahi kuandika maelezo ya nyongeza kutoa ufafanuzi kwamba iweje watu wawili wamekiri halafu maelezo yapo tofauti?

SHAHIDI: Sikuwahi kuandika.

KIBATALA: Je, uliwahi kupeleleza kuhusu hii dawa yanye sumu ambayo ilikuwa apuliziwe Sabaya kuwa ingepatikana wapi?

SHAHIDI: Sijawahi.

KIBATALA: Ni kweli au si kweli Mohammed Ling’wenya hazungumzii kuhusu hiyo dawa yenye sumu katika maelezo yake?

SHAHIDI: Hajazungumzia.

KIBATALA: Ulichukua taarifa kuhusu hii dawa yenye sumu kwa ajili ya upelelezi?

SHAHIDI: Sikuchukua.

KIBATALA: Huyu Sabaya, ambaye Mbowe anasema kwamba Sabaya anashusha bendera, kutisha raia, na mpango wa kuiba kura, je, ni sahihi kahukumiwa kwa matendo kama hayo ya kuwatendea uhalifu wananchi?

SHAHIDI: Siwezi kuzungumzia hilo.

KIBATALA: Ni hutaki, hufahamu au ni jeuri?

SHAHIDI: Sijafuatilia hiyo kesi yenyewe.

KIBATALA: Je, dhumuni la kukubaliana na Dennis Urio mlikuwa mnamtafutia Mbowe vijana wa ulinzi au magaidi? Au walinzi ambao watakuja kugeuka kuwa magaidi?

SHAHIDI: Ni walinzi ambao watakuwa wanarejesha taarifa.

KIBATALA: Kwa ufahamu wako wewe, Mbowe aliomba kwa Denis Urio walinzi au wahalifu?

SHAHIDI: Dennis ndiye aliyebuni hawa waende kuwa walinzi.

KIBATALA: Unaposema katika maelezo kuwa Freeman Mbowe ndiye aliyeanzisha mchakato wa kupata walinzi au kupata wahalifu?

SHAHIDI: Wa kupata wahalifu.

KIBATALA: Ila yeye akapelekewa nini?

SHAHIDI: Akapelekewa walinzi.

KIBATALA: Je, baada ya Mbowe kuomba wahalifu kisha Dennis Urio kupeleka walinzi, bado nyiye mlikuwa mnamuona Urio ni mwaminifu?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Kwa hiyo suala la kuweka watu undercover ni zoezi la kisheria au ni matakwa tu ya DCI na Kingai?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Wewe hukushiriki kwa namna yoyote katika mchakato wa kumweka Luten Dennis Urio undercover?

SHAHIDI: Sijawahi kushiriki mimi.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba kuna mkanganyiko kuwa Dennis Urio anasema aliwapa pesa kuja Dar es Salaam wakati hawa wanasema walipewa pesa kuja Dar es Salaam?

SHAHIDI: Hapana. Sifahamu.

KIBATALA: Kwani wewe kama mpelelezi, baada ya Adamoo na Ling’wenya kupewa pesa na Dennis Urio walienda wapi?

SHAHIDI: Walienda Hai, Kilimanjaro.

KIBATALA: Kwanza maelezo ya Dennis Urio uliandika wewe?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIBATALA: Wakati tunamhoji Dennis Urio alisema kuna maeneo kadhaa ulikosea kuandika maelezo yake, je, unafahamu hilo?

SHAHIDI: Sijawahi kujua.

KIBATALA: Je, ni sahihi kwamba ulipokuwa unaandika maelezo ya Dennis Urio, kuna sehemu anasema kwamba baada ya kuwapa pesa Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya wao walikwenda Dar es Salaam. Je, ulipatia kuandika au ulikosea?

SHAHIDI: Nilipatia.

KIBATALA: Je, unaona kuna mgongano au hakuna mgongano?

SHAHIDI: Hebu rudia swali.

KIBATALA: Wewe unasema ulipopeleleza kwa ufahamu wako baada ya Adamoo na Ling’wenya walienda Hai, lakini wewe pia ukasema umeandika maelezo ya Dennis Urio ambayo yanasema kwamba baada ya kupewa pesa walienda Dar es Salaam. Swali ni je, kuna mgongano au hakuna mgongano?

SHAHIDI: Naomba nisome maelezo ya watuhumiwa.

(Shahidi anasoma maelezo ya Adamoo).

SHAHIDI: Maelezo ya Adamoo anasema “Tarehe 24 Julai 2020 nilikutana na Mohammed Ling’wenya kasisitiza tuende Morogoro tukakutane na Luteni Urio, ambaye alituambia kuwa kuna kazi ya VIP Protection kumlinda Freeman Mbowe. Akatupa 87,000/- kila mtu nauli ya kwenda Moshi. Tulirudi Chalinze kwa pikipiki na siku hiyo hiyo tukaanza safari ya kwenda Moshi.”

KIBATALA: Kwa mujibu wa maelezo hayo, yeye alikwenda wapi na akapolekelewa na Bwire pamoja na dereva aitwaye Willy?

KIBATALA: Soma na ya Ling’wenya.

SHAHIDI: Maelezo ya Ling’wenya yanasema _”Baada ya hapo tuliondoka kurudi Chalinze ambapo baada ya kurudi Chalinze tulinunua shati. Baada ya muda tulipata usafiri wa kuelekea Moshi. Tulifika Moshi Usiku.”

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji sasa Ling’wenya alipopewa nauli anasema alienda wapi?

SHAHIDI: Alienda Moshi.

KIBATALA: Sasa nakuuliza kwamba kati ya taarifa ya undercover wenu Luteni Dennis Urio na maelezo hayo kuna mgongano au hakuna?

SHAHIDI: Hakuna mgongano.

KIBATALA: Yaani shahidi sisi watu wazima unasema maelezo kwamba watu walienda Moshi na mtoa taarifa wenu anasema walienda Dar es Salaam…

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji Shahidi amesema kwamba ana ufafanuzi, lakini siyo kumwambia shahidi kwamba nitu mzima.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, ukweli kabisa sijaona Mr. Hilla kasimama kwa sababu gani.

JAJI: Anasema yale maneno ya ni “mtu mzima”.

KIBATALA: Shahidi unataka nikuonyesha maelezo ya Dennis Urio?

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Mheshimiwa Jaji, sijui kwanini wakili anataka arudie swali wakati kakataa ufafanuzi.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, mimi napokea maelekezo kutoka kwako. Umeniambia kwamba una tatizo na neno wewe ni “mtu mzima.” Hukusema lolote la ziada. Sijui kwanini wakili Abdallah Chavula kasimama. Labda kwa sababu sasa ni saa 11 kasoro dakika chache.

KIBATALA: Naomba tuahirishe mpaka kesho. Wenzetu watakuwa wamechoka hasakwa hoja ya muda kama wenzetu hawatapinga.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji naomba kabla hatujaahirisha utoe ufafanuzi.

JAJI: Wakili Kibatala kote umeuliza kisha ukataka shahidi asome maelezo ya Adamoo, kisha ukataka asome maelezo ya Mohammed Ling’wenya baadaye ukamuuliza kama kuna mkanganyiko akasema “HAKUNA.” Nafikri kinachofuata sasa ni kuachiwa Mahakama kuona kama kuna mkanganyiko au hakuna.

KIBATALA: Sawa Mheshimiwa Jaji. Kama nilivyosema siku zote sina tatizo na malekezo yako. Baada ya hapo naomba nitoe hoja ya kuahirisha mpaka kesho.

JAJI: Unaahirisha kwa sababu ya muda au…

KIBATALA: Ndiyo. Mpaka nitoe hoja dakika tano zitakuwa zimeisha.

JAJI: Kufuatia maombi ya wakili wa utetezi, naahirisha shauri mpaka kesho tarehe 9 Februari 2022 saa tatu asubuhi. Shahidi ataendelea kuwa kizimbani kuendelea kutoa ushahidi wake. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka kesho asubuhi saa tatu.

Jaji anaondoka mahakamani saa 11:01.

Like
1