Kesi ya Mbowe: Shahidi adaiwa kutumia diary, simu kisirisiri kizimbani

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia BJ leo tarehe 12 Novemba 2021.

Jaji ameingia Mahakamani. Muda ni saa 6:43

Kesi inatajwa. Ni kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe.

Wakili wa Serikali Robert Kidando anatambulisha mawakili wa Serikali:

 1. Jenitreza Kitali
 2. Abdallah Chavula
 3. Pius Hilla
 4. Esther Martin
 5. Tulimanywa Majige
 6. Ignasi Mwinuka

Peter Kibatala anatambulisha mawakili wa upand wa utetezi.

 1. Jeremiah Mtobesya
 2. Paul Kaunda
 3. Fredrick Kihwelo
 4. Dickson Matata
 5. Idd Msawanga
 6. John Malya
 7. Nashon Nkungu
 8. Alex Massaba
 9. Hadija Aron
 10. Evaresta Kisanga

Mtobesya na Nashon Nkungu kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza.

Paul Kaunda na John Malya wanamtetea mshtakiwa wa pilli

Frederick Kihwelo na Dickson Matata wanamtetea mshtakowa wa tatu

Kibatala na wengine wote wanamtetea mshitakiwa wa nne.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na leo tuna shahidi mmoja. Tupo tayari kuendelea.

Wakili PETER KIBATALA: Na sisi tupo tayari kuendelea.

JAJI: Shahidi wenu?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Yupo. Amefuatwa.

(Shahidi anaingia)

JAJI: Majina yako?

Shahidi ni Askari namba H4323 Msemwa.

JAJI: Miaka?

SHAHIDI: Miaka 31.

JAJI: Dini yako?

SHAHIDI: Mkristo.

SHAHIDI: Mimi askari namba H4323 D/C Msemwa, naapa kwamba yote nitakayosema ni ya kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema unaitwa nani?

SHAHIDI: Naitwa askari namba H4323 Msemwa.

WAKILI WA SERIKALI: Kazi yako nini?

SHAHIDI: Askari polisi.

WAKILI WA SERIKALI: Kituo cha kazi ni wapi?

SHAHIDI: Nipo Oysterbay.

WAKILI WA SERIKALI: Kabla ya hapo ulikuwa wapi?

SHAHIDI: Kituo cha Polisi Msimbazi na baadaye Kituo cha Polisi Central.

WAKILI WA SERIKALI: Central ya wapi?

SHAHIDI: Central ya Dar es Salaam.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikuwa Central tangu lini?

SHAHIDI: Tangu mwaka 2014 nikitokea Msimbazi na mpaka sasa nipo Central.

WAKILI WA SERIKALI: Agosti 2020 ukiwa Central ulikuwa kitengo gani?

SHAHIDI: Nilikuwa General Duties.

WAKILI WA SERIKALI: General Duties inahusiana na kazi gani?

SHAHIDI: Doria, misako, kulinda mabenki, chumba cha mashtaka…

WAKILI WA SERIKALI: Chumba cha mashitaka maana yake nini?

SHAHIDI: Chumba cha mapokezi tunaita CRO pale ambapo mteja anapokelewa.

WAKILI WA SERIKALI: Wateja wa aina gani wanaopokelewa?

SHAHIDI: Wanakuja kufungua kesi na watuhumiwa wote hao ni wateja kwa Polisi.

WAKILI WA SERIKALI: Majukumu yanayohusiana na mashitaka (CRO)?

SHAHIDI: Kufungua kesi, kupokea watuhumiwa na kutoa au kupokea huduma nbalimbali zinazohitaji huduma za kipolisi.

WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama sasa CRO inahusika kupokea watuhumiwa. Je, utaratibu wa kupokea watuhumiwa ukoje?

SHAHIDI: Pindi mtuhumiwa amepokelewa Polisi pale chumba cha mashitaka, kwanza ni kuona kama ana viambatanisho vya reference number. Na siyo mtuhumiwa lazima awe amefunguliwa kesi. Unaweza kumfikisha mtuhumiwa akafunguliwa kesi palepale.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa ambaye kesi imeshafunguliwa analetwa na nani?

SHAHIDI: Anaweza kuletwa na mtu yoyote hata kama wananchi au maaskari watakaokuwa wamemkamata.

WAKILI WA SERIKALI: Mtuhumiwa anapoletwa, je, ni vitu gani hufanyika?

SHAHIDI: Kumpekua.

WAKILI WA SERIKALI: Kwani mtuhumiwa anafikishwa kwa madhumuni gani?

SHAHIDI: Kwa mahojiano au kwa ajili ya taratibu zingine za upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema akishafika pale anafanyiwa upekuzi? Je, upekuzi wa aina gani?

SHAHIDI: Kuhakikisha kwamba haingii mahabusu na kitu hatarishi. Ndiyo maana huwa tunawapekua.

WAKILI WA SERIKALI: Ukikamilisha upekuzi hatua inayofuata ni nini.

SHAHIDI: Mtuhumiwa kuingiziwa kwenye kitabu cha mahabusu tunaita Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Ni taarifa zipi ambazo huingizwa kwenye hiyo Detention Register.

SHAHIDI: Majina yake halisi ambayo atataja mwenyewe, jinsia yake, ikiwemo umri wake, hali yake ya kiafya. Hizo ndizo particulars zinazoingizwa pale. Pia kuna namba ya kesi anayotuhumiwa nayo.

WAKILI WA SERIKALI: Hali ya kiafya ya mtuhumiwa hapo chumba cha mashitaka hutokea vipi?

SHAHIDI: Huelezwa na yeye mwenyewe wakati tunaandika taarifa zake kama nzuri tunaandika “Good” kumaanisha ni mzima na kama ni mgonjwa tunaandika “SICK” kumaanisha ni mgonjwa.

WAKILI WA SERIKALI: Tofauti na mtuhumiwa kueleza mwenyewe, je taratibu zingine ni zipi?

SHAHIDI: Ukiondoa hiyo ya yeye kusema, kama mtu ni kibaka wakati unampekua unaweza kuona majeraha.

JAJI: Kibaka ni mtu gani?

SHAHIDI: Mtu ambaye ameletwa baada ya kupigwa na wananchi.

WAKILI WA SERIKALI: Kwani dhumuni la kuangalia afya ni nini?

SHAHIDI: Ni sababu ya kutaka kujua kama hali ya mtuhumiwa ni nzuri.

WAKILI WA SERIKALI: Endapo mkaona hali yake kiafya siyo nzuri mnafanyeje?

SHAHIDI: Tunajaza kwenye Fomu ya PF3 na tunampeleka hospitali.

SHAHIDI: Wale ambao wanaumwa kama malaria tunawapeleka hospitali na bado wakirudi tunajaza ‘MGONJWA’.

WAKILI WA SERIKALI: Eleza Mahakama tukufu kwamba tarehe saba Agosti 2020 ulikuwa wapi.

SHAHIDI: Mnamo tarehe saba Agosti 2020 alfajiri nilikuwa naingia kazini Central Dar es Salaam kama askari wa zamu chumba cha mashitaka.

WAKILI WA SERIKALI: Zamu ya namna gani?

SHAHIDI: Zamu ya masaa 12, kwa hiyo robo saa kabla natakiwa kuwa kazini.

WAKILI WA SERIKALI: Ukiwa kama askari za wa zamu siku hiyo majukumu yako yalikuwa yapi?

SHAHIDI: Tulikuwa wengi na in charge anagawa majukumu.

WAKILI WA SERIKALI: Kama mlikuwa wengi? Tutajie hao wengi ni akina nani?

SHAHIDI: Assistant Inspector Fatuma, PC Emanuel, PC Semeni na Constable Samweli.

WAKILI WA SERIKALI: Kazi yako siku hiyo ilikuwa nini?

SHAHIDI: Nilipangiwa charge room.

WAKILI WA SERIKALI: Ambapo kazi yake ni nini?

SHAHIDI: Kuingiza na kuwatoa watuhumiwa chumba cha mahabusu.

WAKILI WA SERIKALI: Unakumbuka siku hiyo ilikuwaje?

SHAHIDI: Alifika Afande Kingai, Afande Jumanne na askari wengine wakiwa wameshikilia bunduki wakiwa pamoja na watuhumiwa wawili.

WAKILI WA SERIKALI: Afande Kingai na Afande Jumanne ni akina nani hasa?

SHAHIDI: Afande Kingai kwa sasa ni RPC.

WAKILI WA SERIKALI: Kipindi hicho alichofika?

SHAHIDI: Afande Kingai alikuwa RCO Arusha na Afande Jumanne alikuwa anatokea Polisi Makao Makuu. Ndiyo nilikuwa nafahamu hivyo.

WAKILI WA SERIKALI: Walifikia eneo gani?

SHAHIDI: Walifika Central Ilala eneo la CRO wakiwa na watuhumiwa na moja kwa moja baada ya kufika Afande Jumanne akauliza pale, nani anahusika na watuhumiwa? Nikamwambia ni mimi.

SHAHIDI: Akasema hawa watuhumiwa wamekamatwa Moshi na reference number zao hizi hapa. Nikafanya utaratibu wa kawaida upekuzi na kuwaandika kwenye Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa- detain ukafanya nini?

SHAHIDI: Kuwachukua watuhumiwa na kuwapeleka mahabusu.

WAKILI WA SERIKALI: Mahabusu ya wapi?

SHAHIDI: Ya Central palepale.

WAKILI WA SERIKALI: Kingai na wenzake baada ya kuwapeleka mahabusu wote?

SHAHIDI: Baada ya kuwapeleka mahabusu watuhumiwa wote na kuwajaza majina yao, umri wao, afya zao na kosa wanalotuhumiwa nalo, baada ya hapo nikawapeleka mahabusu, wao wakina Kingai wakaondoka.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema kwa mujibu wa Reference ulizokuwa umeletewa hawa watu walikuwa na kosa gani?

SHAHIDI: Kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

WAKILI WA SERIKALI: Watuhumiwa walioletwa ni akina nani?

SHAHIDI: Walikuwa ni watuhumiwa wawili wa kiume

WAKILI WA SERIKALI: Je, unawatambua kwa majina?

SHAHIDI: Ndiyo! Mohamed Abdilah Ling’wenya na Adam Hassan Kasekwa.

WAKILI WA SERIKALI: Ikawaje?

SHAHIDI: Afande Kingai alirudi kuja kumchukua mtuhumiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Mtuhumiwa yupi?

SHAHIDI: Adam Hassan Kasekwa.

SHAHIDI: Baada ya Kingai kuja kumchukua Adam Kasekwa, alifika Afande Jumanne kuja kumchukua Mohamed Abdilah Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Afande Kingai alimchukua kwenda wapi?

SHAHIDI: Alipandisha naye kwenda naye juu ofisi ya RCO. Nikaenda naye.

WAKILI WA SERIKALI: Huyu Jumanne alimchukua Mohammed akaenda naye wapi?

SHAHIDI: Alimchukua akiwa na karatasi mkononi akasema nitoleeni mtuhumiwa. Akaenda naye kwenye chumba cha OCS.

WAKILI WA SERIKALI: Alimrudisha saa ngapi?

SHAHIDI: Baada ya muda alimrudisha baada ya Kingai kumrudisha wa kwake.

WAKILI WA SERIKALI: Sasa hali zao kiafya zikoje?

SHAHIDI: Nikiwauliza hali zao za kiafya na majina yao, wakasema nzuri na nikawajazia kwamba ni GOOD.

WAKILI WA SERIKALI: Majina ya washitakiwa uliyapata wapi?

SHAHIDI: Walinipatia wao wenyewe. Nilimuuliza wa kwanza akasema anaitwa Adam Kasekwa na wa pili Mohamed Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama kwamba baada ya kuwa wamerejeshwa mahabusu, lini tena ulishughulika nao?

SHAHIDI: Mimi ndiyo nilikuwa mtunza mahabusu. Niligawanya muda wa kuwatembelea. Muda wa asubuhi wakati wa kuwapelekea uji watuhumiwa wote na chai … za ndugu wengine, na mchana niliwatembelea na jioni wakati wa kukabidhiana.

SHAHIDI: Mbali na kuwaona wakati afande anawarudisha watuhumiwa, niliwaona tena muda wa chai, mchana na jioni.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati unawaona mchana na jioni hali zao zilikuwaje?

SHAHIDI: Zilikuwa nzuri na walivyoingia hapakuwa na mgonjwa.

WAKILI WA SERIKALI: Vitendea kazi kwa maana ya D. R vyenyewe mnapeleka wapi?

SHAHIDI: Zinabaki CRO kwa ajili ya kuendelea kujaza taarifa za watuhumiwa wengine. Lakini kama imejaa unaipeleka kwa OCS anakupa D. R nyingine.

WAKILI WA SERIKALI: Ile uliyowaingiza Adam na Mohammed ilienda wapi baada ya kujaza?

SHAHIDI: Ilibaaki palepale CRO.

WAKILI WA SERIKALI: Ni lini tena ulishughulika nayo?

SHAHIDI: Wakati wa January mwaka huu, nimehamia Kinondoni. Nilipokea samansi ya kuja kutoa ushahidi hapa. Nikaandika barua ya Movement Order, na baada ya kuandika Movement Order kule Central nilimkabidhi D. R Mahakamani kama kielelezo baada kutoa ushahidi.

WAKILI WA SERIKALI: Unasema ulikabidhiwa kwa madhumuni gani?

SHAHIDI: Kuja nayo kama kielelezo.

WAKILI WA SERIKALI: Mahakamani kwa ajili gani?

SHAHIDI: Kutoa ushahidi.

WAKILI WA SERIKALI: Ushahidi wa kesi gani?

SHAHIDI: Shauri namba 16 la uhujumu uchumi.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa ni lini?

SHAHIDI: Septemba 20, 2021 wakati nilipotakiwa kuonyesha kielelezo kama niliwapokea watuhumiwa nikiwa Central wakati ule. Nilitoa kama kielelezo na ikapokelewa hapa Mahakamani.

WAKILI WA SERIKALI: Ilipolewa na nani?

SHAHIDI: Na Mahakama akiwepo Mheshimiwa Jaji Siyani.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kielelezo hicho kupokelewa na Mahakama, baadae nikaruhusiwa kuondoka.

WAKILI WA SERIKALI: Kielelezo ulikiacha Mahakamani. Je, ni lini tena ulishughulika nacho?

SHAHIDI: Nilipokea tena samansi kwamba natakiwa kutoa ushahidi kwenye kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya uhujumu uchumi. Nikamwambia sina kielelezo. Akasema kwamba fika Mahakamani utatakikuta hukohuko. Nilifika kwa Msajili wa Mahakama kumwambia nimekuja kutoa ushahidi Mahakamani. Akanikabidhi kile kielelezo na barua, na baada ya kupokea kielelezo akanisainisha kwenye kitabu kwamba nimepokea.

WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama barua ambayo ametumia Msajili wa Mahakama kukukabidhi kielelezo utaitambuaje?

SHAHIDI: Barua ina Force Number zangu H4323 ambazo ni DC Msemwa.

WAKILI WA SERIKALI: Kingine?

SHAHIDI: Ni sahihi ya Msajili wa Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, shahidi anaonyesha uwezo wa kukitambua.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi hebu tazama nyaraka hii. Elezea Mahakama nyaraka hiyo ni nini?

SHAHIDI: Nyaraka hii ndiyo iliyonipa kielelezo. Ina Force Number zangu H4323 DC Msemwa na pia Ina sahihi ya Msajili wa Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Unaiomba nini sasa Mahakama kuhusiana na barua hiyo?

SHAHIDI: Naomba Mahakama ipokee barua hii kama uthibitisho kwamba mimi ndiye niliyepokea kielelezo cha Detention Register kutoka kwa Msajili wa Mahakama.

(Mawakili wa utetezi wanaingalia na kuijadili kwa pamoja. Baada ya kumaliza anazungumza Mtobesya).

MTOBESYA: Kwa niaba ya mshitakiwa wa kwanza tuna pingamizi ya upokeaji wa hii barua kwa sababu zifuatazo.

MTOBESYA: Kwanza, ukiiaoma inaonekana kwamba mlengwa ni National Prosecution Service. Huyu siyo mtumishi wa ofisi ya National Prosecution Service na hakujitambulisha hivyo wakati wa utambulisho wake. Ni ajabu anaomba kuingiza barua ambayo haimuhusu, na angalau hajasema yeye kwamba anafanya kazi kwenye hiyo ofisi. Kasema kwamba kataja kwenye barua kwa Force Number yake, kwamba force yake ipo kwenye content nyingine. Najua watasema kwamba haturuhusiwi kuingia kwenye content. Lakini shahidi alitumia maneno hayo kujenga misingi ya ushahidi wake. Kwa kuzingati kesi ya Farid Mohammed vs DPP na Charles Gazilabo Abel Gezilahabo vs Jamhuri zimeshasema kwamba shahidi anatakiwa kuwa na ufahamu na ushahidi anaotaka kuutoa.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji naunga mkono pingamizi lililoletwa na Mtobesya. Kama alivyosema mlengwa wa barua ni National Prosecution Service wanaohusika ni DPP na wanafanya huduma hizo za Mashitaka, na shahidi siyo mmojawapo, angalau kwa ushahidi wake, na mmiliki wa barua (Maker) siyo yeye. Fact kwamba ametajwa kwenye barua haitoshi kwa sababu hata mshitakiwa wa tatu ametajawa humu, hawezi kutoa barua hii kwa sababu haimuhusu. Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Jaji tunapinga kupokelewa kwa nyaraka hii.

Frederick Kihwelo: Wakati shahidi anaomba barua hii ipokelewe alisema kwamba yeye ndiye aliyepewa barua hii, lakini barua hii inakwenda ofisi ya mashitaka ya Taifa. Kwa hiyo naungana na mawakili wa mshitakiwa wa kwanza na wa pili kupinga kupokelewa kwa barua hii.

PETER KIBATALA: Na sisi kwa niaba ya mshitakiwa wa nne tunapinga kwa nguvu. Kwanza, shahidi siyo competence, na competence inagawanyika makundi mawili. (a) In isolation, kwamba haja- _lay foundations kwamba inamuhusu. Kama mimi ningekuwa ndiyo Wakili wa Serikali, kwa kuwa shahidi alidai kwamba alisainishwa mahala fulani, ili kuonyesha NEXUS kati ya ofisi ya Msajili na shahidi, kwamba barua isingemfikia kwa kuelea hewani. Wameweka toroli mbele ya farasi na hiyo ndiyo inaondoa competence ya shahidi ambayo pia ni Prequisite ya Tendering.

PETER KIBATALA: (Shahidi) Hajaogozwa kwa namna yoyote ile kwamba National Prosecution Service tena wa P. o. BOX 1733 Dodoma wamempatiaje hii barua shahidi? Ilipaswa barua hii ipokelewe na agent wao wa National Prosecution Service Dodoma ambaye anatambulika na Mahakama afikishe kwa shahidi, Hapo pia wameweka toroli mbele ya farasi. Shahidi anasema kwamba amewasiliana yeye mwenyewe na Msajili kwa ushahidi wake mwenyewe. Ilitakiwa sasa ionekane kwa namna gani imemfikia kutoka NPS. Hatari ambayo tusingependa kufika huko, ni Naibu Msajili N. N Ntandu kuja kuwa shahidi kwenye kesi hii. Mahakama itahusishwa kuja kuziba gap fulani. Aje kuulizwa ulimkabidhi shahidi kwa madhumuni gani wakati shahidi siyo mhusika.

PETER KIBATALA: Sijasikia shahidi akisema kwamba barua hii ni nakala kwake na kwa mamlaka yapi. Lakini pia barua Kama ambayo Ina purport kupokea exhibit kwenye Mahakama, ilitakiwa iwe preceded na Law. It’s jurisdiction issue. Shahidi hakuongozwa kuelezea content yake ndani kwa sababu hakuongozwa kwamba ametajwa ndani ya barua, kwa hiyo mlango huo pia umefungwa. Ni hayo tu.

(Kibatala anakaa chini.)

(Mawakili wa Serikali wanateta pamoja hapa. Kisha anakuja Wakili Abdallah Chavula)

WAKILI WA SERIKALI: (Chavula) Ikupendeze Mheshimiwa Jaji. Tumesikikiza mapingamizi kutoka kwa wenzetu wa utetezi kuhusu upokelewaji wa kielelezo hiki. Kiujumla sisi hatukubaliani nao. Hoja ya kwanza imejengwa kwamba barua kwa maana ya kielelezo hiki hakikuelekezwa kwa shahidi na badala yake, kielelezo hiki kimelezwa kwa NATIONAL PROSECUTION SERVICE yenye anuani yao Dodoma na ni hoja zao kwamba shahidi yeye siyo mhusika wa NATIONAL PROSECUTION SERVICE.

WAKILI WA SERIKALI: Na pia hakuna ushahidi kwamba National Prosecution Service au wakala wake Dar es Salaam ambaye amethibitishwa kumkabidhi shahidi. Kwa hali hiyo shahidi hana uwezo, na haitoshi kwamba shahidi majina yake yameonekama kwenye kielelezo hicho na wenzetu wanadai kwamba majina hayo hayana muunganiko na kilichopo. Na kwamba tulichokifanya, kwa maoni yao, hatujui tunafanya nini na kwa maoni yao tumetanguliza toroli mbele ya farasi na kwamba wangekuwa wao werevu wasingefanya hivyo.

Kibatala anaamka.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji naona wakili tupo emotional sana, na hii siyo vita vya mtaani. Hebu ajielekeze kwenye kujenga hoja.

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Ndiyo sasa uchague cha kusema sasa. Sisi tumeelewa hivyo.

JAJI: Hakusema wao werevu. Amesema angekuwa yeye angefanya…

WAKILI WA SERIKALI: Ndiyo yaleyale tu Mheshimiwa Jaji.

KIBATALA: Basi tumuache aendelee kuelewa anayotaka. Tutapata muda wa kujibu.

WAKILI WA SERIKALI: Sisi tunaona barua ipo sawa kwa sababu inamtaja shahidi dhidi ya kielelezo. Inamuhusisha yeye shahidi na kielelezo ambacho shahidi anakileta.

WAKILI WA SERIKALI: Kingine kwamba barua hii haikupaswa kwenda kwa shahidi bali kwa National Prosecution Service pekee nayo siyo sahihi. Wenzetu wanajaribu kusema kwamba shahidi hakuwahi kutaka kwamba nakala hiyo ya barua hakikuelekezwa kwenda kwake na kwa sababu hiyo ushahidi haupo na hivyo kupata barua hii ni haramu kumfikia kwake bila kupita kwa National Prosecution Service. Ni masuala ya kufikirika tu, yasiyokuwa na uhalisia, na kama tunaamini sote kwamba nyaraka inajizungumza yenyewe, ni maoni yetu kwamba tuache hii barua ijisemee yenyewe. Je iliandikwa kwa National Prosecution Service wenyewe Dodoma au kuna watu wengine walikusudiwa kupata hii barua. Mheshimiwa Jaji ukiangalia ukurasa wa nyuma inaonyesha wakina nani wanapaswa kupewa hii nyaraka. Na miongoni mwa watu waliotajwa shahidi ni mmojawapo. Barua hii imemtaja kwa Force Number yake, majina yake na rank yake. Hoja ingekuwa miongoni mwa wanaopaswa kupata nyaraka hii shahidi jina lake lipo. Sisi tunasema ni mambo ya kufikirika.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji shahidi katika ushahidi wake amesema aliyempa barua ni msajili. Na haikuishia hapo. Amesema anaitambua barua hiyo kwa sahihi ya Msajili. Hali ingelikuwa ni tofauti kama anayeonekana katika barua hiyo ni mtu mwingine na siyo Msajili. Tungeanza kufikiria kwamba shahidi hajaweka misingi, hoja ingekuwa aliyesaini siyo Msajili, basi tungesema shahidi ameshindwa kuweka misingi.

WAKILI WA SERIKALI: Hoja ingekuwa hicho kinachosemakena kimekabidhiwa kwa shahidi sicho shahidi anachokisema kusingekuwa na Misingi. Mheshimiwa Jaji sote tunafahamu kwamba barua imeandikwa halafu ikaandikwa “Copy to” basi wamepata watu wote. Siye maoni yetu tunaona hilo halikuwa la msingi na halikuwa na lazima.

WAKILI WA SERIKALI: Hoja nyingine ni ya competence kwamba shahidi hayupo competent. Mahakama ikarejewa kwenye maamuzi yake Iliyofanya jana, pia kwa Sharif Athuman na wenzake sita. Shauri lingine ni la Charles Gezilabo.

WAKILI WA SERIKALI: Shauri lingine ni la Charles Gezilabo.ambapo kwenye mashauri hayo Mahakama ilikuwa inaongelea katika upokelewaji wa ushahidi Mahakamani, yale ambayo ni testimonial yaani wa maneno ni lazima uwe relevant. Imezungumzwa jumla lakini Mahakama haikuambiwa kwamba ushahidi siyo relevant na kwanini siyo relevant. Haikuelezwa hivyo Mahakamani. Haikuelezwa kwa kigezo cha Material na kwamba ushahidi siyo Material kwa kadha wa kadha. Na haijaelezwa Mahakamani kwenye issue ya Competence. Haijaelezwa Mahakama kivipi kielelezo hiki siyo Competence.

WAKILI WA SERIKALI: Lililoelezea kwa urefu ni moja tu, Competence_ya shahidi, shahidi kushindwa ku- lay foundation kabla ya kutoa kielelezo. Shahidi hana uelewa, lacks knowledge ya kielelezo hiki. Mheshimiwa Jaji sisi tunasema haya yote shahidi amezungumza. Utatizamwa ushahidi wake wa awali. Kabla alionyeshwa nyaraka akaitambua, na akaeleza kwamba alipokutana na Msajili wa Mahakama, Msajili akampatia barua. Akaeleza barua hiyo ina Force Number zake pamoja na majina. Na barua hiyo ina sahihi ya Msajili. Shahidi ameonyesha kwamba baada ya kutoka kwa Msajili kielelezo hiki kilikuwa kwake moja kwa moja.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, siye tunaona kwamba ushahidi huo ni msingi tosha, foundation tosha ya kumpa yeye uwezo wa kutoa kielelezo. Hoja ya kwamba kigezo pekee ni knowledge, kwa mtu kutoa ushahidi Mahakamani sisi tunasema siyo sahihi. Si msimamo wa sheria. Naomba nielekeze Mahakama yako kwenye shauri la DPP vs Milzahi Bilibatish ama jina lingine Haji na wenzake watatu, Rufaa ya Jinai Namba 493 ya mwaka 2016. Ni Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika ukurasa wa saba, aya ya mwisho mpaka aya ya kwanza ukurasa wa nane.

(Wakili wa Serikali Abdallah Chavula anasoma sasa).

WAKILI WA SERIKALI: Siyo lazima awe custodian au awe maker wa hiyo document ndiyo aweze kuitoa nyaraka hiyo. Kinachoangaliwa ana ufahamu wa yaliyomo kwenye nyaraka ya ushahidi huo, amewahi kumiliki kwa wakati fulani kielelezo hicho, kimewahi kumfikia mikononi kielelezo hicho. Shahidi kaonyesha ufahamu walau kwenye nyaraka hiyo. Ameonyesha majina yake. Walau katika nyaraka hiyo ameeleza aliyesaini. Ameeleza alikoitoa nyaraka hiyo. Shahidi ameonyesha ana knowledge. Ameonyesha uwezo. Kwa uchache tu siye tunasema ana taarifa ya kile alichoonyesha ndani ya nyaraka.

WAKILI WA SERIKALI: Wenzetu wanasema eti palipaswa yafanyike maombi na Mahakama itamke.

JAJI: Hawajasema hivyo. Walisema ingetangulia amri ya Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Sote tunafahamu kwamba ili Mahakama itoe amri inapaswa ip[elekwe.

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye maamuzi yaliyofanywa na Mahakama yako siku ya jana, Mahakama katika uamuzi wake ilisema kwamba mambo ambayo yanapaswa kufanywa na siye, ni pamoja na kufanya utaratibu wa kiutawala katika kuipata hiyo nyaraka. Sasa Mahakama imeelekezwa haya, sisi ni akina nani tutafute njia tunayoijua kupata hiyo nyaraka? Na sote tunafahamu kwamba unapofuata utaratibu wa kiutawala maombi yanafanywa kwa kupeleka katika Mahakama. Hivyo basi Mheshimiwa Jaji kwa kuheshimu uamuzi wa Mahakama uliosomwa jana na kwa kufuata uamuzi wa Mahakama uliosomwa jana ambao umetamka wazi wazi kwamba utaratibu wa kiutawala unaweza kufuatwa. Huu ndiyo uthibitisho wa kuonyesha kwamba tumefuata utaratibu wa kiutawala kama ilivyozungumzwa na Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Hivyo Mheshimiwa Jaji hoja ya kwamba tulipaswa tufuate amri ya Mahakama sisi tunasema hapana. Hatukupaswa kwenda njia hiyo. Naomba nimkaribishe mwenzangu Wakili wa Serikali Pius Hilla.

Wakili wa Serikal Pius Hilla ananyanyuka.

(Kabla Wakili wa Serikali hajaongea, Kibatala anasimama na kuongea).

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji. Tunaomba tujiridhishe kama shahidi hana diary na kama kwenye diary anaandika chochote, na pia kama shahidi ana simu pale kizimbani. Na kama ameingia na vitu visivyoruhusiwa kizimbani tunaomba aondolewe kuwa Shahidi. Zitoke pande mbili za mawakili chini ya Mahakama tukamkague kwanza kabla kesi haijaendelea.

(Kabla hata hajakaguliwa, shahidi anaonyesha doary, kalamu, karatasi na simu).

KIBATALA: Tunaomba vitu hivyo viwe chini ya uangalizi wa Mahakama kwanza kama tutaendelea na kesi.

(Afisa wa Mahakama anakwenda kizimbani kuchukua diary, kalamu na simu kutoka kwa shahidi).

(Wakili wa Serikali Pius Hilla anaendelea).

WAKILI WA SERIKALI: Kesi ya Robinson Mwangisi vs Jamhuri TLR 213 ya mwaka 2003 inahusiana na kielelezo cha leo ambacho shahidi alikuwa anaomba kipokelewe. Mheshimiwa Jaji Wakili Mtobesya aliongelea kwamba shahidi amefeli ku- authenticate kielelezo ambacho alikuwa anakiomba. Hoja hii haina mashiko kwa sababu vigezo vyote vilivyowekwa kwenye kesi ya Sharif shahidi amevifanya.

WAKILI WA SERIKALI: Na wakati anatambua vielelezo akasema hiyo Force Number yake ameiona. Lakini pia shahidi aka- authonticate barua hiyo kwa kusema kwamba amemkabidhiwa na Msajili wa Mahakama, kwa maana Authentication of Material, kwa maana nyaraka hiyo imemfikia kwa kukabidhiwa na Msajili wa Mahakama. Mheshimiwa itoshe kusema kwamba zile kanuni za authontication of documents alizifanya kikamilifu. Wakili Mallya alisema kwamba kutaja tu kwenye document hakutoshi kufanya…, Mheshimiwa, shahidi haikuishia kutajwa tu. Yameonyeshwa mengi na shahidi kwa maana alivyoipata madhumuni aliyopewa na kwamba ndiyo kitu alichopewa. Na ameonyesha kwamba ilikuwa kwa ajili ya kukabidhiwa kielelezo kwa mana yupo knowledgeable.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji nizungumzie kuhusu Handover Documents ambayo imezungumzwa kwamba hajasainishwa na National Prosecution Service. Mheshimiwa document hii wala siyo lazima kwa sababu shahidi ame- lay foundation kwamba ameipataje. Na Mheshimiwa haijaelezwa hata kidogo iwapo shahidi haaminiki.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa kwenye Shauri la Yusuf Massalu, Alliance na wenzake watatu, Rufani ya Jinai ya 163 ya mwaka 2017, Mahakama ilisema katika uamuzi wake kwamba kinachotakiwa kuangaliwa ni Assurance. Hakuna ubishi kwamba barua ni ya Msajili wa Mahakama na wala hakuna ubishi kwamba shahidi amekabidhiwa kwa dhumuni la kielelezo. Katika mazingira hayo Mheshimiwa Jaji huhitaji jambo lingine, na wala hicho siyo kigezo cha hiyo barua kuingia katika ushahidi huo, na lingine huwezi barua kama hiyo uki- subject kwenye … Kwa sababu barua imetoka kwa Msajili kakabidhiwa shahidi. Mheshimiwa, Wakili Kibatala alielekeza juu ya prosecutorial arrangements. Hakuna cha Prosecutorial Arrangements hapa. Ni Msajili akimkabidhi barua. Tunaomba hiyo hoja itupiliwe mbali.

WAKILI WA SERIKALI: Nimalizie kwa kusema kwamba, my general assessment ya kile ambacho shahidi amekieleza na barua ambayo imetolewa na Msajili haina ukweli wowote kuhusu kupokelewa kwa barua. Shahidi ni Competent, Material ni Relevance. Pia ime- pass vigezo vyote vya upokelewaji wa ushahidi. Tunaomba Mheshimiwa Jaji mapingamizi yatupiliwe mbali na kielelezo kipokelewe.

(Wakili wa Serikali Pius Hilla anamalizia na kukaa)

Mmemaliza upande wa mashitaka?

(Mawakili wa Serikali wote wanaitika NDIYO)

MTOBESYA: Naomba kuongezea machache nisiichoshe Mahakama yako kwa mwanahistoria. Nitajibu na naomba kuongezea machache.

MTOBESYA: Kaka yangu Chavula anasema nyaraka inatakiwa ijisemee yenyewe na kwamba hata submission tusingefanya. Na kwa maneno ya Mahakama ya Rufaa ya Robinson Rwangisi inasema kwamba nyaraka iwe sahihi, ndiyo maana tunafanya hili zoezi. Aliyetakiwa kuifanya nyaraka ingie siyo mwingine bali ni shahidi. Na sisi tunasema kwamba kesi hii inafanana na misingi ya kesi ya Sharif vs DPP na kesi ya Charles Gazilabo. Sisi tunasema alichokisema hakitoshi kwa sababu, unique features kama tarehe na anuani hakuvitaja.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Objection! Naona kama Unique Features ni kitu kipya.

JAJI: Unique Features ni moja ya criteria ya authentication.

MTOBESYA: Kaka yangu Pius Hilla wakati anasema kuhusu kuna Force Namba sifikirii kama alisema just for cosmetics.

JAJI: Nisaidie kuhusu hizo unique features.

MTOBESYA: Vipo kwenye kesi ya Charles Gazilabo.

JAJI: Sawa.

MTOBESYA: Mimi na Mallya tumesema kwamba hakusema kwamba alipewa nakala ya barua, na kwamba mlengwa wa barua siyo yeye na kitu pekee ambacho kingeondoa utata ni dispatch book ambayo hajaileta. Kitu pekee hapa ni factual expedition. Ni namna barua ilivyomfikia shahidi. Na njia pekee ya ku- prove hiyo fact ilikuwa ni kwa wao kuileta hiyo dispatch book kwa wao kufuata procedure.

MTOBESYA: [Hiyo ni] kwa ajili ya ku- prove competence ya shahidi kupitia knowledge Ilipaswa iletwe hapa. Bahati mbaya hakuwepo hapa Mahakamani kusema kama kweli alimpatia na kwa bahati mbaya sana kaka yangu Pius Hilla anasema dispatch siyo jambo msingi. Na sisi tunasema hajafika viwango vya authentication kama inavyopaswa.

MTOBESYA: Kwa sababu za kaka yangu Pius Hilla anasema Ilimradi shahidi anasema alipewa inatosha na wala haihitaji uthibitisho, lakini kwa bahati nzuri shahidi alisema alisaini kwenye dispatch.

JAJI: Hakusema dispatch.

MTOBESYA: Alisema alisaini kwenye kitabu. Kwa maana hiyo sehemu yoyote ambayo nimesema dispatch isomeke kitabu alichosaini.

JAJI: Sawa.

MTOBESYA: Alisimama pia kaka yangu Chavula akasema kwamba content inatosha kuonyesha kwamba ilikuwa inatosha. Lakini kwa bahati mbaya alizumgumzia suala la content kwa asilimia 75 ya wasilisho lake wakati huo huo Pius Hilla kaongelea kwamba haturuhusiwi kuongelea suala la content kama ilivyo kwenye kesi ya Robison Rwangisi. Sasa Mheshimiwa Jaji hawawezi kula keki na kuendelea kuwa nayo. Waamue jambo moja kama wanaijadili content wakubali wote tujadili. Na kwa bahati mbaya huyo huyo kaka yangu Pius Hilla alianza kuongelea masuala ya Force Number ambapo ndiyo content yenyewe.

MTOBESYA: Ni wasilisho letu sasa kwamba Mahakama ipitie barua hiyo na tunaomba barua hiyo isipokelewe. Ni hayo Mheshimiwa Jaji.

Sasa anaingia Wakili John Mallya.

Malya: Kwa ufupi sana Mheshimiwa Jaji. Kwanza naunga mkono wasilisho la kaka yangu Mtobesya. Wakati Abdallah Chavula anafanya wasilisho alisema mtu kumiliki tu kwa barua hiyo kunatosha kuonyesha kamayupo Competence. Sisi tunasema kwamba hakuonyesha aliipataje hasa barua hiyo na kwamba pande zote mbili tunakubaliana kwamba shahidi siyo mlengwa wa barua hiyo. Chavula alisema kwamba wao ni akina nani wasifuate maamuzi ya Mahakama katika kupata barua hiyo. Kwa maana nyingine ni kwamba wao wakina Chavula ndiyo waliondika barua na wao wakina Chavula ndio waliojibiwa na siyo shahidi.

MALLYA: Na pia Chavula anasema kwamba Mahakama inapoenda kufanyia maamuzi iangalie content ya barua hiyo na kwa maneno hayo maana yake siyo maneno ya shahidi.

Anaingia Frederick Kihwelo

KIHWELO: Naomba kukubaliana na wenzangu mawakili wa upande wa utetezi. Shahidi alisema kwamba alikwenda kwa Msajili yeye mwenyewe na akapewa barua na kielelezo. Na kwa mara ya kwanza shahidi alionana na Msajili.

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Objection! Naona kama analeta jambo jipya.

KIHWELO: Barua anayosema alipewa siyo hii iliyopo hapa Mahakamani, kwa sababu barua inaonyesha mlengwa ni National Prosecution Services. Kwa sababu hiyo sisi tunapinga upokelewaji wa barua hii. Asante sana.

Anaingia Wakili Peter Kibatala.

KIBATALA: Asante Mheshimiwa Jaji. Nianze na suala la hicho kitabu. Tunasisitiza kwamba alichoongozwa shahidi kukizingumzia palikuwa na jaribio la authentication. Wao walikifanya kitabu kuwa mchakato wa barua. Huku kutengenishwa kulianza saa ngapi? Ndiyo maana nilisema wameweka toroli mbele ya farasi, kitu ambacho wamechukia. Lilikuwa ‘legal and not ego’. Wenzetu wanasema Mheshimiwa Jaji sote hatubishani. Ukweli tunabishana kwa sababu mimi sijui wala wewe Mheshimiwa Jaji hujui kama kweli barau hiyo imetoka kwa Msajili kweli.

KIBATALA: Ndiyo maana nikasema, je, ni sahihi kwa sisi kitokutimiza majukumu yetu na kuanza kumuingiza Msajili kwenye authentication ya barua hiyo hapa Mahakamani? Hicho ni kielelezo na ni sehemu ya ushahidi. Wenzetu wanasema eti alitambua sahihi ya Msajili. Shahidi anatambuaje sasa usahihi wa saini ya Msajili. Kuna mazoezi walitakiwa wenzetu kufanya na hawakufanya.

KIBATALA: Na ndipo suala la kuchagua toroli ikae wapi na farasi ikae wapi ni jambo muhimu. Maamuzi ya jana yalikuwa criticism na siyo permissive ndiyo maana Mahakama ika- refuse. Kwamba Mahakama iliwalekeza wao waletwe barua bila kitabu walichosaini kupokea hiyo barua? Nimesikia mtu anasema kuhusu Assurance. Assurance ambayo Mahakama inapata, Mahakama hii ni tofauti na siyo sehemu ya Msajili wa Mahakama.

KIBATALA: Assurance ipo wapi kama hakuna aliposaini? Na hapo ndiyo njia ya chain inapoanzia na kama njia inakosekana, haiwezekani kupokelewa. Kuna argument kaleta sijui Abdallah Chavula au Pius Hilla kwamba eti kwa kuwa barua imemtaja shahidi ndiyo lazima awe amepata, Mallya pia amesema hapa kwamba barua imewataja washitakiwa mbona hawajapata? Kutajwa kwamba unapewa nakala haimaanishi kwamba umepewa nakala ya barua hiyo.

KIBATALA: Kwa maana hiyo barua hiyo inakosa uthibitisho. Mheshimiwa Jaji wenzetu pia walisema hatujaonyesha Lack of Competence ya barua. Mbona nimesema hapa sasa hivi na muda ule, kwamba kunafanywa na barua na shahidi juu ya Competence. Comptence inaangaliwa wamefanya nini katika ushahidi wao. Tunamalizia kwa kusema kwamba Competence ya shahidi ni muhimu na competence ya nyaraka ni muhimu. Tunamalizia kwa kusisitiza kwa mapingamizi yetu kwamba kweli kuna maamuzi ya mahakama kuhusu nyaraka, lakini Mahakama haikusema wenzetu wasifuate taratibu katika kuleta nyaraka Mahakamani, na kwamba isionekene kwamba lawama ni za kwako kwa kuwaelekeza kufanya hivyo. Haya ni mambo mawili tofauti na wala usijione kwamba umekosea kuwaelekeza.

KIBATALA: Na mwisho, kesi ya Mizirahi sina la kuzungumza kwa sababu mambo yote ya Mizirahi yapo kwenye kesi ya Gezilabo. Asante Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Kuhusu vitu ambavyo vimechukua kwa shahidi kizimbani?

KIBATALA: Tungeweza kwenda mbali kwa sababu bado tunahisi kwamba mifukoni bado ana vitu vingine ila kwa sababu ya utu tusifike huko.

KIBATALA: Tunaomba malekezo yako kwamba shahidi amekiuka kiapo chake na ulewa wa kazi yake.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, kwa vyovyote vile wakati suala hilo linaibuliwa na wakili msomi Kibatala, ni wakati wa mawasilisho ya hoja za mapingamizi.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini hatujasikia wakati wowote kwamba vitu hivi vimetumika wakati shahidi anatoa ushahidi. Sifa za shahidi tunafahamu zipo chini ya kifungu cha 127 cha Sheria ya Ushahidi ambapo imeonyesha shahidi anaweza kukosa sifa. Nilikuwa nadhani kwenye hilo tujiongoze vizuri, kwa sababu kitu kama simu ni mali binafsi ya shahidi. Na pia mimi nimeona tu wakati shahidi anatoa hiyo diary yake. Na zoezi analolialika Mahakama kufanya naona ni tofauti na sheria inavyotaka.

JAJI: Nilisikia Kibatala kwamba umesema kwamba shahidi ana simu na ana diary, je, ulisema kwamba alikuwa anavitumia? Je shahidi anapotakiwa kuingia kizimbani anatakiwa kukaguliwa.

JAJI: Nasema hayo kwenye simu naona tunaongelea privacy ya mtu, maana hatujui kwenye simu tutaangalia wapi. Diary ni rahisi kwa sababu tunaweza kupekua.

KIBATALA: Leo wakati kesi inaendelea Profesa Jay alinaindika kwamba shahidi anasoma.

KIBATALA: Tukasema tujiridhishe kwanza. Wakati tunaendelea na hoja alikuwa na pen na diary akiwa busy akiandika. Na kabla hatujasimama tulikuwa tayari tumeshajiridhisha kuanzia vifungu vya 127 vya Sheria ya Ushahidi.

JAJI: Naomba mkatumie week-end hii mkajiridhishe kwa kufanya wasilisho dogo kuhusu shahidi kuwa na diary kizimbani. Na kuhusu simu tumrudishie.

MTOBESYA: Je, hiyo diary itakaa kwa nani?

JAJI: Itakaa Mahakamani.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji sasa haya maombi hayasemi kama ni kwa mujibu wa sheria au la, na kwa sababu hiyo hatujui ni zoezi la kisheria.

KIBATALA: Sheria inakataza na mpaka kesi zipo za marejeo.

JAJI: Ndiyo nimesema Jumatatu tutafanya wasilisho hilo kwanza nini madhara yake ya shahidi kuwa na diary.

(Shahidi anayoosha mkono).

JAJI: kuna Jambo unataka kuongea lakini hautaruhusiwa kuiongelea diary kwa sababu nilishatolea maamuzi.

SHAHIDI: Sawa Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Basi shauri linaahjirishwa mpaka Jumatatu tarehe 15 Novemba 2021. Shahidi utatakiwa kurudi Mahakamami siku hiyo. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka Jumatatu saa tatu asubuhi.

Jaji anaondoka mahakamani.

Like
2