Kesi ya Mbowe: Mahojiano ya mawakili na mashahidi, akiwemo mke wa mtuhumiwa (7)

Kama ilivyoandikwa na ripota raia, BJ, leo Jumatano tarehe 29 Septemba 2021. Endelea.

Ni saa 3:16 asubuhi, washtakiwa wameshafikishwa mahakamani na wamekaa kwenye nafasi zao. Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Peter Kibatala, tayari wameshaingia chumba cha mahakama, lakini mawakili wa Serikali bado wako nje ya chumba.

Jaji ameshaingia mahakamani, amekaa na kesi sasa inatajwa. Ni kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamuhuri dhidi ya Halfan Bwire, Adam Hassana Kasekwa (Adamoo), Mohammed Abdalah Ling’wenya na Freeman Aikael Mbowe.

Jaji anasalimia wote walioko chumba cha mahakama. Kisha anasema: Tuendelee. Ni siku nyingine tena.

WAKILI WA SERIKALI: Naomba radhi tumeingia wakati (Jaji) umeshaingia.

JAJI: Sawa.

Wakili wa Serikali Kidando anawatambulisha wenzake kwa kuanza na yeye mwenyewe.

 1. Robert Kidando
 2. Nassoro Katuga
 3. Ignas Mwanuka
 4. Esther Martin
 5. Tulimanywa Majigo

Jaji anawaita upande wa utetezi.

Kibatala anaamka na kuwatambulisha wenzake kwa kuanza na yeye mwenyewe

 1. Peter Kibatala
 2. Jonathan Mndeme
 3. Fredrick Kiwhelo
 4. John Malya
 5. Sisty Aloyce
 6. Alex Masaba
 7. Idd Msawanga
 8. Gaston Garubindi
 9. Evaresta Kisanga
 10. Faraj Mangula
 11. Maria Mushi
 12. Bonifasia Mapunda

Wakili Dickson Matata anaombewa ruhusa kwa Jaji kwa sababu mdogo wake anafanyiwa upasuaji Hospitali ya Lugalo

JAJI: Wakili wa Serikali?

WAKILI WA SERIKALI: Tumekuja kwa ajili ya kesi ndogo ambapo shahidi wa tatu yupo tayari kuendelea Kutoa ushahidi wake.

JAJI: John Mallya?

MALLYA: Tunaye shahidi, na shahidi yupo tayari kutoa ushahidi.

Jaji anainama na anaandika kidogo huku ukimya ukiwa umetawala mahakamani.

JAJI: Shahidi wa tatu upande wa utetezi ambaye ameandaliwa tafadhali anaweza kuja.

Shahidi mmoja mwanamke anajitokeza na kuingia chumba cha mahakama. Anakwenda kupanda kizimbani.

JAJI: Shahidi upo Mahakamani kwa hiyo ondoa hofu. Nitakuuliza majina yako na nitakuapisha. Wakili wa utetezi atakuongoza na Mawakili wengine watakuuliza swali na mawakili wa Serikali watakuuliza maswali pia. Huna haja ya kuogopa. Tupo hapa kutafuta haki … Shahidi unaitwa nani?

SHAHIDI: Lilian Kibona. Dini Mkristo.

Shahidi anaapa mbele ya Mahakama kwamba “Ushahidi nitakao toa utakuwa ukweli na ukweli mtupu. Mungu nisaidie.

JAJI: Liliani utachagua kukaa au kusimama. Hata ukikaaa nitakuona.

JAJI: Wakili Mallya endelea.

MALLYA: Shahidi unaishi wapi?

SHAHIDI: Chalinze mkoa wa Pwani.

MALLYA: Sehemu gani huko Chalinze?

SHAHIDI: Ramboni.

JAJI: Ni mtaa?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Unaishi na nani?

SHAHIDI: Na mume wangu na watoto ambaye kwa sasa mume wangu ameshikiliwa.

JAJI: Ni miongoni mwa washitakiwa?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Mume wako anaitwa nani?

SHAHIDI: Adamu Khalfani Kasekwa.

MALLYA: Hapa aliko namwita mshitakiwa wa pili, nitakuwa namaanisha pia ni yeye?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Mmeoana lini?

SHAHIDI: 05.08.2016.

MALLYA: Ndoa ya kiserikali?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Mlikuwa mnaishi wapi?

SHAHIDI: Palepale Chalinze.

MALLYA: Unaweza kukumbuka mume wako alikuwa anafanya kazi gani wakati huo?

SHAHIDI: Askari jeshi wa JWTZ kikosi cha 92 Ngerengere.

MALLYA: Alikuwa anafanya kazi gani nyingine?

SHAHIDI: Alikuwa hana kazi nyingine zaidi ya hiyo ya Serikali.

MALLYA: Naruka nakuja 2020, Mume wako alikuwa anafanya kazi gani?

SHAHIDI: Alikuwa anafanya shughuli zake za biashara.

MALLYA: Mwanzoni mwa mwezi wa nane mwaka 2020 unakumbuka kilitokea kitu gani kati yako na mume wako?

SHAHIDI: Mume wangu alikuwa Moshi. Tulikuwa tunawasiliana naye vizuri.

MALLYA: Kabla ya kwenda Moshi mlikuwa na hali gani kati yako na mume wako?

SHAHIDI: Palikuwa na mawasiliano.

MALLYA: Kabla hajaenda Moshi kitu gani kilitokea?

SHAHIDI: Rafiki yake Ling’wenya waliwasiliana kuwa kuna kazi imepatikana Moshi.

MALLYA: Unaweza kukumbuka siku na saa ya hayo mawasiliano?

SHAHIDI: Hapana. Sikumbuki.

JAJI: Unasema palikuwa na mawasiliano kati ya mume wako na Ling’wenya?

SHAHIDI: Ndiyo. Kwamba Ling’wenya alimpigia simu kuwa kuna kazi imepatikana huko Moshi.

JAJI: Ndiyo.

MALLYA: Simu zilikuwa zinapigwa kati ya Ling’wenya na mume wako wewe ulijuaje?

SHAHIDI: Mimi kama mke wake alinishirikisha. Mimi kama mke nilimruhusu.

MALLYA: Jambo gani lilifanyika kabla ya mume wako kwenda Moshi?

SHAHIDI: Nakumbuka walikutana na Ling’wenya wakaenda kwanza Morogoro, wakarudi. Waliporudi wakajiandaa wakaenda Moshi.

MALLYA: Hali ya mume wako kiafya wakati anaenda Moshi hali yake ilikuwaje?

SHAHIDI: Ilikuwa nzuri inamruhusu kwenda kufanya kazi.

MALLYA: Hali nzuri unamaanisha nini? Mwambie Mheshimiwa Jaji.

SHAHIDI: Haumwi na kwamba anaweza kwenda Moshi.

MALLYA: Kitu gani kilifuata baada ya kwenda huko Moshi?

SHAHIDI: Alinitaarifu kuwa amefika Moshi.

MALLYA: Mlikuwa mnatumia njia gani kufanya mazungumzo?

SHAHIDI: Kwa njia ya simu.

MALLYA: Siku ya tarehe tani mwezi wa nane mwaka 2020 kitu gani kilitokea?

SHAHIDI: Alinipigia na akaongea na watoto. Tulipokuwa tunaongea akasema hebu subiri. Nikamsubiri.

MALLYA: Ilikuwa saa ngapi?

SHAHIDI: Kama saa moja.

MALLYA: Alipokuambia subiri kidogo nitakupigia kidogo kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Nilipoona muda umeenda ilipofika saa 10 ilibidi nimpigie. Simu iliita ikawa imepokelewa lakini kila nikisema “Hallo” sisikii mtu akiongea.

MALLYA: Unaweza kukumbuka namba ya simu uliyopiga ambayo ulipiga ikapokelewa?

SHAHIDI: Sikumbuki kichwani lakini ipo kwenye simu yangu.

MALLYA: Baadaye kilifuata nini baada ya simu kutokupelewa?

SHAHIDI: Baadaye ikawa haipatikani.

MALLYA: Kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Kwa kuwa nilikuwa na namba ya mwenzake Ling’wenya nikampigia Ling’wenya.

MALLYA: Baada ya kumpigia Ling’wenya?

SHAHIDI: Ikawa inaita mpaka jioni, mpaka usiku, mpaka kesho yake inaita haipokelewi.

MALLYA: Sasa wewe ulipata hisia gani baada ya kuona inaita hadi kesho yake haipokelewi?

SHAHIDI: Niliona labda ni mambo ya kazi. Sikuwa na wasiwasi wowote.

MALLYA: Baada ya hapo kitu gani kilifuata baada ya kuhisi ni mambo ya kazi?

SHAHIDI: Sikuwa na mtu mwingine yeyote wa wa kumuuliza zaidi ya Ling’wenya.

SHAHIDI: Wewe ulichukua hatua gani?

SHAHIDI: Sikuwa na namna yoyote zaidi ya kusubiri simu kutoka kwao.

MALLYA: Una mtoto umesema ana umri gani?

SHAHIDI: Miaka 3 na miezi tisa.

MALLYA: Nataka kukupeleka tarehe tisa mwezi wa nane ni kitu gani kilitokea?

SHAHIDI: Nakumbuka ilikuwa tarehe tisa mwezi wa nane mwaka 2020 niliamka asubuhi ikiwa siku ya Jumapili. Mtoto alikuwa anasumbuliwa na tumbo.

JAJI: Mtoto wa jinsia gani?

SHAHIDI: Wa kike.

MALLYA: Kwanini unakumbuka kuwa ilikuwa siku ya Jumapili?

SHAHIDI: Kwa sababu ilikuwa ni siku ya ibada.

MALLYA: Ikawaje?

SHAHIDI: Sikwenda ibadani badala yake nikaenda hospitali.

MALLYA: Ikawaje huko hospitali?

SHAHIDI: Nilipokelewa.

MALLYA: Hospitali gani?

SHAHIDI: Hospitali ya Serikali palepale Chalinze.

MALLYA: Baada ya kupokelewa hospitali?

SHAHIDI: Nilipatiwa huduma nikarudi nyumbani … Baada ya kurudi nyumbani niliona miguu ya watu kama imekanyaga. Wakati natoka nyumbani nilifunga mlango lakini niliporudi nikakuta milango ipo wazi.

MALLYA: Ule mlango ulikuwa katika hali gani?

SHAHIDI: Mlango ulikuwa wazi na kitasa nikakuta kimevunjwa.

MALLYA: Kitu gani kikatokea?

SHAHIDI: Kwa akili ya haraka haraka nilijua wezi. Cha ajabu kila kitu nilikuta vipo, kitu kama TV vipo.

MALLYA: Eheeee. Halafu ikawaje?

SHAHIDI: Nikaingia chumbani nikakuta nguo za zimemwagwa chini.

JAJI: Za mume wako?

SHAHIDI: Zote zimemwaga. Na mabegi yamefunguliwa. Kuna begi alinunua Congo nilipokuja kikakuta halipo.

JAJI: Ukisema begi la jeshi alinunua Congo unamaanisha nini?

SHAHIDI: Alinunua Congo begi lenye mabaka mabaka ya Jeshi.

MALLYA: Kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Nilienda kuuliza majirani zangu.

MALLYA: Jirani yako anaitwa nani?

SHAHIDI: Judith Charles.

MALLYA: Lengo la kwenda kwa jirani lilikuwa nini?

SHAHIDI: Nilienza kuuliza kama mume wangu amekuja nyumbani? Na kama wamemwona. Kwamba kuna kitu huenda alikuja kukitafuta kwa haraka haraka.

MALLYA: Jirani alikuambiaje?

SHAHIDI: Kuna magari yalikuja hapa ya kipolisi. Moja walikuwa wamevaa sare na mengine walikuwa wamevaa kiraia.

JAJI: Ndiyo.

MALLYA: Taarifa nyingine alikupa jirani yako ni ipi?

SHAHIDI: Kwamba mapolisi walimwita kwa lengo la kuniulizia mimi. Baada ya hapo mapolisi walishuka kwenye gari wakaingia ndani.

MALLYA: Yeye jirani alikuwa anafanya nini wakati huo?

SHAHIDI: Alikuwa anashuhudia wakati wanaingia ndani ya nyumba yangu.

MALLYA: Kitu gani kingine walikufahamisha au kumpatia.

SHAHIDI: Walisema walichukua begi, vyeti vyake vya kijeshi vya Adamu. Walichukua hati ya uwanja. Walichukua kadi ya pikipiki.

MALLYA: Kitu gani kingine alikuambia?

SHAHIDI: Aliongozana na Mkuu wa Upelelezi wa Chalinze.

MALLYA: Aliyeongozana na Mkuu wa Upelelezi wa Chalinze alikuwa ni ameongozana na akina nani?

SHAHIDI: Jirani yangu aliongozana na Mkuu wa Upelelezi na aliacha namba ya simu kwa jirani.

JAJI: Kwa ajili ya nini?

SHAHIDI: Alisema kama kuna lolote ambalo hajalielewa ampigie.

MALLYA: Siku ya Jumapili tarehe nane mwezi wa tisa nyumba imesachiwa na umekuta namba ya simu ya Mkuu wa Upelelezi Chalinze. Ni kitu gani kilifuata baada ya hapo?

SHAHIDI: Nilimpigia simu. Yeye aliniambia kuwa alipigiwa tu simu kuwa inabidi waongozane kwenda kusachi kwenye nyumba ya Adamu Kasekwa.

MALLYA: Alikufahamisha kuwa alipigiwa simu na nani?

JAJI: Mnasikia au mvua inasababisha kupoteza usikivu tuhairishe kidogo?

JAJI: Labda nisikilize mawakili.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji naomba tu- break kidogo kwa sababu shahidi akitumia sana nguvu kuongea anaweza akupoteza energy na huenda akawa na siku ndefu.

JAJI: Upande wa Serikali?

WAKILI WA SERIKALI: Hatuna pingamizi

JAJI: Kama mvua imeacha kidogo. Hebu tuendelee kidogo. Ikirudi na tukashindwa kusikilizana tutaahirisha.

JAJI: Uliishia kuhusu kumpigia simu Mkuu wa Upelelezi Chalinze.

MALLYA: Nilimuuliza Mkuu wa Upelelezi alijibu kitu gani?

SHAHIDI: Alisema amepigiwa simu kutoka Moshi.

Mvua inaendelea kunyesha.

JAJI: Naona mvua haitoi muda wa kuendelea. Siwezi kukadiria ni kwa muda gani. Siwezi kusema ni kwa muda mchache. Naahirisha shauri.

Jaji ananyanyuka na kutoka.

Jaji amerejea.

Kesi inatajwa.

Wakili John Mallya uko tayari?

MALLYA: Ndiyo Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Tuendelee.

MALLYA: Baada ya kuwa ameshakwambia kuwa alipigiwa simu kutoka Moshi ni kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Muda ulikuwa umeshaenda. Nikasema itabidi kesho yake niende kwa sababu sikuamini alichoniambia.

MALLYA: Kesho yake ikawaje?

JAJI: Tunasikilizana? Kama mvua inanisubiri mimi.

MALLYA: Ulisema ulienda kituoni kesho yake wapi?

SHAHIDI: Kituo cha Chalinze.

JAJI: Sasa ilikuwa Jumatatu.

MALLYA: Tarehe tano umepiga ukamkosa. Tarehe tisa ukakuta umesachiwa. Kitu gani kilitokea tarehe kumi ya Jumatatu pale kituoni?

SHAHIDI: Nikaomba kuonana na mpelelezi. Nilipomwona nikajitambulisha kuwa mimi ni yule dada ambyae mmekuja nyumbani kusachi.

MALLYA: Akakuambiaje?

SHAHIDI: Akasema kama nilivyokueleza sina ambacho nakijua zaidi ya kuchukuliwa na kuwasindikiza kwenda nyumbani kwako kusachi. Sina ninachojua zaidi.

MALLYA: Wewe ulikuwa unafanya jitaihada gani zingine?

SHAHIDI: Nilianza kutafuta namba za mke wa Ling’wenya.

MALLYA: Awali ulituambia namba za Ling’wenya ulikuwa nazo na ukampigia. Za mke wake unazitafuta. Za Ling’wenya ulitoa wapi?

SHAHIDI: Ni mtu wa karibu wa mume wangu. Ni rafiki yake tuseme siku wanaondoka walikuwa naye.

MALLYA: Ulitumia njia gani za kupata namba za mke wa Ling’wenya?

Nilimtafuta mwenzao Shikunzi aliyekuwa anaishi nao Kimara.

JAJI: Mwenzo kwamba alikuwa Askari Jeshi?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Alikuwa Kimara anakaa na nani?

SHAHIDI: Alikuwa anakaa karibu na Ling’wenya.

MALLYA: Kilichokufanya umtafute Shikunzi ili umtafute mke wa Ling’wenya ni nini?

SHAHIDI: Nilitaka kumuuliza mke wa Ling’wenya ili kumuuliza huko kwake ni nini kilikuwa kinaendelea.

JAJI: Kwanini ukimtafuta Shikunzi?

SHAHIDI: Walikuwa ni majirani.

MALLYA: Shikunzi akafanyaje?

SHAHIDI: Alinipatia namba ya mke wa Ling’wenya.

MALLYA: Ulifanya hatua gani?

SHAHIDI: Nilimpigia mke wa Ling’wenya.

SHAHIDI: Ilikuwa siku ya Jumatatu na yeye akaniambia siku ya Jumapili ambayo ni jana yake walienda nyumbani lwake wakafanya upekuzi.

MALLYA: Nini kilifuata baada ya hapo?

SHAHIDI: Akaniambia baada ya hapo walienda kwa mwingine anaitwa Bwire. Tumtafute kke wa Bwire. Nikamwambia wewe huko jirani huko mtafute mke wa Bwire.

MALLYA: Kitu gani alikueleza mke wa Ling’wenya?

SHAHIDI: Kwamba nilitaka kujua kama kwake walienda kusachi akaniambia wameenda kusachi. Akaniambia pia tutafute mke wa Bwire.

MALLYA: Ulipata namba ya mke wa Bwire na unaweza kukumbuka majina yao?

SHAHIDI: Mke wa Bwire anaitwa Mama Itham na mke wa Ling’wenya anaitwa Mama Somoye.

MALLYA: Nini kikafuata?

SHAHIDI: Mke wa Bwire alikuwa Dar es Salaam akasema inabidi nitoke Chalinze nije Dar es Salaam.

JAJI: Alisema utoke wapi?

SHAHIDI: Chalinze nije Dar es Salaam.

MALLYA: Hii sintofahamu yote ilitokana na nini?

SHAHIDI: Kutokana na kuto kujua mwenza wangu yupo wapi, namtafuta simpati halafu nyumbani wamekuja kusachi.

MALLYA: Baada ya kushauriwa ulichukua hatua gani?

SHAHIDI: Nilitafuta nauli nikaja Dar es Salaam.

MALLYA: Ilikuwa lini?

SHAHIDI: Sikumbuki.

MALLYA: Baada ya kufika Dar es Salaam nini kilifuata?

SHAHIDI: Tulishauriana tuanze kutafuta vituo vyote vya Polisi.

MALLYA: Unaweza kujua nyumbani kwake Bwire?

SHAHIDI: Maeneo ya Temeke.

MALLYA: Unaweza kukumbuka mlianzia wapi?

SHAHIDI: Kituo cha Polisi Chang’ombe.

MALLYA: Ndiyo.

SHAHIDI: Tukajitambulisha kuwa sisi waume zetu wamekamatwa hatujui wamepelekwa kituo gani.

MALLYA: Mlimkuta polisi gani?

SHAHIDI: Polisi wa zamu.

MALLYA: Mkajitambulishaje?

SHAHIDI: Kwa majina yetu na waume zetu.

MALLYA: Baada ya hapo yule askari alifanyeje?

SHAHIDI: Alianza akupekua kitabu kwa kuangalia yale majina ya waume zetu hatukuyaona.

MALLYA: Baada ya kutoyaona majina ya mnaowatafuta kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Tulienda kituo kingine.

MALLYA: Kituo gani?

SHAHIDI: Cha Central Police Dar es Salaam.

MALLYA: Ikawaje?

SHAHIDI: Villevile tukajitambulisha na kwamba sisi waume zetu wameletwa polisi na hatujui kituo gani.

MALLYA: Baada ya kujitambulisha kwa sskari nini kilifuata?

SHAHIDI: Aliangalia kile kitabu hakuona yale majina.

MALLYA: Wakati anaangalia majina ya waume zenu nyie mlishiriki vipi?

SHAHIDI: Wakati anaangalia kitabu, wote tuliinama kuangalia majina ya waume zetu kwa usahihi.

MALLYA: Mmeangalia pamoja na askari majina wenza wenu hamjayaona. Nini kiliendelea baada ya hapo?

SHAHIDI: Tulitoka kituo cha Polisi Central Police tukaenda Oysterbay.

SHAHIDI: Tukajitambulisha kwa askari wa zamu. Akaangalia kwenye kitabu. Majina yao hayakwwepo.

MALLYA: Baada ya kuwakosa Central nini kilifuata?

SHAHIDI: Tulienda Tazara.

MALLYA: Unaweza kueleza kwanini mlienda Tazara?

SHAHIDI: Tulienda kwa sababu tulikuwa kwenye kuendelea kuwatafuta kituo gani cha Polisi wamepelekwa.

MALLYA: Unaweza kuiambaia Mahakama mara zote mlipokuwa mnatafuta mlikuwa mnawatafuta kwa namna gani?

SHAHIDI: Mara zote tunataja majina na mimi nilitaja jina la mume wangu Adamu Khalfani Kasekwa.

MALLYA: Kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Hatukuyaona majina yao.

MALLYA: Mmeshaenda vituo vinne kutafuta wenza wenu. Hatua gani ilifuata baada ya hapo?

SHAHIDI: Tulirudi nyumbani kwa sababu muda ulikuwa umeenda. Na tuliacha watoto wadogo.

MALLYA: Nyumbani kwa maana ya wapi?

SHAHIDI: Kwa mke wa Bwire.

MALLYA: Kwa mazungumzo yako na mke wa Bwire alikuambia nini kimetokea kule Moshi?

SHAHIDI: Akaniambia kule Moshi kuna wifi yake ambaye ni dada wa Mohammed Abdillah Ling’wenya

JAJI: Twendeni taratibu. Mmeshazunguka vituo vyote. Ilikuwa ni siku gani?

SHAHIDI: Tarehe 13.

JAJI: Ohh!!. Tunakosa mtiririko kwa sababu nilikuwa bado nipo kwenye vituo vya Polisi.

MALLYA: Samahani Mheshimiwa Jaji. Nilirudi nyuma kumuuliza kama waliongea na mke wa Bwire.

MALLYA: Alikuambia nini sasa?

SHAHIDI: Kwamba wifi yake amempigia simu kuwa Adam wakiwa Moshi na Mohammed akiwa anakunywa chai Adamu alikuwa anazungumza na simu ikawa kama kelele za mvutano “Niache! Niache! Niache!” Baada ya hapo wakawa wanamvuta kumleta sehemu za vyakula.

MALLYA: Nini kilifuata?

SHAHIDI: Kwamba alikuwa amepigwa akawa anavuja damu.

JAJI: Hii ni habari ambayo umesema umeambiwa na mke wa nani?

SHAHIDI: Mke wa Ling’wenya tukiwa kwa mke wa Bwire.

MALLYA: Huyo wifi yake anaitwa nani?

SHAHIDI: Anaitwa Asma.

JAJI: Nafikiri tulirudi kwenye mstari hapo tunaanza kuzungumzia “hearsay” yeye kaambiwa na mke wa Ling’wenya na mke wa Ling’wenya kaambiwa na wifi. Nafikiri mkiona kuna umuhimu mumwite wifi aje kutoa uUshahidi ila hatuwezi kwenda hivyo.

MALLYA: Aawa Mheshimiwa Jaji.

MALLYA: Mliporudi nyumbani ikawaje?

SHAHIDI: Tulikubaliana tupite hospitalini.

MALLYA: Mlikuwa na nyenzo gani katika kuwatafuta.

SHAHIDI: Tulikuwa na picha zao.

MALLYA: Na mlianzia wapi?

SHAHIDI: Tulianzia Hospitali ya Muhimbili.

JAJI: Kwanini mlianza kuwatafuta kwenye mahospitali?

SHAHIDI: Ni baada ya kuwakosa kwenye vituo vya Polisi.

JAJI: Kwa off record tu. Moshi waliawambiaje?

SHAHIDI: Kwamba huku hawapo kwamba wameletwa Dar es Salaam. Tukahisi labda wamepata ajali.

MALLYA: Mlipofika Muhimbili ikawaje?

SHAHIDI: Tukijambulisha na kueleza kuwa tunawatafuta waume zetu. Tulizunguka kwenye wodi na mochwari hatukuwaona.

MALLYA: Nini kikafuata?

SHAHIDI: Tukaenda Hospitali ya Amana. Tukajitambulisha na kuingia kwenye mawodi na mochwari. Hatukuwaona pia.

MALLYA: Baada ya Amana?

SHAHIDI: Tulienda Mwananyamala tukajitambulisha na kuwatafuta waume zetu kwenye mawodi na mochwari hatuwaona.

MALLYA: Siku ya tatu sasa mmmeanda Muhimbili, Amana na Mwananyamala mkawakosa. Ulichukua hatua gani?

SHAHIDI: Ilibidi nirudi Chalinze kwa sababu nauli ilikuwa imeshaaanza kuisha na kwa sababu nina wawasiliano ikabidi nirudi Chalinze.

MALLYA: Baada ya kurudi nyumbani kwa mara ya kwanza ulipata taarifa ya mume wako yupo wapi?

SHAHIDI: Ilikuwa kwenye taarifa ya habari ya jioni.

MALLYA: Uliwaona wakiwa wapi?

SHAHIDI: Mahakamani Kisutu.

MALLYA: Kituo gani cha habari?

SHAHIDI: ITV.

MALLYA: Uliwaona au ulisimuliwa?

SHAHIDI: Niliona.

MALLYA: Wanatuhumiwa kwa makosa gani?

SHAHIDI: Anashitakiwa kwa ugaidi na uhujumu uchumi.

MALLYA: Mara ya mwisho mume wako wakati anakuaga alikwambia anaenda Moshi kufanya nini?

SHAHIDI: Kwamba kuna kazi imepatikana anaenda kuifanya.

MALLYA: Ikawaje?

SHAHIDI: Niliwasiliana na wenzangu.

MALLYA: Uliona hiyo taarifa ya habari ITV saa ngapi?

SHAHIDI: Ilikuwa saa mbili usiku.

MALLYA: Mkafanya mawasiliano gani?

SHAHIDI: Tulikubaliana twende mahabusu kwa sababu hatukujua wamepelekwa mahabusu gani.

MALLYA: Baada ya hapo nini kilifuata?

SHAHIDI: Mzee Ling’wenya alikuja kutoka Mtwara.

MALLYA: Kitu gani alifanya baada ya kutoka Mtwara Mzee Ling’wenya?

SHAHIDI: Tulikuwa hatuelewi wapo mahabusu gani. Tulianza kutafuta mahabusu waliopo.

MALLYA: Mlianza kutafuta mahabusu gani?

SHAHIDI: Mimi sikuwepo nilikuwa Chalinze. Tulifanya mawasiliano.

MALLYA: Wakakuambiaje?

SHAHIDI: Kwamba wameenda Keko wamewakosa ila Segerea wamewakuta.

JAJI: Ni akina nani?

SHAHIDI: Mke wa Mohammed Abdilah Ling’wenya na Mzee Ling’wenya.

JAJI: Mke wa Ling’wenya na nani?

SHAHIDI: Na Baba mke wake, Mzee Ling’wenya.

MALLYA: Aasa ushajua mwenza wako yupo Segerea. Hatua gani ilifuata?

SHAHIDI: Nilikuja Jumapili kutoka Chalinze. Jumatatu tuliamka wote mke wa Bwire, Ling’wenya tukaenda sote Segerea.

MALLYA: Mlipofika Segerea ikawaje?

SHAHIDI: Tulipokelewa na askari wa jinsia ya kike akatueleza leo si siku ya kuwaona mahabusu mje Jumamosi au Jumapili.

MALLYA: Baada hapo ulifanya hatua gani mlichukua?

SHAHIDI: Nilienda Jumamosi. Niliskia maaskati wakisema “ndiyo yule jamaa ambaye yupo kabatini?”

MALLYA: Ni nani aliyaongea hayo?

SHAHIDI: Ni maaskari niliowaeleza majina kuwa namtafuta mume wangu.

MALLYA: Hatua gani ilifuata?

SHAHIDI: Wakachukua funguo wakasema tunaenda kumleta.

MALLYA: Unaweza kutuambia hapo ulipokuwepo pana taswira gani ili Mheshimiwa jaji apate picha?

SHAHIDI: Ukiingia Segerea maeneo ambayo kuna meza ya kuwekea chakula na kuna chuma kama grill lililotenganisha.

MALLYA: Kitu gani kilifuata?

SHAHIDI: Nilimwona mume wangu akitembea kwa tabu kama vile inaonekana ameteswa.

MALLYA: Unaweza kukumbuka mume wako amevaaje?

SHAHIDI: Alikuwa amevaa kama ‘singled’.

MALLYA: Hali yake ilikuwaje?

SHAHIDI: Amedhoofika. Alikuwa amekonda sana.

MALLYA: Mwendo wake ulikuwaje alivyokuwa anatembea?

SHAHIDI: Alikuwa anachechemea.

MALLYA: Ulichukua hatua gani?

SHAHIDI: Kama utaratibu ulivyo wa pale. Nilibeba kwa ajili yake.

JAJI: Ulikuwa umeleta vitu gani?

SHAHIDI: Chakula ,shuka na sabuni.

JAJI: Vitu ulimkabidhi nani?

SHAHIDI: Askari akishakagua anachukua ukiwa unamuona.

MALLYA: Ulisema ulikuwa unamwona mume wako sasa anaelekea sehemu. Ni sehemu gani?

SHAHIDI: Eneo la nyavu ambalo mnaweza kuzungumza.

MALLYA: Ilikuwaje mazungumzo kati yenu?

SHAHIDI: Nilimuuliza hali yake na kilichotokea.

MALLYA: Alikujibu nini?

SHAHIDI: Hali yangu ni hivyo hivyo ila siyo nzuri.

MALLYA: Alikwambia kwanini hali yake siyo nzuri?

SHAHIDI: Aliniambia kuna mateso alipitia wakati yupo Moshi. “Nilipigwa sana ndiyo maana unaniona nipo kwenye hali hii.”

MALLYA: Baada ya hapo?

SHAHIDI: Alichukuliwa akapelekwa mahabusu.

MALLYA: Nitakurudisha nyuma kidogo. Kilichokufanya utamtafute vituo vya polisi na mahospitali mume wako ni kitu gani?

WAKILI WA SERIKALI: Objection! Wakili ameshauliza.

MALLYA: Sikuuuliza. Kama aliulizwa ni off record. Nataka sasa iingie kwenye records.

WAKILI WA SERIKALI: Ameshaliuliza hilo swali.

JAJI: Sijachoka kuandika. Muuulize tena.

MALLYA: Nitakurudisha nyuma kidogo. Kilichokufanya utamtafute vituo vya polisi na mahospitali mume wako ni kitu gani?

SHAHIDI: Kwa sababu tuliambiwa kuwa walitolewa Moshi kuja Dar es Salaam na tulienda vituo vya Polisi kwa sababu tuliamini kama wangetusaidia.

MALLYA: Vipi kuhusu ushiriki wa ndugu zake mwanamume?

SHAHIDI: Alikuja mama yake. Tukaenda naye Moshi.

MALLYA: Kwanini wewe namba ya mume wako umesema huikumbuki kwa kichwa? Mie ya mke wangu naikumbuka.

SHAHIDI: Kwa sababu alikuwa na line mpya aliyotoka kuisajili.

MALLYA: Kwanini unasema ulipoenda Segerea hali yake ilikuwa tofauti?

SHAHIDI: Alikuwa amekonda sana na macho yameingia ndani kama yameganda. Amekonda kwa kweli na pia nilimuona akiwa na alama kwenye mkono. Wakati anaenda Moshi alikuwa hana.

JAJI: Ulisema uliona nini kwenye mkono?

SHAHIDI: Alama ya kovu kwenye mkono. Awali alikuwa hana wakati anaenda Moshi.

MALLYA: Ya kwangu ni hayo.

JAJI: Asante sana Mallya pamoja na mvua kutuharibia ratiba yetu.

JAJI: Lakini tuta- break tena kidogo kama dakika 17. Tutarejea saa sita kamili.

Jaji ameondoka chumba cha mahakama.

Tumerejea mahakamani. Shahidi ndiyo anapanda tena kizimbani.

Kesi inatajwa na washitakiwa wanakaa kwenye kizimba chao.

JAJI: Wakili Nashon kama una swali lolote.

Nashon: Sitakuwa na swali kwa Shahidi.

JAJI: Wakili Fredrick Kihwelo kama una swali?

FREDRICK KIHWELO: Sitakuwa na swali. Kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu hatutakuwa na swali.

JAJI: Wakili Kibatala kwa niaba ya mashtakiwa wa nne?

KIBATALA: Shahidi ulijisikiaje uliporudi nyumbani kukuta nyumba yako imevunjwa na mume wako alikuwa hapatikani muda wote?

SHAHIDI: Niliogopa sana. Kwanza nilihisi ni wezi.

KIBATALA: Ulitegemea kuwa polisi wanaweza kufanya hivyo?

SHAHIDI: Hapana. Sikuwahi kutegemea polisi wanaweza kufanya tendo hilo.

KIBATALA: Umeongelea kwamba ulikuta TV na vingime kukuta vipo, ila kadi ya pikipiki na hati ya kiwanja vilikuwa vimechukuliwa.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mpaka leo hii hujawahi kuambiwa kuwa nani ana hivyo vitu Kituo cha Polisi Chalinze au afisa yeyote wa Polisi.

SHAHIDI: Hakuna aliyewahi kuniambia.

KIBATALA: Mpaka leo hii hujui nani wa kumdai hivyo vitu.

SHAHIDI: Sahihi. Sijui nani nimdai.

KIBATALA: Kuna mgogoro wowote wa kiwanja sehemu unayoishi au kupelekwa hata kwa mjumbe?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Ushawahi kujua kwanini Adamoo alisimamishwa kazi au utumiahi wake wa kijeshi ulivyokoma?

SHAHIDI: Nafikiri huko kwenye mambo ya kijeshi tusiende sana miye sijui lolote kuhusu Jeshi.

KIBATALA: Sawa. Tuachane na hilo.

KIBATALA: Nimesikia kuwa ulienda kumtafuta mumeo vituo vya Polisi. Naomba nikuonyeshe kielelezo Namba Moja, kitabu fulani.

(Mahakama inampatia Kibatala Kielelezo Detention Register).

KIBATALA: Unasema ulienda polisi ukaoneshwa kijitabu kama hiki au kinachofanana na hiki na bado baada ya kupekua hukuona katika kitabu kama hiki bado jina la mume wako halikuwapo?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Una sababu yoyote ya kutunga story ya uongo kuwa hukwenda Polisi Central halafu leo uje useme ulienda Polisi Central? Je, una sababu yoyote ya kutunga?

SHAHIDI: Hapana. Sina sababu yoyote.

KIBATALA: Nimesikia kuwa kilichowafanya muanze kumtafuta Dar es Salaam ni baada ya mke wa Ling’wenya kuwasiliana na dada yake Ling’wenya kule Moshi akasema kuwa Adamoo na Ling’wenya wameletwa Dar es Salaam. Je, nilikusikia kwa usahihi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Nimekusikia kwa usahihi kuwa mlipita kote ikiwemo Chang’ombe, Central Station na Tazara pamoja na vyumba vya kuhifadhia maiti kwa sababu ya kukosa taarifa?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mlilazimika kufunguliwa mwili mmoja baada ya mwingine kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti?

SHAHIDI: Ndiyo. Nililazimika kufungukiwa maiti moja baada ya nyingine ili kuweza kuthibitisha kama mume yupo huko.

KIBATALA: Ni sahihi kwamba wakati unapitia hali hii ulikuwa na miaka 25 tu?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Na wakati huo ulikuwa na mtoto mdogo.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Wakati huo ulikuwa kwenye ndoa kwa muda gani mpaka unapitia matukio haya mazito? Mitatu?

JAJI: Hesabu zenu zipo vizuri? Kutoka 2016 Agosti mpaka 2020 ni miaka mingapi?

KIBATALA: Minne.

JAJI: Naona hakuna tatizo mtu kukosea hesabu Mahakamani. Hilo swali tunaweza kuliacha.

KIBATALA: Ni sahihi wakati unakuja kupekuliwa Ilikuwa ni kabla ya tarehe tisa au ni baada ya tarehe tisa?

SHAHIDI: Ni baada ya tarehe tisa.

KIBATALA: Asante Mheshimiwa Jaji. Ni hayo tu.

JAJI: Wakili gani wa Serikali ataanza kuuliza maswali?

Wakili Kidando: Ataanza Jenitreza Kitali.

WAKILI WA SERIKALI JENITREZA KITALI: Ni sahihi shahidi umesema Adamu ni mume wako? Ni sahihi hujatoa cheti cha ndoa? Ni sahihi umesema kuwa Adamu walikuaga wanaenda Moshi mwanzoni mwa mwezi wa nane?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli umeeleza kuwa walikuaga wanakwenda kwa Mheshimiwa Mbowe?

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Ni kweli au si kweli mume wako na Ling’wenya walikuwa marafiki sana?

SHAHIDI: Ni kweli.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Mume wako pamoja na Ling’wenya waliondoka pamoja Chalinze. Sahihi?

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Wakati mume wako anajianda kwa ajili ya safari, mazingira ya nyumba yenu yakoje.

SHAHIDI: Nyumba ina vyumba vinne. Kuna sebule, dinning na choo.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Wakati mumeo anajiandaa na safari nitakuwa sahihi nikisema kuwa Adamu alikuwa ndani ya chumba wakati mgeni akiwa sebuleni?

SHAHIDI: Sahihi. Mgeni alikuwa sebuleni.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Katika ushahidi wako mwanzo mpaka mwisho hujasema ni lini walianza safari.

SHAHIDI: Sikusema. Sikumbuki ilikuwa tarehe ngapi.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Nitakuwa sahihi nikisema kama hukumbuki tarehe na unachokisema siyo sahihi?

SHAHIDI: Sikumbuki tarehe lakini walianza kusafiri pamoja mwishoni mwa mwezi wa saba.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Baada ya Adamu na Ling’wenya kufika Moshi ulipewa taarifa kwamba wamekamatwa?

SHAHIDI: Niliambiwa.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Umesema aliyekuambia ni Mke wa Ling’wenya, nitakuwa sahihi kuwa mtu aliyekwambia wamekamatwa Moshi siyo mtu aliyekwepo wakati wanakamatwa Moshi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Naomba nikurejeshe nyuma. Wakati mumeo anajianda na safari, Ling’wenya alikuwa sebuleni. Ni kweli Ling’wenya hakujua vitu gani vimewekwa katika begi?

SHAHIDI: Ni sahihi hawezi kujua.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Ni sahihi kwamba hujaiambia Mahakama kwamba wakati mumeo anapaki vitu vyake alibeba vitu hivi na hivi? Kweli au si kweli?

SHAHIDI: Si kweli.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Ni kweli umesema kwamba Adamu alipigwa Moshi mpaka akatoa damu?

MALLYA: Objection! Hicho anachouliza tayari Mahakama ishatoa malekezo kuhusu ‘hearsay’.

JAJI: Wakili wa Serikali?

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Labda Mahakama ituonyeshe kama ilitoa mwongozo huo.

JAJI: Ngoja niseme kuwa wakati tunaanza zoezi nilisema vitu amabavyo shahidi anaweza asiulizwe ni vile vinavyotezwa utu wake. Sasa vingine vyote unaweza kuuliza na anaweza kujibu.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Ulisema ulisikia kuwa Adamoo amepigwa mpaka kutoa damu.

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Umesema ulisema kuwa baada ya kuwa hapatikani kwenye simu mlianza kumtafuta Vituo vya Polisi.

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Mlianza kituo gani cha Polisi?

SHAHIDI: Kituo cha Polisi Chang’ombe.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Mlipofila Kituo cha Polisi wewe na wenzako mlianza kuomba huyo mtu aangaliwe kama yupo kituoni hapo?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Ilikuwa tarehe ngapi?

SHAHIDI: Tarehe 13 mwezi wa tisa.

JAJI: Mwenzi wa ngapi?

SHAHIDI: Mwezi wa nane.

JAJI: Sasa niandike lipi? Mwezi wa nane au wa tisa?

SHAHIDI: Mwezi wa nane.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Utakubaliana na mimi kuwa wakati nyumba inasachiwa hukuwepo?

SHAHIDI: Ndiyo. Nimeeleza.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Kwa hiyo maneno ya kwamba kuna vitu vimechukuliwa ni maneno ya kuambiwa.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Baada ya kukosekana Adamu mpaka wakati unamtafuta hukuwahi kumtafuta Mheshimiwa Mbowe mbali na kwamba walikuambia wanaenda Moshi kufanya kazi kwake?

SHAHIDI: Ndiyo sikumtafuta.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Hujaieleza Mahakama kwamba wakati mnaenda mochwari mlifuata utaratibu wa kukagua.

SHAHIDI: Nilifuata utaratibu.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Lakini wakati unatoa ushahidi hukusema ni taratibu zipi ulizifuata?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Wakati wote wa shauri hili linaendelea Mahakamani ulipata kulifuatilia?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (JENITREZA): Kwa njia gani?

SHAHIDI: Kwa njia gani?

Hadhana inalia na mahakama inakaa kimya.

JAJI: Tuendelee.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa kuwa ulikuwa unafuatilia kesi hii kwenye vyombo vya habari, na kwa kuwa ushahidi uliokuwa unaendelea kuwa Adam Kasekwa kateswa, ni sahihi ulisikia?

SHAHIDI: Nilisikia kupitia vyombo vya habari na yeye pia aliniambia,

WAKILI WA SERIKALI: Ni sahihi kwamba wakati mumeo anaelekea Moshi alikuwa ni mzima wa afya na hakuwa na majeraha?

SHAHIDI: Nisahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Na wakati unamtembelea Segerea uliona makovu. Je, uliyaona wapi?

SHAHIDI: Niliona kwenye mikono.

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye mikono yote miwili?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe kama mke wa Adamu Kasekwa utakubaliana na mimi kuwa unaieleza Mahakama kama Adamu Kasekwa aliwahi kuwa na makovu mengine kabla ya wewe kumkuta na hayo Segerea?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini hukuieleza Mahakama kama alipigwa wapi na lini.

SHAHIDI: Sikueleza ni lini.

WAKILI WA SERIKALI: Unaifahamu sana Dar es Salaam?

SHAHIDI: Kiasi kidogo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ulitembelea vituo vya Tazara, Chang’ombe, Central na Oysterbay?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Hukuiambia Mahakama sababu kwanini hukutembelea vituo vingie vidogo.

SHAHIDI: Nisahihi sikusema sababu.

WAKILI WA SERIKALI: Ni sahihi ulimuona Adamu amakekonda sana?

SHAHIDI: Ni sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Hukuieleza Mahakama kwanini alikonda.

SHAHIDI: Ni sahihi sikueleza sababu za kukonda.

Wakili Jenitreza Kitali: Naomba niwachie wenzangu.

Anasimama Wakili Robert Kidando

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Mpaka siku nyumba yako inafanyiwa upekuzi, ni kweli ulikuwa hujui Adam yupo wapi?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Huwezi kujua kama alikuwa ameridhia?

SHAHIDI: Sijui.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Mpaka sasa askari waliovaa uniforms hujui walikuwa ni akina nani?

SHAHIDI: Sijui.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na mpaka sasa wale waliovalia kiraia hujui walikuwa akina nani?

SHAHIDI: Ndiyo sijui kwa sababu sikuwepo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na pale Chalinze mtaa wako unaoishi unasema unaitwaje?

SHAHIDI: Ramboni.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na nyumba yako bila shaka itakuwa na grill.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na ulikuwa umelifungwa?

SHAHIDI: Hapana. Huwa naurudishia. Mlango ndio huwa nafunga.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Baada ya kwenda kwa jirani yako Kuuliza alikuambia Mwenyekiti wa Mtaa alikuwepo?

SHAHIDI: Hapana. Alikuwepo Mjumbe wa Nyumba 10.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Mpaka sasa yupo pale Chalinze?

SHAHIDI: Ndiyo. Mpaka sasa yupo pale Chalinze.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Unasema uliambiwa kuwa wamechukua begi la Adamu alilotoka nalo Congo. Je lipo tofauti na sare za Jeshi la JWTZ?

SHAHIDI: Lipo tofauti na mabaka mabaka ya Tanzania.

JAJI: Weka vizuri mabaka mabaka ya nini? Isije kuwa unasema Watanzania wana mabaka mabaka.

SHAHIDI: Mabaka mabaka ambayo ni maua ya sare za JWTZ yapo tofauti na mabakabaka ya lile begi.

JAJI: hapo umeweka sawa.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Ni sahihi hukumbuki tarehe ambazo waliondoka kwenda Moshi?

SHAHIDI: Ndiyo. Sikumbuki.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Kwa hiyo inaweza ikawa hata mwishoni mwa mwezi wa saba?

SHAHIDI: Ndiyo inawezekana.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Hujaieleza Mahakama kama mumeo aliondoka na kiasi gani cha fedha.

SHAHIDI: Sijaeleza.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Hujaeleza kwamba wakati wanaenda Moshi walitumia usafiri gani.

SHAHIDI: Sijaeleza. Ilan walitumia usafiri wa basi.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Umeeleza Polisi walichukua kadi ya pikipiki na hati, ila hujasema ni pikipiki ya aina gani wala namba gani. Hujasema.

SHAHIDI: Ndiyo. Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Pia Mahakamani hujasema namba ya kiwanja wala block au namba ya hati ya kiwanja.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Pia Kuwa hiyo pikipiki ama kiwanja vimesajiliwa kwa jina la nani.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Turudi kabla hawajaondoka kwenda Moshi. Ulisema walienda kwanza Morogoro wakarudi.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Ila hujasema kwamba Morogoro walienda kufanya nini?

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Kwa sababu ulisema kadi ya pikipiki ilichukuliwa, hujasema pikipiki hiyo ipo wapi.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Tuje tarehe tano mwezi wa nane mwaka 2020 kwamba uliwasiliana na Adam Kasekwa kuwajulia hali wewe na watoto, akasema subiri nitakupigia. Lakini hakukupigia tena.

SHAHIDI: Hakunipigia.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na hakukupigia.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Na ilipofika jioni wewe mwenyewe uliamua kumtafuta.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI (KIDANDO): Hujasema mahakamani kwamba kazi hiyo ya ulinzi alikuwa ameianza.

JAJI: Wakili tu- break kidogo kwa saa moja. Tutaendelea saa nane na dakika 15. Kwa hiyo naahirisha shauri hili mpaka saa nane na dakika 15.

Jaji ameshaingia.

Mawakili pande zote wamesema wako tayari kuendelea na shauri.

Shahidi ameshapanda kizimbani kuendelea kutoa ushahidi.

JAJI: Nakukumbusha kuwa upo chini ya kiapo. Wakili wa Serikali atakuuliza maswali au bado hujawa tayari?

JAJI: Wakil ungependa nikukumbushe?

WAKILI WA SERIKALI: Liliani, kipindi chote mumeo Adam Kasekwa kipindi yupo Moshi, ni kweli kuwa hujaiambia Mahakama mumeo alikiwa anaishi wapi huko Moshi?

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Kabla ya tarehe tano palikuwa hakuna tatizo. Ni sahihi kwamba hamkuwasiliana na Mohammed Ling’wenya kabisa?

SHAHIDI: Hatukukuwasiliana naye.

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli kwamba wakati mmepoteza mawasiliano na mumeo Adam Kasekwa mpaka mnakwenda mahospitalini ulikuwa hujaongea na Athima Dada yake Ling’wenya?

SHAHIDI: Ni sahihi. Nilikuwa sijaongea naye.

WAKILI WA SERIKALI: Na taarifa za kwamba wamekamatwa kule Moshi ulizipata kwa mke wa Mohammed Ling’wenya?

SHAHIDI: Sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Na kwamba wamesafirishwa kuja Dar es Salaam na Polisi?

SHAHIDI: Ndivyo alivyoniambia.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati mnamtafuta vituoni, hujasema katila ushahidi wako kwamba hujamuona kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam wala kiongozi yeyote wa Polisi.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Hapa Mahakamani umeonyeshwa kitabu kuwa kilikuwa na kitu gani kinachofanya kufanana na vitabu vingine kule kituoni.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Na hufahamu kwenye kitabu kuna mahitaji gani yanayomwongoza askari kukitunza au kukiandika. Hizo taratibu huzifahamu.

SHAHIDI: Sizifahamu.

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli kwamba wakati mkipita Vituo vya Polisi tarehe 13 mwezi wa nane mwaka 2020 nipo sahihi?

SHAHIDI: Upo sahihi.

WAKILI WA SERIKALI: Na kule mlipoenda monchwari ilikuwa tarehe 14 mwezi wa nane mwaka 2020?

SHAHIDI: Kweli.

WAKILI WA SERIKALI: Tuje ukaguzi wa mochwari. Hujasema kama ulionyeshwa miili ya waliokufa wote au ile isiyotambuliwa na ndugu zao.

SHAHIDI: Sijasema hayo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulitaja hospitali tatu tofauti: Muhimbili, Amana na Mwananyamala. Hujasema hospitali hizi hapa. Dar es Salaam zipo wilaya gani.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Hujatuambia kuwa katika kila mochwari jina la afisa wa mochwari aliyewaruhusu kukagua miili.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Wala hujasema cheo chake.

SHAHIDI: Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Hujasema katika kila moja ya mochwari hizo hospitalini ni miili mingapi mliikagua.

SHAHIDI: Hapana. Sijasema.

WAKILI WA SERIKALI: Mlipokuwa pale hospitali na hata sasa, kama kweli mlikagua miili, mlikuwa mnakiuka taratibu za afya.

SHAHIDI: Nilikuwa sifahamu kama nakiuka taratibu.

WAKILI WA SERIKALI: Tueleze kama unafahamu na kama umeeleza katika ushahidi wako, kama taratibu za kujilinda kiafya ulizingatia kama ulivyojifunga na barakoa hapa Mahakamani.

SHAHIDI: Nilijikinga. Nilivaa barakoa.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini hujasema katika ushahidi wako.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Kwanini umevaa barakoa leo?

SHAHIDI: Ndiyo najikinga na virusi vya corona.

WAKILI WA SERIKALI: Na tatizo hilo mwaka jana lilikuwepo.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Je, unakubali unaidanganya mahakama kwa sababu wasingekuruhusu uingie tu kukagua miili?

SHAHIDI: Hapana. Sijaidanganya Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe umesema hujawahi kuwasiliana moja kwa moja tangu tukio la kukamatwa kwa Adamu Kasekwa.

SHAHIDI: Ndiyo sijawahi.

WAKILI WA SERIKALI: Katika ushahidi uliopo Mahakamani, Adamu hajawahi kusema Mahakamani kwamba alipokuwa Moshi aliwahi kupigwa na kutoa damu. Je unaweza kutuambia hizi taarifa ulipozitoa?

SHAHIDI: Kama nilivyosema mwanzo, kwamba hizi taarifa nilizipokea kwa mke wa Ling’wenya na yeye alizitoa kwa wifi yake huko Moshi.

WAKILI WA SERIKALI: Mambo yaliyokuwa yanaendelea Moshi hakuna hata moja ulilowahi kushuhudia?

SHAHIDI: Ndiyo. Sikuwahi kuwa Moshi.

WAKILI WA SERIKALI: Utakubaliana na mimi kwamba hujawahi kutoa taarifa iwe Serikali ya Mtaa au Polisi?

SHAHIDI: Sikutoa taarifa.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa sababu hukutoa taarifa Polisi na hukuwa na taarifa kwamba amekufa, wewe ukaenda kukagua mochwari?

SHAHIDI: Nilienda. Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Tuje katika tukio unalodai kwamba nyumbani kwenu pale Chalinze. Umekubali kuwa palikuwa na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa na Unice Charles wakati wa upekuzi wewe hukuwepo na wao walikuwapo. Sema kama umeongea nao waje kutoa ushahidi.

SHAHIDI: Siyo kazi yangu kuleta mashahidi.

WAKILI WA SERIKALI: Una taarifa kuwa siku ya upekuzi walikuwa na Adam Kasekwa?

SHAHIDI: Sina taarifa.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa sababu wewe hukuwepo na sababu wanasema kuwa nyumba yenu ina grill tu haina mlango.

SHAHIDI: Mimi kama mwenye nyumba ndiyo nasema nina mlango wa grill na mlango wa kawaida ambao ulivunjwa.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ulipoenda Segerea unasema ulimuona Adam Kasekwa alikuwa na makovu. Je, yalikuwa maeneo gani kama unaweza kuonyesha?

SHAHIDI: Maeneo Hayaaa (Anaonyesha kwenye viungo vya mikono kabla ya kabla ya kufika kiganjani)

WAKILI WA SERIKALI: Unasema uliona taarifa zake kwenye taarifa za habari. Ilichukua muda muda gani kwenda kumwona?

SHAHIDI: Ilikuwa Jumamosi. Nikaja Jumapili na siku iliyofuata Jumatatu tukaenda lakini hatukuruhusiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Ikatokea kuna tofauti ya sehemu anayosema Adam na unayoonyesha wewe nani atakuwa anaongea ukweli?

SHAHIDI: Ni yeye Adam ndiye aliyeumia.

WAKILI WA SERIKALI: Sasa wewe huna uhakika?

SHAHIDI: Naongea nilichokiona.

WAKILI WA SERIKALI: Ndiyo sasa ikitokea …….

MALLYA: Objections! Nafikiri shahidi ameshajibu swali.

JAJI: Wakili wa Serikali unasemaje?

WAKILI WA SERIKALI: Naomba Mahakama iseme kama imerekodi kuwa amejibu.

JAJI: Ndiyo amejibu hilo swali.

WAKILI WA SERIKALI: Sawa Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Tuendelee.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema kuna namba uliyokuwa unatumia kumpigia Adam Kasekwa?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Unayo hapa Mahakamani?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini hukuiomba Mahakama ruhusa ya kuionyesha.

SHAHIDI: Ndiyo. Sikuomba.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisema ile hati ya kiwanja hujui wapi pa kuanzia?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Hukusema kwenye ushahidi wako kama ulimuuliza Mkuu wa Upelelezi alikuwa navyo au hakuwa navyo.

SHAHIDI: Sikusema.

(Mawakili wa Serikali wanashauriana).

Mawakili wa Serikali wanapeana vikaratasi. Wanapasiana.

Mahakama bado kimya.

JAJI: Ndiyo!

Bado wapo wapo kimya. Wanaendelea kunong’ona.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji mimi nimemaliza naomba mwenzangu aendelee.

JAJI: Sawa. Lakini msirudierudie maswali kama yameshaulizwa.

JAJI: Shahidi bado unanguvu ya kuendelea?

Wakili wa Pili wa Serikali: Liliani wewe ushawahi kutunga story?

SHAHIDI: Hapana.

WAKILI WA SERIKALI: Kwanini wakili alikuwa ana wasiwasi kuwa unatunga story?

SHAHIDI: Nilivyomuelewa ni kwamba mimi siwezi kutunga story kwa sababu mimi ni mke wake nilihusika sehemu zote.

WAKILI WA SERIKALI: Kwanini sasa wakili akuulize?

SHAHIDI: Nimemuelewa vizuri. Labda wewe hukumuelewa.

JAJI: Wewe shahidi umeelewaje?

SHAHIDI: Nimeelewa mimi ni mhusika kama mke wake siyo wa kuhadithiwa.

JAJI: Wakili endelea sasa.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini Kibatala alikuuliza hilo swali.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulionyeshwa kitabu fulani hapa kuwa vinafanana na vile mlivyokuwa mnapekua.

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe na Polisi nani anaweza kukizungumzia kile kitabu?

SHAHIDI: Polisi.

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli ulishindwa kutaja namba ya mume wako?

SHAHIDI: Ni kweli. Ilikuwa namba ngeni ndiyo imetoka kusajiliwa.

JAJI: Sasa namba mpya anaishikaje kichwani?

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli leo hujamuonyesha kuwa yule pale ndiyo Adamu Kasekwa?

SHAHIDI: Ndiyo.

JAJI: Unamaanisha kuwa anaweza asiwe anamfahamu mume wake?

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli kwamba kwenye kile kitabu hujaangalia ndani kuna nini?

SHAHIDI: Ndiyo. Nimeeleza kinafanana kwa nje.

WAKILI WA SERIKALI: Ni kweli kwamba hujawasiliana na ndugu zake Adamu wakati wote?

SHAHIDI: Nilishirikiana nao kwa njia ya simu. Wengi wapo Mbeya.

WAKILI WA SERIKALI: Unasema uliambiwa ameshatolewa Moshi kuja Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ndiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Ulikiwa unajua yupo Polisi lakini ukaenda mochwari?

SHAHIDI: Nilienda Polisi kwanza sababu sikuwa nafahamu.

JAJI: Hilo swali limejirudia. Sasa wakili kama mmemaliza uniambie.

WAKILI WA SERIKALI: Mengi yameshamalizwa naomba nimalize.

JAJI: Mallya kama kuna maswali karibu sana.

MALLYA: Nitauliza moja au mawili tu.

MALLYA: Umeulizwa kuhusiana na kitabu. Kwani hicho kitabu ulihusika nacho vipi?

SHAHIDI: Nilikitumia kuangalia majina.

MALLYA: Majina gani?

SHAHIDI: Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya na Khalifan Bwire.

MALLYA: Wakati wakili Robert Kidando anakuuliza swali kuhusiana ulienda mochwari licha ya kuwa umesikia amekufa…

WAKILI WA SERIKALI: Objection! Amesikia vibaya swali letu. Anarudia swali.

MALLYA: Mie sasa nauliza kabla ya kwenda mochwari ulikuwa umeenda wapi?

SHAHIDI: Nilienda Polisi

MALLYA: Shahidi tunakushukuru sana.

JAJI: Wakili Mallya?

MALLYA: Tumekubaliana na upande wa wenzangu kuwa kwa ushahidi tuishie hapa … na kwamba tuna ombi Mheshimiwa Jaji tupate fursa na Mahakama yako tufanye wasilisho (Submission). Na kama diary ya Mahakama tupate muda wa kufanya wasilisho mpaka Jumatatu.

JAJI: Upande wa Serikali?

WAKILI WA SERIKALI: Tunakubaliana na wenzetu kuwa tupate muda wa kufanya wasilisho, na kama ikiwezekana iwe mpaka tarehe nne Oktoba.

JAJI: Hizo final submission naomba ziwe kwa muhtasari sana. Nimesiliza ushahidi wote. Nisingependa ziwe ndefu. Ningependa mlete hizo submission zisizozidi kurasa tano tano.

JAJI: Ikiwezekana wekeni reference tu na muweke rejea ya kesi ambazo mnegependa nione maamuzi yake yalifanyika vipi. Nakubaliana na nyie kuwa tukutane hiyo Jumatatu. Nilitaka niwape mpaka ijumaa lakini kwa kuwa kesho Alhamisi basi mkajiandae.

JAJI: Sasa mawakili wameomba mawasilisho yao yaje tarehe nne mwezi wa 10 kupitia Ofisi ya Msajili wa Mahakama na mimi nitatoa maamuzi juu ya kesi ndogo siku ya tarehe 19 mwezi wa kumi mwaka 2021. Naahirisha shauri hili mpaka tarehe 19 mwezi wa kumi.

Tukijaliwa ni hadi tena hiyo Oktoba 19.

Like
1