Kesi ya Mbowe: Jaji aipiga chini Jamhuri kwa mara ya kwanza. Afuta kielelezo cha shahidi

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia BJ leo tarehe 11 Novemba 2021.

Jaji ameingia Mahakamani. Ni saa 5:15

Kesi inatajwa. Ni kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe.

Wakili wa Serikali Robert Kidando anatambulisha mawakili wa Serikali

 1. Pius Hilla
 2. Abdallah Chavula
 3. Jenitreza Kitali
 4. Nassoro Katuga
 5. Esther Martin
 6. Tulimanywa Majige
 7. Ignasi Mwinuka

Wakili Peter Kibatala anawatambulisha mawakili wa utetezi

 1. Jeremiah Mtobesya
 2. Paul Kaunda
 3. Fredrick Kihwelo
 4. Dickson Matata
 5. Idd Msawanga
 6. John Malya
 7. Alex Massaba
 8. Hadija Aron
 9. Evaresta Kisanga
 10. Maria Mushi

Jaji anawaita washtakiwa wote wanne, na wanaitika wote

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, shauri linakuja kwa ajili ya kusikiliza uamuzi wa Mahakama.

WAKILI PETER KIBATALA: Nasi pia kwa uhusa yako tupo tayari kupokea uamuzi na kuendelea na kesi.

(Jaji anaandika kidogo huku Mahakama ikiwa kimya).

JAJI: Jana nilisikikiza pingamizi la upande wa utetezi, na baada ya kusikiliza pande zote mbili, maamuzi yapo tayari. Jana wakati shahidi akitoa ushahidi alieleza kwamba baada ya kupewa maelekezo ya kumwandika maelezo mshitakiwa namba tatu, na kwamba alipoenda CRO aliwaomba wahusika aweze kumchukua mshitakiwa namba tatu.

JAJI: Kama ilivyo utaratibu alichukua kitabu cha Detention Register kwa ajili ya kuweka kumbukumbu yake. Na moja alisema angeweza kukitambua kielelezo hicho kwa majina yake, sahihi yake na majina ya mtuhumiwa. Na akaweka hizo kumbukumbu. Na baada ya hapo wakili wa Serikali Robert Kidando akamuuliza kama angeweza kutambua nyaraka hiyo. Baada ya hapo Wakili wa Serikali Robert Kidando akaomba Mahakama Iimpatie nyaraka hiyo.

JAJI: Na baada ya kupitia nyaraka hiyo shahidi alisema anaitambua na baada ya hapo aliomba mahakama ipokee nyaraka hiyo kwa ajili ya utambuzi. Kitu ambacho mawakili wa washitakiwa wote wanne awalipinga vikali. Katika pingamizi lao walisema kwamba shahidi hakujemga misingi katika kuaminika kwake kama alikuwa akijua kielelezo. Na hii ikapelekea kutoa rejea la shauri katika Mahakama ya Rufani Arusha. Katika kesi ya DPP vs Sharif imesema kwamba Shahidi anatakiwa kuaminika kwake na kwamba features zinapaswa zitambuliwe … Na jambo lingine ni Chain of Custody, na kwamba yapo maamuzi kadhaa ya Mahakama kwamba Chain of Custody inaweza kuamuliwa baada ya kesi kuisha, ila kwa kesi hii inapaswa Chain of Custody inapaswa kutazamwa sasa. Inapaswa shahidi ajenge misingi kwamba kwa namna gani kielelezo kimemfikiaje Mahakamani.

JAJI: Na mawakili wakasema kinachotolewa Mahakamani ni Register_siyo _Entry._Kwa mfano ingekuwa na _features ambazo zinaonesha Register hiyo inatumika Central tu na siyo mahala mengime popote. Shahidi anaweza kuileza Mahakama namna gani anakijua kielelezo hicho. Kwa mkazo kwenye Chain of Custody haijaelezwa kabisa Mahakamani kwamba kuna muunganiko wake yeye na ushahidi. Wakaeleza kwamba kielelezo kinachotolewa Mahakamani kuna ushahidi wa kutosha kwamba kilikuwa kwenye kesi ya Trial Within Trial ya Adam Hassan Kasekwa kabla ya kesi hii.

JAJI: Na mawakili wakasema kinachotolewa Mahakamani ni Register_siyo _Entry._Kwa mfano ingekuwa na _features ambazo zinaonesha Register hiyo inatumika Central tu na siyo mahala mengime popote. Shahidi anaweza kuileza Mahakama namna gani anakijua kielelezo hicho. Kwa mkazo kwenye Chain of Custody haijaelezwa kabisa Mahakamani kwamba kuna muunganiko wake yeye na ushahidi. Wakaeleza kwamba kielelezo kinachotolewa Mahakamani kuna ushahidi wa kutosha kwamba kilikuwa kwenye kesi ya Trial Within Trial ya Adam Hassan Kasekwa kabla ya kesi hii.

JAJI: Kielelezo hicho kilipaswa kiwe kwenye store ya Mahakama na kwamba hawajaeleza ni taratibu gani zimetumika kufika Mahakamani, kitu ambacho kimezua shaka. Na upande wa mashitaka walipata nafasi ya kujibu. Kwa kuwakilishwa na Abdallah Chavula na Pius Hilla walisema kwamba mapingamizi hayana mashiko. Wakaja na kesi ya DPP vs Sharif kwamba authentication ya Mahakama inapaswa kufanywa na ushahidi wa shahidi. Kielelezo hicho kilipaswa kiwe kwenye store ya Mahakama na kwamba hawajaeleza ni taratibu gani zimetumika kufika Mahakamani, kitu ambacho kimezua shaka. Na upande wa mashitaka walipata nafasi ya kujibu. Kwa kuwakilishwa na Abdallah Chavula na Pius Hilla walisema kwamba mapingamizi hayana mashiko. Wakaja na kesi ya DPP vs Sharif kwamba authentication ya Mahakama inapaswa kufanywa na ushahidi wa shahidi.

JAJI: Wakaiomba Mahakama itofautishe kesi ya DPP vs Sharif Athumani kwamba kwenye kesi ile kielelezo kilikuwa gari na kwenye kesi hii kielelezo ni nyaraka. Wakarejea kesi ya Charles Gazilabo dhidi ya Jamuhuri kwamba kesi hiyo iliweka mambo matatu ya relevance, competence na shahidi husika. Wakasema kwamba kwa namna ambavyo shahidi alikuwa anatoa ushahidi wake ni competent.

JAJI: Wakasema kwenye kesi ya Charles Gazilabo kwamba mtu anayeweza kuelezea kielelezo na kukitambua, kitu ambacho shahidi alifanya. Na pale ambapo shahidi ametoa ushahidi wake anaweza kufafanua. Wakaomba Mahakama ione kwamba kielelezo kilichopo Mahakamani shahidi anaweza kutoa ushahidi wake. Wakaeleza siku ya tarehe saba Agosti 2020 namna alivyofika saa 11 alfajiri na jinsi ambavyo shahidi aliweka Entry na aliweza kukitambua. Na wakaendelea kusema kwamba suala zima la Chain of Custody, kwamba Mahakama imeshatolea Maamuzi kwamba Chain of Custody inaweza kujadiliwa mwishoni. Wakasema Shahidi alijitahidi kueleza kwamba aliweka entry na hilo pekee ndiyo linafanya shahidi aonekane anaweza kukitambua.

JAJI: Shahidi alieleza kwamba alifika kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, hiyo inathibitisha kwamba shahidi anaweza kufanya utambuzi na wakaomba Mahakama itupilie mbali. Upande wa utetezi walipata tena nafasi ya kujibu na kuona bado mapingamizi yao yanayo sababu. Kwenye kesi ya Sharif ni kwamba wanaona kanuni inaweza kutumika kwenye kesi yoyote, na kwamba shahidi ameeleza entry na a siyo kielelezo chenyewe na kwamba suala la authentication halijaweza kukidhiwa, na suala zima la kuamua Chain of Custody waliendelea kusema suala la kupinga kielelezo ni jukumu lao kupinga wakati wa uchukuliwaji. Upande wa mashitaka wamekosa hoja za msingi kuhusiana na mapingamizi yao.

JAJI: Na Kwamba hakuna features mahususi kuhusiana na kielelezo hicho ili kutofautisha Detention Register na Detention Register zingine zinazotumika katika vituo vingine. Na suala la Chain of Custody haijaelezwa vizuri ni wapi walipotoa kielelezo hicho, kwamba kwa kumbukumbu zilizopo bado kielelezo kipo chini ya Mahakama. Huo ndio ulikuwa mwisho wa muhtasari. Sasa niende kwenye maamuzi.

JAJI: Tunakubaliana kwa pamoja kwamba pingamizi linapinga upokelewaji wa vielelezo na siyo jambo geni Mahakamani. Na maamuzi yamefanywa na Mahakama zetu katika upokeaji wa vielelezo Mahakamani. Maamuzi yameonyesha taratibu, kanuni na miongozo. Kufuatia maamuzi ya Sharif Mohammed na wenzake Mahakama ya Rufani Ilitoa maamuzi kwamba tunao ushahidi wa namna nneUhalisi, Testimonial, Documentary Evidence, na kwamba Mahakama inaweza kupokea ushahidi Mahakamani wakati wowote. Mahakama ijiridhe kama ushahidi ni Relevance, Material na Competence. Na katika maamuzi yake wamejadili kwa kina kuhusu ushahidi halisi. Nimesoma mpaka mwisho Sijaona kwamba vigezo ambavyo vinatumika katika Real Evidence haitakiwi kutumika katika kupokea Documentary Evidence. Nakubalina na upande wa utetezi kwamba kanuni zinazotumika kupokea Real Evidence zinaweza kupokelewa kwenye Documentary Evidence.

JAJI: Nakubalina kwamba vigezo vilitumika kwenye kesi ya Sharif Mohammed vinaweza kutumika katika Shauri hili Mahakamani. Basi Mahakama hii ina maoni kwamba vigezo vinavyotaka kutumika ni Relevance, Competence na Material na kwamba Mahakama kwa maoni ya kesi mbili kanuni zake zinaweza kutumika na Mahakama. Ili kujadili relevance basi inapaswa kuangalia kigezo cha authentication ni mambo matatu yatatumika. Identification of Exhibit, Establishing Chain of Custody, Identification of Objects. Haya siyo maneno yangu, ni maneno ya maamuzi ambayo nimeyanukuu hapo juu.

JAJI: Lengo la Chain of Custody wanapaswa kueleza kielelezo wamekitoa wapi. Na kuhusiana na competence ya shahidi imeelezwa kwenye kesi ya Charles Gazilabo , Khamis Adam kwamba mtu ambaye amekifanyia kazi kielelezo siyo tu anaweza kukitolea ushahidi bali anaweza pia kukitolea maelezo.

(Jaji anasoma maamuzi ya shauri hilo kama rejea)

JAJI: Kimsingi hayo ndiyo maamuzi ya Mahakama ya Rufaa. Kwa sababu hiyo sasa, ili kupima Competence ya shahidi, na kwa kesi hii shahidi ameeleza vizuri kuhusu kielelezo hicho ambacho alikitumia kuweka entry ili kumtoa shahidi kwenda kumchukua mtuhumiwa maelezo yake. Kwa maana hiyo anayo competence.

JAJI: Kuhusiana na relevance ni ukweli kwamba kipo relevant sababu onnadaiwa ndiyo walitumia kielelezo hicho kumtoa mtuhumiwa. Kuhusiana na materiality ni kweli kabisa kwamba kitasaidia Mahakama kufanya maamuzi, ikiwemo katika pingamizi kwamba mshitakiwa hakuwahi kuwapo katika kituo hicho cha Polisi. Mahakama hii Inaona kwamba ni sahihi kabisa kuendelea kutumika.

JAJI: Limebakia suala la Chain of Custody. Ni kweli shahidi namba moja ameeleza kwamba anaweza kutambua kielelezo hicho kwa majina yake na sahihi yake na majina ya mtuhumiwa. Ukweli ni kwamba ameweza kukitambua, ingawa Mr Mtobesya amepinga kwamba features zilizoelezwa ni za Entry na siyo Register yenyewe.

JAJI: Lakini Mahakama yenyewe inaweza kutambua kuwa kielelezo hicho huwezi kutenganisha Entry na Register. Na kuhusiana na Chain of Custody shahidi hajaeleza Chain of Custody kwamba ni kwa namna gani kielelezo hicho kimemfikia. Ni kweli kwamba hajaeleza ametoa wapi. Ni kweli kwamba kielelezo kipo kwenye kumbukumbu ya Shauri lingine.

JAJI: Ili Mahakama ionekama kilifuata utaratibu kilipaswa kionekane kwamba ni kweli kilifuata utaratibu wa kiutawala kutoka Mahakamani. Na kwa namna hiyo kielelezo kinajifuta chenyewe kwa sababu shahidi hakuonyesha namna gani kilimfikia. Assumption ni kwamba kielelezo kipo kwenye chumba cha Mtunza Kielelezo Cha Mahakama. Hakuna ushahidi kwamba shahidi alikipataje kuja Mahakamani.

JAJI: Kwa sababu hiyo Mahakama inakikataa kielelezo hiki. Natoa amri.

Mawakili wa pande zote wanasimama kukubaliana na uamuzi wa Jaji

JAJI: Shahidi wenu yupo wapi tuendelee?

(Wakili wa Serikali Robert Kidando amesimama tayari kumhosji shahidi, naye shahidi tayari amepanda kizimbani).

JAJI: Shahidi nakukumbusha upo chini ya kiapo ambacho ulikiapa wakati unatoa ushahidi wako.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi ulisema kwamba siku ya tarehe saba Agosti 2020 ulimchukua Mohammed Ling’wenya kwenda kumchukua maelezo. Eleza siku hiyo alikuwa na hali gani?

SHAHIDI: Wakati nachukua Mohammed Abdilah Ling’wenya alikuwa mwenye afya njema na hakuwa na tatizo lolote. Hata saa mbovu kuna wakati huonyesha majira sahihi!

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumchukua ulimpeleka wapi?

SHAHIDI: Nilimpeleka pembeni kidogo kwenye chumba kwa ajili ya mahojiano na mtuhumiwa huyo.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea baada ya kukaa pamoja nini kiliendelea?

SHAHIDI: Nikajitambulisha kwa majina kwamba mimi ni ASP Jumanne MALANGAHE. Na mtuhumiwa akajitambulisha kwa majina yake kwamba anaitwa Mohammed Abdilah Ling’wenya alimaarufu kama Doyi.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea ni kitu gani sasa ulifanya baada ya kujitambulisha.

SHAHIDI: Nilimuonya kwamba anatuhumiwa kwa makosa ya kula njama za kutenda matendo ya ugaidi. Nilimweleza kwamba katika tuhuma hizo halazimiki kueleza chochote isipokuwa kwa hiari yake mwenyewe, na Chochote atakachokieleza kinaweza kutumika kama ushahidi Mahakamani. Vilevile anayo haki ya kuwapo mwanasheria wake, ndugu yake, jamaa yake, au rafiki ili ashuhudie wakati maelezo hayo yakiandikwa. Baada ya hatua hiyo, mimi nilisaini na mtuhumiwa alisaini ili kuonyesha kwamba nilimuonya. Baada ya kumaliza hatua hiyo mtuhumiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya alimaarufu Doyi alijibu onyo hilo. Kwamba yeye Mohamed Abdilah Ling’wenya alimaarufu Doyiu ameonywa na mimi ASP Jumanne MALANGAHE anatuhumiwa kwa kosa la kula njama kutenda vitendo vya ugaidi chini ya Sheria namba 24 ya Sheria ya Kupambama na Ugaidi, na kwamba halazimishwi kusema lolote isipokuwa kwa hiari yake mwenyewe. Kwamba chochote atakachoandika kinaweza kutumika kama ushahidi Mahakamani. Na pia anaweza kuwepo mwanasheria wake, ndugu yake, jamaa yake, au rafiki ili ashuhudie wakati maelezo yake yakiandikwa.

SHAHIDI: Baada ya mtuhumiwa kuulizwa onyo hilo kama yupo tayari kutoa maelezo yake, mtuhumiwa akajibu NDIYO. Nipo tayari. Nilimuuliza nani awepo wakati anatoa maelezo yake, mtuhumiwa alijibu yeye mwenyewe anatosha wakati wa kutoa maelezo yake. Baada ya hapo alisaini na mimi nikasaini. Na baada ya hapo akawa tayari kutoa maelezo yake. Saa 2 na dakika 20 nilianza kuandika maelezo ya mtuhumiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe ulifanya nini baada ya yeye kusema yupo tayari kutoa maelezo?

SHAHIDI: Nilimuuliza mtuhumiwa ushiriki wake kuhusu tuhuma nilizomweleza. Nilimueleza kila anapohusika na ambapo yeye alikiri.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe baada kueleza ulifanya nini?

SHAHIDI: Nilikuwa naandika kwenye karatasi, fomu kile alichokuwa ananieleza.

WAKILI WA SERIKALI: Kilikuchukua muda gani?

SHAHIDI: Muda wa masaa mawili na dakika 42.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumalizia kuandika ulifanya nini?

SHAHIDI: Nilimpatia maelezo ayasome ili kuweza kuongeza, kupunguza au kufanya marekebisho kwa yale aliyoyasema.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya mtuhumiwa kusoma maelezo hayo akasemaje?

SHAHIDI: Ameridhika na hana cha kupunguza wala kuongeza.

WAKILI WA SERIKALI: Ulifanya nini baada ya kuandika?

KIBATALA: Objection! Anachofanya wakili anajua hakiruhusiwi

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumaliza kuandika ulifanya nini?

SHAHIDI: Alisaini na mimi nikasaini. Na baada ya hapo nikaandika uthibitisho wangu mimi mwenyewe.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumaliza kuandika uthibitisho huo ulifanya nini?

SHAHIDI: Niliandika muda wa kuandika maelezo.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumalizia kuandika maelezo ulifanya nini na mtuhumiwa?

SHAHIDI: Nilimchukua na kumrejeaha chumba cha Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Maelezo ya mshitakiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya uliyapeleka wapi?

SHAHIDI: Kwa Assistant Inspector Swila.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa ni lini?

SHAHIDI: Ilikuwa ni siku hiyo hiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea baada ya shughuli hiyo ulikutana wapi tena na mtuhumiwa?

SHAHIDI: Niliondoka kwenda kufanya majukumu mengine kwa kadri nilivyokuwa naelekezwa na ACP Kingai.

SHAHIDI: Siku ya tarehe nane Agosti 2020 majira ya saa tano asubuhi tukiwapo na Inspector Mahita, tulielekezwa na Afande Kingai kumhamisha mtuhumiwa na kumpeleka Kituo cha Polisi Mbweni.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya maelekezo hayo ulifanya nini?

SHAHIDI: Tukiwa na Inspector Mahita na Goodluck nilimuelekeza Inspector Mahita kuwachukua watuhumiwa hao wawili.

WAKILI WA SERIKALI: Wawili nani na nani?

SHAHIDI: Mohamed Abdilah Ling’wenya na Adam Hassan Kasekwa.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwachukua wewe ulikuwa wapi?

SHAHIDI: Nilikuwa naye palepale anawachukua naangalia, anawapandisha kwenye gari nashuhudia.

WAKILI WA SERIKALI: Ukiacha watuhumiwa hawa wawili nani mwingine alikwepo kwenye gari?

SHAHIDI: Alikuwepo Inspector Mahita, Assistant Inspector Swila, Goodluck na Dereva wa Gari anaitwa Wendo.

WAKILI WA SERIKALI: Mlitumia muda gani kutoka Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam mpaka Mbweni.

SHAHIDI: Kama dakika 45 kwa sababu tulikuwa tunatumia gari yenye kimulimuli cha polisi Mkoa wa Kilimanjaro.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati mkielekea Mbweni ni kitu gani kiliendelea?

SHAHIDI: Hakuna kilichoendelea. Tulipofika tukiwakabidhi watuhumiwa.

SHAHIDI: Na kwenda kuonana na kiongozi wetu ACP Kingai kwa upelelezi wa watuhumiwa wengine.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea baada ya hapo ulionana naye wapi?

SHAHIDI: Sikuwahi kuonana tena na mtuhumiwa huyo.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa ufahamu wako vituo ambavyo Mohammed Abdilah Ling’wenya aliweza kufikishwa ni vingapi?

SHAHIDI: Ni viwili tu. Ni Kituo cha Kati Dar es Salaam na Kituo cha Polisi Mbweni.

WAKILI WA SERIKALI: Unasema siku mnampeleka Kituo cha Polisi Mbweni hakuna kilichofanyika zaidi ya kumkabidhi pale. Sababu hasa ni nini?

SHAHIDI: Sababu zilikuwa za kiupelelezi. Sababu kuna mwingiliano wa watuhumiwa wengi wanaingia na kutoka ni wengi. Tulihofia taarifa zinaweza kufika kwa watuhumiwa ambao bado tunawatafuta kwa urahisi.

WAKILI WA SERIKALI: Siku unaandika maelezo ya mtuhumiwa pale, unasema ulimpa Inspector Swila. Je, Inspector Swila alipeleka wapi?

MTOBESYA: Objection! Mheshimiwa Jaji huyo siyo Swila. Hawezi kujibu kwa niaba ya Swila

WAKILI WA SERIKALI: Ngoja nirudie swali. Ulipompa Swila hizi karatasi, alifanya nini na hizo Karatasi?

SHAHIDI: Ndiyo tulikuwa tunampa nyaraka zetu. Kwa hiyo alizichukua akaenda kuweka kwenye jalada.

MTOBESYA: Objection! Mheshimiwa Jaji hizo ni hearsay.

JAJI: Jiande uje kumuuliza labda walikuwa naye.

SHAHIDI: Swila muda mwingi tulikuwa naye. Alienda kuweka kwenye jalada la upelelezi.

KIBATALA: Objection! Mheshimiwa Jaji wakili anahama eneo. Je, ulichokiandika siyo hearsay?

WAKILI WA SERIKALI: Sisi bado hatuoni tatizo.

WAKILI WA SERIKALI: Huyu Mohamed Abdilah Ling’wenya amepinga maelezo ya onyo kwamba hakuwahi kufika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na hajawahi kuandika maelezo hayo.

SHAHIDI: Siyo kweli. Mimi mwenyewe ndiyo niliyempeleka pale, nikaenda kumchukua mimi mwenyewe kutoka kwenye chumba cha mashitaka nikiwa peke yangu bila uwepo wa askari mwingine yoyote, akiwa na hali nzuri, na mimi niliondoka nikawa nje ya kituo na yale maelezo, nikampigia Assistant Inspector Swila ili aweke yale maelezo kwenye jalada la kesi.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe una utbitisho gani kwamba uliandika hayo maelezo siku ya tarehe saba Agosti 2020?

SHAHIDI: Alikuweppo askari aliyekuwepo pale chumba cha mashitaka. Na baada ya kumaliza kuandika maelezo, askari huyo huyo alimpokea na kumrudisha lock up.

WAKILI WA SERIKALI: Anachosema ni kwamba ulimtishia kwa bastola ili kutoa maelezo.

SHAHIDI: Siyo kweli. Sikuwahi kumtishia mtuhumiwa huyo kwani alikuwa na ushirikiano. Sikuwa na sababu hiyo…

KIBATALA: Objection! Hajasikia vizuri mapingamizi.

WAKILI WA SERIKALI: Sawa. Ngoja nirudie. Ulimtishia kwamba asiposaini ile karatasi ya maelezo basi yale mateso mliyompatia Moshi mtayarudia.

SHAHIDI: Si kweli. Sikumtishia kwa sababu sikuwa na sababu hiyo.

WAKILI WA SERIKALI: Maelezo ya Mohammed Abdilah Ling’wenya ukiyaona unaweza kuyatambuaje?

SHAHIDI: Naweza kuyatambua kwa majina yangu, sahihi yangu, uwepo wa majina ya mtuhumiwa na sahihi zake na yote aliyonieleza nikaandika kwenye karatasi ya maelezo.

WAKILI WA SERIKALI: Samahani Mheshimiwa Jaji tunaomba tumpatie nyaraka kwa sababu ya utambuzi.

(Shahidi anakabidhiwa nyaraka).

WAKILI WA SERIKALI: Angalia nyaraka hiyo kama umeitambua na useme ni kitu gani.

SHAHIDI: Ndiyo nimeitambua nyaraka hii kama maelezo niliyoaandika kutoka kwa Mohamed Abdilah Ling’wenya maarufu kama Doyi.

WAKILI WA SERIKALI: Umeitambuaje?

SHAHIDI: Kwa majina yangu, sahihi yangu pamoja na saini zake pamoja na aliyoyaeleza.

KIBATALA: Objection! Kwa stage ya utambuzi anatakiwa asifike kwenye aliyoyaandika sababu ni content.

WAKILI WA SERIKALI: Sisi hatuoni tatizo.

KIBATALA: Kwa Stage ya utambuzi, aliyoyaandika ni content.

JAJI: Content yake hatuingii, anaishia kusema ameyaona.

WAKILI WA SERIKALI: Ungependa Mahakama ifanye nini katika hayo maelezo uliyoandika kutoka kwa Mohammed Abdilah Ling’wenya alimaarufu kama Doyi?

SHAHIDI: Ningependa Mahakama iyapokee kwa utambuzi.

MTOBESYA: Hatupingi upokelewaji wa maelezo haya kwa niaba ya mshitakiwa wa kwanza. Sababu ni zifuatazo, naomba iwe on record kwamba Mahakama inajua hayo maelezo lakini mshitakiwa wa tatu amekataa hayo maelezo. Kutokupinga huku hakumaanishi kwamba mshitakiwa anakubaliana na content.

Pius Hilla: Objection! Mheshimiwa Jaji natafakari kwamba hupingi lakini kwa conditions kwamba lazima sababu zieleweke kama hupingi.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini unapoongezea vitu vingine ina maana hukubaliani. Tunatengeneza record gani kwa Mahakama? Kama kuna jambo it’s better akapinga.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Kwa kuongezea tu, hili zoezi la Trial Within Trial na hii condition alizotoa hapa hairuhusiwi.

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji, sijui kwanini wenzangu wamesimama. Wenzangu waniambie kwamba ni sheria gani inakataza ninaposema sipingi. Siruhusiwi kuongeza maneno. Sijui wenzangu wana hofu. Wakasome kesi ya Martha Weja. Sisi kama utetezi tunaruhusiwa kuhoji content.

JAJI: Katika kesi yoyote Mahakama haijui chochote bila nyinyi kuieleza Mahakama. Mahakama imeelekezwa kwamba isiyapokee yanayovunja sheria yoyote. Sioni tatizo kwa Mtobesya kuzungumza alicholizungumza na huwezi jua atakitumia wapi.

MTOBESYA: Naomba nikumbushwe niliishia wapi.

JAJI: Uliishia Mheshimiwa Jaji…

(Mahakamani watu wanaangua kicheko).

JAJI: Unakubaliana na Mahakama kupokea, lakini hukubaliani na content.

MTOBESYA: Naomba niishie hapo.

(Anaamka wakili Paul Kaunda).

Kaunda: Kwa niaba ya mshitakiwa wa pili tunaomba kuunga mkono kilichozungumzwa na wakili wa mshtakiwa wa kwanza.

FREDERICK KIHWELO: Tunakubaliana na uwepo wa nyaraka hii lakini hatukubaliani na kilichopo ndani.

Peter KIBATALA: Kwa niaba ya mshitakiwa wa nne na sisi hatupingi. Tunategemea kuitumia nyaraka hii katika kuhoji dodoso katika kesi hii ndogo.

JAJI: Yaliyosemwa na Mtobesya mnalolote la kujibu upande wa mashtaka?

(Mawakili wa Serikali wananong’onezana kidogo).

JAJI: Napokea kama ID namba moja.

(Mawakili wa pande zote wanakubaliana).

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Naomba dakika mbili nishauriane na wenzangu kuhusu hoja ya Mtobesya kama kuna la kumjibu.

WAKILI WA SERIKALI: Off record kwanza. Kuna jambo la Mtobesya kwamba kwemye kesi ya Martha Weja, tukasema tunaomba tujiridhishe kwanza.

MTOBESYA: Kwa haki tuwaache wajiridhishe tu. Ni kesi ambayo imeripotiwa kwemye ‘Tanzania Law Report’ ya mwaka 1982 ukurasa wa 35.

KIBATALA: Nawakumbusha kwamba wenzetu wazingatie na muda kwa sababu leo tumeamza saa tano na shahidi ana siku mbili kizimbani.

JAJI: Siku tatu labda kwenye kesi ndogo ndiyo siku mbili.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa tupewe tu muda wa kutosha kwa sababu hatuna hapa na hatuwezi kupata. Ipo ofisini.

JAJI: Mtobesya ametaja mpaka kurasa. Labda anayo hapo.

MTOBESYA: Hapana. Sina hapa. Ni kesi ya siku nyingi lakini tunatumia sana. Naweza kuiomba na mimi ofisni waka- scan wakanitumia.

JAJI: Natoa ahirisho la dakika 45. Tutarudi saa nane.

(Jaji anaondoka katika chumba cha mahakama).

Jaji ameingia na kesi imeshatajwa. Ni Kesi namba 16 ya mwaka 2021 kati ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe.

Wakili wa Serikali anasema column yake iko vile vile, kwamba hakuna mabadiliko.

Wakili Peter Kibatala naye anasema kwa upande wa utetezi wapop tayari kuendelea na kesi.

Anaanza Mtobesya.

MTOBESYA: Shahidi, wakati mnamkamata Ling’wenya ni taarifa zipi mlikuwa nazo tayari?

SHAHIDI: Taarifa tulizokuwa nazo alikuwa ni miongoni mwa kundi ambalo linafanya njama kwa kufanya vitendo vya kigaidi ambavyo ni kushiriki katika kulipua vituo vya kuuzia mafuta. Kukata miti na kuweka barabarani, kulipua maeneo yenye mkusanyiko wa watu na kuhamasisha maandamano yasiyo na kikomo.

MTOBESYA: Ni hizo taarifa tu au mlikuwa na zingine?

MTOBESYA: Ni nani aliwasaidia kuwapa taarifa mpaka mkajua eneo alilokuwa Ling’wenya?

SHAHIDI: Nilikuwa na mkuu wangu Afande Kingai. Yeye ndiye alikuwa anajua aliyekuwa anampa taarifa.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi kwamba mpelelezi yoyote kabla hajaanza kufanya upelelezi anakuwa na dhana kichwani unapoenda field unaenda kuthibitisha kama ni chanya au hasi? Ni sahihi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji kwenye shauri hili dhana yako ilikuwa ni nini?

SHAHIDI: Nilikuwa naenda field kuthibitisha tuhuma kama mtuhumiwa huyo anahusika.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji ilichukua muda gani tangu unatengeneza dhana hiyo mpaka mnamkamata Ling’wenya.

(Shahidi anakaa kimya kidogo. Jaji anamuuliza shahidi kama ameelewa swali. Shahidi anapata kigugumizi kidogo. Anashindwa kuongea).

SHAHIDI: Ni palepale nilipopata taarifa na kuanza kutafakari na haikuchukua muda mrefu.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji taarifa hizo ulizipata lini.

SHAHIDI: Siku ya tarehe nne Agosti 2020.

MTOBESYA: Na Ling’wenya mlimkamata tarehe ngapi?

SHAHIDI: Naomba nirejee nyuma ya swali lako ulilokuwa umeniuliza.

MTOBESYA: Enheeee!!!!

SHAHIDI: Umeniuliza nilichukua muda gani kuniwezesha kwenda field.

MTOBESYA: Sijakuuliza swali hilo.

SHAHIDI: Dhana ni kama kitu ambacho huna uhakika nacho.

MTOBESYA: Hapana. Namaanisha ‘hypothesis’. Mpelelezi yeyote lazima awe na ‘hypothesis’. Nakurudisha kwenye swali sasa. Je, mlimkamata lini Ling’wenya?

SHAHIDI: Tarehe tano Agosti 2020.

MTOBESYA: Maelezo ya Ling’wenya uliyaandika lini?

SHAHIDI: Tarehe saba Agosti 2020.

MTOBESYA: Kwa hiyo nitakuwa sahihi kwamba wakati unamuhoji ulikuwa na taarifa.

SHAHIDI: Hapana. Sikuwa na taarifa.

MTOBESYA: Siwezi kukunyonga kwa majibu yako. Haya umesema Ling’wenya alikiri kujihusisha kufanya vitendo hivyo. Ni vipi?

SHAHIDI: Kwamba kweli alijihusisha na vitendo vya kupanga njama.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi nikisema kwamba mpelelezi asiandike maelezo ya mtuhumiwa kwa sababu mpelelezi anataarifa nyingi wakati anampeleleza?

SHAHIDI: Hapana. Siyo sahihi.

MTOBESYA: Kwa hiyo pale ambapo kuna askari mwingine na mpelelezi yupo hairuhusiwi askari mwingine kuchukua maelezo?

SHAHIDI: Hapana. Inaruhusiwa.

MTOBESYA: Zoezi la kuchukua maelezo lilianzishwa na nani?

SHAHIDI: Mimi ndiyo wajibu wangu.

MTOBESYA: Kwa hiyo iingie kwenye record kwamba ni wewe ndiyo uliomba kuchukua maelezo?

SHAHIDI: Ni wajibu wangu.

MTOBESYA: Nitakuwa Sahihi kuna aina mbili za uchukuaji wa maelezo, pale ambapo mshitakiwa anaomba au askari anataka kufanya hivyo.

SHAHIDI: Hapana. Mtuhumiwa hawezi kuomba.

MTOBESYA: Kwa hiyo hakuna sehemu ambayo mtuhumiwa anaweza kuomba kuandikwa maelezo yake?

SHAHIDI: Inategemea na mazingira.

MTOBESYA: Kwa hiyo tunakubaliana kwamba mtuhumiwa mwenyewe anaweza kuomba kuandikwa maelezo.

JAJI: (Anamuuliza shahidi) Kama hujamuelewa uliza swali.

SHAHIDI: Natafakari kidogo.

JAJI: Ujibu kwa spidi sasa!

MTOBESYA: Kwa hiyo kuna namna mbili au moja?

SHAHIDI: Hakuna namna mbili.

MTOBESYA: Maelezo uliyachukua kwa namna ipi?

SHAHIDI: Kwa namna mbili baada ya kumuuliza na yeye kuwa anajibu.

MTOBESYA: Kwa hiyo maelezo yake yanatokana na majibu yako.

SHAHIDI: Kulikuwa na maswali na sehemu zingine pana maelezo.

MTOBESYA: Nilikusikia wakati hujaanza kuchukua maelezo kwamba ulimpatia haki zake za kuwa na wakili na ndugu halafu akasema ataandika mwenyewe. Lakini hukusema kwamba wakati wote mnamkamata mpaka mnamchukua maelezo kwamba hamkuwezesha kukutana na ndugu.

SHAHIDI: Sahihi. Sikusema.

MTOBESYA: Kwa hiyo tunakubaliana kwamba nitakuwa sahihi nikisema kwamba mtu pekee anayejua kama mtuhumiwa alikamatwa ni nyiye mliomkamata, yeye aliyekamatwa na mtu aliyekamatwa wakiwa pamoja.

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Unaeleza nini kuhusu maelezo ya onyo?

SHAHIDI: Ni yale yanayochukuliwa kuhusu mtuhumiwa anahusishwa na kutenda aina fulani ya kosa.

MTOBESYA: Ni hivyo tu?

SHAHIDI: Inatosha.

MTOBESYA: Nitakuwa Sahihi nikisema maelezo ya onyo yanatakiwa kuonyesha mtuhumiwa kosa analotuhumiwa nalo?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Nitakuwa Sahihi kwamba kosa unalomuonya nalo ni lazima liwe limetamkwa kwenye sheria?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi kwamba maelezo ya onyo yanatakiwa kuwa sheria na inatakiwa kuonyesha kifungu unachomuonya nacho?

SHAHIDI: Siyo kweli. Unaweza kumwambia kwa maneno tu.

MTOBESYA: Kwa hiyo siyo muhimu kumtajia kifungu unachomuonya nacho?

SHAHIDI: Ni muhimu kwa minajili ya kumuonya mashitaka yenyewe.

MTOBESYA: Kwa hiyo kwako wewe siyo muhimu?

SHAHIDI: Nilisahua lakini nilikuwa nishamwambia.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi kwamba ni matakwa ya kisheria, baada ya zoezi la kuonya kuisha tarehe, mwaka na muda lazima viwe katika fomu unayotumia kumuonya?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Na wewe uliweka hivyo?

SHAHIDI: Ndiyo. Niliweka.

MTOBESYA: Tutaona baadae kama uliweka. Na nitakuwa sahihi muda wa kuonya siyo muda wa kuchukua Maelezo? Unamuonya kwanza kisha unamchukua maelezo.

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Kwa hiyo ni sahihi kwamba muda wa kuonya ni tofauti na muda wa kuchukua maelezo.

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Twende kwenye hitimisho la kuandika maelezo pale unapotakiwa kuthibitisha.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi nikisema ufungaji wa maelezo ya onyo una namna mbili au tatu, kwanza wa mtu anayejua kusoma na kuandika na ameridhia kwa anayeandika, ambaye hajui kusoma na kuandika au amekataa na mwisho mtu ambaye amekataa.

SHAHIDI: Siyo sahihi.

MTOBESYA: Haya. Tueleze wewe wa kwanza anathibitisha vipi?

SHAHIDI: Yeye mwenyewe anaandika kwamba nimeyasoma na kuyaelewa.

MTOBESYA: Na hiyo inaonekana katika _statement_uliyoiandika? Na wewe mwenyewe unaandikaje mwishoni?

SHAHIDI: Unathibitisha kuandika maelezo ya mtuhumiwa huyo.

MTOBESYA: Huyo ambaye amesoma na kuandika, anathibitisha vipi? Kwa signature na dole gumba maana havitumiki kwa pamoja.

SHAHIDI: Vyote vinatumika.

MTOBESYA: Na huo ndiyo ushahidi wako?

SHAHIDI: Ndiyo.

MTOBESYA: Unafahamu PGO ni nini?

SHAHIDI: Nafahamu ndiyo.

MTOBESYA: Nitakuwa sahihi kwamba ndiyo kitendea kazi chenu cha kila siku?

SHAHIDI: Ndiyo.

MTOBESYA: Haya. Mwambie Mheshimiwa Jaji inasemaje.

SHAHIDI: Kwa yule ambaye anajua kusoma na kuandika ataweka Sahihi na kuweka dole gumba na yule ambaye hajui kusoma na kuandika atashindwa kuweka dole gumba.

MTOBESYA: Huyo Ling’wenya alifanya nini kama ulivyotueleza?

SHAHIDI: Alisaini pamoja na dole gumba.

MTOBESYA: Kule chini kule mnapoweka ithibati kuna vifungu mnaviandika.

SHAHIDI: Ni sahihi.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji kwenye maelezo yenu mlitumia vifungu gani?

SHAHIDI: Ilikuwa Imeshaandikwa kwenye karatasi. Niliona hakuna haja ya kuweka hicho kifungu.

MTOBESYA: Kitaje.

SHAHIDI: Kilikuwa kifungu cha 57(3).

MTOBESYA: Umekitaja maana yake unakifahamu. Mweleze Mheshimiwa Jaji kama hicho kifungu hakina aya zake.

SHAHIDI: Sikumbuki kama zipo hizo aya.

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji naomba nipatiwe ID 1.

(Mahakama inampatia Mtobesya ID1)

MTOBESYA: Nakuonyesha kKielelezo cha Mahakama nikuulize maswali machache.

MTOBESYA: Iambie Mahakama kama baada onyo uliweka muda.

(Shahidi anakuwa mbishi kidogo lakini mwishoni anasema…)

SHAHIDI: Hakuna muda.

MTOBESYA: Tuonyeshe uthibitisho amesoma na kuyaelewa sehemu gani.

SHAHIDI: Mtuhumiwa amesaini na kuweka dole gumba.

MTOBESYA: Na kifungu cha sheria…..

SHAHIDI: Ndiyo nimesema kwamba karatasi ilikuwa tight sikupata nafasi ya kuweka.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji pale ambapo maelezo ya mtuhumiwa anathibitisha kuna kifungu cha Sheria au hakipo.

SHAHIDI: Hakipo kifungu cha sheria.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji ulipoishia wewe kuthibitisha kama kipengele cha mwisho kifungu kimeelezwa ni kifungu 57(3) na aya zake au hapana.

SHAHIDI: Tunaona kifungu cha 57(3).

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji naomba kurudisha kielelezo.

MTOBESYA: Ni kwanini hamkuweza kuchukua maelezo ya mtuhumiwa mkiwa Moshi?

SHAHIDI: Kwa sababu tulikuwa tunaendelea kutafuta watuhumiwa wengine na watuhumiwa walikuwa ni sehemu ya kusaidia, na pia shauri lenyewe lilikuwa Dar es Salaam na pia nature ya tukio ilikuwa inaenda kutokea mikoa ya Dar es Salaam, Arusha Kilimanjaro, Mbeya, Mwanza na Morogoro.

MTOBESYA: Mweleze Mheshimiwa Jaji kama unatambua utaratibu wa kuchukua maelezo halafu baadaye unaweza kuandika maelezo ya ziada (Additional Statement).

SHAHIDI: Sitambui.

MTOBESYA: Mtajie Mheshimiwa Jaji kama ni kanuni au sheria gani inayokulazimisha kwenda kuchukua maelezo sehemu uliyofumgulia shauri.

SHAHIDI: Siyo sheria wala kanuni lakini….

MTOBESYA: Hakuna cha lakini. Mheshimiwa Jaji naomba kuishia hapo.

Anaamka wakili John Mallya.

MALLYA: Kabla hujahamia Arusha ulikuwa ofisi ya Upelelezi Dar es Salaam.

SHAHIDI: Sahihi.

MALLYA: Kwa muda gani?

SHAHIDI: Kwa miaka saba.

MALLYA: Ni sahihi ulikuwa katika Ofisi ya DCI?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MALLYA: Nitakuwa sahihi nikisema unaijua Dar es Salaam?

SHAHIDI: Siyo sahihi.

MALLYA: Ramadhan Kingai kabla hajawa RCO alikuwa msaidizi wa ZCO Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MALLYA: Kwenye timu yenu nikisema kwenye timu yenu angalau kuna watu wawili wanaijua vizuri Dar es Salaam nitakuwa sahihi?

SHAHIDI: Siwezi kusemea wote.

MALLYA: Ofisi ya DCI ipo katikati ya Jiji la Dar es Salaam au sema ipo wapi.

SHAHIDI: Mtaa wa Ohio.

MALLYA: Makao Makuu ya Polisi mpaka Dar es Salaam ni umbali gani kwa kukadiria?

SHAHIDI: Siwezi kukadiria.

MALLYA: Lakini unajua kuwa Makao Makuu ya Polisi na Polisi Mjini Kati Dar es Salaam vipo wilaya moja.

SHAHIDI: Sahihi.

MALLYA: Kituo cha Polisi Mbweni unakifahamu?

SHAHIDI: Nakifahamu.

MALLYA: Kituo cha Polisi cha Mbweni ni kituo cha Wilaya ya Kipolisi Kawe.

SHAHIDI: Siha uhakika.

MALLYA: Kwamba wakati unapeleka watuhumiwa Mbweni ulikuwa hujui kuna kituo cha polisi cha wapi?

SHAHIDI: Nilikuwa najua ni kituo cha polisi tu.

MALLYA: Je, kuna kesi yoyote umeshawahi kusikia kwamba kuna mtu alienda kutoa taarifa kwamba watuhumiwa wamekamatwa ututajie?

SHAHIDI: Ni mambo ya siri.

MALLYA: Nimesikia unamwambia Mtobesya wakati mnawakata kipaumbele kilikuwa matukio yasitokee.

SHAHIDI: Ni sahihi.

MALLYA: Ni sahihi kwamba wakati wote Polisi mnapaswa kutenda kazi kwa mujibu wa sheria?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Wakati mnapokea simu ya Boaz kwamba mrudi Dar es Salaam ilikuwa mkoa gani?

SHAHIDI: Kilimanjaro, Moshi

MALLYA: Kilichowafanya msiwaandike maelezo muda huo ni nini baada ya kuambiwa zoezi la kuacha kumtafuta Lijenje?

SHAHIDI: Tulikuwa tunawahi kuja kuendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine Dar es Salaam na kuendelea na upelelezi.

MALLYA: Je, Mohammed Ling’wenya alitishiwa au alitoa kwa hiari?

SHAHIDI: Alitoa kwa hiari.

MALLYA: Ulipata kufahamu kuwa Mohammed Ling’wenya alishawahi kuwa Moshi?

SHAHIDI: Nakumbuka alikwenda mara mbili.

MALLYA: Alikaa kwa muda gani?

SHAHIDI: Safari ya kwanza … alilala siku moja.

MALLYA: Wapi?

SHAHIDI: Hotel ya Aishi.

MALLYA: Mlango ua bar?

SHAHIDI: Alilala ndani.

MALLYA: Alikaa wapi?

SHAHIDI: Mara ya pili alifika Aishi Hotel na baadaye katoka akawa anakaa Moshi mpaka tunamkamata.

MALLYA: Usiku huo alikuwa ametokea kulala wapi?

SHAHIDI: Sikumbuki.

MALLYA: Kwa kumbukumbu zako Mohammed Ling’wenya ni mwenyeji wa wapi?

SHAHIDI: Mtwara.

MALLYA: Wewe umekaa Moshi kwa muda gani?

SHAHIDI: Kwa nyakati mbalimbali na mafunzo mbalimbali.

MALLYA: Ulielezea Mahakama utafutaji wenu ulikuwa wa namna gani?

SHAHIDI: Tulikuwa tunafika maeneo mbalimbali.

MALLYA: Kwa siku ya kwanza Pasua mlienda saa ngapi?

SHAHIDI: Majira ya alasiri.

MALLYA: Ambapo exactly mlipoanzia ni wapi?

SHAHIDI: Rau Madukani.

MALLYA: Kutoka Rau kwenda Moshi Police Central ni umbali wa kilomita ngapi?

SHAHIDI: Siwezi kukadiria.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji naomba jibu lake lirekodiwe.

MALLYA: Kutoka Rau kwenda KCMC mlitumia muda gani?

SHAHIDI: Dakika 15.

MALLYA: Kutoka Rau kwenda Moshi Police Central ni umbali wa kilomita ngapi? Baada ya KCMC mlienda wapi?

SHAHIDI: Tulirudi mpaka Majengo.

MALLYA: Kutoka Rau kwenda Moshi Police Central ni umbali wa kilomita ngapi? Unaweza kukadiria kama muda gani?

SHAHIDI: Kwa sababu hatukuwa na mwendo sana tulitumia walau dakika 45.

MALLYA: Moja ya tunachojivunia Wachagga Moshi haina foleni, ila endelea tu kujibu.

MALLYA: Baada ya Majengo mlienda wapi?

SHAHIDI: Tukaenda Pasua.

MALLYA: Miye napajua kote.

MALLYA: Mlitumia muda gani kutoka Majengo kwenda Pasua?

SHAHIDI: Sikumbuki muda exactly. Nilikuwa siangalii muda.

MALLYA: Ulikuwa ni muda gani?

SHAHIDI: Ulikuwa muda wa jioni.

MALLYA: Baada ya kutoka Pasua mkaenda wapi?

SHAHIDI: Machame, Aishi Hotel.

MALLYA: Aishi ni kitu gani? Kijiji, kata au wapi?

SHAHIDI: Ni hotel.

MALLYA: Ulipofika Aishi mkafika maeneo gani?

SHAHIDI: Kingai aliingia kama anaingia ndani.

MALLYA: Kwa hiyo ni ushahidi wako kwamba Kingai aliingia ndani?

SHAHIDI: Hakuingia ndani alielekeza sehemu ya majengo.

MALLYA: Unaweza kutuchorea picha ya eneo la Aishi Hotel?

SHAHIDI: Siwezi kuchora sababu sikushuka kwenye gari.

MALLYA: Baada ya Aishi Hotel mkaenda wapi?

SHAHIDI: Tukielekea maeneo ya Boma Ng’ombe.

SHAHIDI: Mlitumia muda gani kufika Boma Ng’ombe?

SHAHIDI: Siwezi kujua muda niliotumia. Kikubwa tulichokuwa tunakifanya ni kufanikisha kazi yetu.

MALLYA: Baada ya Boma Ng’ombe mlienda wapi?

SHAHIDI: Mbele ya Boma Ng’ombe kama unaenda Arusha.

SHAHIDI: Tulifika maeneo ambayo tulihisi kwamba tungeweza kuwakuta.

MALLYA: Kwa hiyo wewe ulikuwa unajiongeza kwenda sehemu zingine ambazo watuhumiwa hawajakutajia?

SHAHIDI: Ni sahihi.

MALLYA: Kwa hiyo siyo lazima uende na watuhumiwa kwa sababu ulikuwa ukitajiwa sehemu A unaweza kwenda sehemu B?

SHAHIDI: Watuhumiwa walikuwa wanatusaidia na pia tulikuwa hatumjui.

MALLYA: Baada ya Boma mlienda wapi?

SHAHIDI: Tulirudi Moshi.

MALLYA: Palikuwa na mwanga na au giza?

SHAHIDI: Palikuwa pameshaanza giza.

MALLYA: Kwa makadirio yako kutoka Boma mpaka Moshi ni kilometa ngapi hivi?

SHAHIDI: Inaweza ikawa kilometa 50 au zaidi.

MALLYA: Nilikusikia unasema mlifika Moshi saa tano usiku.

SHAHIDI: Saa nne kwenda saa tano.

MALLYA: Ulipata kueleza kwamba kilichokufanya usiandike maelezo muda huo ni nini?

SHAHIDI: Nilishaeleza.

MALLYA: Hivi Mbowe ulifika kumhoji saa ngapi za usiku vile…?

JAJI: Suala la maelezo ya Mbowe havipo katika kesi ndogo.

MALLYA: Naomba nimuachie mwenzangu amallizie kuuliza machache.

(Anaamka wakili Paul Kaunda).

Kaunda: Ulisema ulipomkamata mshitakiwa wa tatu ulimpeleka Central Police?

SHAHIDI: Nili fikisha kituoni.

Kaunda: Wakati huo mlishafungua kesi ya madawa ya kulevya?

SHAHIDI: Ndiyo. Unga unaodhaniwa kuwa madawa ya kulevya.

Kaunda: Wakati huo uliwaacha kwenye gari muda wao wote wakiwa na pingu mikononi.

SHAHIDI: Ndiyo.

Kaunda: Hukuiambia Mahakama kwamba ulipowarudisha uliwafungulia pingu.

SHAHIDI: Ndiyo. Sikusema.

Kaunda: Na hukusema Mahakamani kwamba uliwakabidhi askari gani wa chumba cha mashitaka kwa majina yao na force number zao.

SHAHIDI: Sikuongozwa kusema hivyo.

Kaunda: Na wala hujui kilichotokea kuanzia muda unawakabidhi watuhumiwa muda ule usiku mpaka asubuhi.

SHAHIDI: Sahihi.

(Anaingia wakili Frederick Kihwelo)

KIHWELO: Ni sahihi kwamba wewe ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru?

SHAHIDI: Nisahihi.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba wewe kazi yako kuwasimamia kazi askari wa chini yako?

SHAHIDI: Sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba Jeshi la Polisi limewafukuza askari wanne na wasaidizi wa polisi wawili wamesimamishwa?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi wewe ni mmoja wa Polisi wasaidizi waliosimamishwa kazi Arumeru?

SHAHIDI: Ni Masuala ya kiutawala siyo kesi hii.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba Mohammed Ling’wenya mlimtafuta kupitia mitandao ya simu?

SHAHIDI: Siyo sahihi.

KIHWELO: Akitokea mtu akasema kwamba Boazi alitoa malekezo ya watuhumiwa kuletwa Dar es Salaam siku ile ile ya Dar es Salaam, Je kati yake na wewe nani atakuwa mwongo?

SHAHIDI: Siwezi kumsemea mtu mwingine.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba watuhumiwa hawakupokelewa kituoni Moshi?

SHAHIDI: Hakuna utaratibu wa kupokelewa bali kuna sehemu ya kuandika kuwakabidhi watuhumiwa.

KIHWELO: Ni sahihi hapa Mahakamani hapa kuna nyaraka ya kukabidhi watuhumiwa?

SHAHIDI: Siwezi kulisemea.

KIHWELO: Nitakuwa sahihi nikisema watuhumiwa waliingizwa Kituo cha Polisi Moshi Kwa dhumuni la kuwatesa?

SHAHIDI: Utakuwa haupo sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi hukusaini Detention Register wakati unawakabidhi watuhumiwa Kituo cha Polisi Moshi?

SHAHIDI: Ni sahihi.

KIHWELO: Ni sahihi kwamba watuhumiwa mliowakamata hawakuwa wenyeji wa Moshi?

SHAHIDI: Hakuwa wenyeji wa Moshi.

KIHWELO: Nitakuwa sahihi nikisema mlikuwa mnapoteza muda kuwatembeza watuhumiwa ambao hawakuwa wenyeji wa Moshi?

SHAHIDI: Hautokuwa sahihi.

KIHWELO: Una nyaraka yoyote inayoonyesha kwamba mlipata break down Njia Panda Himo?

SHAHIDI: Sina kwa sababu magari ya Serikali ya utaratibu wake.

KIHWELO: Akitokea mtu akasema kwamba Central Police Dar es Salaam siyo sehemu ya kuhifadhi watuhumiwa wa ugaidi atakuwa sahihi?

SHAHIDI: Sijui hilo.

KIHWELO: Akitokea mtu akasema walipotoka Moshi walifikia Kituo cha Polisi Tazara ambao watuhumiwa wa ugaidi huhifadhiwa?

SHAHIDI: Mimi ndiyo nilikuwa na watuhumiwa. Sikwenda huko.

KIHWELO: Ni hayo tu.

JAJI: Ingekuwa inaruhusiwa ningekupigia makofi, ila upo Mahakamani. Umetumia muda vizuri.

JAJI: Kibatala muda utakutosha?

KIBATALA: Nitajitahidi.

KIBATALA: Shahidi unafahamu kwamba ugaidi ni kesi kubwa sana?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Je, ulichukua maelezo kwa kifungu cha 57(3)?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba kifungu hicho kinakuruhusu kuchukua record ya video au sauti wakati anakiri?

SHAHIDI: Siyo lazima kutumia hiyo.

KIBATALA: Sasa ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba palikuwa na fursa hiyo ya kisheria lakini hukutumia kwa sababu fulani?

SHAHIDI: Si kumwambia.

KIBATALA: Unafahamu kwamba mtu anapokiri makosa yake kuna haitaji la kumpeleka kwa Mlinzi wa Amani?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Unafahamu kwa mujibu wa maelekezo ya Jaji Mkuu kwamba mtu anapopelekwa kwa Mlinzi wa Amani kwanza anatakiwa kumkagua mtuhumiwa kama ana majeraha?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Je, Mohammed Ling’wenya alipelekwa kwa Mlinzi wa Amani?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Na unafahamu kwamba kukiri kwa Mohammed Ling’wenya kulipaswa kupelekwa kwa Mlinzi wa Amani?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Unafahamu na hukumpeleka?

KIBATALA: Je, ulimpeleka Mohammed Ling’wenya kwa daktati kuona kama alikuwa na majeraha?

SHAHIDI: Hilo sina jibu.

KIBATALA: Uliwaza kumpeleka mtuhumiwa kwa daktari kuthibitisha kwamba hana majeraha?

SHAHIDI: Siyo taratibu zangu za kazi.

KIBATALA: Kuna sehemu kwenye CPA au PGO inakataza wewe kumpeleka mtuhumiwa kwa daktari kwa ajili ya kujiridhisha?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Ili tuone kama kweli hamkuwa mmetumia muda huo kuwatesa, je dada wa Moses Lijenje unamfahamu jina lake?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Maelezo yako ya kuharibikiwa gari Himo kwenye maelezo yako uliandika au hukuandika?

SHAHIDI: Sikuandika.

KIBATALA: Watuhumiwa wanasema mlipowatoa Moshi mliwapeleke watuhumiwa Tazara kisha Mbweni. Je, sababu za kuwahamisha ni za kiupelelezi au kiusalama?

SHAHIDI: Zote zote.

KIBATALA: Tuanze na suala la upelelezo. Kama Mohammed Ling’wenya ameshakiri tayari uliogopa nini?

SHAHIDI: Taarifa kutoka nje, kuna wengine tulikuwa tunawatafuta.

KIBATALA: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba walipokuwa Central walikuwa in isolation na watuhumiwa wengine?

SHAHIDI: Sikumwambia.

KIBATALA: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba ulipowapeleka Mbweni kwamba waliwekwa in isolation na watuhumiwa wengine?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Je, kupima ukweli wenu, ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba ulimwambia Mkuu wa Kituo au OCD kwamba watuhumiwa watengwe?

SHAHIDI: Sikumwambia.

KIBATALA: Nimesikia umesema kwamba sababu ya kuwahamisha watuhumiwa kutoka Central Dar es Salaam kwenda Mbweni ni kwamba watuhumiwa walipo Dar es Salaam wasijue kinachoendelea. Je, Mbweni ni Mkoa gani?

SHAHIDI: Ni Dar es Salaam.

KIBATALA: Unamfahamu Afisa wa Jeshi anaitwa Chuma Chugulu?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama kule Arusha kuna washitakiwa wa ugaidi au hawapo.

SHAHIDI: Wapo wapi?

KIBATALA: Gereza la Kisongo. Masheikh.

SHAHIDI: Wapo.

KIBATALA: Maelezo yao yalichukuliwa Dar es Salaam?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, kuna kifungu chochote cha Sheria ya Mwenendo Wa Makosa ya Jinai na PGO inayolazimisha mtuhumiwa achukuliwe maelezo sehemu tu ambapo faili lilifunguliwa?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Na ulijua kwamba shauri hili litafika Mahakamani?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Na wewe kama Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru (OC-CID), jukumu lako ni kufunga mianya yote ya kuharibu kesi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji kama kuna sehemu yoyote ambayo umeonyeshwa kwamba kama angekuwa tayari ningempa simu yake au simu yangu awasiliane na ndugu, jamaa na marafiki.

SHAHIDI: Sikusema.

KIBATALA: Kule Moshi, nakuuliza kuhusu ufahamu wa kuingia na kutoka Polisi Central Police.

SHAHIDI: Nafahamu kwa sababu nilisaini.

KIBATALA: Wewe ndiye uliyemuingiza Mohammed Ling’wenya na kumtoa mahabusu Moshi?

SHAHIDI: Nilikuwa na Afande Mahita.

JAJI: (Anamwambia Kibatala) Liweke vizuri hilo swali.

KIBATALA: Una taarifa sahihi kuhusu Detention Register. Je, uli- sign out saa ngapi?

SHAHIDI: Tarehe sita Agosti 2010 saa 11 alfajiri.

KIBATALA: Kati yako wewe na Mahita nani alikuwa Custodian Officer wa Mohammed Ling’wenya?

SHAHIDI: Mimi mwenyewe.

KIBATALA: Aliyekimkabidhi Mohammed Ling’wenya pale CRO central?

SHAHIDI: Mimi.

KIBATALA: Kingai alikuwepo wakati mnawakabidhi Polisi Central Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ndiyo alikuwepo. Lakini ……

KIBATALA: Hakuna cha lakini.

KIBATALA: Wakati unahojiwa na wenzangu ulisema kwamba DCI Boazi aliwaambia kwamba watuhumiwa tuwapeleke Moshi.

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Una personal knowledge ya malekezo ya DCI au Kingai ndiye anayejua?

(Shahidi anakaa kimya).

KIBATALA: Naomba niishie hapo Mheshimiwa Jaji

JAJI: Serikali?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Asante Mheshimiwa Jaji.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi umeulizwa swali kuhusiana na kutosema kwenye ushahidi wako kama hukusema kama ulimpa simu. Kwa nini hukusema?

KIBATALA: Objection! Kwani siyo swali nililouliza.

JAJI: Swali halijaingia kwenye record za Mahakama.

SHAHIDI: Kama angeomba mtu aje, utaratibu ungefanyika na simu ingepatikana.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa kuhusu watuhumiwa kutemgenishwa Central na kule Mbweni, ukasema hukusema kwenye ushahidi wako.

SHAHIDI: Mahabusu wanatenganishwa …..

MTOBESYA: Objection! Kuna mpaka kwenye ufafanuzi. It’s not an open check.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea kwanini hukusema kama mliwatenga?

SHAHIDI: Kwa sababu anayeweza kujua watuhumiwa wamekaaje huko lock up ni mtu wa chumba cha lock up.

WAKILI WA SERIKALI: Ukaulizwa swali ulikiri kwamba mtuhumiwa anayekiri anatakiwa kupelekwa kwa Mlinzi wa Amani. Ukaulizwa ulimpeleka kwa Mlinzi wa Amani ukasema hapana. Ni kwanini?

SHAHIDI: Hatukumpeleka kwa Mlinzi wa Amani, kwa sababu tulikuwa tunawahi kuhakikisha hivyo vitendo vya kigaidi havifanyiki.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa swali na Mtobesya kwamba kama ulikuwa na taarifa za awali ukasema hukuwa na taarifa.

SHAHIDI: Nilikuwa na taarifa za awali. Siyo aza kina wakati namkamata mtuhumiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji tunaomba tukomee hapa.

JAJI: Shahidi tunakushukuru kwa ushahidi wako kwenye kesi ndogo.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji tunaomba ahirisho mpaka kesho tarehe 12 mwezi wa 11, 2021

WAKILI WA SERIKALI: Ilituendelee na shahidi mwingine na ili tuweze kujiandaa. Tunaomba kesi ianze saa nne asubuhi.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji hatuna pingamizi.

JAJI: Nawaombamawakili wa pande zote mbili mtunze muda . Tunaposema saa nne na iwe ni saa nne kweli.

Mawakili wa pande zote mbili wanakubaliana na Jaji

JAJI: Maombi ya ahirisho yamekubaliwa. Kwa hiyo naahirisha mpaka tarehe 12 mwezi wa 11 2021. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka kesho asubuhi saa nne asubuhi.

Jaji anaondoka mahakamani.

Like
1