Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo tarehe 4 Februari 2022.
Wakili wa Serikali (Robert Kidando) Ikupendeze Mheshimiwa Jaji naitwa Robert Kidando na nipo pamoja na wakili
- Abdallah Chavula
- Jenitreza Kitali
- Nassoro Katuga
- Esther Martin
- Ignasi Mwinuka na
- Tulimanywa Majige
Wakili Peter KIBATALA: Mheshimiwa Jaji ikupendeza naitwa Peter Kibatala nipo pamoja
- Michael Mwangasa
- Gaston Garubindi
- Michael Lugina
- Sisty Aloyce
- Iddi Msawanga
- Maria Mushi
- Evaresta Kisanga
- Hadija Aron
- Dickson Matata
- John Malya
- Nashon Nkungu
KIBATALA: Kwa nafasi ya pekee naomba kumtambulisha Wakili Alute Mughwai Lissu, pamoja Kwamba hayupo katika quorum yetu, lakini ni mgeni wetu wa pekee leo.
Wakili Alute Mughwai Lissu: Mheshimiwa Jaji kwa nafasi ya pekee nashukuru kuwepo mahala hapa na kusikiliza shauri hili.
JAJI: Karibu sana.
(Jaji anawaita washitakiwa wote wanne na wote wanaitika wapo Mahakamani).
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, shauri limekuja kwa ajili ya kusikilizwa na leo tuna shahidi mmoja. Tupo tayari kuendelea.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji na sisi pia tupo tayari kuendelea.
JAJI: atakuwa shahidi wa ngapi?
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji ni shahidi wa 13.
JAJI: (Shahidi) majina yako?
SHAHIDI: Naitwa Tumaini Sosthenes Swila.
JAJI: Umri wako?
SHAHIDI: Miaka 46.
JAJI: Kabila lako?
SHAHIDI: Mndali.
JAJI: Dini yako?
SHAHIDI: Mkristo.
JAJI: Kazi yako?
SHAHIDI: Askari Polisi. Naapa mbele ya Mahakama hii kuwa ushahidi nitakaotoa utakuwa wa kweli. kweli tupu, Ee Mwenyezi Mungu nisaidie.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Shahidi Unasema Unaitwa nani?
SHAHIDI: Tumaini Sostenes Swila.
WAKILI WA SERIKALI: Unafanya kazi gani?
SHAHIDI: Ni askari polisi.
WAKILI WA SERIKALI: Una cheo gani?
SHAHIDI: Ni Mkaguzi wa Polisi.
WAKILI WA SERIKALI: Kituo chako cha kazi?
SHAHIDI: Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke.
WAKILI WA SERIKALI: Majukumu yako ni yapi?
SHAHIDI: Ni kuzuia, kukamata, na kupeleleza makosa ya jinai.
WAKILI WA SERIKALI: Kazi hiyo sasa umefanya kwa muda gani?
SHAHIDI: Miaka 24.
WAKILI WA SERIKALI: Katika shughuli hiyo ya upelelezi, kitu gani hasa unafanya?
SHAHIDI: Shughuli mbalimbali katika upelelezi, ikiwamo kukagua eneo la tukio, kuchora eneo la tukio, kukusanya vielelezo. Kuhoji mashahidi, kukamata watuhumiwa, kuwahoji watuhumiwa, kuandaa barua mbalimbali za kuomba uchunguzi wa vielelezo, kupeleka vielelezo maabara, kuchukua maandishi ya sampuli za watuhumiwa, kuandaa taarifa za wapelelezi, kusimamia gwaride la utambuzi wa watuhumiwa, kuwafikisha watuhumiwa mahakamani ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi Mahakamani.
WAKILI WA SERIKALI: Umesema umekuwa katika upelelezi kwa miaka mingapi?
SHAHIDI: 24.
WAKILI WA SERIKALI: Taaluma ya upelelezi umepataje?
SHAHIDI: Kwa kuhudhuria kozi mbalimbali pamoja na uzoefu kazini.
WAKILI WA SERIKALI: Unasema uko Mkoa wa Kipolisi Temeke, Ofisi ya RCO, elezea upo kwa muda gani katika kituo hicho cha kazi?
SHAHIDI: Nipo tangu Oktoba 2015. Lakini ulipofika mwezi Januari mwaka 2020 nilipata uhamishoni wa muda kwenda Makao Makuu ya Upelelezi, Jijini Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupata uhamishoni huo wa muda, ieleze Mahakama ulikaa kwa muda gani.
SHAHIDI: Nilianza kufanya kazi Ofisi ya Makao Mkuu ya Upelelezi toka Januari 2020 mpaka Agosti 2021 nikarudi kituo changu cha kazi.
WAKILI WA SERIKALI: Nini kilitokea mpaka ukarudi kituo chako cha awali?
SHAHIDI: Kama nilivyosema kwamba nilipata uhamishoni wa muda. Ulipofika muda huo nilitakiwa nirudi katika kituo changu cha kazi.
WAKILI WA SERIKALI: Na wakati unapata uhamishoni wa muda, kwenda Ofisi Ndogo ya Upelelezi, ni shughuli gani ulikuwa unafanya?
SHAHIDI: Nilikuwa nafanya kazi katika kitengo X.
JAJI: Rudia. Kitengo gani?
SHAHIDI: Kitengo X.
JAJI: Unaweza ku- spell?
SHAHIDI: X ya herufi.
WAKILI WA SERIKALI: Kitengo X kinajishughulisha na nini?
SHAHIDI: Makosa yanayotishia usalama wa nchi pamoja na ustawi wa Taifa.
WAKILI WA SERIKALI: Katika makosa yanayotishia usalama na ustawi wa nchi, kitu gani kinafanyika haswa?
SHAHIDI: Kinahusika na makosa yanayotishia usalama wa nchi nzima.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa ukiwa hapo ulikuwa na nafasi gani?
SHAHIDI: Nilikuwa naendelea na upelelezi pamoja na makosa mengine.
WAKILI WA SERIKALI: Hebu elezea mnamo tarehe 14 Julai 2020 ulikuwa wapi na unafanya nini?
SHAHIDI: Nilikuwa katika ofisi za Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, ofisi ndogo za Dar es Salaam, nikiendelea na majukumu yangu. Ndipo nilipopokea simu kutoka kwa Katibu muhtasi kutoka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, akitaka nifike katika ofisi ya mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini. Wakati huo alikuwa Afande Robert Boaz.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupokea wito huo ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilienda moja kwa moja mpaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini, nikawakuta Afande Robert Boaz na Ramadhan Kingai.
WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa muda gani?
SHAHIDI: Majira ya saa nne asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Ulichukua muda gani kufika.
SHAHIDI: Ilikuwa kama dakika 15 kufika ofisi Ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kukuta DCI pamoja na Kingai nini kiliendelea?
SHAHIDI: Baada ya kuwakuta pamoja Kamishina Robert Boaz wakati huo akiwa DCI alinitaka kupokea maelekezo kutoka kwa Afande Ramadhan Kingai ambaye ni Kamishina Msaidizi wa Polisi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa DCI kukwambia upokee maelekezo hayo nini kiliendelea?
SHAHIDI: Baada ya kupokea maelekezo hayo tukitoka pamoja na Afande Ramadhan Kingai Kamishina wa Polisi, ofisini kwangu, akanipa maelekezo ya kufungua jalada la uchunguzi. Maelekezo hayo alinipa yakiwa tayari yameandikwa katika karatasi.
SHAHIDI: Yalikuwa yanaeleza kuwa mnamo tarehe 14 Julai 2020 majira ya saa 2:30 asubuhi, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Robert Boaz, Kamishina Msaidizi wa Polisi alipokea taarifa kutoka Kwa Luten Dennis Urio, juu ya uwepo wa kundi linaloratibiwa na Freeman Aikael Mbowe la kutaka kufanya vitendo vya uhalifu ambavyo ni kulipua vituo vya kuuzia mafuta, kuchoma masoko moto pamoja na maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi, kukata miti mikubwa katika Barabara Kuu kwa lengo la kuzuia magari yasipite, kufanya maandamano nchi nzima yasiyokuwa na ukomo, na kuwadhuru viongozi mbalimbali wa Serikali lengo la kuleta taharuki nchini kufanya nchi isitawalike.
WAKILI WA SERIKALI: Endelea kuilezea hiyo taarifa.
SHAHIDI: Na matendo hayo yalipangwa kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha na Kilimanjaro.
WAKILI WA SERIKALI: Endelea kueleza kilichotokea baina yako na Kingai.
SHAHIDI: Baada ya kupokea maelekezo hayo alinitaka nifungie jalada kisha nipeleke Ofisi ya DCI. Nilienda moja kwa moja katika ofisi inayohusika na kitabu cha kufungua majalada, Ofisi ya Mnadhimu, ambapo nilienda na kuchukua kitabu hicho na kufungua jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba CD HQ/PE/60/2020.
WAKILI WA SERIKALI: Elezea hizo taratibu za kufungua hilo jalada baada ya kuchukua hichi kitabu.
SHAHIDI: Kitabu kile kinaonyesha tarehe ya kifungua, muda, jina la mlalamikaji na taarifa yenyewe.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati unafungua jalada hilo, mlalamikaji alikuwa nani?
SHAHIDI: Mlalamikaji alikuwa Afande Robert Boaz, Kamishina wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini.
WAKILI WA SERIKALI: Nani alikuwa analalamikiwa?
SHAHIDI: Mlalamikiwa katika jhilo alikuwa ni Freeman Aikael Mbowe.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umefungua jalada hilo, ulifanya nini?
SHAHIDI: Baada ya kufungua jalada hilo, niliweza kuandika minutes kwenda kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, nikimjulisha kuwa nimefungua jalada la uchunguzi dhidi ya Freeman Mbowe, kwa kutaka kufanya vitendo vya uhalifu, kama ambavyo nimevitaja hapo juu, nikaandika naleta jalada kwako kwa maelekezo zaidi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umeandika hiyo minutes ulifanya nini sasa na hilo jalada?
SHAHIDI: Nilienda moja kwa moja mpaka ofisini kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupeleka jalada hilo nini kilifuata?
SHAHIDI: Siku ya tarehe 15 Julai 2020 saa 5 asubuhi nikiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, nilikabidhiwa jalada hilo la uchunguzi ambalo kumbukumbu namba zake nilizitaja ambalo lilikuwa limetolewa maelekezo na Robert Boaz, Kamishina wa Polisi na DCI akinitaka nimsaidie Kamishina Msaidizi wa Polisi Ramadhan Kingai Kufanya upelelezi, ambaye wakati huo alikuwa ni RCO wa Arusha.
WAKILI WA SERIKALI: Maelekezo yaliyolewa kwenda kwa nani?
SHAHIDI: Maelekezo yalitolewa kwemda kwa Ramadhan Kingai, Kamishina Msaidizi wa Polisi pamoja na mimi kumsaidia upelelezi.
WAKILI WA SERIKALI: Hayo maelekezo ya kumsaidia ACP Kingai yalikuwa ni maelekezo gani?
SHAHIDI: Yalikuwa ni maelekezo ya kutaka ACP Kingai kuendelea kuwasiliana na mtoa taarifa ili aweze kumtafutia watu ambao walikuwa wanahitajika na Freeman Mbowe katika kutenda vitendo hivyo. Maelekezo yalikuwa pia kuwa alikutana nao watu hao, awape tahadhari ya vitendo ambavyo wataenda kukutana navyo huko.
WAKILI WA SERIKALI: Dhumuni hasa la maelekezo hayo yalikuwa ni nini?
SHAHIDI: Ilikuwa ni kupata taarifa na kuwajua watu wanaoshirikiana na Freeman Mbowe, na pia watu ambao watakuwa wamepatikana kutoka kwa Luten Dennis Urio afikishwe kwa ACP Ramadhan Kingai kisha na yeye afikishe kwa DCI.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya kuwa umepewa jalada na maelekezo hayo ulifanya nini?
SHAHIDI: Niliwasiliana kwa simu na ACP Ramadhan Kingai ambaye kwa wakati huo alikuwa Arusha. Baada ya kumjulisha alisema nilihifadhi jalada hilo nitakupa maelekezo.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya sasa kuwau umemjulisha ACP Kingai, nini kiliendelea katika ushauri huo?
SHAHIDI: Baada ya kuwasiliana na ACP Kingai na kumjulisha maelekezo ambayo yapo katika jalada na yeye kuniambia kuwa nihifadhi, niliweza kuandika taarifa ya kukiri kupokea, kisha nikahifadhi jalada hilo katika kabati langu la chuma ambapo natumia kuhifadhi vifaa vyangu vya kazi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya mawasiliano hayo na Kingai nini kiliendelea?
SHAHIDI: Tarehe 18 Julai 2020 nikiwa naendelea na majukumu yangu katika ofisi ndogo ya DCI nilipokea simu kutoka kwa Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi, akinijulisha kuwa Luteni Dennis Urio tayari amepata vijana wa kuwapeleka kwa Freeman Aikael Mbowe.
SHAHIDI: Na akanitaka niende kufungua jalada la kesi katika kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Unamaanisha nini ukisema kufungua jalada la kesi?
SHAHIDI: Ni jalada ambalo linafunguliwa katika Report Book tofauti na lile jalada la upelelezi na linalofunguliwa katika vituo vya polisi.
SHAHIDI: Pia alinielekeza baada ya kufungua jalada hilo niongee na Mkuu Upelelezi Mkoa wa Polisi wa Ilala aweze kuhamisha jalada hilo ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini.
WAKILI WA SERIKALI: Wewe ukafanya nini?
SHAHIDI: Niliweza kwenda kufungua jalada hilo kama nilivyoelekezwa na ACP Kingai, nikafungua jalada la kutaka kula njama za kutenda vitendo vya kigaidi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupokea maelekezo hayo shughuli hiyo uliweza kuitekelezaje?
SHAHIDI: Niliweza kufika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, nikafungua jalada hilo. Mlalamikaji ni Robert Boaz Kamishina wa Polisi. Jalada hilo alinielekeza kufungua kuwa kati ya mwezi Mei na Julai 2020 kuna kundi la watu wamepanga kufanya vitendo vya kigaidi katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kuleta taharuki.
SHAHIDI: Aidha nilifungua taarifa hiyo kufuatia maelezo ya ACP Kingai ambaye alitaka nisiandike jina la mtuhumiwa Freeman Aikael Mbowe katika taarifa hiyo ili kuepusha uvujaji wa taarifa kwani kama jina lake lingekwepo katika taarifa hiyo angeweza kujua na kusitisha utejelezaji wa alilokuwa amepanga pamoja na wenzake.
WAKILI WA SERIKALI: Kitu gani kingine kiliendelea?
SHAHIDI: Baada ya jalada kufunguliwa ambapo lilikuwa na kumbukumbu namba CD/IR /2097 /2020, nilimjulisha ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala ambapo wakati huo alikuwa Fadhil Bakari.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya kumjulisha ACP Fadhil Bakari nini kiliendelea?
SHAHIDI: Niliondoka na kuendelea na kazi zingine.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa elezea baada ya siku ya tarehe 18 Julai 2020. Nini kiliendelea?
SHAHIDI: Tarehe 27 Julai 2020 nikiwa ofisi ndogo ya upelelezi Dar es Salaam nilipokea Jalada lenye kumbukumbu namba CD/IR/2097/2020 kosa kula njama za kutaka kufanya vitendo vya kigaidi. Jalada hilo lilikuwa limetolewa maelekezo na Afande Robert Boaz Kamishina wa Polisi na Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai nchini akitoa maelekezo kwa Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi pamoja na mimi akitutaka tuendelee na upelelezi wa kosa hilo.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa kitu gani Kingine kiliendelea?
SHAHIDI: Niliweza kumjulisha Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi, kuwa nimepokea kwa niaba yako jalada. Na mimi ni msaidizi wako katika upelelezi wa jalada hilo.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumjulisha Kingai nini hasa kiliendelea?
SHAHIDI: aliniambia kuwa yeye anaendelea na ufuatiliaji wa mtoa taarifa na atanipa maelekezo ya nini cha kufanya.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya hapo sasa, kitu gani hasa kiliendelea katika jalada hili?
SHAHIDI: Nilikiri kupokea jalada hilo kisha nikalitunza katika kabati langu la chuma. Ilipo fika tarehe 6 Agosti 2020, mimi nikiwa hapa Dar es Salaam majira ya saa 2 usiku, nilipokea simu kutoka kwa Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi akinijulisha kwamba tayari wamekamatwa watuhumiwa wawili na wapo njiani kuja nao Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na upelelezi zaidi. Akaniambia akifika atanijulisha.
WAKILI WA SERIKALI: Baada sasa ya kukupa taarifa hiyo, elezea kama alikufahamisha kuhusu watuhumiwa hao wamekamatwa wapi na ni akina nani.
SHAHIDI: Alichokisema ni kwamba amekamata watuhumiwa wawili katika mji wa Moshi. Hakuniambia majina.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya ACP Kingai kukupa taarifa hiyo?
SHAHIDI: Ilipofika tarehe 7 Agosti 2020 majira ya kati ya saa 11 na saa 12 alfajiri nilipigiwa simu na Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi akinitaka nikutane naye Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam mapema saa moja asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji. Samahani kabla ya kuendelea kuna jambo moja naomba tukutane faragha na wenzetu kuhusu mwenendo wa kesi.
KIBATALA: Sawa Mheshimiwa Jaji.
JAJI: Kwa muda gani?
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Kwa dakika 10 mpaka 15 hivi.
JAJI: Sawa.
Jaji anaondoka kwenye chumba cha mahakama.
Kwa hali ninayoiona hapa mahakamani, si ajabu wakatuambia leo kuwa kesi imefikia mwisho, kwamba Jamhuri hawana nia nayo tena. Labda wakati wakiendelea kumhoji huyo shahidi michongo imeletwa taarifa ya DPP na huenda ndiyo wamekwenda kuijadili.
Saa 5:32 Jaji amesharejea mahakamani kuendelea na kesi.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, kwa upande wa Jamhuri tupo tayari kuendelea.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, na sisi tupo tayari kuendelea.
JAJI: Sehemu ya mwishoni alisema alieleza kufika kituo cha Kati kati ya saa 11 na 12 asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupokea maelekezo hayo wewe ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilijiandaa kwenda Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam ambapo nilifika kabla ya saa moja asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Ulipofika hapo ulifanya nini?
SHAHIDI: Niliweza kumkuta Afande Ramadhan, Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi akiwa pamoja na askari wawili ambao siwafahamu na mmoja nilikuwa namfahamu ambaye ni ASP Jumanne Malanghe. Wale wawili nilikuja kuwafahamu baadaye ambao ni Inspector Mahita na Constable Goodluck.
WAKILI WA SERIKALI: Na unasema ulimkuta ACP Kingai na ASP Jumanne. Hivi ASP Jumanne yeye ulimfahamu vipi?
SHAHIDI: ASP Jumanne nilimfahamu zaidi ya miaka 10 wakati akiwa anafanya kazi mkoa wa Pwani.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa hawa akina ACP Kingai na ASP Jumanne uliwakuta sehemu gani pale kituo cha Polisi?
SHAHIDI: Niliwakuta nje ya Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, ambapo Afande Kingai alinitaka nipokee simu mbili kutoka kwa Goodluck ambapo zilikamatwa kutoka Moshi kwa watuhumiwa.
SHAHIDI: Nilipokea simu mbili, moja aina ya Itel nyeusi na nyingine ni Tecno nyeusi pia.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuzipokea ikafuata nini baada ya kukabidhiwa?
SHAHIDI: Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi alinitaka pia nikabidhiwe maelezo ya mashahidi yaliyoandikwa huko Moshi pamoja na hati za kuchukulia mali.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umemkabidhiwa vitu hivyo ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilichukua na kwenda kuvihifadhi katika kabati langu la chuma lililopo katika ofisi ambayo nilikuwa natumia katika Makao Makuu madogo ya upelelezi Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa siku hiyo kitu gani kiliendelea?
SHAHIDI: Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi alinitaka nishirikiane na Inspekta Mahita na DC Goodluck kuhusu watuhumiwa wengine kwa lengo la kuwakamata.
WAKILI WA SERIKALI: Hebu fafanua katika eneo la ufutailiaji.
SHAHIDI: Siku hiyo alituelekeza tumfuatilie mtuhumiwa Khalfani Bwire katika maeneo ambayo taarifa zimeelekeza.
WAKILI WA SERIKALI: Maelekezo hayo walikuwa wamepewa akina nani?
SHAHIDI: Inspekta Mahita na m imi mwenyewe.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya kukuambia kuwa kuna watuhumiwa ambao walikuwa wamekamatwa, hebu elezea ni watuhumiwa gani walikuwa wamekamatwa?
SHAHIDI: Ni Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdilah Ling’wenya ambapo watuhumiwa hao nilikuwa nimekabidhiwa simu zao.
WAKILI WA SERIKALI: Ni wakati gani ulifahamu kuwa watuhumiwa hawa walikamatwa?
SHAHIDI: Ni baada ya kukabidhiwa simu. Kwa Adam mbali na kuwa na simu aina ya Itel, kwenye hati ya kukamatia mali pia ilionyesha amekamatwa na bastola aina ya Luger yenye namba 5340.
WAKILI WA SERIKALI: Rudia tena namba.
SHAHIDI: 5340.
WAKILI WA SERIKALI: Kwa Ling’wenya alikatwa na nini?
SHAHIDI: Simu aina ya Tecno ambayo ilikuwa na rangi nyeusi.
SHAHIDI: Tulifutilia maeneo mbalimbali kulingana na taarifa zilizokuwapo. Ilipofika majira ya saa tano asubuhi, nilipigiwa simu na Afande Jumanne Malangahe wakati huo akiwa Mrakibu wa Polisi walitaka nirudi ili niweze kukabidhiwa maelezo ya watuhumiwa ambao walikuwa wamemaliza kuwahoji yeye na Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi.
WAKILI WA SERIKALI: Elezea sasa Mkiwa na Mahita na Goodluck ni maeneo gani mlifuatilia hizo taarifa.
SHAHIDI: Tulifutilia maeneo ya Sinza, Oysterbay na Coco Beach na baadaye Temeke.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati unapigiwa simu na ASP Jumanne ulikuwa wapi?
Shahidi:Wakati huo nilikuwa maeneo ya Sinza.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kupokea simu ulifanya nini?
SHAHIDI: Mimi na wenzangu tulirudi Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam ambapo ASP Jumanne aliweza kunikabidhi maelezo ya Mohammed Ling’wenya wakati huo ACP Kingai aliweza kunikabidhi maelezo ya Adam Kasekwa.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa maelezo haya ulikabidhiwa ukiwa wapi?
SHAHIDI: Nilikabidhiwa Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umepokea maelezo hayo ya watuhumiwa wawili wewe ulifanya nini?
SHAHIDI: Niliyachukua na kuyapeleka katika ofisi niliyokuwa natumia katika Makao Makuu ndogo ya upelelezi Dar es Salaam na kuhifadhi katika jalada kisha katika kabati la chuma.
WAKILI WA SERIKALI: Ulisema wakati huo ulikuwa ofisi ya DCI Makao Makuu ndogo Dar es Salaam, na umekuwa ukielezea hapa kufuata maelezo Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na vielelezo vingine. Kwanini ilikuwa hivyo?
SHAHIDI: Kwa sababu pale ndipo jalada lilipokuwa limefumguliwa na watuhumiwa walipokuwa wamefikishwa kwa hiyo shughuli nyingi zilikuwa zinafanyikia pale.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umechukua maelezo ya ASP Jumanne na ACP Kingai nini Kiliendelea?
SHAHIDI: Mimi na wenzangu Inspekta Mahita, DC Goodluck tuliendelea na zoezi la kumtafuta Khalfani Bwire kwa kurudi eneo la Sinza.
WAKILI WA SERIKALI: Maeneo gani ambayo mlienda?
SHAHIDI: Temeke tulifika saa 12 jioni.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya hapo nini sasa kiliendelea?
SHAHIDI: Tuliahirisha kuendelea na zoezi hilo mpaka siku inayofuata.
WAKILI WA SERIKALI: Siku inayofuatia ni siku gani?
SHAHIDI: Ni siku ya tarehe 8 Agosti 2020 majira ya saa nne asubuhi, nikiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, nilipigiwa simu na Afande Jumanne Malangahe Mrakibu Msaidizi wa Polisi.
SHAHIDI: Alinitaka nifike kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam kwa ajili ya kazi.
WAKILI WA SERIKALI: Elezea kama ulifanya maelekezo aliyokupa.
SHAHIDI: Nilifika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam muda mfupi nikakuta yupo na Inspekta Mahita na DC Goodluck akanijulisha kuwa amepewa maelekezo na Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi ya kuhamisha watuhumiwa Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya kutoka Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mbweni.
WAKILI WA SERIKALI: Baada sasa ya hapo nini sasa kiliendelea?
SHAHIDI: Tuliwachukua watuhumiwa hao kutoka mahabusu ya Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na kuwasafirisha kwa kutumia gari na kwenda nao kituo cha Polisi Mbweni.
WAKILI WA SERIKALI: Na ulisema maelezo hayo ya kuhamisha watuhumiwa yalikuwa yanahusu watuhumiwa gani?
SHAHIDI: Ni Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Ling’wenya.
WAKILI WA SERIKALI: Mlitumia gari gani?
SHAHIDI: Gari ya Polisi ambayo alikuja nayo Ramadhan Kingai kutoka Mkoa wa Arusha, gari aina ya Fortunner.
WAKILI WA SERIKALI: Kituo cha Polisi Mbweni kipo wapi?
SHAHIDI: Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni na Wilaya ya Kipolisi Kawe.
WAKILI WA SERIKALI: Akina nani wengine walishiriki zoezi hilo?
SHAHIDI: zoezi liliongozwa na ASP Jumanne Malangahe, Inspekta Mahita na Constable Goodluck.
WAKILI WA SERIKALI: Na wewe ulishiriki vipi?
SHAHIDI: Na mimi pia nilishiriki.
WAKILI WA SERIKALI: Iliwachukia muda gani kufika Kituo cha Polisi Mbweni?
SHAHIDI: Ilichukua muda usiozidi saa moja.
(Huyu shahidi wa leo sauti iko chini sana kiasi kwamba kila mara jaji anamtaka aongeze sauti)
WAKILI WA SERIKALI: Kitu gani kingine kiliendelea kule Kituo cha Polisi Mbweni?
SHAHIDI: ASP Jumanne alimwagiza Ispekta Mahita kuwakabidhi watuhumiwa katika chumba cha mashitaka.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwakabidhi watuhumiwa katika chumba cha mashitaka nini kiliendelea?
SHAHIDI: Baada ya kuwakabidhi watuhumiwa hao tuliendelea na zoezi la kutafuta watuhumiwa wengine. Liliongozwa na ASP Jumanne ambapo alikuwa anaendelea kupokea taarifa, akiwepo mtuhumiwa Khalfani Bwire.
WAKILI WA SERIKALI: Zoezi liliendelea kwa namna gani?
SHAHIDI: Tuliendelea kuwatafuta watuhumiwa hao mpaka saa moja usiku.
WAKILI WA SERIKALI: Saa moja usiku nini kilitokea?
SHAHIDI: Samahani Mheshimiwa Jaji nilikuwa naomba kwenda short call. Kuna dawa ninazotumia, kwa hiyo naomba Mahakama inivumilie nitakuwa naenda mara kwa mara.
SHAHIDI: anatoka kwa kusindikizwa na askari Magereza mmoja.
(Shahidi amerejea).
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi ulisema kwamba zoezi la kufuatilia taarifa liliendelea mpaka saa moja jioni. Nini kiliendelea?
SHAHIDI: Ilipofika jioni saa moja, ASP Jumanne alituambia tusitishe zoezi mpaka siku inayofuata.
WAKILI WA SERIKALI: Iliyofuata ni siku gani?
SHAHIDI: Ni tarehe 9 Agosti 2020.
WAKILI WA SERIKALI: Tarehe 9 Agosti 2020 nini kiliendelea?
SHAHIDI: Ilipofika tarehe 9 Agosti 2020 jioni nikiwa katika majukumu mengine, nilipigiwa simu na Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi akinijulisha kuwa amefanikiwa kumkamata Khalfani Bwire akiwa na simu mbili na akanitaka nisiondoke katika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam ili anikabidhi simu za Khalfani Bwire.
WAKILI WA SERIKALI: Nini kiliendelea?
SHAHIDI: Majira ya saa 3:30 nikiwa kwenye Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam Afande Ramadhan Kingai alifika akiwa pamoja na Afande ASP Jumanne Malangahe, Inspekta Mahita na Constable Goodluck. Baada ya kufika alimwagiza Constable Goodluck anikabidhi simu mbili zilizokamatwa kwa Khalfani Bwire.
SHAHIDI: Simu hizo nilizokabidhiwa, simu moja aina ya ‘Bundy’ yenye rangi nyeusi, simu nyingine aina ya Tecno ambayo ni smart phone yenye rangi ya blue na ilikuwa na cover jeusi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kukabidhiwa simu hizo ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilienda kuhifadhi simu hizo ofisini kwangu ndani ya kabati.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa ni shughuli gani nyingine iliendelea?
SHAHIDI: Wakati nakabidhiwa simu hizo, Afande Kingai alinitaka pia niziandikie barua kwenda ofisi y auchunguzi ya Makosa ya Mtandao.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya maelekezo hayo sasa nini hasa kiliendelea?
SHAHIDI: Siku inayofuatia tarehe 10 Agosti 2020, Afande Ramadhan Kingai alinijulisha kuwa tayari amewasiliana na shahidi Luteni Dennis Urio, wa JWTZ ili afike siku inayofuatia kwa ajili ya kuandika maelezo yake.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya ACP Kingai kukupa taarifa hiyo kuhusu tarehe 10 Agosti 2020, nini kiliendelea?
SHAHIDI: Niliweza kuwasiliana na Luteni Dennis Urio kwa njia ya simu, ili aweze kufika kwa ajili ya kuandika maelezo yake.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya mawasiliano hayo nini kiliendelea?
SHAHIDI: Siku inayofuatia tarehe 11 Agosti 2020 Luteni Dennis Urio alifika ofisi ndogo za upelelezi Dar es Salaam ambapo niliweza kuonana naye na kuandika maelezo yake.
WAKILI WA SERIKALI: Alifika muda gani katika hiyo tarehe 11 Agosti 2020?
SHAHIDI: Alifika majira ya asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya Luteni Dennis Urio kufika nini kiliendelea?
SHAHIDI: Niliweza kuandika maelezo yake na aliweza kueleza jinsi alivyopata taarifa.
WAKILI WA SERIKALI: Ongeza sauti.
SHAHIDI: Niliweza kushuka naye na kwenda katika ofisi niiliyokuwa natumia, na niliweza kuchukua maelezo yake.
WAKILI WA SERIKALI: Ulichukua muda gani kuandika maelezo yake?
SHAHIDI: Ilikuwa asubuhi, ulichukua saa nzima.
WAKILI WA SERIKALI: Kitu gani kingine kiliendelea?
SHAHIDI: Wakati naandika maelezo yake alieleza kuwa alikuwa akifanya mawasiliano na Freeman Mbowe kwa kutumia mtandao wa Telegram, na alisema kwamba alikuwa anawasiliana na Freeman Mbowe kwa namba yake ya 0719 933386. Namba ya Freeman Mbowe, pia alinitajia namba zake aliyokuwa anatumia 0787555200.
SHAHIDI: Alinitajia namba yake aliyokuwa anatumia 0787555200 ya mtoa taarifa Dennis Urio, na pia 0754612518 namba ya Dennis Leo Urio. Pia alinitajia namba nyingine ya mtuhumiwa Freeman Mbowe 0784779944.
WAKILI WA SERIKALI: Wewe ulichukua hatua gani sasa?
SHAHIDI: Nilimtaka anikabidhi simu ambazo amekuwa akifanya naye mawasiliano, ambapo aliridhia kunipa simu aina ya Tecno.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini wewe ulitaka akukabidhi simu?
SHAHIDI: Ilikuwa ni kwa ajili ya kwenda kufanya uchunguzi wa kisayansi.
SHAHIDI: Urio alisema mawasiliano yalikuwa kwa Telegram.
WAKILI WA SERIKALI: Wewe ulipotaka yeye akukabidhi simu hiyo, alikuambia nini?
SHAHIDI: Aliridhia lakini akaomba atoe line ambayo alikuwa akifanyia mawasiliano na Freeman Mbowe ambapo angeiwasilisha siku inayofuatia.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya yeye kusema ameridhia na akaomba atoe card ya VodaCom, wewe ulijibu nini?
SHAHIDI: Nilimkubalia, huku nikijua mawasiliano ambayo yanafanyika kwenye Telegram yanabakia kwenye kifaa na siyo sim card.
WAKILI WA SERIKALI: Nini kiliendelea baada ya kumkubalia kutoa ile sim card?
SHAHIDI: Niliandika hati ya makabidhiano, huku nikiandika IMEI namba kwa ajili ya kupokea hiyo simu.
WAKILI WA SERIKALI: Hati hiyo ya makabidhiano ilikuwa na nini?
SHAHIDI: Hati ilikuwa inaonyesha simu nimepokea kwa nani, jina lake, mtu anayemkabidhi pamoja na kuandika IMEI namba zake kwa kuanzia namba 35 na kuishia 040 na IMEI nyingine inaanza namba 35 na kuishia namba 057.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umerekodi vitu hivyo, gani kitu gani kingine ulifanya katika hiyo hati?
SHAHIDI: Hiyo hati nilisaini na niliyemkabidhi naye alisaini.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kusema alikukabidhi simu aina Tecno, je, zile simu nyingine alikuambia zipo wapi?
SHAHIDI: Alisema zipo nyumbani Morogoro na akaahidi kuleta siku inayofuatia.
WAKILI WA SERIKALI: Siku inayofuatia ilikuwa lini?
SHAHIDI: Ilikuwa tarehe 12 Agosti 2020 katika ofisi ndogo ya upelelezi Dar es Salaam. Alifika majira ya asubuhi.
WAKILI WA SERIKALI: Nini kiliendelea?
SHAHIDI: Aliweza kunikabidhi simu tatu Samsung Duos yenye rangi nyeupe, simu nyingine ni simu aina ya Tecno C9 yenye rangi nyeusi, simu nyingine aina ya Itel yenye rangi nyekundu.
WAKILI WA SERIKALI: Haya makabidhiano wewe ulifanya nini?
SHAHIDI: Niliandaa hati ya makabidhiano ya kila simu, nikamsainisha na mimi nikasaini.
WAKILI WA SERIKALI: Hebu elezea Mahakama ni simu ngapi ulipokea kutoka kwa Luteni Dennis Urio.
SHAHIDI: Simu ambazo nilipokea zilikuwa Jumla ya simu nne.
WAKILI WA SERIKALI: Mara baada ya kuzipokea ulifanyia nini?
SHAHIDI: Niliweka Exhibit Lebel PF 143 kwenye kila simu.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini uliziwekea Exhibit Lebel kwa kila simu?
SHAHIDI: Kwa lengo la kuzitofautisha, ili zisiweze kuchanganganyika.
WAKILI WA SERIKALI: Na hiyo PF 143 ilikuwa na nini?
SHAHIDI: Kituo cha kesi ilipofunguliwa, namba ya jalada, tarehe ya kuweka hiyo lebel, jina la mmiliki, kosa, aina ya kielelezo na utambulisho wake.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuviweka Exhibit Lebel PF 145 ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilichukua na kwenda kuvihifadhi katika ofisi ninayotumia na kuhifadhi ndani ya kabati la chuma, ambalo mimi nalitumia.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji bado tunaendelea na cross examination. Kwa ruhusa yako tunaomba break fupi ili tukirejea tuweze kuendelea.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji sisi hatuna pingamizi.
JAJI: Basi tuta- break mpaka saa 7:45 halafu tutarudi kuja kuendelea.
Jaji anaondoka katika chumba cha mahakama.
Jaji amesharejea Mahakamani. Kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe inatajwa tena.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, quorum ya upande wa Jamhuri ipo vile vile kama mwanzo na tupo tayari kuendelea.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji na sisi pia quorum yetu ipo vile vile na tupo tayari kuendelea.
JAJI: Shahidi nakukumbusha ulikuwa chini ya kiapo na utaendelea kuwa chini ya kiapo.
SHAHIDI: Sawa Mheshimiwa Jaji.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Ulikuwa ukiieleza Mahakama jinsi gani ulivyokabidhiwa simu kati ya tarehe 12 Agosti 2020 … Je, ulikuwa na idadi ya simu ngapi mpaka siku hiyo?
SHAHIDI: Mpaka tarehe hiyo ya 12 Agoti 2020 nilikuwa nimeshapokea jumla ya simu nane.
WAKILI WA SERIKALI: Na tukianza na simu hizo, je, ukiziona utaizitambuaje?
SHAHIDI: Nitaiona kwa kutambua jina, rangi pamoja na PF 145 ambayo itaonyesha jina la mmiliki, kosa, namba ya jalada.
WAKILI WA SERIKALI: Unamaanisha nini unaposema kwamba kwenye PF 145 itaonyesha jina la mwenye mali?
SHAHIDI: Katika vielelezo nilivyopokea, simu nne zilitoka kwa shahidi Luteni Dennis Urio na simu nne zilitoka mbili kwa Khalfani Bwire na simu moja moja zilitoka kwa Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya.
WAKILI WA SERIKALI: Na unaposema kwamba Kwenye PF 145 ina majina, je, majina gani hayo.
SHAHIDI: Majina ya watuhumiwa ambayo ni Adam Kasekwa, Khalfani Bwire na Mohamed Ling’wenya.
WAKILI WA SERIKALI: Na vielelezo vingine vina majina ya nani?
SHAHIDI: Vina majina ya Luteni Dennis Urio.
WAKILI WA SERIKALI: Ambae ni nani?
SHAHIDI: Ni shahidi katika shauri hili.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, shahidi ameonyesha uwezo wa kuitambua. Naomba kwa ajili ya kumbukumbu nipatiwe kielelezo namba P28 mpaka kielelezo namba 35.
(Wakili wa Serikali anafungua mfuko wa nailoni wenye vielelezo).
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi angalia vielelezo hivyo kama unavitambua ieleze Mahakama.
(Shahidi anapekua na na kukagua kielelezo kimoja baada ya kingine. Ni kama vile mikono inatetemeka).
WAKILI WA SERIKALI: Elezea sasa kama umevitbua kwa kuanza na tarehe 7 Agosti 2020.
SHAHIDI: Tarehe 7 Agosti 2020 nilipokea simu aina ya Itel ambayo inaonyesha kwenye PF 145 jina la Adam Kasekwa. Namba ya jalada ni CD/IR 2097/2020.
WAKILI WA SERIKALI: Simu aina gani?
SHAHIDI: Simu aina ya Itel.
WAKILI WA SERIKALI: Ulizungumzia kuhusu IMEI.
SHAHIDI: IMEI kwenye simu hii ni 353736820265.
WAKILI WA SERIKALI: Unasema kenda, kenda ni namba gani?
SHAHIDI: Namba tisa (9).
WAKILI WA SERIKALI: Simu nyingine?
SHAHIDI: Ni Simu aina ya Tecno yenye rangi nyeusi, ambayo nimeitambua kupitia Exhibit Lebel ambayo inaonyesha namba ya jalada la CD/IR/2097/2020.
SHAHIDI: Pia imeandikwa aina ya simu.
WAKILI WA SERIKALI: Na inaonyesha simu hiyo imepatikana kwa mtuhumiwa ambaye ni Mohammed Abdillah Ling’wenya.
WAKILI WA SERIKALI: Vipi Kuhusu IMEI namba?
SHAHIDI: IMEI namba imeandikwa ‘IMEFUTIKA’.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji naona shahidi ametambua P 35.
WAKILI WA SERIKALI: Twende kwenye simu za tarehe 9 Agosti 2020.
SHAHIDI: Simu nilizopokea tarehe 9 Agosti 2020 ni mbili ambazo ni za Khalfani Bwire. Simu aina ya Bundy, nimeitambua kupitia lebel namba ambayo inaonyesha namba ya jalada ambayo ni CD/IR/2097/2020. Na simu hii inaonyesha ni aina ya Bundy IMEI namba 359440075933775. Na simu hii ilipatikama maungoni mwa Khalfani Bwire.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji ametambua exhibit P30.
WAKILI WA SERIKALI: Simu nyingine kwa hiyo tarehe 9?
SHAHIDI: Simu nyingine ni simu aina ya Tecno yenye IMEI namba 355019115930845. Simu hii nayo ilipatikana maungoni mwa Khalfani Bwire. Inaonyesha namba ya kesi ambayo ni CD/IR/2097/2020.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji ametambua Exhibit P32.
WAKILI WA SERIKALI: Twende simu uliyokabidhiwa tarehe 11 Agosti 2020.
Shahidi Naitambua simu aina ya Tecno yenye IMEI namba 358721101132040.
WAKILI WA SERIKALI: Imetoka kwa nani?
SHAHIDI: Imetoka kwa Dennis Leo Urio ambaye ni mmiliki ambayo inaonyesha namba ya kesi CD/IR/2097/2020.
WAKILI WA SERIKALI: PF uliandaa lini?
SHAHIDI: Tarehe 13 Agosti 2020.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, ametambua Exhibit P33.
SHAHIDI: Simu nyingine ni Sumsumg yenye IMEI namba 354767086468291.
WAKILI WA SERIKALI: Ulipokea kutoka kwa nani?
SHAHIDI: Kwa Luteni Dennis Urio yenye namba ya jalada namba CD/IR/2097/2020.
WAKILI WA SERIKALI: PF uliandaa lini?
SHAHIDI: Tarehe 13 Agosti 2020.
WAKILI WA SERIKALI: Ametambua kielelezo namba 29.
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi umesema kwenye hizi simu za tarehe 12 Agosti 2020, halafu PF145 uliandaa tarehe 13 Agosti 2020?
SHAHIDI: Niliandika PF145 kutokana na tarehe 12 Agosti 2020 kutokuwa na PF pale ofisini.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati unatoa ushahidi wako kuhusiana na makabidhiano ya simu baina ya wewe na Dennis Leo Urio, ulisema kwamba uliandaa hati ya makabidhiano siku hiyo. Je, ukiona utaitambuaje?
SHAHIDI: Nitaitambua kwa jina langu kwa sababu wakati huo nilikuwa na cheo cha Assistant Inspector Swila, ambaye ndiyo mimi. Niliandika jina la Dennis Urio ambaye ndiye amenikabidhi na aina ya simu na IMEI namba ambayo namba ya kwanza inaanza na 35 na namba tatu za mwisho ni 040.
SHAHIDI: Na IMEI namba ya pili ni 35 na mwisho ni 057.
WAKILI WA SERIKALI: Hii hati ya makabidhiano ambayo uliandaa wakati anakabidhi simu, yenyewe ina matumizi gani?
SHAHIDI: Tunatumia kukabidhiwa vitu ambavyo vimekamatwa kutoka kwa mtuhumiwa, kukabidhiana kutoka kwa askari kwenda kwa askari.
WAKILI WA SERIKALI: Mwanzoni ulisema kwamba hati hiyo ni ya watuhumiwa, kwanini ulitumia hati hiyo kwa Dennis Urio ambaye unasema ni shahidi?
SHAHIDI: Nimeitumia kwa sababu yeye ni shahidi, kama ambavyo tunakabidhiana kutoka kwa askari kwenda kwa askari.
WAKILI WA SERIKALI: Kwenye fomu hiyo tutatambuaje kama yeye ni shahidi?
SHAHIDI: Kwa sababu yeye haionyeshi tarehe ya kukamatwa kielelezo hicho.
WAKILI WA SERIKALI: Utaitambuaje?
SHAHIDI: Niliandika jina langu Assistant Inspector Swila na niliandika jina la Luteni Dennis Urio. Sehemu za kujaza tarehe ya kukamatwa na muda niliweka alama ya ‘deshi’.
WAKILI WA SERIKALI: Na Luteni Urio alifanya nini kwenye hati hiyo?
SHAHIDI: Aliweza kusaini na mimi nikasaini kisha nikaandika tarehe ya siku anayonikabidhi.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, naomba kumwoyesha shahidi kielelezo.
WAKILI WA SERIKALI: Angalia kama unatambua ni kielelezo gani.
SHAHIDI: Kielelezo hichi nimekitambua kama hati ya makabidhiano baina yangu na Luteni Dennis Urio. Jina langu, tarehe, namba ya kesi ya jalada na sehemu ambazo nimejaza ‘deshi’.
WAKILI WA SERIKALI: Unaomba Mahakama ifanye nini?
SHAHIDI: Naomba Mahakama ipokee kielelezo hiki kama kielelezo.
(Hati ya Makabidhiano inapelekwa kwa mawakili wa utetezi. Mawakili nao wanaikagua).
Wakili Nashon Nkungu: Mheshimiwa Jaji, kwa niaba ya mshitakiwa wa kwanza sina pingamizi.
JOHN MALLYA: Mheshimiwa Jaji, kwa niaba ya mshitakiwa wa pili sina pingamizi.
DICKSON MATATA: Mheshimiwa Jaji, kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu sina pingamizi.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, kwa niaba ya mshitakiwa wa nne hatuna pingamizi.
(Hati ya Makabidhiano inapelekwa mezani kwa Jaji).
JAJI: Kitakuwa ni kielelezo namba ngapi?
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Tulikomea kielelezo namba 38 kwa hiyo hii itakuwa ni kielelezo namba 39.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa Inspekta Swila soma kielelezo hiki kuanzia hapa,
SHAHIDI: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Polisi Tanzania, Hati ya Makabidhiano. Mimi Dennis Urio wa Kihonda Morogoro, namkabidhi Inspekta Swila vitu ambavyo vilikamatwa tarehe ‘deshi’, kutoka kwa mtuhumiwa ‘desh’, CD/IR2097/2020, simu aina ya Tecno, IMEI namba 358721101132040, jina la sahihi la anayekabidhi lipo, hapo chini, Jina na sahihi la anayekabidhiwa limeandikwa.
WAKILI WA SERIKALI: Lisome.
SHAHIDI: Sahihi ya anayekabidhiwa na kukabidhi zipo hapo chini.
WAKILI WA SERIKALI: Jina la anayekabidhi ni la nani?
SHAHIDI: Luten Dennis Urio.
WAKILI WA SERIKALI: Jina la anayekabidhiwa?
SHAHIDI: Ni mimi ambaye kwa kipindi hicho nilikuwa Assistant Inspector.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini unasema hiyo sahihi ni ya Dennis Urio?
SHAHIDI: Kwa sababu wakati anasaini nilikuwepo.
WAKILI WA SERIKALI: Eneo ambalo ni ‘deshi’, ‘deshi’?
SHAHIDI: Kuna ‘deshi’ palipokamatwa, tarehe pia ‘desh’, saa pia ‘desh’, kutoka kwa mtuhumiwa ambaye ni ‘desh’ ambaye anatuhumiwa kwa kosa la ‘desh’.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini?
SHAHIDI: Kwa sababu yeye ni shahidi.
WAKILI WA SERIKALI: Unasema zile simu katika siku nne tofauti ulizopokea ulikuwa unaenda kutunza katika kabati lako. Hebu ifahamishe mahakama ni eneo gani hilo?
SHAHIDI: Nilikuwa natuma kwenye ofisi, ndani ya kabati ambapo natunza vitu vyangu na kubaka na funguo.
WAKILI WA SERIKALI: Kwanini ulikuwa unavifungia katika kabati?
SHAHIDI: Nilikuwa navifungia katika kabati la chuma kwa ajili ya kulinda usalama wa vielelezo.
WAKILI WA SERIKALI: Ni watu wangapi mlikuwa mnatumia hilo kabati?
SHAHIDI: Kwa kipindi hicho nilikuwa natumia mimi mwenyewe.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya hapo nini kiliendelea?
SHAHIDI: Niliweza kumpigia simu Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi kumfahamisha kuwa nimeshapokea simu nne za Dennis Urio.
SHAHIDI: Na Afande Kingai akanielekeza kuandaa barua kwenda katika Ofisi Uchunguzi Makosa ya Mtandao kwa ajili ya uchunguzi.
WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa ni lini?
SHAHIDI: Ilikuwa ni tarehe 12 Agosti 2020.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya wewe kumpa taarifa hiyo nini kiliendelea?
SHAHIDI: Alinitaka nikabidhi simu hizo kwa DC Goodluck siku ya tarehe 13 Agosti 2020. Niliweza kuandaa barua ambayo ilisainiwa na Afande Hamad Msangi Kamishina Msaidizi wa Polisi aliyopo Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Ofisi Ndogo za Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Ukisema ilisainiwa na Hamad Msangi wakati uliandaa wewe. Ni kwanini?
SHAHIDI: Kwa sababu barua yoyote inayotoka kwenda maabara ya uchunguzi au taasisi nyingine lazima isainiwe na mtu wenye cheo cha Kamishina Msaidizi au zaidi ya cheo hicho.
WAKILI WA SERIKALI: Barua hiyo ilikuwa inaenda wapi na kwa ajili gani?
SHAHIDI: Ilikuwa inaenda maabara ya uchunguzi wa kisayansi kwa ajili ya uchunguzi wa simu nane.
WAKILI WA SERIKALI: Hizo simu nane ni zipi?
SHAHIDI: Moja ni ile aliyokamatwa nayo Mtuhumiwa Adam Kasekwa aina ya Itel yenye rangi nyeusi. Nyingine ni Tecno aliyokamatwa nayo Mtuhumiwa Mohammed Ling’wenya, yenye rangi nyeusi. Simu zingine ni alizokamatwa nazo Khalfani Bwire moja aina ya Bundy, simu ndogo na nyingine ni smart phone Tecno yenye rangi ya bluu.
SHAHIDI: Pamoja na simu nne ambazo nilikabidhiwa na shahidi Luteni Dennis Urio, Tecno nyeusi, Itel ya blue, Tecno rangi tatu mchangamyiko (bluu, nyeusi na dhahabu).
WAKILI WA SERIKALI: Katika ile barua ambayo unasema ilisainiwa na Hamad Msangi, simu hizo nane ulizitambulisha kwa namna gani?
SHAHIDI: Kwa majina na IMEI namba.
WAKILI WA SERIKALI: Wakati unazichambua simu hizi Mahakamani. Kuna simu ulisema kwamba IMEI namba ilifutika. Je, IMEI namba yake kwenye barua hiyo uliandikaje?
SHAHIDI: Niliwasha simu, nikatumia formula ya *#06# baada ya hapo ikawa imefuata IMEI namba.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya hapo unafanyeje?
SHAHIDI: Unabonyeza OK. Baada ya kumalizia kupata namba hiyo nilirudisha simu katika hali yake ya kawaida kwa kuzima.
WAKILI WA SERIKALI: Katika barua hii uliyoandika kwenda katika Kamisheni ya Makosa ya Mtandao, kitu gani ulikuwa unahitaji?
SHAHIDI: Tuliomba kupata mawasiliano yaliyofanyika katika hizo simu kupitia mitandao ya Telegram, Facebook, Instagram na WhatsApp. Pia tuliomba kupatiwa taarifa za miamala ya fedha pamoja na usajili.
WAKILI WA SERIKALI: Ni namba zipi hizo ulizoomba kupatiwa taarifa za usajili?
SHAHIDI: Ni 0719933386. Namba nyingine ni 0784779944, nyingine ni 0782 237913, nyingine ni 0787555200 na pia nyingine 0754612518.
SHAHIDI: Pamoja na namba zingine ambazo siwezi kuzikumbuka.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa ulifanya nini?
SHAHIDI: Nilimwita DC Goodluck akaja ofisini Makao Makuu madogo ya upelelezi. Nilifunga kwenye bahasha na yeye akiwepo. Kisha nikamkabidhi pamoja na barua.
WAKILI WA SERIKALI: Ulimkabidhi kwa ajili gani sasa?
SHAHIDI: Ili apeleke kwenye kitengo cha uchunguzi wa makosa ya mtandao.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umemkabidhi vitu hivyo kupeleka maabara kitu gani ulifanya?
SHAHIDI: Tarehe 14 Agosti 2020 Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi alinitaka nifike Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, katika chumba cha kutunzia vielelezo.
SHAHIDI: Ili niweze kukagua na kubadilisha, kutoka katika kidaftari kilichokutwa kutoka nyumbani kwa mtuhumiwa Khalfani Bwire ili niweze kubaini maeneo yaliyopo Dar es Salaam na niweze kuyatembelea kwa lengo la kubaini kama yapo au hayapo na kubaini anafanya shughuli gani.
WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama.
SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji samahani. Naomba niende washroom.
(Kabla hajaruhusiwa shahidi anatoka nduki kizimbani).
(Shahidi amesharejea kizimbani).
WAKILI WA SERIKALI: Sasa hebu elezea maelekezo hayo ambayo una ACP Kingai uliyatekeleza kwa namma gani.
SHAHIDI: Tarehe 14 Agosti 2020 nilifika chumba cha kutunzia vielelezo kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na kumkuta mtunza vielelezo Koplo Johnson ambaye aliweza kunionyesha vielelezo ambavyo vilikamatwa kwa Khalfani Bwire, ingizo namba 211/2020 kutoka katika kitabu kinachohifadhi vielelezo. Tuliweza kupata kidaftari hicho na kukagua eneo mbalo linaonyesha ni daftari, kilikuwa kina michoro ya barabara.
Wakili JOHN MALLYA: Mheshimiwa Jaji, naomba shahidi azuiwe kuhusu kujadili content ambayo haipo Mahakamani, na hawezi kui- tender.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji. Kwa kuongezea tu, Kidando alikuwa anasimama hapa kwa sababu ya muda. Linalotendeka kwa mwingine lifanyike kote kote.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, naona pingamizi halina mashiko. Shahidi anasema jambo ambalo ni ushahidi wa moja kwa moja.
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji tukubaliane Rule of the game. Asije kusimama mbele mtu akasema suala la muda.
MALLYA: Mheshimiwa Jaji. Nakubalina na Wakili Peter Kibatala, ila miye nazungumzia content ambayo bado haijaingia Mahakamani. Pia anachokizungumzia kilikuja Mahakamani kikafukuzwa.
JAJI: Bwana Robert Kidando umeelewa?
JAJI: Kwanza tukubaliane kwamba kilichonkataliwa ni kielelezo, kuhusu content mie sijasoma kama nyie. Suala la kukubaliwa au kukataliwa ni jukumu la Mahakama kuja kujadili mbeleni. Kwa sasa sioni kama ni sahihi kumkataza shahidi kitu ambacho anaamini alikifanyia kazi. Kuhusu muda tulikuwa tunazumgumzia kuhusu kurudia maswali, na Mr Kidando aliposamama alikuwa anasema usirudie maswali. Ndiyo maana juzi ulizungumza muda mrefu niliona kwenye vyombo vya habari.
WAKILI WA SERIKALI: Tuendelee.
SHAHIDI: Niliweza kuangalia kwenye kidaftari na kujua ni maeneo yapi.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa ulienda eneo gani ambalo ulikuwa umeona kwenye kidaftari?
SHAHIDI: Makutano ya Barabara ya Kilwa na Mandela, nilibaini kituo cha mafuta cha GBP, pia kituo cha kuuzia mafuta cha Puma, pia nilitembea eneo la Kariakoo jirani na Mwendo Kasi kuna kituo cha Big Bon, pia nilienda kituo cha basi cha Morocco pia nilikuta kituo cha kuuzia mafuta cha jina la Total. Kituo hicho nacho kilikuwa kinafanya Kazi ya kuuza mafuta.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kutembelea maeneo hayo, ulifanya nini?
SHAHIDI: Baada ya kufika na maeneo hayo, niliweza kumjulisha Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi, akanitaka nichukue sampuli za maandishi ya Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Khalfani Bwire.
SHAHIDI: Siku inayofuatia tarehe 15 Agosti 2020 kuanzia majira kati ya saa 4:00 na saa 5:15 niliweza kumchukua mahabusu mtuhumiwa Khalfani Bwire nikampelela kwenye jengo la mkuu wa upelelezi wa Mkoa wa Temeke ambapo tuliweza kuchukua sampuli ya maandishi kutoka Kwa mtuhumiwa huyo.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa umemchukua Khalfani Bwire ni utaratibu gani ulitumia sasa?
SHAHIDI: Niliweza kumpa karatasi nane, na kumpa aandike maneno ambayo yalikuwa kwenye kidaftari. Chini aliweza kuandika jina na saini katika kuthibitisha kuwa sampuli hiyo ya maandishi ni ya kwake. Kisha na mimi nikathibitisha na kumrudisha kituo cha Polisi Chang’ombe.
WAKILI WA SERIKALI: Je, uliweza kumfahamisha ni kwanini ulikuwa unachukua sampuli hizo?
SHAHIDI: Niliweza kumwambia kuwa nachukua sampuli katika kuthibitisha kuwa nataka kuthibitisha uliyeandika ni wewe au mtu mwingine.
WAKILI WA SERIKALI: Ikawaje baada ya kumwambia?
SHAHIDI: Aliweza kuthibitisha na kusaini.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya shughuli hiyo hapo Chang’ombe, kitu gani pia ulifanya?
SHAHIDI: Siku hiyo hiyo tarehe 15 Agosti 2020 nilifika Kituo cha Polisi Mbweni ambapo palikuwa na watuhumiwa Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya majira ya saa nane mpaka saa tisa na robo. Niliweza kuchukua sampuli zao.
WAKILI WA SERIKALI: Ulitumia utaratibu gani baada ya kumtoa mahabusu?
SHAHIDI: Niliweza kumfahamisha kuwa kuna daftari imekamatwa kutoka kwa mtuhumiwa Khalfani Bwire, ambapo yeye amekataa maandishi siyo ya kwake. Nikampa karatasi nane, aweze Kuandika sampuli ya mwandiko wake.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya kuchukua sampuli zake wewe ulifanya nini?
SHAHIDI: Aliweza kuthibitisha kwa mwandiko wake.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya hapo ulifanya nini kwa mtuhumiwa Adam Kasekwa?
SHAHIDI: Nilimrudisha Adam Kasekwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Mbweni, nikamchukua Mohammed Ling’wenya ambaye nilimfahamisha kuhusu azima yangu ya kuchukua sampuli ya maandishi na yeye aliridhia.
SHAHIDI: Aliridhia kuanzia saa 12 mpaka saa moja jioni.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuchukua sampuli hizo ukawa umechukua sampuli ngapi?
SHAHIDI: Na yeye mtuhumiwa nilichukua sampuli ya karatasi zote nane, na akaweza kuthibitisha kuwa maandishi yaliyopo katika karatasi hizo ni ya kwake kisha akasaini.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kukamilisha zoezi hilo ulifanya nini?
SHAHIDI: Baada ya kukamilisha zoezi hilo na kumrudisha mtuhumiwa mahabusu niliendelea na majukumu mengine. Nikamjulisha Afande Ramadhan Kingai, ambapo siku inayofuata alinitaka niandae jalada hilo.
WAKILI WA SERIKALI: Siku inayofuata ya tarehe ngapi?
SHAHIDI: Tarehe 16 Agosti 2020 alinitaka niandae jalada hilo na kupeleka kwa DPP kwa mapendekezo ya kuandaa mashitaka.
WAKILI WA SERIKALI: Baada sasa ya maelekezo ya Kingai ulifanya nini?
SHAHIDI: Tarehe 17 Agosti niliweza kuandaa jalada hilo na kuweza kumpatia Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi ambapo alilisoma na kisha kuliandalia barua na kulipeleka ofisi ya DPP zilizopo hapa Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Ieleze Mahakama sasa mnamo tarehe 19 Agosti 2020 ulikuwa wapi na ulifanya shughuli gani kuhusiana na shauri hili.
SHAHIDI: Siku hiyo tarehe 19 Agosti 2020 nilikuwa hapa Dar es Salaam, niliweza kushiriki katika kuwapeleka watuhumiwa watatu Mahakama ya Kisutu.
WAKILI WA SERIKALI: Watuhumiwa hao watatu ni akina nani?
SHAHIDI: Ni Adam Hassan Kasekwa, Mohammed Abdilah Ling’wenya na Khalfani Hassan Bwire.
WAKILI WA SERIKALI: Hatua ipi ya kiupelelezi iliyokuwa imefika mpaka mnawapeleka washitakiwa Mahakamami?
SHAHIDI: Baadhi ya vielelezo vilikuwa vimeshapelekwa maabara ya uchunguzi, watuhumiwa walikuwa wameshaandikwa maelezo yao, pamoja na hati za kukamatia vielelezo hivyo vilikuwepo jaladani. Katika hatua nyingine upelelezi ulikuwa unaendelea ili kupata taarifa za simu nane zilizokuwa zimepelekwa katika ofisi ya uchunguzi wa makosa ya mtandao.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya siku hiyo ni shughuli gani zingine ulizofanya katika shauri hilo?
SHAHIDI: Watuhumiwa wengine waliendelea kukamatwa na kufikishwa Mahakamani mwezi Septemba, ambapo watuhumiwa hao ni Justin Elia Kaaya, Khalid Athuman na Gabriel Mhina.
WAKILI WA SERIKALI: Watuhumiwa walikamatwa kipindi gani?
SHAHIDI: Walikamatwa kwa tarehe tofauti kuanzia mwezi Agosti mpaka Septemba na mahakamani walifikishwa kwa tarehe tofauti.
WAKILI WA SERIKALI: Zaidi ya ukamataji wa watuhumiwa hao watatu shughuli gani nyingine ulifanya?
SHAHIDI: Tarehe 16 Septemba 2020 niliweza kuandika barua ya kupeleka sampuli za maandishi ya watuhumiwa watatu Khalfani Bwire, Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya katika kitengo cha uchunguzi kwa ajili ya uchunguzi wa miandiko yao na kufanya ulinganifu wa daftari lililokamatwa kwa mtuhumiwa Khalfani Bwire. Siku hiyo hiyo kabla ya kuandaa barua niliweza kufika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukua daftari na notebook kutoka katika ingizo namba 211/2020.
WAKILI WA SERIKALI: Ulichukua kutoka kwa nani?
SHAHIDI: Coplo Johnson wa chumba cha kutunzia vielelezo kituo cha polisi Kati Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuchukua ukafanya nini?
SHAHIDI: Nilienda navyo ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Dar es Salaam kuandaa hiyo barua, nikaambatanisha na sampuli za maandishi, kidaftari na barua ambayo ilisainiwa na Afande Hamad Msangi Kamishina Msaidizi wa Polisi anayefanya kazi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi Makosa ya Jinai, ofisi ndogo za Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Kidaftari na notebook vilienda wapi?
SHAHIDI: Niliweza kuambatanisha na Barua, na vielelezo nikavipa namba kuanzia B1 mpaka B9. Kielelezo ambacho kinabishaniwa niliandika A1 ambacho ni kidaftari chenye michoro. Halafu B1 mpaka B 9 ni sampuli ya maandishi ya Khalfani Bwire pamoja na notebook pamoja na maandishi akiwa katika shughuli zake za kawaida.
WAKILI WA SERIKALI: Za watuhumiwa wengine ilikuwaje?
SHAHIDI: C1 mpaka C10 zilikuwa za sampuli za maandishi ya Mohammed Ling’wenya. Pia D1 mpaka D9 zilikuwa sampuli za Adam Kasekwa.
WAKILI WA SERIKALI: Hizi sampuli ambazo umeambatanisha kupeleka katika maabara ya uchunguzi, je, tarehe ulikitoa wapi hicho kidaftari?
SHAHIDI: Nilikuwa nimekifungia mimi katika kabati la chuma ambalo mimi nilikuwa nalitumia. Nilienda kukabidhi katika maabara ya uchunguzi kwa Koplo Khamis.
WAKILI WA SERIKALI: Shughuli gani sasa nyingine ulifanya?
SHAHIDI: Niliendelea na majukumu mengine, mpaka tarehe 25 Novemba 2020 nilipokea maelekezo kutoka kwa Afande Ramadhan Kingai Kamishina Msaidizi wa Polisi akinitaka niandae barua mbili, barua moja ya kwenda kwa Mrajisi wa Silaha ili kupata taarifa za mmiliki wa silaha iliyokamatwa kutoka kwa mmiliki Adam Kasekwa ambayo ni bastola aina ya Luger yenye namba A5340. Ya pili alinitaka niandae barua ya kumkabidhi Detective Constable Goodluck kwa ajili ya kupeleka silaha bastola aina ya Luger yenye namba A5340 katika maabara ya uchunguzi wa kisayansi, kitengo cha uchunguzi wa silaha, pia barua hiyo ilikuwa inahusisha kukabidhi risasi tatu ambazo zilikutwa kutoka kwenye magazine kutoka kwa mtuhumiwa Adam Kasekwa.
WAKILI WA SERIKALI: Ni kwanini sasa silaha hizo mlikuwa mnaandikia barua? Ni ili nini sasa?
SHAHIDI: Kwa ajili ya uchunguzi, ila pia ili kujua kama silaha hizo zinafanya kazi.
WAKILI WA SERIKALI: Kazi ya kuandaa barua hizi ulifanyia wapi?
SHAHIDI: Nilifanya ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, ofisi ndogo za Dar es Salaam.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuandika barua hizo elelezea upelekaji wa bastola na risasi.
SHAHIDI: Kabla ya kuandika barua hizo niliweza kumuita Detective Constable Goodluck aweze kuja na kuchukua bastola na risasi na baada ya kuja nazo niliweza kuhakiki silaha hiyo aina ya Luger A5340 yenye risasi tatu. Ndipo niliandaa barua hiyo ambayo ilisainiwa na Hamad Msangi Kamishina Msaidizi wa Polisi ambaye anafanya kazi katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, ofisi ndogo za Dar es Salaam. Na barua ya pili pia ilisainiwa na huyo huyo ACP Hamad Msangi.
WAKILI WA SERIKALI: Unasema ulikuwa unahakiki, wewe ulikuwa unahakiki nini?
SHAHIDI: Nilikuwa nahakiki serial number ya silaha na kuiangalia hiyo silaha kama yenyewe.
WAKILI WA SERIKALI: Kipi ulikiona?
SHAHIDI: Niliona kweli hiyo ni silaha aina ya Luger yenye namba A5340.
WAKILI WA SERIKALI: Hayo maandishi A5340 yapo wapi katika bastola?
SHAHIDI: Yapo nje ya silaha, upande wa kulia ukishika silaha.
WAKILI WA SERIKALI: Sasa hii bastola amekuja nayo Goodluck. Je, upande wa risasi ulihakiki nini?
SHAHIDI: Nilihakiki kama risasi ni tatu, nikakuta kweli ni risasi tatu.
WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuthibitisha kama risasi ni tatu ulifanya nini?
SHAHIDI: Niliweza kufungia silaha hiyo katika bahasha, akaweza kuondoka nayo kwenda kukabidhi katika kitengo cha uchunguzi wa kisayansi wa silaha na milipuko.
WAKILI WA SERIKALI: Ulifanya nini kuhusu ile barua ya Mrajisi?
SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji, samahani naomba niende CHOONI.
(Kabla Jaji hajamruhusu shahidi ameshachomoka kizimbani na ameshafika mlangoni).
Shahidi amesharejea kizimbani.
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi nasema ulifanya nini sasa kuhusu ile barua ya kwenda kwa Mrajisi wa silaha?
SHAHIDI: Nilifunga na kupeleka katika Masjala ya Siri, kwa ajili ya kwenda Ofisi ya Mrajisi Dodoma. Na barua iliondoka siku ileile.
WAKILI WA SERIKALI: Hebu ieleze Mahakama silaha hiyo ukiona leo unaweza kutambuaje?
SHAHIDI: Naweza kuitambua kwa aina yake ya Luger serial namba yake A5340 na kama nilivyosema mwanzo serial namba hiyo ipo upande wa kulia.
WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, naomba kupatiwa kielelezo namba P3.
WAKILI WA SERIKALI: Shahidi kwa kuchukua tahadhari zote, hebu tizama silaha hiyo na useme kama unaweza kuitambua.
SHAHIDI: Kama nilivyosema awali, silaha hii ina jina upande wa kushoto Luger na upande wa kulia ina serial number ya A5340. Hii ni silaha ambayo niliandikia barua kwenda kitengo cha uchunguzi.
WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji bado tuna maswali katika examination in chief, na sasa ni saa 11 kasoro dakika 5, hivyo tunaomba ahirisho mpaka Jumatatu tarehe 7 Februari 2022.
(Mahakama iko kimya)
KIBATALA: Mheshimiwa Jaji hatuna pingamizi.
JAJI: Kufuatia ombi lililoletwa na upande wa mashitaka, Mahakama inakubali kuahirisha kesi mpaka Jumatatu tarehe 7 Februari 2022.
JAJI: Shahidi utaendelea kuwa kizimbani kutoa ushahidi wako. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza.
Jaji anaondoka Mahakamani.