KAMARI ‘YATAFUNA’ TAIFA KIMYA KIMYA

Vijana walio mtaani, waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata sekondari wamenasa kwenye michezo hii wakiamini ndiyo njia ya haraka ya kufanikiwa. 

SASA ni dhahiri kwamba michezo ya kubahatisha au kamari (ijulikanayo kama kubeti), sasa inalitafuna taifa.

Zamani, michezo hiyo ilichezwa katika maeneo maalumu ya starehe kama casino na mahoteli makubwa ya kitalii, wakati huo ikionekana ni michezo ya matajiri katika kujiburudisha zaidi.

Hata hivyo, Sheria Na.4 ya mwaka 2003 mahsusi kwa ajili ya kusimamia na kuendesha michezo hii, inaitambua kamari kama ni burudani na si ajira.

Ujio wa kampuni kutoka China kuingia kwa wingi katika biashara hiyo kumesababisha kamari kusambaa kila kona vikiwamo vituo vya mabasi, maeneo ya wazi, vichochoroni na kwenye maduka madogo ya mtaani maarufu ‘duka la Mangi’.

Kamari pia inachezwa kupitia simu za mkononi, kompyuta, mashine (slots) maarufu dubwi au mashine za mchina, redio, magazeti na televisheni navyo vinaendesha michezo hiyo kwa kiwango kikubwa.

Vijana walio mtaani, waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu, wanafunzi wa vyuo vikuu na hata sekondari wamenasa kwenye michezo hii wakiamini ndiyo njia ya haraka ya kufanikiwa.

SAUTI KUBWA imefuatilia kwa kina undani wa uwekezaji wa michezo ya kubahatisha jijini Dar es Salaam na kubaini mambo kadhaa ukiwamo ulegevu wa sheria zinazosimamia sekta hiyo.

Uchunguzi wetu umebaini baadhi ya maduka madogo ya bidhaa mchanganyiko za matumizi ya majumbani maarufu kama maduka ya ‘Mangi’ pia kumefungwa mashine za michezo ya kubahatisha.

Mashine hizo hazilipiwi kodi na kulifanya taifa kukosa pato ambalo lingesaidia katika utoaji wa huduma kwa jamii na ujenzi wa miundombinu kwa ustawi wa nchi.

Uchunguzi wetu umebaini kwenye maduka yenye mashine za ‘dubwi’ hufunguliwa jioni, usiku na asubuhi siku za mwisho wa wiki ili kukwepa mkono wa sheria kwa kufanya biashara bila leseni.

Baadhi ya maduka katika maeneo tofauti ya Manispaa za Kinondoni na Ilala, wamekabidhiwa mashine za kamari na Wachina huku wakielezwa kuwa zimekwishalipiwa kodi zote za serikali, na zimewekwa stika maalum zinazowalinda wasikamatwe na mamlaka za serikali.

Barua pepe kutoka kitengo cha huduma kwa wateja cha TRA kwa SAUTI KUBWA inasema kuwa ukaguzi wa mashine za michezo ya kubahatisha upo nje ya majukumu yao.

Hata hivyo TRA hawaweka wazi kuhusu utaratibu wa utozaji kodi kwenye biashara ya michezo ya kubahatisha.

“Asante kwa kutuandikia, japo ukaguzi wa mashine za michezo ya kubahatisha upo nje ya majukumu yetu, tafadhali wasiliana na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kupata majibu ya maswali yako,” unasomeka ujumbe wa barua pepe kutoka TRA.

Kwenye ‘dubwi’ katika duka la ‘Mangi’ eneo la Mabibo Manispaa ya Kinondoni kumeandikwa maneno haya: United Republic of Tanzania, Ministry of Finance and Planing, Gaming Board of Tanzania.

Katika kituo cha basi cha Moroco Manispaa ya Kinondoni, ambako kuna mashine moja inayofahamika na wengi kama ‘dubwi bonanza’ wacheza kamari wanasema ingawa wanashiriki mchezo huo lakini hawaoni faida kwani malengo yao hayafikiwi.

Godfrey Njechele, mpiga debe kituoni hapo, anasema hakuna aliyewahi kushinda zaidi ya Shilingi 20,000 katika mashine hiyo na kusisitiza kuwa “kamari hii inatuletea umasikini tu”.

Fundi viatu wa kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina la Ibra Msafiri, anasema kwenye kamari hakuna pesa ya kutunza familia wala mtaji wa biashara, bali mahitaji madogo madogo tu, hivyo anashauri serikali iangalie namna bora ya michezo hii ya kamari kwani inawapumbaza vijana.

Mmiliki wa duka la kamari lililopo Mwananyamala A Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliieleza SAUTI KUBWA kuwa kamari ni biashara kama ilivyo nyingine na kuongeza kuwa kuna urasimu wa kupata vibali na inahitaji mtaji mkubwa.

“Uwekezaji katika michezo ya betting umetawaliwa na kampuni na raia kutoka China na kwamba Watanzania wanaendelea kuwa vibarua na wachezaji wa michezo hiyo inayozidi kuwafukarisha zaidi.”anasema mmiliki huyo.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe amezungumza na SAUTI KUBWA na amesisitiza kuwa mashine za betting hazipaswi kuwekwa kwenye vituo vya mabasi au maeneo ya wazi na kwenye maduka ya ‘Mangi’ bali maeneo maalum yanayoruhusiwa kisheria.

Mbalwe pia alitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa kuhusiana na uwekezaji wa michezo ya kubahatisha nchini zikiwamo faida za kiuchumi ambazo Tanzania inazipata.

Mkurugenzi huyo amesema pamoja na michezo hiyo kuwa na uwezekano wa kusababisha uraibu kwa wanaotumia fedha nyingi kwenye casino, lakini ina faida kwa uchumi wa nchi na ajira, na kuongeza kuwa waombaji wa leseni kwa ajili ya uwekezaji huo hufanyiwa upekuzi mkali ndani na nje ya nchi ili kubaini kama kuna rekodi ya uhalifu.

“Masharti mengine ya kisheria ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi kupitia Polisi wa Kimataifa (Interpol) kama hajawahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai au kukosa uaminifu.

“Lakini pia kwa wanaotaka kuagiza mashine kutoka nje wanaomba kibali kwa GBT na zikifika nchini zinakaguliwa na kuwekewa stika maalum zinazosaidia wakati wa ukaguzi.”anasema mkurugezni huyo na kusisitiza kuwa sekta nzima ya michezo ya kubahatisha inahitaji teknolojia ya hali ya juu na GBT imejitahidi kuiendesha kupitia mifumo.

Vibali vya dubwi vyasitishwa

Hata hivyo Mbalwe anakiri uwezekano wa kuwapo udanganyifu kupitia mashine hizo kwa wasiosajiriwa ingawa GBT inafanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miji mikubwa Dar es Salaam ikiwamo.

Mbalwe anasema kutokana na ugumu wa udhibiti wa mashine kuwa na mianya mingi ya udanganyifu, GBT imestisha utoaji wa vibali kwa uagizaji wa mashine hizo nje ya nchi mpaka watakapokuwa na mfumo bora wa kuzihakiki kupitia mifumo rasmi.

Kuhusu mapato yanayotokana na uwekezaji wa michezo ya kubahatisha, anasema lengo la serikali limefikiwa kwani makusanyo kwa mwaka 2022/2023 ni Shilingi Billion 173, na mwaka huu wa fedha 2023/2024 yanaweza kuongezeka na kufikia Shilingi Bilion 200.

Mapato hayo ni tofauti na kodi zingine zikiwamo uingizaji mashine kutoka nje, hivyo kuna uwezekano makusanyo yataongezeka zaidi.

Kuhusu ajira, Mbalwe anasema kuna Watanzania wanaofikia 25,000 wanaendesha maisha yao kupitia sekta hiyo.

Wakati huo kiwango cha uwekezaji wa michezo ya kubahatisha katika jiji la Dar es Salaam kinaonyesha kuna jumla ya mashine 3038.

Itaendelea toleo lijalo…

 

 

Like
1