Kagame, Magufuli wagawiana fadhila. Mmoja atoa ulinzi, mwingine mgodi wa madini

Askari wa Rwanda walio Mererani hawalindi ukuta wa madini, bali wanalinda nyumba ya Kagame, na siri zake na Magufuli

 

URAFIKI wa karibu kati ya Rais John Magufuli na Rais Paul Kagame wa Rwanda, unaleta shaka na unajenga mazingira ya kifisadi, SAUTI KUBWA linaeleza.

Mbali na mazingira ya kifisadi yanayojengwa, zipo dalili pia kwamba “matumizi mabaya ya uswahiba” wa marais hao wawili yanaweza kuhatarisha usalama wa nchi, iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Baadhi ya wasaidizi wa rais wasiokubaliana na mazingira haya, wameliambia SAUTI KUBWA kuwa ingawa si vema kuchaguliana marafiki, kinachoendelea kati ya Magufuli na Kagame ni “jambo la watu binafsi linalohusisha nchi, na haliwezi kutuacha salama.”

Kwa urafiki wao binafsi, wawili hao wamefika mahali ambapo wanafanya uamuzi wa masuala nyeti katika taifa ambayo Baraza la Mawaziri halijui.

Miongoni mwa mambo ambayo huko nyuma yalivuma kama tetesi na sasa yamethibitika ni ukweli, ni hili kwamba Magufuli ameingia “mkataba wa siri” kati yake ni Kagame kuhusu masuala ya ulinzi na usalama.

Viongozi wengi waandamizi serikalini hawajui kiini cha urafiki wa marais hawa wawili, lakini wanashuhudia wageni wakiingizwa katika mifumo ya ulinzi wa nchi, hasa usalama wa rais; na majuzi wamepata taarifa za kikao cha siri Ikulu kuhusu ulinzi wa ukuta wa Mererani, yanakochimbwa madini ya Tanzanite. Si makamu wa rais wala waziri mkuu aliyejulishwa wala kuhusishwa katika masuala hayo nyeti na vikao hivyo.

“Wote wawili (Magufuli na Kagame) hawaamini mtu yeyote katika masuala haya. Wanajadili peke yao. Wasaidizi wanabaki kutumwa tu kutekeleza makubaliano ambayo hawajui na hawakushiriki. Kificho hiki ndicho kinaleta wingu la ufisadi, kwani wanaomjua Kagame wanasema hawezi kufanya dili la namna hii akaondoka mikono mitupu,” kinaeleza chanzo chetu.

Kikao cha hivi karibuni ni cha tarehe 19 Aprili 2018, siku pekee ambayo watu wachache walishirikishwa mazungumzo kadhaa ya kiutekelezaji. Siku hiyo, Magufuli alikuwa na ugeni wa viongozi waandamizi sita (6) waliotumwa na Kagame kukutana naye. Walifanya kikao kifupi usiku Ikulu, Dar es Salaam, kuanzia saa 2:30 hadi saa 3:30.

Mtoa habari mmoja anasema: “Kikao chenyewe hakikuwa kirefu kwa kuwa mambo karibu yote yalishamalizwa na wakubwa. Na mkuu mwenyewe alikuwa hajatulia, kwani ndicho kipindi ilipokuwa imeibuliwa kashfa nyingine ya shilingi trilioni 1.5, na wakati huo alikuwa anahaha kuifunika. Wakaja wageni, akawapa maelekezo, wakamrudishia Kagame.

“Lakini kwa kifupi ni kuwa pale Mererani hatuna chetu tena. Kagame ameshampiga Magufuli changa la macho, na Magufuli haelewi kitu, anasema haamini watu wetu wa usalama, eti wanavujisha siri. Sasa siri za kuibiwa raslimali kwanini zisivuje? Kwani kazi ya vijana wetu ni kulinda usalama wa Rwanda au wa Tanzania?”

Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, walijadiliana kuhusu ulinzi wa mgodi wa Tanzanite na ulinzi wa rais, mambo ambayo yalikuwa ya kiutekelezaji kwani marais wawili walikuwa wameshakubaliana.

“Ni makubaliano ya miaka 10. Kagame amekubali kumpatia ulinzi maalumu Magufuli hadi amalize kipindi chake, kama atakuwa amefika huko. Inasemekana rais wetu ana shaka na mifumo ya ulinzi aliyoikuta, anasema watu wanajuana mno, wanavujisha mambo, sijui mambo gani anaficha,” kinahoji chanzo kingine cha habari.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, mashushushu wapato 300 wa Rwanda watahusika na shughuli hiyo, na wataifanya kwa awamu kadiri ya mahitaji ya Magufuli. Walinzi hawa watatumika kama sehemu ya kikosi maalumu cha ulinzi wa rais, na baadhi yao watashirikishwa katika ukachero na ulinzi wa ukuta wa Mererani, na maeneo mengine kadiri ya maono ya Magufuli, wakishirikiana na wenyeji.

Mtoa taarifa mwingine anasema: “Si kwamba Kagame anatoa msaada huu bure. Naye amepewa dili yake huko Manyara. Ndiyo maana unasikia watu wake ndio wanalinda ukuta unaozunguka mgodi wa Tanzanite huko Mererani.

“Tangu mwaka jana 2017 Kagame amekuwa akiingia nchini kisirisiri kila mara kupitia uwanja wa ndege wa Arusha… inasadikika kuwa hicho kipindi alikuwa anakuja kukagua maeneo, pia kutoa ushauri juu na jinsi ya kujenga ukuta.

“Mbali na ukuta, kumejengwa pia nyumba yake (Kagame) ya kufikia ndani ya ukuta huo. Sasa utaelewa kwanini anataka lazima askari wake ndio walinde ukuta. Kinacholindwa pale si ukuta bali Kagame. Vyote viwili, ukuta na nyumba vilishakamilika, na unaambiwa  Kagame huwa anakuja na kuingia, na kukaa mgodini mpaka siku tatu hivi, halafu anaondoka.

“Watu wanao tumia airport (uwanja wa ndege) ya Arusha wanakwambia kuwa kila mara kuna kuwepo na delay (ucheleweshaji) ya ndege kuondoka bila kuambiwa  kuna tatizo gani, matokeo yake wanaanza kuona movements za hapa na pale za wanajeshi na kusikia miongoni mwao wakisema ni Kagame. Yaani inauma sana huyu jamaa anachokifanya.”

Ingawa mpango wenyewe ulianza kama siri, tayari unajulikana kwa watu wengi ndani ya serikali lakini wanaishia kunung’unika. Manung’uniko haya ndiyo yalisababisha baadhi ya wanajeshi kushauri mkuu wao, Jenerali Venance Mabeyo, na mkurugenzi mkuu wa idara ya usalama wa taifa Dk. Modestus Kipilimba waingilie kati kumshauri rais.

Hata hivyo, rais hakupendezwa na ushauri huo, kama ambavyo matoleo mawili yaliyopita, ya SAUTI KUBWA, yalivyoeleza. Kinachokera watumishi wa serikali na baadhi ya wasaidizi wa rais ni kutoshaurika kwa rais katika suala hili, hasa baada ya kujua hisia zake kwamba yeye haamini vyombo vyetu vya usalama katika suala la ulinzi binafsi na kuhusu sakata hili la Mererani.

Kwa hakika, hata Kagame asingeweza kukubaliana na ulinzi asiouamini hasa kama anajua kuwa suala lenyewe ni nyeti kiasi hiki. Bahati mbaya kwa wote wawili, kile walichodhamiria kuficha kimejulikana.

Ikumbukwe kuwa kabla ya Rais Magufuli kuingia madarakani mwaka 2015, Rwanda na Tanzania hazikuwa na uhusiano mzuri, kutokana na msuguano wa chinichini kati ya Kagame na Rais Jakaya Kikwete ulioteteresha mustakabali wa kidiplomasia wa nchi hizi, hasa baada ya Kikwete kukerwa na kauli ya Kagame kwamba kama Tanzania ingempatia Bandari ya Dar es Salaam kwa miezi sita tu ingewezesha nchi kujitosheleza kimapato.

Uhusiano wa nchi hizi mbili ulirejea ghafla, mara tu baada ya  Magufuli kuwa rais; na katika ziara yake ya kwanza alienda Rwanda. Baada ya muda mfupi Kagame naye alimtembelea Magufuli, na katika moja ya ziara za Kagame akiwa Ikulu, Dar es Salaam, Magufuli aliwambia waandishi wa habari kwamba Kagame ndiye “anamfundisha” kuongoza nchi.

Wanaofuatilia uhusiano wa Kagame na jirani zake, hasa Congo na Uganda, wanatilia shaka “wema wa ghafla” ambao ameuonyesha kwa Tanzania; na ukarimu wa haraka haraka wa kusaidia ulinzi kwa rais wa nchi jirani. Mmoja wa wanyarwanda aliyezungumza na SAUTI KUBWA alisema:

“Kwa kawaida, Kagame anadharau. Hata anapokuwa na marais wenzake hupenda kujionyesha kuwa yeye ni bora. Lakini nilipomwona katika mazungumzo na Magufuli mjini Kigali, Kagame alionyesha sura ya unyenyekevu mkubwa ambao kwa kawaida hafanyi hivyo, nihisi huyu kuna kitu anatafuta kwa Magufuli. Sasa nimeelewa alichokuwa anavizia.”

Chanzo kingine kinasema: “Kikwete alimnyima bandari, sasa Magufuli amempatia mgodi wa Tanzanite kirahisi. Wenye akili wanajua kuwa huu ni mchezo wao wote wawili. Juu juu wanajifanya wanapiga vita ufisadi, wanajiita wazalendo, huku kisirisiri wanajihusisha na biashara za ajabu. Mliokuwa mnawasema Mkapa na Kikwete subirini matokeo baada ya Magufuli kuondoka madarakani.”

Wanaojua kiini cha mgogoro wa Kagame na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), kwa sababu ya kugombania madini ya Wakongo, wanashangaa imani ya haraka haraka ya Magufuli katika dili la ukuta wa Mererani, kwenye machimbo ya Tanzanite, madini yanayopatikana Tanzania pekee.

Hofu ya wananchi, wakiwemo viongozi serikalini, wanaokerwa na miradi hii ya marais hawa wawili ni kwamba iwapo hali itaendelea hivi, madini yetu yatajenga zaidi uchumi wa Rwanda kuliko Tanzania. Wanasema Kagame ni mjanja, mwerevu, na mzoefu kuliko Magufuli katika masuala haya ya “kusaka raslimali nje ya mipaka yake.”

Na kwa kuwa makubaliano ya marais hawa wawili yanafanyika “gizani,” kunajengeka ushahidi wa kimazingira kwamba wamejimilikisha mgodi wa Tanzanite kama ambavyo marasi wengine wamekuwa wanajinufaisha binafsi kwa migodi ya madini katika mataifa yao au ya nchi jirani.

Hata taarifa ya wiki hii Bungeni kuwa Tanzanite imeingiza faida kubwa ndani ya miezi mitatu kuliko iliyopatikana kwa miaka mitatu, inatafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama kiini macho cha kuonyesha faida kubwa iliyopatikana kutokana na kujengwa ukuta, ili kuhalalisha wizi wa wakubwa, kwa kuwa hakuna mwenye uwezo wa kufuatilia au hata kukagua mali halisi inayozalishwa na kuuzwa.

Wengine wanafananisha taarifa hiyo na zile za mamlaka ya mapato ambazo zimekuwa zinaonyesha kupanda kwa makusanyo ya kodi kila mwezi, lakini makusanyo hayo hayaonekani katika hali halisi ya huduma wanazopewa wananchi, na hata katika ripoti za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali.

Kinachotia shaka zaidi ni aina ya siasa za Kagame za muda mrefu, hasa dhidi ya wakosaji na wapinzani wake, ambazo Magufuli anaziiga, na tayari zimeanza kusababisha maafa kwa taifa.

Kagame anajulikana kama rais ambaye amegeuza nchi yake kuwa “taifa la vitisho.” Magufuli naye, ndani ya miaka miwili, amekwishapata sifa ya kugeuza Tanzania kuwa nchi ya vitisho.

Katika miaka ya awali ya utawala wake, Kagame alihadaa dunia kuwa angekuwa rais mwema, mpenda haki, na mpiga vita ufisadi. Baadaye ametumia taswira hiyo kuumiza na kupoteza wapinzani, na kukomesha wasiokubaliana naye – hasa waliokuwa na matatizo kadha ya uadilifu – akawatumia kama mfano wa kupiga vita ufisadi.

Magufuli naye alianza hivyo hivyo, akasifiwa na wengi kama kiongozi mkali, anayeweza kuleta mabadiliko, hasa kwa kupiga vita ufisadi. Ndani ya miaka miwili, sura yake halisi imedhihirika. Sasa dunia nzima inamuita dikteta. Anachukua hatua kwa ubaguzi, anateua baadhi ya watu wake wa karibu wenye uadilifu wenye shaka na kuwapa nafasi kubwa serikalini, huku akihusika yeye na rafiki zake katika miradi kadhaa mipya ya kifisadi, kama uwanja wa ndege wa Chato.

Nchini Rwanda, vyombo vya habari vimefungwa mikono na migumu, vimezibwa macho na masikio ili visione wala visiseme ufisadi wa wakubwa. Hali ile ile inatokea Tanzania. Vyombo vya habari    vinaogopa kuandika habari za uchunguzi au kuchapisha makala za kumkosoa rais. Hata mitandao ya kijamii imetungiwa kanuni dhalimu ili kuzuia wananchi wenye taarifa sahihi kuzitoa, kuibua na kujadili ufisadi wa wakubwa.

Nchini Rwanda, viongozi wa upinzani wanatekwa na kuuawa. Waliobahatika “wamepiga kambi” nje ya nchi. Katika Tanzania ya Magufuli, nchi imegeuka dola la kipolisi, wapinzani wanafananishwa na wahaini, wanaitwa wasaliti, wanaburuzwa mahakamani kwa makosa ya kubuni, wanafungwa jela kwa kumsema rais; vikosi vya wahuni (watu wasiojulikana) vinateka, vinatesa na kuua baadhi yao.

Kagame analazimisha utii wa watumishi wa umma na wananchi wake kwa kuwatia hofu. Magufuli naye anajengea wananchi hofu na anaitumia kama silaha ili asihojiwe, akisisitiza kuwa anataka nidhamu.

Kagame haoni shida kudhalilisha kiongozi hadharani kwa ajili ya kujipatia umaarufu mbele ya umma. Magufuli naye vile vile. Amekuwa anafokea na hata kufukuza kazi watumishi wa umma hadharani, kinyume cha utaratibu, kanuni na haki za binadamu. Ipo mifano ya wengi waliofariki dunia muda mfupi baada ya kudhalilishwa hivyo.

Kagame ana tabia ya kufilisi wapinzani na kuwaweka kizuizini – kama alivyomtendea binti mdogo tu aliyetamani kugombea urais, ambao hata hivyo alizuiwa kuugombea – Diane Rwigara. Diane na familia yake baadaye walifisiliwa mali zao, wakawekwa kizuizini.

Kabla ya Diane, Kagame aliwahi kuumiza vibaya baadhi ya watu ambao huko nyuma walimsadia akiwa katika mazingira magumu wakati wa harakati za kutafuta madaraka. Kwa mfano, Jenerali Kayumba Nyamwasa, aliwahi kumnusuru Kagame Desemba 22 na 23, 1990 katika hatari ya kifo.

Sethi Sendashonga (aliyekuwa ofisa mwandamizi katika ofisi za umoja wa mataifa), ndiye alikuwa mwenyeji wa Kagame kila alipokwenda Nairobi kwenye ziara za kikazi. Assinapol Rwigara – baba yake Diane – na Tribert Rujugiro ndio waliokuwa wanagharamia sehemu kubwa ya ziara hizo za Kagame.

Baada ya Kagame kuwa rais, alitofautiana na Kayumba kisiasa; Kayumba akahisi angeuawa, akakimbilia Afrika Kusini. Hata akiwa nje ya nchi, amenusurika mara nne kuuawa hata akawekewa ulinzi mzito na serikali ya Afrika Kusini. Lakini kaka yake Kanali Rugigana Ngabo yupo jela nchini Rwanda.

Sendashonga, baada ya kutofautiana na Kagame, alikimbia nchi – akajificha Kenya. Baadaye aliuawa akiwa huko huko Kenya. Mkewe na binti zake wapo jela. Rwigara naye aliuawa. Sasa familia yake inasumbuliwa, mkewe na watoto wapo kizuizini na wamefilisiwa.

Kwa Magufuli kusema Kagame ndiye anamfundisha jinsi ya kuongoza nchi, ni ujumbe unaopaswa kutisha Watanzania. Na tunapochanganya hilo na haya tunayoona yanawapata wapinzani, viongozi wa dini, vyombo vya habari, taasisi za kiraia, wanasheria, na wakosoaji wengine wa serikali, wakiwemo wanafunzi; Watanzania wana haki ya kutilia shaka urafiki wa Magufuli na Kagame.

Wana kila sababu ya kuwa waangalifu, kwani Magufuli amejichomeka katika dili chafu zinazomwondolea uadilifu anaojipa wa kupambana na ufisadi.

Like
36
1 Comment
  1. Amour justine 6 years ago
    Reply

    Ni nani wa kulikomboa taifa hili,najaribu kutafakari mbeleni tuendako napata wasiwasi kua taifa letu linaagamia tusipochukua hatua.

    5

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.