Ndugai akuza deni la matibabu nje ya nchi. Adaiwa kulamba milioni 500 ndani ya miezi mitano

JOB Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, na Rais John Magufuli wamenyoshewa kidole, wakihusishwa na ongezeko kubwa la deni la matibabu nje ya nchi.

Deni hilo limeongezeka kwa kasi isiyo ya kawaida katika kipindi ambacho watumishi wa serikali wanaotibiwa nje ya nchi wanadhibitiwa na rais, na Ndugai mwenyewe amekuwa “mgonjwa mkuu” aliyetibiwa nje katika kipindi hicho.

Mwaka jana, serikali ililiambia bunge kuwa nchi ilikuwa inadaiwa Sh 28.60 bilioni kwa ajili ya matibabu ya viongozi nje ya nchi, hasa India. Ndani ya miezi sita tu, deni hilo limekua hadi Sh. 45.73 bilioni. Hili ni ongezeko la Sh.17.13 bilioni.

Ongezeko la asilimia 60.71 ya deni ndani ya kipindi kifupi, wakati idadi ya viongozi wanaotibiwa nje imepungua, ni doa kwa dhamira ya Rais John Magufuli ya kupiga vita ufisadi na kudhibiti matibabu ya nje.

Kwa mujibu wa ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG), ongezeko hili ni la kati ya tarehe 30 Juni 2017 na tarehe 31 Desemba 2017.

Kwa kuwa limeongezeka katika kipindi ambacho wagonjwa wanaokwenda nje lazima waruhusiwe na rais, na “mgonjwa mkuu” aliyetibiwa nje ni Ndugai, ongezeko la deni la matibabu linahusu wote wawili – rais na spika.

Taarifa zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya deni hili imesababishwa na Job Ndugai. Kwa mujibu wa takwimu za CAG, Ndugai amekaa India kwa takriban miezi mitano, akiwa na wasaidizi wake na familia yake.

Posho ya mbunge anapokuwa nje ya nchi kwa siku moja ni dola 500; mtumishi wa bunge ni dola 450; mwenzi wa ndoa ni dola 300.

Kwa uchambuzi wa ripoti ya CAG, Ndugai amekaa India kwa miezi mitano, ambayo ni siku 150. Kama kwa siku moja alilipwa dola 500, ina maana kuwa kwa miezi mitano alilipwa dola 75,000. Kwa shilingi za Kitanzania, kwa viwango vya ubadilishaji fedha vya Sh. 2,170 kwa dola moja, Ndugai alitumia shilingi 162,750,000 kama posho ya kuishi India.

Akiwa India alikuwa na wasaidizi wawili – maana alihamishia ofisi yake huko huko hotelini. Kwa gharama ya dola 450 kwa siku, mara mbili, watumishi hawa walilipwa dola 900 kwa siku. Kwa siku 150 walizokaa India, maana yake walilipwa dola 135,000, sawa na Sh. 292,950,000.

Chanzo chetu kutoka Bungeni kimeliambia SAUTI KUBWA: “Kwa ujumla, matibabu ya Ndugai kwa miezi mitano yametumia posho za shilingi 455,700,000, na hapo bado gharama za hospitali huko India, na tiketi za ndege kwa watu wote hao, na bado gharama alizokuwa anatumia mkewe.”

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa ukaguzi wa CAG katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika hospitali za India.

Wakati ofisi ya spika inatoa gharama zote hizi kwa ajili ya matibabu ya Ndugai, kuna orodha ndefu ya wabunge ambao wamenyimwa huduma hiyo ambayo ni haki yao kisheria.

SAUTI KUBWA limeelezwa kuwa baadhi ya wabunge walionyimwa huduma hiyo, ni wapinzani, na wamekuwa wakitibiwa ndani na nje ya nchi kwa gharama zao binafsi, mikopo au michango ya ndugu na jamaa zao.

Chanzo kimoja kutoka bungeni kimesema: “Kwa kuanzia na Mheshimiwa Tundu Lissu, ambaye maisha yake yaliokolewa na michango ya watanzania, yupo pia Mheshimiwa Zubeda Sakuru ambaye hadi sasa anajigharamia matibabu, na ofisi ya spika imegoma kutoa chochote. Mheshimiwa James Mbatia alipovunjika mkono, alitibiwa India kwa jitihada binafsi; ofisi ya bunge ikakaa kimya.

“Mheshimiwa Ester Bulaya amegharamia matibabu yake mwenyewe, na Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza amejilipia gharama za kwenda Muhimbili, Nairobi na India, na hadi sasa ofisi ya spika inapiga danadana. Majuzi tu, tulimpoteza Mheshimiwa Kasuku Bilago, ambaye hadi anaaga dunia kwa kukosa matibabu ya uhakika, alikuwa anahangaika kujilipia, huku ofisi ya spika ikiwa imegoma kugharamia matibabu yake.

“Hii yote ni kujaribu kuonesha ni jinsi gani gharama za matibabu zinavyotolewa kwa upendeleo wakati wabunge wote kwa mujibu wa sheria wana haki sawa ya kupatiwa matibabu.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Bunge ya mwaka 2008, katika kifungu cha 24(1), “matibabu ya mbunge yatagharamiwa na Bunge ndani na nje ya Tanzania.”

Bunge limekuwa linatumia kifungu hiki kuidhinisha malipo ya matibabu ya Ndugai na baadhi ya wabunge, hasa wa CCM, lakini limekataa kutumia kifungu hicho hicho kutibu wabunge wengine, hasa wanaotokana na vyama vya upinzani.

Like
12

Leave a Comment

Your email address will not be published.