Jukwaa la wahariri lampasha Rais Magufuli kuhusu wasiojulikana

JUKWAA la wahariri Tanzania (TEF) limemtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua dhidi ya “watu wasiojulikana” wanaohatarisha uhuru na amani ya waandishi wa habari na raia wengine.

Ujumbe wa wahariri uliwasilishwa na Deodatus Balile (pichani), kaimu mwenyekiti wa TEF, katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari Duniani mjini Dodoma.

TEF imesema uhuru wa habari Tanzania upo “kitanzini,” na imeorodhesha matukio kadhaa yanayothibitisha kuwa waandishi wa habari, wahariri, wamiliki wa vyombo vya habari na raia wengine wanaishi kwa hofu.

Katika ujumbe wake, TEF imetumia fursa hiyo kukumbusha rais kuhusu kupotezwa kwa Azory Gwanda mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi ambaye alitekwa na “watu wasiojulikana” tarehe 21 Novemba 2017 na hajulikani alipo hadi sasa.

Lilimkumbusha pia madhira yaliyompata Ansbert Ngurumo, mhariri na mwandishi wa safu ya Maswali Magumu, alivyoponea chupuchupu kutekwa na “watu wasiojulikana” hatimaye Wasamaria Wema wakamficha nchi jirani, na sasa anaishi uhamishoni Ulaya.

Jukwaa la wahariri limerejea kauli yake liliyotoa awali katika tamko mwezi uliopita, juu ya haja ya kuwepo maridhiano ya kitaifa, kama njia ya kurejesha taifa katika misingi ya amani na mshikamano.

Liliitaka serikali kutotumia vibaya sheria za nchi dhidi ya waandishi wa habari, kama ambavyo maofisa wake wamekuwa wanapindisha kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari kufunga magazeti badala ya kushughulikia taarifa au habari husika katika gazeti, kama sheria inavyotaka.

Like
9
3 Comments
  1. Mtanzania 7 years ago
    Reply

    Sasa wanamwambia nani? Huyo raisi ndiye muhusika wa watu wasiojulikana?? . Hao ni watu wake.

    1

    0
  2. Kekofya Kamala 7 years ago
    Reply

    Watu kupotezwa, kutekwa, kuteswa, kusingiziwa Kesi, kuaibishwa katika jamii, kubaguliwa, kuharibiwa mali zao, kufungwa kinyume cha Katiba na sheria yanapaswa kukemewa na Watanzania wote bila kujali itikadi, vyama, dini au umahalia! Kamwe hatutabaki salama tusipokemea, kuzilinda na kuzitetea tunu hizi tulizoachiwa na wazee wetu! Hongereni Jukwaa la wahariri. No mwanzo mzuri.

    2

    0
  3. Jaimee 7 years ago
    Reply

    Upumbavu utaliangamiza taifa.Maana tumetumia muda na nguvu nyingi kupambana na ujinga tukasahau kupambana na upumbavu.Upumbavu ni ile hali ya kuujuwa ukweli,kuuona ukweli,lakini bado unaendelea kuamini katika uongo.

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.