Asilimia 40 ya digrii kutoweka katika miaka 10 ijayo

ASILIMIA 40 ya shahada zinazotolewa na vyuo vikuu sasa zitatoweka kwa kukosa umuhimu kwenye jamii katika miaka 10 ijayo, utafiti mpya umebaini.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya Ernst & Young unahusu shahada za kwanza na za uzamili. Badala yake, vyuo vikuu vitajikita katika kujenga na kuthamini “mafunzo yanayojengwa katika stadi za kazi na uzoefu,” na itakuwa inatolewa mtandaoni kuliko ya kukaa vyuoni.

Taasisi hiyo ilifanya utafiti kuhusu “chuo kikuu cha baadaye.” Ulifanyika katika vyuo vikuu vya Australia.

Utafiti huo umenukuu Michael Nguyen, ofisa masoko katika jiji la Sydney, Australia, akisema miaka mitatu aliyotumia chuoni haikumwandaa kwa kazi anayofanya sasa.

Utafiti umebainisha: “Mafunzo mengi tunayopewa vyuoni hayaendani na hali halisi ya maisha ambayo wanafunzi wakishahitimu hukumbana nayo. Miaka 10 ijayo, mafunzo katika vyuo vikuu yatatokana na halisi halisi kuhusu majukumu na changamoto za kazini.

Kuna watu watakataa shahada ya chuo kikuu ili wasomee fani wanayotaka katika mfumo wa vitendo zaidi kuliko nadharia, ili elimu yao iweze kuwafaa kazini. Hali hii imetokana na ukweli kuwa waajiri wengi wanapendelea waajiriwa wasio na shahada, na wasomi wenye shahada wanasikitikia kukosa elimu inayojikita katika vitendo.

Watu wapatao 3000, wakiwemo wanafunzi, waajiri na na viongozi wa vyuo vikuu, walihojiwa.

Ripoti inasema: “Wasomi wengi wanapohitimu wanakuwa na madeni makubwa, huku wakitumbukia kwenye jamii isiyoweza kuwaajiri. Zaidi ya nusu ya waajiri wa Australia wanasema baadhi ya shahada za menejimenti na biashara hazifai.”

Hata hivyo, asilimia 36 ya wanaosomea shahada za sanaa, utamaduni na sayansi ya jamii; na asilimia 41 ya wanaosomea sayansi na hisabati wanasema shahada zao zina umuhimu mkubwa. Shahada nyingine muhimu ni za unesi (87%) na ualimu (80%).

Kwa mujibu wa Press Scott, makamu mkuu wa University of Technology Sydney, anayesimamia kitivo cha elimu, tayari baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kubadili mitaala ili kutoa elimu inayoendana na mahitaji ya wakati.

Like
12

Leave a Comment

Your email address will not be published.