HUWEZI KUENDELEA KIUCHUMI NA KIFIKRA KWA KUIPINGA MITANDAO NA KUIPINGA GOOGLE

Ndugu zangu watanzania nawasilimu sana!

Ikumbukwe kwamba mpaka hapa ulimwengu ulipofikia ni juhudi za mwanadamu kuhakikisha dunia inakuwa ndogo hata kwa kiwango cha kijiji. Dhumuni likiwa ni kurahisisha mawasiliano ya kibiashara, kiuchumi, kisiasa na muingiliano wa kijamii (social integration). Lengo hasa la uanzishwaji wa mitandao, hasa katika ulimwengu huu wa Kibepari (capitalist world) ambao umejikita kwenye ukoloni mamboleo (Neo-colonialism) ni kufanya biashara, kukuza chumi za nchi husika, kutoa ajira na kuimarisha ulinzi.

Mitandano ya kijamii kama Twitter, Facebook, Instagram, LinkedIn, SnapChat n.k. haikuanzishwa kwa bahati mbaya! Uanzishwaji wake ni matunda ya taaluma ambayo vijana waliipata vyuo vikuu kama Harvard University. Mark Elliot Zuckerberg ni mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook mwaka 2004 akiwa chuoni Harvard na wenzake; ambapo mpaka kufikia mwezi wa huu (Aprili) 2018 Zuckerberg anamiliki utajiri unaofikia USD 66.4 billion. Ni miongoni mwa matajiri 100 duniani. Jan Koum na mwenzake Brian Acton ndio waanzilishi wa WhatsAPP mwaka 2009. Miaka 9 kutoka sasa ambapo baadae Facebook waliinunua kwa USD 19.3 billion.

Mitandao hii iliweza kusambaa ndani ya vyuo na ikatoka na kuanza kutumiwa na wamarekani na baadae kusambaa dunia nzima. Mitandao hii sio mali tena ya Wamarekani. Haiwanufaishi wamarekani peke yao. Kwasasa kila mtu, shirika, taasisi ama serikali mbalimbali duniani huitumia mitandao hii kwa malengo mbalimbali ya kimaendeleo. Mitandao imekuwa nyenzo bora ya kufanyia tafiti mbalimbali zikiwemo afya, elimu, mahusiano, maswala ya uzazi, magonjwa, vifo vya kina mama na watoto pamoja na maswala ya jinsia.

Jambo la msingi hapa ni kuifikiria nchi kama China na Urusi ambazo kwa nyakati tofauti zimekuwa zikitumiwa kama mifano na sababu za kuzima mitandao kwenye nchi nyingine. Baadhi ya nchi za kiafrika Tanzania ikiwemo zimekuwa zikiiona mitandao ya kijamii kama ‘laana’. Kama kitu cha ‘uchochezi” ama kudaiwa kuzichonganisha serikali za nchi husika na wananchi wake!

China na Urusi hawatumii mitandao (media platforms) kama Facebook, YouTube, Twitter, Instagram nk. Hii haimaanishi wananchi wa nchi hizi hawawasiliani. Mitandao yao (media platforms) ambayo hufanya kazi kama jinsi mitandando ya mataifa mengine hufanya. Mfano, Weibo (Twitter ya China), WeChat, Tancent QQ, Toudou Youku (YouTube ya China), Vkontakte (Urusi) nk. Imekuwa kiungo na kichecheo cha uchumi kwa nchi hizo. Wachina na Warusi hupoteza muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii huenda kuliko hata kwa nchi kama Tanzania. Imekuwa ikitumika kwa mawasiliano baina na miongoni mwa watumiaji wake. Imekuwa kichocheo kikubwa kibiashara na hivyo kuchochea uwekezaji na ufanyikaji wa biashara kubwa (macro business) n.k. Mfano mpaka kufikia mwezi Juni mwaka 2017 pekee, Urusi ilikadiriwa kuwa na watumiaji mitandao takribani 109.6 million, ikiongozwa na China, India, Marekani, Brazil na Japan.

Kwahiyo, ukijiona uko bado nyuma ya technolojia, kama anavyoandika “chotera” kule JamiiForums, jua uko katika giza nene ambalo ni sawa na kua ndani ya boksi wewe mwenyewe ukadhani unajua vitu vingi kumbe hujui kitu. Hivyo Google ni search ambayo imegeuka kuwa shule huria kwa kila mmoja wetu. Imekuwa ni chanzo cha taarifa na habari mbalimbali. Inasikitisha kuona hata wapiga vita mitandao walipata na kuandika kazi zao mbalimbali za kitaaluma (thesis and dissertations) kwa msaada wa google na kwingineko. Wengine wamepata degree zao, masters, PhD na hata u-Professor kwa msaada wa mitandao hiyo.

Siku hizi sio ajabu tena kuona hospitali mbalimbali na wataalamu katika nyanja ya afya (doctors and specialists) kuwaona wakiitumia mitandao kuwasiliana na wagonjwa wao. Kadhalika, kutoa na kupokea taarifa na maendeleo ya wagonjwa. Lakini, ni wanasiasa hawahawa waliitumia mitandao ya kijamii kutangaza na kunadi sera zao kipindi chote cha uchaguzi mkuu kutoka miaka ya 2000. Wameitumia kupiga kampeni, kukutana na wanachama wao, kupanga timu za kampeni, kushawishi na kuwakutanisha watu wa makundi mbalimbali n.k. Ni mitandao hii hii ambayo iliwasaidia wengine kupata matokeo ya kura kabla hata ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi nakujua hali zao kisiasa. Lakini ni mitandao ambayo mpaka leo imekuwa ikitumiwa kueneza propaganda za vyama vya siasa na imebaki kuwa kiunganishi pekee kati ya wananchi na Bunge lao baada ya uhuru huo kufinywa. Hivyo mitandao itabaki kuwa muhimu. Imetufanya twende na wakati na kukimbizana na maendeleo ya Dunia! Kwenye mitandao ndipo watu hufanya biashara za pesa nyingi. Kwenye WhatsApp wafanya biashara
wakubwa na wadogo wamekuwa wakitumiana picha za bidhaa mbalimbali na kufanya mauzo yao huko. Kumekuwepo na urahisi kwenye biashara. Wafanyabiashara na wateja wamekuwa wakiwasiliana na kukutana kwa urahisi zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Watu wamekuwa mabilionea kupitia mitandao. Maisha yamebadilika na mitandao imekuwa mbadala wa mama ntilie, machinga, na hata sehemu ya ‘dada poa’ (sexual workers) kupungua. Kwa lugha nyepesi imetoa mwanya kwa vijana kujiajiri.

Mfano mzuri ni mmiliki wa mtandao mkubwa wa biashara wa Alibaba, Amazon, ZoomTanzania, JamiiForums na Ebay. Wote hawa wameweza kujiajiri na kuajiri. Mitandao imebadili kipato na maisha yao na familia zao. Leo hii sio ajabu tena kuona vijana wengi wamejiajiri na kuendesha familia zao kupitia mitandao hii. Na sio ajabu huenda sehemu ya pato la taifa (GDP) letu linaweza kuwa linatokana na uwepo wa mitandao.

Teknolojia hurahisisha maisha, hatuwezi kama taifa tukawa na fikra zinazofanana au tuwe na fikra wanazotaka viongozi tu. Hapana! Kuna usemi wa kizungu ambao husema The minds that think alike are not think! Tukiwa na taifa lenye mfumo mmoja wa kufikiri (linear thinking) basi hilo haliwezi tena kuitwa taifa. Lazima tufikiri tofauti na kuvumiliana. Ujenzi wa nchi sio ujenzi wa familia. Ujenzi wa nchi si lele mama. Ujenzi wa nchi una makwazo, unakukatishana tamaa lakini kama watu wa jamii moja (WATANZANIA) ujenzi wa nchi ni wajibu wetu sote. Serikali inawahitaji wananchi na wananchi wanaihitaji serikali. Uhai, afya na kipato kwa kila mmoja wetu kama Taifa utatujengea ujasiri, uzalendo na kusonga mbele kama Taifa. Tutazalisha Taifa la watu wenye furaha na wenye kuwajibika kwa moyo.

Nchi hii itastawi! Kama taifa lazima tuwaze na kufikiri tofauti lakini kwa kuheshimiana. Tuwe tayari kujifunza, kukosoa, kukosolewa na kuwa watu wakufikia muafaka/maridhiano. ‘Double standards’ zitaliangamiza Taifa. Lakini zaidi, tufikirie kuwazalisha kina Alibaba, Amazon, Ebay na ZoomTanzania wakutosha kuliko kuwaza kuibana mitandao. Kuliko kuwaza kuiuwa JamiiForum ama blogs zilizoanzishwa na vijana kama sehemu ya kujiajiri. Tutafakari upya gharama zilizowekwa na Serikali kuhudumia mitandao Tufikirie kuanzisha mbadala wa Twitter, Facebook, Google, WhatsApp n.k. kama walivyofanya uchina na urusi. Ambapo walipoona mitandao kutoka mataifa ya Magharibi haina tija, waliamua kuwekeza kwenye teknolojia na kufungua njia mpya za kimawasiliano kwa wananchi wao. Lakini lazima tukiri, siasa za China na Urusi sio siasa za Tanzania. Katiba ya China na Tanzania zinatofautiana kwa kiwango kikubwa sana. Sera na dira za kimaendeleo zinatofautiana kwa kiwango kikubwa.

Uchumi wa Tanzania na China ama urusi ni mbingu na ardhi. Leo hii nchini China zipo simu za lugha ya kichina tu. Tuwatumie wataalamu wetu na kuwashawishi wawekezaji zaidi kuja kuwekeza na hatimaye tuwe na simu zenye Kiswahili tu ama hata Kipare na Kingoni ikiwezekana. Tuwape watanzania mbadala wa mawasiliano sio kuwanyamazisha kama tulivyofanya kwenye Bunge! Na ikumbukwe kwamba, teknolojia ni pana sana na huwezi kupambana nayo. Marekani nchi yenye teknolojia yenye nguvu leo hii inalia kudukuliwa na Urusi. Ni kweli mitandao ina changamoto zake. Ina madhara yake kama hatatumiwa ipasavyo. Lakini faida ni kubwa kuliko hasara. Tuzidi kusambaza elimu kwa watanzania ya namna bora ya kuitumia mitanzao! Tuangalie mitandao kama resource and not a liability! Kama fursa na sio mzigo. Kwahiyo, tuimarishe uchumi wa Tanzania na watanzania wenyewe.

Tukishajiimarisha kiuchumi ni rahisi kuwa na mifumo yetu ya kimawasiliano. Huwezi kujitenga na dunia ilihali uchumi wako unachechemea. Tuboreshe mifumo yetu ya elimu na kuwekeza huko. Hakika Taifa litapona! Kwa muktadha huo HUWEZI KUENDELEA KIUCHUMI NA KIFIKRA KWA KUIPINGA MITANDAO NA KUIPINGA GOOGLE.

Wenu Katika Ujenzi wa Taifa.
Goodluck Mshana © 2018
0717935721

Like
16
2 Comments
  1. Mtanzania 7 years ago
    Reply

    Licha ya kudhibiti waandishi na kutishia mitandao. Dikteta anajisahau kuwa Tz siyo kisiwa kiuchumi. Wakati wa mkutano wa Common Wealth, maraisi wenzake wamekutana na kupanga business deal. Yeye kamtuma mama Samia??. Yeye kabaki nyumbani anafukuzana na wapinzani na kufungua kuta au kupokea kandegea ka ATC nk. Nafikiri dikteta hajiamini kabisa hata kutoka nje ya nchi, kila atakapofika, atachukuliwa kama dikteta muuaji, bora kukaa nyumbani au kutembelea dikteta wenzake Kagame na Museveni. Wtz tuna bahati mbaya sana kumpata Magufuli.

    0

    0
  2. Mtanzania 7 years ago
    Reply

    Waziri wa habari na wa masiliano, nilimshangaa akiongea bunguni kuwa nchi zote duniani hata USA, zina-control mitandao. Ni kichekesho kitupu na huzuni kudanganya watu kitoto na kijinga. Kiongozi mkongwe kama Mwakyembe hatungetegemea amu- support dikteta, na kuongea ujinga na unafiki bungeni, ili tu amfurahishe mkubwa wake, bahati, mbaya sana Tz yetubya leo. CCM iko wapi? Ni ile ya baba wa taifa? Najiuliza kila siku?

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.