DIWANI wa Kata ya Sombetini, Jiji la Arusha, Bakari Msangi, amefunguka namna alivyoshambuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya akiwa na walinzi binafsi.
Anadai kwamba Sabaya wakati akimshamblia, alikuwa na walinzi wake binafsi sita waliobeba silaha ikiwamo bastola mbili.
Diwani huyo ameiambia SAUTI KUBWA kwamba ameamua kuyasema hayo baada ya Sabaya na wapambe wake kusambaza taarifa kuwa Februari 9, mwaka huu, alipigwa na baaadhi ya watu baada ya kumfumania “akiwa na mke wa mtu.”
Msangi akielezea namna tukio hilo lilivyokuwa anasema, Februari 9, mwaka huu majira ya saa 11 jioni alipokea simu kutoka kwa Mohamed Asaad, akimweleza kuwa mkuu huyo wa wilaya amevamia dukani kwake, hivyo kama anafahamiana naye anaomba akamsikilize na kumsaidia. Assad ni mmiliki wa duka la mapazia la Shaahidi Storea lililopo Barabara ya Nyamwezi karibu na Soko Kuu jijini Arusha.
Msangi anasema: “Mimi nikaenda pale dukani nikakuta mlango wa chuma umefungwa nikagonga hawakufungua, nikaamua kuuvuta juu nikaingia. Kweli nikamkuta Sabaya na vijana wake sita wamewaweka chini ya ulinzi wafanyakazi na wateja waliokuwa kwenye hilo duka, wanawapiga,” anasema Msangi na kuongeza.
“Nikamuuliza Sabaya kuna shida gani? Akaniambia hawa Waarabu ni wahujumu uchumi, wanafanya biashara haramu wanauza dola feki, wanauza bidhaa hawatoi risiti, akaniorodheshea makosa kibao…
“Nikamwambia mimi kama diwani wajibu wangu ni kuwatetea wananchi wa Arusha, lakini wewe hapo ulipo siyo TRA, (Mamlaka ya Mapato Tanzania), siyo Takukuru wala Usalama wa Taifa na siyo polisi, iweje uwanyanyase hawa badala ya kutumia vyombo husika vikaja kuwakamata hawa watu?”
Msangi anasema kuwa kauli hiyo ilionekana kumuudhi Sabaya ambaye bila simile alimgeukia na kuanza kumshushia kipigo.
“Aliwaamuru vijana wake waninyang’anye simu zangu, wakachukua na fedha walizonikuta nazo kama laki tatu na elfu tisini, wakanipiga vibao wakanikalisha chini,” anasema Msangi na kuongeza.
“Walipokuwa wananikalisha, niligoma, wakaamua kunifunga pingu mikononi. Wakaanza kunipiga, nikamwambia Sabaya haki ya Mungu mtaniua, lakini sitaondoka hapa mpaka nisimamie haki ya hawa watu.
“Wakati haya yakiendelea, Sabaya alimchukua mdogo wa mwenye duka na kuingia naye chumba kingine ambako walikuwa wakizungumza. Baadaye nikagundua kuwa alikuwa akimuamuru ampigie simu kaka yake, Asaad ili aje dukani kwake…”
Diwani huyo anasema kuwa iIlipofika saa tatu usiku alimwambia Sabaya awaache, lakini aligoma na baadaye kuwapiga vibao wateja waliokuwamo ndani ya duka na wadogo wa Asaad, kisha aliwaambia waondoke.
“Sabaya akapiga simu kwa OC CID akamwambia kuna watu nimewakamata ni wahujumu uchumi nataka kuwaleta hapo polisi. Wale ndugu zake Assad wawili wakaingizwa kwenye gari la walinzi aliokuwa nao – mabaunsa, mimi nikaingizwa kwenye gari alilokuwa amepanda Sabaya…
“Msafara ukaanza kuelekea Central, tulipofika tukamkuta OC CID, Gwakisa kasimama nje anatusubiri na mimi nikataka kushuka, lakini Sabaya akanizuia.”
Diwani Msangi anasema Sabaya alimwambia hajamshusha polisi kwa sababu hajamaliza kazi naye, anataka akamuonyeshe nyumbani kwa Ally Assad Ajirin na kwa kaka yake Mohamed Assad Ajirin. Anazidi kusimulia:
“Tukaenda kwa Ally Assad Ajirin, tukafika tukagonga mlango hawakufungua. Kidogo wakati tunatoka, tukakutana na mzee mmoja anaongea na simu akajua labda ni mzee wa familia hiyo akamkamata baadaye akamuacha” anasema Msangi na kuongeza.
“Tukaondoka tukaenda kwa Mohamed Assad tulipofika akavunja mlango akaingia ndani akawakuta mke wa Mohamed na watoto. Hawakumkuta Mohamed, hivyo tukaondoka.
“Tukatoka tukazunguka mjini mimi nikiwa nimefungwa pingu. Baadaye wakaenda supermarket ya Panone pale Ngarenaro wakanunua vinywaji wakawa wanakunywa, kisha tukaondoka mpaka pale Hoteli ya Tulia, iko pale WhiteRose,”.
“Tulipofika hapo wakaingia ndani wakaniacha mimi kwenye gari wakawa kama wamenisahau. Palepale nikaona mfuko waliokuwa wameweka simu, nikavivuta nikafanikiwa kuchukua simu.
“Simu kubwa nikaiicha ndani ya chupi nyingine ndogo nikaitumia kumpigia mke wangu. Nikamwambia yote yaliyonikuta, nikamwambia anifuate ila aje na jirani yetu hapo nyumbani.
“Baadaye kidogo, Sabaya akatoka akiwa kabadili nguo, mwanzo alikuwa kavaa kaunda suti sasa ametoka kavaa koti, akaja kwenye gari akaniambia nasikia kuwa watu wanakutafuta ni nani, nikamwambia sijui…
“Sabaya akasema itakuwa ana simu huyu embu mpigeni ‘teru’ (mkagueni). Walinikagua, lakini walishindwa kuziona kwa sababu zilikuwa ndani ya suruali.
“Sabaya alimuona mke wangu eneo lile, jirani na gari lake, akahoji akisema ‘huyu malaya anayekufuatilia ni nani?’
“Akawa anawaagiza mabaunsa wake waende wakamchukue, nikawaambia mtamchukuaje mke wangu, baadaye nikaamuriwa kwenda kuzungumza naye nikiwa chini ya ulinzi…
“Sabaya akaja akamtolea mke wangu bastola akamwambia leo naenda kumuua Bakari. Mke wangu akapiga ukunga, Sabaya akaona kuna shida, lakini mimi nikamwambia mke wangu asiwe na wasiwasi kwani hapo walipofika hawezi kufanya chochote nikamwambia akanisubiri Arusha Technical …
“Mabaunsa wakaniingiza kwenye gari tukaondoka tulipofika pale Petrol Station ya Mount Meru, kabla ya taa za barabarani, wakasimamisha gari wakaniambia nishuke nikimbie. Nikagoma, wao wako na bunduki na bastola nakimbia vipi? Wangeweza kunipiga risasi nikawaambia wanipeleke mahali mke wangu yupo…
“Wakaenda wakanishusha pale Arusha Technical ambapo mke wangu alikuwa wakanipiga mkwara. Nikaondoka kufika nyumbani ndiyo nikaanza kusikia maumivu, nikawapigia viongozi wenzangu sikuwapata ….
“Nikaamua kumpigia simu Mkuu wa Mkoa, Iddi Kimanta nikamweleza kila kitu, yule mzee alilia kabisa wakati naongea naye. Akawapigia RPC na OCD akawaeleza kisha akaniambia tukutane Polisi, nilipofika nikawakuta viongozi wamejaa …
“Ilikuwa saa sita usiku, wakaniandikia PF3 nikaenda hospitali kutibiwa, hivi napokwambia naendelea na matibabu na polisi wako kwenye uchunguzi.”
Diwani huyo alisema kuwa hakuweza kutambua namba za gari alilokuwa akitumia Sabaya kwani wakati wakitoka dukani kwa Assad alikuwa ameweka namna za DFP na walipokuwa wakitoka hoteli ya tulia alikuwa amebandika namna za UN.
Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, James Ruge alisema endapo tukio hilo lilitokea, halina uhusiano na taasisi anayoiongoza, na kubainisha kuwa “hiyo ni jinai.”
Sabaya hakujibu simu za mwandishi wetu wala ujumbe mfupi wa simu uliomtaka azungumzir sakata hili na tuhuma hizi.