CHAUMMA KUTUMIA GESI ASILIA, MADINI KUFUTA UMASKINI

EDWARD Kinabo, Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma, wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) amesema chama hicho kikiingia madarakani kitatumia “sera ya kuthaminisha ardhi kuwa hisa” ili kuwezesha wananchi kuwa wabia, wamiliki na wanufaika wa moja kwa moja wa miradi mikubwa ya uwekezaji katika gesi asilia na madini kupitia serikali zao za mitaa na vijiji.

Kwamba, chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa maeneo ya uwekezaji, wamekuwa wakiambulia fidia na kisha “kuachwa solemba” katika lindi la umaskini usiokwisha, kwasababu mapato mengi yatokanayo na miradi hiyo huishia kwa mwekezaji na serikali kuu.

Akihutubia wananchi wa jimbo la Mtama katika mikutano ya Operesheni Chaumma for Change (C4C) hivi karibuni, Kinabo amesema mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) hauwezi kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa Lindi na Mtwara kwasababu wananchi wameachwa nje kabisa ya umiliki wa mradi huo na wataishia tu kuwa wateja wa kuuziwa mitungi ya gesi kama watu wengine.

“CCM sera yao wanawapa fidia mara moja, mnaachia ardhi, mnaondoka, halafu wao wanaendelea na mwekezaji. Chaumma sera yetu ni kuhakikisha ile ardhi yenu inayochukuliwa kwaajili ya mradi inapimwa, inathaminishwa na kugeuzwa kuwa mtaji na hisa ili ninyi wananchi muwe wamiliki, muwe wabia na mnufaike na mradi wa gesi kila mwaka”, alisema Kinabo na kuongeza:

“Ni kweli gesi asilia ni mali ya Watanzania wote, lakini gesi asilia ni mali ya watu wa Lindi na Mtwara kwanza kabla ya Watanzania wote. Haiwezekani mapato ya gesi asilia yaende Dar-es-Salaam, yaende Dodoma halafu ninyi watu wa Lindi na Mtwara mnabaki kwenye umaskini. Tunataka wale ambao Mwenyezi Mungu aliamua kuwaweka juu ya ardhi yenye gesi, ndiyo wawe watu wa kwanza kunufaika na gesi yao,” alisema.

Alisema sera hiyo ya Chaumma ndiyo jibu la kumaliza umaskini wa mkoa wa Lindi ulio katikati ya gesi asilia, dhahabu, nikeli na madini ya marble na pia ndiyo jibu la kumaliza umaskini wa wananchi wa mikoa yote nchini inayozungukwa na madini

“Kwa sera hii, ambayo kwa kimombo inaitwa “land for equity policy”, yaani sera ya kuigeuza ardhi yenu kuwa hisa zenu, watu wa Lindi na Mtwara mtakuwa mnapata gawio kila mwaka kwa kipindi chote cha uhai wa Mradi wa Gesi Kimiminika”, alisema Kiongozi huyo na ambaye pia ni mdau wa sekta mipangomiji na urasimishaji ardhi.

“Fedha zitakazopatikana zitaboresha makazi yenu, tutavunja nyumba za udongo, watu wa Lindi mtapata nyumba bora, mtapata maji ya uhakika na mtapata huduma bora za afya kwasababu ya mapato ya gesi asilia ya kila mwaka.Chaumma itawakomboa”, alifafanua.

“Tunajua serikali imetoa fidia ya bilioni 5.71 kwa wananchi waliopisha eneo la hekta 2071. Tunajua Mradi wa Gesi Kimiminika utaanza Kata ya Mbanja, mitaa ya Likong’o, Mto Mkavu, Likong’o na Masasi ya Leo, lakini hoja ni kwamba fidia pekee haitoshi. Sisi tukiingia madarakani tutahakikisha mnakuwa wanufaika kwa wakati wote wa mradi,” alisisitiza.

Akizungumzia suala la gesi asilia kwa jimbo la Mtama, alisema.

“Hapa Mtama, serikali kupitia shirika la maendeleo ya petroli (TPDC) inaendelea kufanya tafiti za kutafuta gesi asilia katika vijiji nane vinavyopakana na mkoa wa Mtwara. Na hapa pia gesi ikigundulika, wanakijiji wataambulia fidia tu, hamtanufaika moja kwa moja na mapato yatokanayo na mauzo ya gesi asilia.”

Akitoa mfano wa gesi asilia ya kisiwa cha Songosongo, Kinabo alisema ukiondoa fidia, ushuru wa huduma na umeme, wananchi wa Songosongo bado si wanufaika wa moja kwa moja wa mradi huo licha ya kutoa ardhi yao.

“Chaumma tukiingia madarakani tutapitia upya mikataba iliyoingiwa na serikali katika gesi asilia na madini ili kuhakikisha nchi yetu inapata mapato ya kutosha na Watanzania wote wanafaidika…lakini tutapiga hatua moja mbele kwa kuhakikisha wananchi walio katika maeneo yaliyotoa ardhi kwaajili ya uwekezaji wanakuwa ni wabia na wanufaika wa moja kwa moja wa uwekezaji kupitia serikali zenu za vijiji na mitaa,” alisisitiza Kinabo.

Like