Chanjo ya Corona: Padri Kayombo ajibu maswali ya Gwajima

KUMEKUWEPO na mjadala mkali kuhusu chanjo ya Corona, hawa wakiipinga na wengine wakiitetea. Katika mnyukano wa maoni kuhusu chanjo hii, Askofu Josephat (Rashid) Gwajima na Waziri wa Afya Dorothy Gwajima wamekuwa katika mvutano mkali ambao umechanganya baadhi ya wananchi. Wakati askofu anasema chanjo ni hatari hazifai, waziri (ambaye huko nyuma alikuwa kundi moja la askofu) anasema chanjo ni muhimu, zinafaa. Baadhi ya maswali ambayo yanaendelea kuulizwa ni iwapo chanjo zinaharibu DNA, iwapo zinaua uzazi, iwapo ni salama, na hasa kwanini chanjo ya Corona imewahi kuliko chanjo nyingine. Katika andiko hili, Padri Laurean Kayombo wa Jimbo Katoliki Njombe, anatoa maoni yake akijaribu kujibu baadhi ya maswali hayo. Anaanza kwa kusema Kanisa halizuii chanjo ya Corona. ENDELEA.

KANISA KATOLIKI HALIPINGI CHANJO DHIDI YA UVIKO-19.

Tangu awali naomba kutangaza upande gani nipo, katika mjadala ambao umedumu kwa muda mrefu miongoni mwetu. Mimi nimechanjwa chanjo dhidi ya UVIKO-19 tarehe 3 Agosti 2021; kadi yenye namba 5250.

Kanisa katoliki halipingi chanjo ya uviko-19: Papa amechanja, makardinali wake pia wamechanja, Askofu Mkuu wa Dar es Salaam amechanja na maaskofu wengi wengine pia wamechanja. Yaliyobakia ni maoni binafsi, nayo ni haki ya kikatiba kwa kila Mtanzania.

Naomba kutoa maoni yangu binafsi katika jukwaa hili si kwa lengo la kuwapa amri bali kupanua uelewa na kuongeza hamasa. Nakaribisha pia kwa moyo wa kujifunza maoni tofauti na yangu yenye nguvu ya hoja.

Mimi ni padre mkatoliki na mwanafunzi wa Kemia katika ngazi ya masters mwaka wa mwisho. Miongoni mwa kozi nilizosoma ni pamoja na utengezaji wa madawa na chanjo; usajili; usafirishaji; utunzaji na matumizi sahihi ya madawa na cha chanjo maridhawa!

ASILI YA CHANJO

Kwa miaka mingi, chanjo ilikuwa ikitengenezwa kwa kufubazwa makali ya “mdudu” anayesababisha ugonjwa kwa kumfanya nusu mfu ( kwa joto, umeme au kemikali) na kumwingiza katika mwili wa mwanadamu au mnyama! Seli ndiyo sehemu chanjo huenda kufanya kazi.

Seli ni kama nyumba yenye chumba; sebule na veranda. Katika seli chumba ni nucleus, nayo ni makao makuu ya malkia wa seli. Malkia huyu huitwa kitaalam kama DNA.

Malkia hatoki chumbani ,lakini hutawala shughuli zote za seli. Lolote alitakalo hulitanya kwa njia ya watumishi wake. Mtumishi au mjumbe mmojawapo wa malkia DNA ni mRNA. Kazi ya DNA ni pamoja na kutawala utengenezaji wa protini mbali mbali katika seli.

Protini zote hutengenezwa sebuleni mwa seli (cytoplasm). Malkia (DNA) hutoa amri kwa sebule kutengeneza aina ya protini inayohitajika. Mjumbe anayeleta amri ya DNA sebuleni ni mRNA.

Kinga zote za mwili ni aina fulani fulani za protini. Mdudu wa ugonjwa fulani aliyefubazwa anapoingizwa mwilini kama chanjo kwa njia ya sindano au matone au vidonge huenda kukaa sebuleni mwa seli.

Malkia (DNA) hushituka kuwa sebuleni kuna mgeni aliyeingia bila hodi. Hutoa amri kwa mRNA kwenda sebuleni kutengeneza aina fulani ya protini itakayotumika kumwangamiza mgeni huyu.

Kwa vile mgeni mwenyewe kafubazwa, mashambulizi humwangamiza kwa urahisi kwa kutumia protini chache tu. Protini nyingi hubakia hapo sebuleni kama kinga endapo “mdudu” anayesababisha ugonjwa husika ataingia, ili aweze kushambuliwa na kuharibiwa na kutolewa nje kama uchafu kwa ya jasho; makamasi; mkojo na kadhalika.

Utaalam huu wa kumwingiza “mdudu” aliyefubazwa mwilini kama chanjo una changamoto nyingi. Kubwa ni uwezekano wa “mdudu” huyu kuzinduka kabla ya protini za kinga kutengenezwa, na hivyo kumdhuru mwenyeji wake, hata kumwangamiza kwa kifo.

Changamoto hiyo iliwafanya wataalamu kutafuta njia mbadala ya chanjo. Badala ya kumwingiza “mdudu” aliyefubazwa ili mRNA atoke chumbani kwa malkia kuja sebuleni kutengeneza protini za kinga, ilibidi mRNA atengenezwe kwenye maabara nje ya seli, aingizwe sebuleni kwa njia ya sindano, matone na vidonge ili kutengeneza protini za kinga kwa “mdudu” husika.

KWA NINI CHANJO YA UVIKO-19 IMEWAHI SANA?

Mwaka 2003 ulizuka ugonjwa wa virus huko China ulioitwa SARS (Severe and Acute Respiratory Syndrome). Tekinolojia ya kutengeneza tRNA kwenye maabara ilitumika kupata chanjo ya ugonjwa huu.

Mwaka 2013 ulizuka ugonjwa wa MERS (Middle Eastern Respiratory Syndrome) huko Saudi Arabia. Teknolojia hii hii ilitumika pia kupata chanjo.

Kuna makabila mengi sana ya virusi na ndani ya makabila hayo koo nyingi sana na ndani ya koo familia nyingi za virusi. Virusi vya Uviko-19 ni ukoo mmoja na SARS na MERS hivyo imekuwa rahisi kutumia tekinolojia ile ya kutengeneza tRNA katika maabara na kutumika kama chanjo dhidi ya uviko-19 kama ilivyotumika kwa SARS na MERS.

MAUDHI YA CHANJO

Chanjo zote na dawa zote ni sumu, iwapo hazitatumika kwa kufuata kanuni na taratibu zake. Hivyo, anayepokea chanjo huweza kupatwa na maudhi mbali mbali kama vile kutokwa na jasho jingi, kuharisha, kichefuchefu, kutapika, kuchoka na kadhalika. Kama ilivyo kwa dawa nyingine zote, kanuni na taratibu zikikiukwa, hata vifo huweza kutokea. Maudhi haya madogo madogo huweza kutokea lakini si kwa kila mtu.

Mifano michache: Miaka ya 1970 chanjo ya ndui ilipotolewa, madonda makubwa yalijitokeza sehemu za chanjo na kuacha makovu ya kutisha katika mabega ya mkono wa kushoto.

Chloroquine, dawa ya Malaria, ilipokuwa inafutwa ili kuingiza SP, maudhi mengi yalijitokeza. Na kwa kukiuka kanuni na taratibu, vifo vichache pia vilitokea. Hali hiyo hiyo pia ilijitokeza wakati SP inafutwa ili kuingiza ALU kama tiba ya Malaria.

UPINZANI DHIDI YA CHANJO

(i) Historia
Mnamo 1994, chanjo ya Pepopunda ilipoingizwa Tanzania ilileta taharuki kubwa kwa jamii. Taharuki hii ilienea hata kwa baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini.

Hoja kubwa ilikuwa, “kwa nini kuchanja wasichana wa miaka 15 na akina mama wenye umri wa kuzaa tu?” Katika shule za msingi na sekondari, watoto wa kike walihimizwa kutoroka chanjo hiyo.

Hoja iliyojengwa ni kuwa “Wazungu walikusudia kupunguza rutuba ya uzazi kwa Waafrika.” Sasa imepita miaka 20 na zaidi. Hali ya rutuba ya uzazi kwa binti zetu au akina mama katika familia ipoje?

(ii) Mamboleo
Upinzani dhidi ya Uviko-19 unasababishwa na hoja mbali mbali kama:

(a) Uchumi
Kampuni kubwa kadhaa zimetengeneza chanjo mbali mbali, hadi sasa zikadiriwa kuwa zaidi ya kampuni 11. Kila mwamba ngozi huvutia kwake ili kutumia fursa hii ya kujulikana na kujinufaisha kiuchumi. Mzozo wa kuchafuana na kuharibiana biashara ulianzia hapo.

(b) Siasa
Ili kujipatia umaarufu wa kisiasa kwa wapiga kura wao, baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wanatoa matamko mbalimbali kuhusu Corona au chanjo – tena mengine yanakizana. Kwa mfano, kwa nyakati tofauti, viongozi wa siasa wamewahi kutamka hadharani “hakuna Uviko-19 Tanzania.” Baadaye wakasema Uviko-19 ilikuwepo, ila imeondoka kwa dua, kupiga nyungu na kutumia kwa wingi limau, ndimu tangawizi na kadhalika. Baadaye, viongozi hao hao wakatwambia kuwa kuvaa barakoa na kutumia chanjo ni kutomtegemea Mungu. Kwa hiyo, hakuna haja ya barakoa wala chanjo!

Leo, baadhi ya viongozi wa siasa, tena walio katika nafasi zile zile walizokuwepo zamani, ndio wanatuhimiza tutumie chanjo. Wamechangia katika sintofahamu. Wananchi waamini lipi? Waache lipi?

(c) Mitandao ya kijamii
Katika ulimwengu wa leo, hatuwezi kuishi kiufanisi bila mitandao ya kijamii. Kwa njia ya mitandao ya kijamii, habari hutufikia kwa wepesi zaidi, kutuunganisha wanajamii, kupatikana kwa misaada mbali mbali kwa njia ya “mikeka” ndani ya mitandao.

Hata hivyo, si kila kiandikwacho mitandaoni ni sahihi. Lazima kichunguzwe, na watu wahoji kila wanachopokea mitandaoni, ili kujiridhisha kuwa habari hiyo imetoka katika chanzo cha kuaminika.

Mbona mara kadhaa tumesoma mitandaoni kuwa Papa ameruhusu mapadre waoe au ameruhusu ushoga kanisani au mashoga waruhusiwa kuwa mapadre wa Kanisa Katoliki? Yote hayo ni ya uwongo, lakini wapo ambao wameyatumia kama taarifa sahihi, na wakayatumia kushawishi wenzao dhidi ya Kanisa.

Si tu kwa Papa, bali hata kwa maaskofu au viongozi wa vyama vya siasa, na hata serikali. Wamewahi kuzushiwa taarifa nyingi za uwongo, zikaenea kwa kasi kwa nguvu ya wabaya wao. Watu wakaziamini.

Baadaye, kwa kuchelewa sana, ndipo inaletwa taarifa kuonyesha kuwa taarifa hizo si sahihi – na haiwafikii wote waliosoma taarifa ya awali. Kwa hiyo, jambo muhimu hapa si kuamini kila kiandikwacho mitandaoni, bali muhimu ni kuzingatia CHANZO cha taarifa hiyo.

(d) Maono/ufunuo wa kidini
Baadhi ya viongozi wa kiimani wameenda mbali hadi kueleza kuwa wamepewa ufunuo wa Mungu kuhusu haya wanayosema juu ya maradhi mbalimbali, ikiwemo Uviko- 19na chanjo ya Uviko-19, kwamba ni hatari kwa mstakabali wa Mwafrika.

Miaka si mingi iliyopita, tuliambiwa juu ya “ufunuo wa kunywa Kikombe Kimoja Tu cha Babu wa Loliondo (apumzike kwa amani) ambacho kilisemekana kinatosha kutibu magonjwa mengi sugu kama Ukimwi, Kisukari na BP, kuyataja kwa uchache! Bahati mbaya “ufunuo” huo waonekana kama vile ulipita katika jamii yetu pasipo kuacha funzo. Ni bahati mbaya kwamba bado kuna watu wanatafuta au wanafuata ufunuo kuhusu Uviko-19 na chanjo yake!

KUCHANJA NI HIARI AU LAZIMA?

Kisiasa, chanjo hii ni hiari; ndivyo tulivyoambiwa na viongozi wetu. Kwa maoni yangu, kiutendaji, chanjo ni ya lazima. Ukichanja unapata cheti na sasa cheti kitakuwa si cha karatasi bali cha kielectoniki kama kadi ya ATM ya banki.

Hivyo, vyeti hivi vitarahisisha udhibiti wa wahusika – walio navyo na wasio navyo. Hapa ni rahisi kukumbuka sakata la vyeti feki, jinsi vilivyotambuliwa kwa njia ya kielekroniki. Kwa wale watakaosafiri nje ya nchi, haitawezekana kuruka kwa ndege bila mfumo wa kielektroniki kuitambua kadi popote duniani.

Mchezaji wa timu ya Simba Bernard Morison aliikataa chanjo hii lakini kwa ajili ya kuruka kwenda Morocco alilazimika kuchanja! Hapo hiari iliyotangazwa na viongozi wetu haikuzingatiwa.

Si ajabu, muda si mrefu, ukaambiwa bila kadi hii ya chanjo ya uviko-19 mwalimu hatafundisha watoto; watoto hawataenda shuleni; wahudumu wa afya hataruhusiwa kuingia kazini; kumbi za sherehe; nyumba za ibada; vyombo vya usafiri hatutaingia bila kadi hizi.

Hili si jambo geni. Miaka michache tu imepita kujiunga na jeshi la kujenga taifa (JKT) ilikuwa hiari, lakini ambaye hakujiunga na JKT hakuruhusiwa kujiunga na chuo kikuu au taasisi nyingine za juu za elimu nchini, wala kupata ajira serikalini na kwenye mashirika ya umma! Kumbe hii ilikuwa ni hiari iliyo lazima?

UZOEFU WA CHANJO HII

Wenzetu wa mataifa ya Ulaya na Marekani, wakati wa Uviko-19 awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu, walishuhudia vifo vya mamia kwa maelfu kila siku. Baada ya chanjo kupatikana, vifo vimepungua sana.

Milango ya lockdown imevunjwa! Sasa viwanja vya michezo vimefunguliwa. Shule, hoteli supermarkets, hali kadhalika kumbi za starehe ziko wazi. Ukali wa ugonjwa unepungua.

WALIOCHANJWA HAWAAMBUKIZWI?

Waliochanjwa waweza kuambukizwa na Uviko-19 lakini uwezekano wa kupona ni mkubwa zaidi kuliko kwa mtu asiyechanjwa ambaye ana asilimia kubwa sana ya kuwa hoi na kupoteza maisha.

Waziri wa Afya Dorothy Gwajima

WAZUNGU WANA AJENDA YA SIRI?

Uporaji wa madini na maliasili za Afrika na nchi nyingine zinazoendelea si jambo geni. Uporaji wa waziwazi kwa njia ya mikataba mibovu na uporaji wa chini chini ni dhahiri. Si kila mzungu ni mtu mwema kama ilivyo pia si kila Mwafrika ni mtu mwema.

Lakini kwamba WAZUNGU wote kwa umoja wao wanaweza kutengeneza chanjo ili kuangamiza Waafrika wote wakati huo huo wao wenyewe pia wajichanje kwa chanjo hiyo hiyo, ni jambo lisiloingia akilini.

Aina fulani ya watu yaweza kuwa wahanga, lakini “modus opperandi” isingekuwa hii. Hasa ukizingatia kuwa asilimia 90 ya tekinolojia ya tiba, vifaa tiba na dawa zote tunazotumia, vinatoka kwao, njia hizo pekee zingetosha kukamilisha ajenda yao, kama wangetaka. Kwa nini tuwe na hofu na chanjo dhidi ya Uviko-19 na tusiwe na hofu juu ya hayo mengine?

WAKATOLIKI WA TANZANIA

Tangu kuzuka kwa Uviko-19, Kanisa liliwahimiza sana waamini wake kusali sala maalumu ilitolewa na Balaza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Wengine walienda mbali hata kufunga chakula na vinywaji. Tulihimizwa kumwomba Mwenyezi Mungu katika mambo mengi, lakini yafuatayo nayahitaji zaidi katika makala hii:

(a) Atukinge na ugonjwa huu
(b) Awaponye wagonjwa wa Uviko-19
(c) Awafunulie wanasayansi kupata chanjo na tiba kwa haraka.

Ni matarajio yangu kuwa sala na dua zetu ambazo hazikusaliwa tu na Wakatoliki bali na kila Mtanzania wa kila imani, zimejibiwa mapema. Hivyo, hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kuipokea chanjo kwa haraka. Si jambo jema kabisa kiimani na kimaadili kumhoji Mungu kwa nini ametupatia chanjo mapema ilhali sisi wenyewe tulimwomba sana kwa magoti na machozi.

TUKACHANJE. NI SALAMA.

TANBIHI YA MHARIRI:

Katika kueleza sababu za chanjo kupatikana haraka, mwandishi hakutaja suala la upatikanaji wa raslimali fedha. Katika kuandaa chanjo, mara nyingi wataalamu hutumia muda mrefu kwa sababu ya ukosefu wa fedha za kukamilisha utafiti wao. Katika hili la sasa, mashirika makubwa na mataifa makubwa duniani yaliweka kipaumbele na kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utafiti huu. Kwa sababu hiyo, hata hatua tatu za majaribio ya kiutafiti ili kuthibitisha ubora wa chanjo zimefanyika katika kipindi kifupi, kwa wakati mmoja. Kutokana na wingi wa maambukizi, ilikuwa rahisi pia kupata wagonjwa wa kujitolea kwa ajili hiyo. Hata hivyo, ukweli ni kwamba utafiti juu ya chanjo ya Corona umetegemea zaidi ufanisi wa utafiti wa awali juu ya SARS NA MERS (wenye kirusi kinachofanana na hiki) tangu 2003. Kwa taarifa zaidi, JISOMEE HAPA.

Like
4