CCM yahofia kushindwa kwa asilimia 70 Buyungu

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza matumaini ya ushindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma. Tathmini ya ndani ya chama hicho inaonyesha kuwa mgombea wao, Christopher Chiza, atapata kura zisizozidi asilimia 30.

SAUTI KUBWA ina taarifa kwamba viongozi wa CCM waliambizana ukweli huo katika kikao chao maalumu cha “mkakati wa ushindi” kilichofanyika juzi Alhamisi tarehe 26 Julai 2018.

Mbali na tathimini ya kikao hicho, baadhi ya vyanzo vyetu kutoka ndani ya chama vinasema hata mgombea mwenyewe amekuwa anasema kuwa wananchi hawamtaki, na kwamba siasa za Buyungu zimetawalwa na “mzimu ya hayati Kasuku Bilago” aliyekuwa mbunge wao tangu 2015 akafariki dunia mwaka huu.

Chanzo kimoja kimesema: “Kiukweli, tutashindwa kwa asilimia 70. Yule kijana wa Chadema (Elia Michael) ana nguvu sana, sana. Mgombea wetu Chiza anajua, na sisi tunajua, kuwa hatukubaliki, lakini pamoja na hayo yote, lazima tutangazwe washindi. Sisi tuna mbinu zetu bwana, na bila hizo hatutoboi; huo ndio ukweli!”

Kwa sababu ya tahadhari kubwa na usiri ambao wajumbe wa kikao walidhamiria kuweka kwa unyeti wa ajenda nzito ya kikao chao, walikifanyia mbali, katika njia panda ya kuelekea Biharamulo, kwenye mji mdogo wa Nyakanazi.

SAUTI KUBWA inatambua kuwa wajumbe zaidi ya 30 walihudhuria kikao hicho. Vigogo walioonekana maeneo yale ni pamoja na Dk. Bashiru Ally, katibu mkuu wa CCM, ambaye vyanzo vinasema alishiriki kwa muda mfupi kwani alikuwa njiani kurudi Dar es Salaam.

Wengine ni katibu wa wilaya, katibu mwenezi, na ofisa usalama wa wilaya ya Kakonko. Kutokana na tathmini hiyo, wameweka mikakati mizito ya kusaka ushindi kwa gharama yoyote.

SAUTI KUBWA imeelezwa kuwa CCM wameamua kuongeza nguvu kwa kamati yao ya ununuzi wa shahada za wapiga kura, hasa katika kata yenye wapiga kura wengi – Gwarama.

Katika ununuzi wa shahada hizo, wanakamati hao wataambatana na wahuni waliokodiwa kutoka Burundi na baadhi ya wenyeji ambao kazi yao ni kutisha wapiga kura.

Vile vile, wameazimia kuunda kamati maalumu ya akina mama ambayo itatembea nyumba kwa nyumba kugawa rushwa ya sukari, viberiti na chumvi, ambavyo kwa ujumla wake havizidi gharama ya shilingi 2000.

Walijadili pia jinsi ya kudhibiti vituo vya kura kwa kutumia mgambo, ambao tayari wapo kambini mazoezini. Mgambo hao wataapishwa na kuagizwa kulazimisha wasimamizi wa vituo wabadili matokeo ya Chadema yawe ya CCM pale pale vituoni.

Waliamua pia kwamba mkurugenzi lazima alazimishwe kutangaza mgombea wa CCM hata kama kura hazitatosha. Kwa kuanzia, wamesema watamtaka mkurugenzi kunyima mawakala wa upinzani barua za utambulisho hadi dakika ya mwisho, kama walivyofanya Kinondoni mwezi Februari 2018.

Jambo jingine ambalo wamepanga ni kubadili kituo cha majumuisho ya mwisho, kwamba wasitumie kinachofahamika kilichotumika 2015, bali wakisogeza mbali ambako watalazimika kubeba masanduku ya kura kwa muda mrefu – ili wapate fursa ya kuyabadilisha njiani.

Hata hivyo, katibu mkuu, kabla hajaondoka – maana aliondoka katikati ya kikao – alisema kuwa itabidi wasubiri maelekezo kutoka makao makuu kuhusu mabadiliko ya kituo cha mwisho, kwa maelezo kuwa linahitaji umakini mkubwa, kwa sababu linaamuliwa na tume.

Watoa taarifa wetu wameiambia SAUTI KUBWA kuwa CCM bado inafanya majadiliano na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu mabadiliko ya kituo cha majumuisho.

Wanapima upepo wa jamii, hasa wakihofia kwamba wakijulikana mapema jambo hili linaweza kuleta sokomoko kubwa. Tayari limevuja!

Like
8

Leave a Comment

Your email address will not be published.