MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeua uchumi wa zao la kahawa na kurudisha nyuma maendeleo ya mkoa wa Kagera kutoka nafasi ya pili ya baada ya uhuru hadi kuwa mkoa wa mwisho hivi sasa.
Amesema kwamba sera mbaya ya CCM, ya kulazimisha mazao kuuzwa kwenye soko la ndani, imesababisha kahawa kuuzwa kwa bei ndogo wakati ingeweza kuuzwa kwa bei kubwa zaidi kwenye nchi jirani kama Uganda.
Mbowe amewaomba Watanzania kuzidi kujisajili kwa wingi kuwa wanachama wa Chadema, kwani ndiyo tumaini pekee la kuwakomboa Watanzania na kuwaongoza katika misingi ya haki, uhuru, demokrasia na maendeleo ya kweli.
Akihutubia maelfu ya wananchi katika uwanja wa Mayunga mjini Bukoba leo, Mbowe alisema mbali na kahawa, CCM imeharibu pia uchumi wa zao la ndizi kwa kushindwa kudhibiti ugonjwa hatari wa mnyauko wa migomba, licha ya ugonjwa huo kuibuka takribani miaka ishirini iliyopita.
“Mimi nimesoma sekondari ya Ihungo hapa Bukoba wakati ule wa vita vya Idd Amin. Kagera iliyosifika kwa maendeleo na kuzalisha wasomi na maprofesa wengi baada ya uhuru, si Kagera hii ya leo. Kagera ipo kwenye eneo zuri la kijiografia, imezungukwa na Ziwa Victoria na ina ardhi yenye rutuba ya kutosha. Kagera ni mkoa wa mpakani. Mipaka ni uchumi, mipaka ni biashara, lakini leo takwimu za benki kuu zinaonesha Kagera ndiyo mkoa maskini kwa kuwa na wananchi wenye kipato kidogo zaidi kuliko mikoa yote”, alisema Mbowe.
“Mkoa wote huu una viwanda viwili tu unavyoweza kuvitaja, TANICA na Kagera Sugar. CCM wanawalazimisha kuuza kahawa yenu kwa bei ndogo ya shilingi 2,000 kwa kilo, wakati mngeweza kuuza kwa shilingi 8,000 hadi 9,000 hapo nchi jirani Uganda. CCM wameua uchumi wenu na kuwatia umaskini”, alisema.
Aliongeza kuwa katika jitihada za kujikwamua kiuchumi, wananchi wa Kagera waliamua kulima zao mbadala la vanilla, lakini serikali imewatelekeza kwa kushindwa kutafuta masoko ya uhakika na matokeo yake ni kuporomoka vibaya kwa bei ya zao hilo.
Hali ya soko la vanilla katika maeneo mbalimbali ya Bukoba Mjini, Muleba, Bukoba Vijijini, Karagwe na Misenyi inaonesha bei ya vanila imeporomoka kutoka shilingi 45,000 kwa kilo, mwaka 2018 hadi kufikia shilingi 3,000 hivi sasa.
Akizindua rasmi Operesheni ya +255 yenye ujumbe wa “Katiba Mpya: Okoa bandari zetu”, Mbowe alihamasisha wananchi wa Bukoba kupaza sauti ya kudai katiba mpya na kupinga mkataba wa serikali ya Tanzania na Dubai unaohusu uwekezaji wa bandari na maeneo mengine ya kiuchumi, kwani mkataba huo unairejesha nchi katika ukoloni na utumwa kwa kugawa raslimali za nchi kiholela na kuuweka rehani uhuru na usalama wa nchi.
Mkutano huo pia ulihutubiwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu na Katibu Mkuu, John Mnyika, ambao wote kwa pamoja, walichambua upungufu wa mkataba huo na kuwaomba wakazi wa Kagera kuikataa CCM, kwani miongoni mwa bandari zilizolengwa na mkataba huo ni pamoja na bandari za mji wa Bukoba.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, aliwaomba wananchi kudai kurejeshwa kwa serikali ya Tanganyika ili Tanzania iweze kupata muungano wa serikali tatu, utakaoondoa utata na msigano wa masuala ya muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.
Mikutano ya “Operesheni +255 Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu,” inaendelea tena kesho katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera.