Matumaini ya timu ya Barcelona kuhakikisha nyota wao mkongwe Leo Messi anasalia klabuni hapo yameongezeka maradufu baada ya bodi ya Ligi ya nchi hiyo kutangaza kuwa itatoa mkopo wa dola bilioni 3,2 kwa timu za soka nchini humo.
Hiyo imetokana na La Liga kukubali kuuza asilimia 10 ya biashara yake kwa kampuni binafsi inayojulikana kama CVC Capital Partners. Dili hilo tayari limepitishwa na Mkurugenzi wa ligi hiyo pamoja wa wawakilishi kutoka Atletico Madrid, Villareal, Real Sociedad na wengine wengi. Hatua pekee iliyosalia ni kwa vilabu vinavyoshiriki kwenye ligi hiyo, kupiga kura ya kukubaliana au kutokubaliana na dili hilo na imeelezwa kuwa tukio hilo litafanyika ndani ya wiki chache zijazo.
Asilimia 90 ya fedha hizo, itapelekwa kwenye vilabu vya soka vinavyopatikana Uhispania zikiwemo timu za soka kwa wanawake. Licha ya kuwa fedha hiyo ni mkopo utakaopaswa kulipwa, timu nyingi nchini humo zimepokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa kutokana na mtikisiko wa kiuchumi uliowakumba kutokana na janga la UVIKO 19.
Vyanzo kadhaa vimeripoti kwamba timu za Real Madrid na Barcelona zitapokea kitita cha Euro milioni 250 kila mmoja, kulingana na itifaki ya ugawaji fedha kwenye ligi hiyo.
“Mgawanyo wa fedha utazingatia kiasi cha michango inayotokana na haki za matangazo ambayo timu zimekuwa zikitoa kwenye ligi tangu mwaka 2015, wakati ambao ni muhimu sana kwa La Liga,” kilisema chanzo cha ligi hiyo. “Hatutoangalia msimu mmoja au miwili bali wastani wa jumla ya michango ya timu kwa muda wa miaka yote saba iliyopita.”
Lengo la fedha hiyo ni kwa minajili ya mustakabali wa timu hizo, hivyo bodi ya ligi itavilazimu vilabu kukubaliana na mkakati wake wa kutumia fedha hiyo kuboresha miundombinu na kuongeza mvuto, kiliongeza chanzo hicho.
Timu zitapaswa kutumia asilimia 70 ya fedha hizo kwenye uwekezaji wa ukuaji wa muda mrefu, asilimia 15 kwenye kulipa madeni huku asilimia 15 ikitumiwa katika kuongeza kiwango cha matumizi ya vilabu katika ligi.
Kwa timu ya Barcelona, hii inakuja kama neema kwao kutokana na kwamba walishindwa kuongeza kandarasi ya Messi pamoja na kuwasajili wachezaji wake kadhaa akiwemo Memphis Depay na Kun Aguerro ili kuepuka kuvunja sheria ya Maputo na matmizi ya ligi hiyo.
Kwingineko, timu ya Real Madrid inatarajiwa kuipokea fedha hiyo kwa furaha kubwa kutokana na matatizo ya kifedha yanayoikumba timu hiyo kongwe ambayo yametokana na gonjwa la UVIKO 19 pamoja na kukosa ushuru kwa kutoingiza mashabiki uwanjani.
Bodi ya ligi ya La Liga, imeamua kuuita mkakati huu “Boost La Liga” kama mkakati wa kuingozea nguvu ligi hiyo ambayo hivi karibuni imeonekana kusuasua na ubora wake kuwa mashakani.
Je mkakati huu utafanikiwa?