Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lapata rais mpya

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limefanya mabadiliko ya uongozi na kupata viongozi watatu wapya – rais, makamu wa rais na katibu mkuu.

Katika mabadiliko hayo, Mhashamu Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga (Jimbo la Mpanda) ndiye amechaguliwa kuwa rais wa TEC.

Makamu wake ni Mhashamu Askofu Flavian Kasalla (Jimbo la Geita), na katibu mkuu ni Padri Charles Kitima (Jimbo la Singida), aliyewahi kuwa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Mt Augustine (SAUT), Mwanza.

Mabadiliko hayo yamefanyika wiki hii katika kikao chao cha kawaida kilichofanyika katika Jimbo la Sumbawanga, na yametangazwa na rais anayestaafu, Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, katika ibada ya kumweka wakfu Askofu Beatus Urassa kuwa Askofu wa Sumbawanga leo tarehe 24 Juni 2018 katika Kanisa la Epifania.

Askofu Nyaisonga na makamu wake watashikilia washifa huo kwa miaka mitatu. Wanaweza kuchaguliwa kwa kipindi kingine kimoja cha miaka mitatu.

Wafuatao ndio wamewahi kuwa marais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania:

1969-1970: Mhashamu Plasidius Gervasius Nkalanga, Askofu wa Jimbo la Bukoba.

1970-1976: Mhashamu James Dominick Sangu, Askofu wa Jimbo la Mbeya.

1976-1982: Mhashamu Mario Epifanio Abdalah Mgulunde, Askofu wa Jimbo la Iringa, baadae Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Tabora, na hatimaye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora.

1982-1988: Mhashamu Antony Petro Mayala, Askofu wa Jimbo la Musoma, baadaye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza.

1988-1994: Mhashamu Josephat Louis Lebulu, Askofu wa Jimbo la Same na baadae Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha.

1994-2000: Mhashamu Justine Tetim Samba, Askofu wa Jimbo la Musoma.

2000-2006: Mhashamu Severine NiweMugizi, Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara.

2006-2012: Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ich, Aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Mbulu, baadaye Jimbo la Dodoma na Jimbo Kuu la Mwanza, ambaye kwa sasa ni Askofu Mkuu Mwandamizi mwenye haki ya kurithi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam.

2012-2018: Mhashamu Tarsisius Ngalalekumtwa, Askofu wa Jimbo la Iringa.

2018 hadi atakapomaliza ngwe yake: Mhashamu Gervas Nyaisonga, aliyewahi kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma, na sasa ni Askofu wa Jimbo la Mpanda.

Jimbo la Sumbawanga na kauli ya Pengo

Jimbo la Sumbawanga limepata askofu mpya baada ya Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi (78) kustaafu. Askofu Kyaruzi ameongoza jimbo hilo tangu alipoteuliwa kuwa askofu mwaka 1997.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alitumia fursa hiyo kushauri askofu mpya na maaskofu wenzake kuhakikisha wanaendelea kupigania na kuimarisha umoja wa kanisa na wa taifa.

Alisema: “Ni muhimu sisi maaskofu tusisitize juu ya umoja wa waamini waliokombolewa kwa damu moja ya Kristu. Kwa mazingira ya Tanzania, wewe na mimi na maaskofu wote tusisitize umoja wa Watanzania na Tanzania.

“Tusikubali  kuruhusu damu mbalimbali zinazotufanya kuwa wenye kabila hili au lile zikatawala na kuvunja umoja  wa Taifa letu. Tuombeane katika kazi hii. Tutunze umoja wa waumini na wa Taifa letu.

“Wewe umezaliwa mkoani Kilimanjaro ni Mchaga unayetoka Rombo. Katika utandawazi wa Tanzania siku hizi ni muhimu kuzingatia yafuatayo, unayo damu ya kichaga ndani ya mwili wako, nakuomba wala usikatae na usijaribu kuificha damu hii.

“Hakuna sababu wala uhalali kwako wa kujaribu kuficha ukweli huu. Neno moja lazima ulikumbuke ni kuwa wewe na mimi na kundi lote hatujakombolewa kwa damu ya kichaga wala ya kifipa na kinyakyusa. Sote tumekombolewa kwa damu ya Kristo.

Kauli ya Kardinali Pengo imekuja kama jibu kwa makundi ya mashabiki wa kisiasa ambayo yamekuwa yanaandika habari na makala kwenye vyombo vya habari kutuhumu kanisa kuwa lina ukabila, hasa yakisisitiza kuwa kanisa linatawaliwa na “uchagga.”

Vyombo hivyo vya habari vinamilikiwa na kuendeshwa na watu wanaojinasibu kama “wanazi wa Magufuli,” wanaopambana kudhalilisha kanisa, wakionyesha kukerwa na Waraka wa Kichungaji wa Kwaresima 2018 uliokuwa unasisiiza imani na amani, huku ukikemea mwenendo wa siasa za kikatili unaohatarisha amani na umoja wa taifa.

Mbali na waraka wa Kanisa Katoliki, waraka mwingine uliokera serikali na “wanazi wa Magufuli” ulitolewa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ukibeba ujumbe wa Pasaka wenye dhima ile ile ya amani, haki, na umoja wa kitaifa.

Kutokana na nyaraka hizi kukemea siasa za ukatili na visasi dhidi ya raia wanaokosoa serikali, makanisa haya mawili yamepata msukosuko kutoka kwa vyombo vya dola na idara mbalimbali za serikali.

Katika mwezi uliopita, wizara ya mambo ya ndani iliandikia makanisa yote mawili barua ya onyo, ikiyataka yajieleze kwanini yasichukuliwe hatua kwa “kujiingiza katika siasa.”

Zaidi ya hayo, serikali iliyataka makanisa hayo yaandike nyaraka mpya za kukanusha nyaraka za Kwaresima na Pasaka, vinginevyo ingeyachukulia hatua kali, ikiwemo kuyafuta katika orodha. Moja ya barua hizo za serikali (iliyokwenda KKKT) ilivuja mitandaoni na kusababisha taharuki kutoka kwa waamini na wananchi wengine.

Hatimaye, Mwigulu Nchemba, waziri wa mambo ya ndani, alilazimika kutoa kauli ya kujikosha, akidai barua zilizopelekwa kwa makanisa hayo zilikuwa “feki.” Hata hivyo, maaskofu viongozi wa mabaraza ya maaskofu ya makanisa yote mawili walikuwa wameshasumbuliwa kwa wito binafsi na kuhojiwa pale wizarani kwake, licha ya majibu ya barua ambayo KKKT na TEC walikuwa wametoa.

Wakati waziri akidai kuwa barua ya serikali ilikuwa “feki” alitangaza kumsimamisha kazi msajili wa vyama na mashirika ya dini, jambo ambalo liliibua hisia hasi dhidi ya kanusho lake.

Na licha ya Samia Suluhu, makamu wa rais, kusema serikali ipo radhi kukosolewa na viongozi wa dini, magazeti ya “wanazi wa Magufuli” yanaendelea kuchapisha habari za kutunga dhidi ya kanisa na viongozi wa kiroho wanaokosoa serikali.

Wizara ya Habari, kupitia Idara ya Habari (MAELEZO), haijachukua hatua yoyote dhidi ya magazeti hayo, jambo linaloonyesha kuwa magazeti hayo yanatumika kama sauti ya wenye nguvu wanaoogopa, na wanaodiriki kutisha au kuzima sauti ya kinabii inayokemea uovu uliojikita katika mfumo wa utawala.

Wajuzi wa masuala ya kanisa wanasema kauli ya Kardinali Pengo inaakisi msimamo wa maaskofu wenzake wa TEC, hasa baada ya kikao chao cha wiki iliyopita.

Like
3

Leave a Comment

Your email address will not be published.