Asili ya Kitabu Hiki – 002

Awali, sikudhamiria kuandika kitabu. Hili ni zao la makala zangu za uchambuzi wa kisiasa, hasa katika gazeti RAI tangu 1997, na baadaye katika safu ya Maswali Magumu, ambazo zilichapishwa katika magazeti ya Mwananchi Jumapili (2002-2004), Tanzania Daima (2004-2015), MwanaHALISI, Mseto, na Mawio (Juni 2016-Septemba 2017).
Huu ni uchambuzi na mkusanyo wa sehemu ya makala zinazojadili masuala muhimu ambayo yamekuwa yanasababisha maswali magumu kuhusu haki na usawa, utu wetu, utawala bora, uadilifu wa viongozi, usalama wa raia, usitawi wa jamii, wajibu wa raia, na kadhalika. Zote zimeandikwa kutokana na hulka ya mwandishi ya kutia shaka na kuhoji mbinu, mikakati, mipango, mwenendo, na kauli za watawala kwa miaka 20 mfululizo.
Makala hizi zilipata umaarufu mkubwa kuanzia mwaka 2006 katika mwaka wa kwanza wa utawala wa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kutokana na hali na matukio ya kisiasa ya wakati ule, makosa ya “rais mpya mwenye mvuto,” ubabe wa baadhi ya wasaidizi wa rais, na ujasiri wa mwandishi kukosoa rais na wenzake bila woga, aibu, wala upendeleo katika mazingira yaliyokuwa yamefanya waandishi wa habari wengi kujiona kuwa ni sehemu ya “mtandao” wa utawala wa Rais Kikwete.
Katika mwaka huo, wananchi walishuhudia serikali ikifanya kazi katika mfumo uliosaidia kulea, kukuza, na kusimika ufisadi wa vigogo waliokuwa karibu na rais. Mwaka 2007 ulikuwa wa mashambulizi kati ya serikali na wakosoaji wake. Ndani ya miaka miwili, “kupendwa” kwa rais kulikuwa kumeanza kuingia doa. Serikali ilikuwa inafanya kila jitihada kulinda kashfa za vigogo, kwa kutumia baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na baadhi ya watendaji katika vyombo vya habari; huku wapambanaji wa ufisadi wakiwa mstari wa mbele kuibua ufisadi mmoja baada ya mwingine. Septemba 15, 2007 wapinzani walitangaza rasmi orodha ya mafisadi 11, akiwemo rais, rais mstaafu, na waziri mkuu. Mapambano hayo yaliamsha ari ya wananchi kila mahali, serikali ikanyong’onyea.
Mwaka 2008 ulikuwa mwaka wa anguko la kwanza la serikali ya Kikwete. Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alijiuzulu baada ya Kamati Teule ya Bunge kumhusisha na ufisadi wa zabuni ya Richmond. Baraza la Mawaziri lilivunjwa na kuundwa upya. Kwa mara ya kwanza, kulijengena ufa kisiasa kati ya Kikwete na Lowassa. Ufa huu haukuishia kwa wawili hao. Ulizidi kupanuka na kurefuka ndani ya chama na serikali. Lowassa akawa nje ya serikali lakini ana nguvu ndani. Ufa huu haukuwahi kupata mtu wa kuuziba hadi Kikwete alipohitimisha miaka 10 ya urais. Na kuwema ukweli, ufa huu haukukiacha salama Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mwaka 2009 serikali ilianza kujipanga upya, ikashikamana na mafisadi wake kujiandalia uchaguzi wa serikali za mitaa 2009 na uchaguzi mkuu wa 2010. Lakini tayari wananchi waliona kuwa taifa lilikuwa linakabiliwa na ombwe la uongozi. Katika kipindi hiki, nilindika kila wiki kuchambua matukio, kauli, na mienendo ya watawala, hasa rais. Wapo walionizomea, walionituhumu, walionichukia, na walioniunga mkono. Mapambano ya fikra na masuala yaliyojitokeza wakati ule, ni sehemu ya uchambuzi uliozaa kitabu hiki.
Wakati naandika masuala hayo, zaidi ya miaka 10 iliyopita, sikuwahi kuwaza kama Edward Lowassa angekosana kabisa na CCM, na kuhamia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichomshutumu na kumkosesha amani alipokuwa madarakani. Sina shaka kwamba maswali magumu aliyoulizwa yakamkera alipokuwa madarakani, yalisadia kumjenga na kumwimarisha baadaye alipohama na kuanza kukabiliana na walio madarakani, akiwa mpambanaji mpya kwenye chama cha upinzani.
Maswali Magumu niliyoandika katika miaka ya awali ya utawala wa Rais Kikwete, yanaposomwa leo, yanaonekana kama yameandikwa jana kuhusu hali ya kisiasa tuliyomo. Kwa upande mwingine, yanaonekana kama utabiri uliotimia ndani ya muda mfupi.
Nimejumuisha baadhi ya masuala hayo katika kitabu hiki ili kuhuisha historia, na kuboresha uchambuzi wa matukio na hali ya kisiasa ya wakati huu, ili tujifunze kutokana na yaliyopita.
Yameandikwa jana, yanaishi leo. Yanamulika matendo, mienendo, na kauli za wakubwa wenye mamlaka katika nchi yetu. Yanachambua mfumo wa utawala. Yanasaidia wananchi kujitambua na kujitetea. Yanapanda mbegu ya kupigania haki na mabadiliko ya kweli ya kimfumo badala ya mabadiliko ya awamu za utawala sura za viongozi. Hii ndiyo asili ya kitabu hiki.

Like
9