Maswali Magumu: Tutafute majibu ya kuridhisha – 001

Yameandikwa jana lakini yanaishi leo. Yanamulika matendo, mwenendo, na kauli za wakubwa wenye mamlaka. Yanachambua mfumo wa utawala wa Tanzania na kuonyesha uzi mwembamba unaounganisha mtawala mmoja na mwingine aliyetangulia au anayefuata. Ni maswali yanayosaidia wananchi kujitambua na kujitetea. Yanapanda mbegu ya kupigania haki na mabadiliko ya kweli ya kimfumo badala ya mabadiliko ya sura za viongozi.

Tangu nilipokuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, miongoni mwa masomo niliyotamani ni fasihi na falsafa. Katika kidato cha tano na cha sita, nilipata fursa ya kusomea fasihi kwa Kiingereza. Baadaye nilipata fursa ya kusomea falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho, Tanzania; na Chuo Kikuu cha Hull, Uingereza. Kwa sababu hiyo, fasihi na falsafa ni sehemu ya misingi ya maisha yangu kijamii na kitaaluma.

Kwa maelezo ya kikamusi, mwanafalsafa ni mtu ambaye amejifunza falsafa; au mtu ambaye anafikiri au anatafakari kuhusu ujuzi, ukweli, maumbile, maana ya maisha; mtu ambaye anaishi na kufikiri kwa mwelekeo fulani wa kifalsafa; mtu mtulivu mwenye kufanya uamuzi baada ya tafakuri pana katika mazingira yoyote.

Kwa asili, mwanafalsafa ni mtafuta ukweli – ukweli halisi, ukweli asilia, ukweli katika sura zake nyingi. Mwanafalsafa ni mpenda hekima. Kwa hiyo, ni sahihi pia kusema mwanafalsafa ni mtafutaji wa haki. Wanafalsafa huishi kwa kudadisi, kutia shaka, kujenga hoja, na kusaka majibu ya kweli.

Kwa zaidi ya miaka 2500, wanafalsafa wamekuwa wakijiuliza maswali magumu, na bado wanaendelea. Ni maswali ya kudumu yasiyopitwa na wakati. Wanajadili ukweli, maisha, kifo, haki, uwepo wa vitu, Mungu, maadili, ujuzi, utawala, na kadhalika.

Mwanafalsafa mmoja, sikumbuki jina lake, aliwahi kuhoji: Unawezaje kujua kwa uhakika kwamba mtu fulani anakupenda? Je, unawezaje kujua watu wengine wanawaza nini au wanahisi nini wasipokwambia? Au hata wakikwambia, utajuaje kwa hakika kwamba walichokwambia ndicho walikuwa wanawaza au wanahisi? Kwa msingi huo, je, tunaweza kujua jambo lolote kwa uhakika kabisa?
Tunamaanisha nini tunaposema kwamba jambo fulani ni kweli? Ukweli ni kitu gani? Unapatikana wapi? Je, ni jambo gani linalowapatia wanasiasa haki ya kutumia mamlaka na madaraka yao jinsi wafanyavyo?

Je, kuna serikali yoyote duniani inayozingatia na kutenda haki kwa watu wake? Zaidi ya hayo, nini maana ya haki? Tunaposema jambo fulani ni sahihi au si sahihi tunakuwa tunaonyesha kukubali au kukataa nini? Uadilifu una maana yoyote? Je, ni zaidi ya kuwa sahihi na kukosea?

Hivi kuna Mungu? Je, hoja zinazojengwa kuthibitisha uwepo wa Mungu (si imani za kidini) zina nguvu yoyote? Zinaridhisha akili inayofikiri sawa sawa? Je, wazo au dhana ya uwepo wa Mungu inakubalika katika akili ya binadamu?

Wakati au muda ni kitu gani, na kina umbile au hulka gani? Muda unaweza kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine? Je, mimi ni nani? Mimi ni nini? Ni jambo gani linanifanya mimi niwe mtu yule yule kama nilivyokuwa miaka kadhaa, tuseme 10 au 20 au 40 iliyopita?
Utu wangu ni akili yangu? Je, akili ni nini? Kuna tofauti kati ya akili na ubongo? Uliwahi kuhisi kwamba mara nyingi mambo mengi huishia pale mambo mazuri yanapoanzia au yanapokaribia kujitokeza?

Ulishatambua kwamba kuna mambo ambayo huwa tunazuiwa kufanya hata kabla hatujafikiria kuyafanya? Unajua kwamba kuna mambo ambayo ulifundishwa au ulilelewa usiyahoji? Kwanini? Au wewe ni mmoja wa watu ambao hupokea na kuamini busara ya wakubwa tu bila kujipa mwanya wa kuitilia shaka?

Maswali haya ya mwanafalsafa huyu ni baadhi ya maswali magumu ambayo ufafanuzi wake ndiyo hujaribu kujenga misingi ya majibu yanayotafutwa na wanafalsafa, watu wadadisi wanaohoji na kuhoji na kuhoji, bila kuweka au kuwekewa mipaka ya kuhoji au kufikiri. Lakini kuhoji si kazi ya wanafalsafa peke yao. Ni jukumu la kila binadamu mwenye akili timamu.

Katika kufanya kazi ya uandishi wa habari, kwa sehemu kubwa, nimeongozwa zaidi na mwenendo huu wa kifalsafa na stadi zake nilizojifunza miaka kadhaa kabla ya kufunzwa uandishi wa habari. Naamini kwamba zinamfaa mtu yeyote anayetafuta kujua jambo lolote kutoka chanzo chochote.

Kudadisi na kuhoji ni mambo muhimu na ni tabia njema ingawa yanakera baadhi ya watu waliolelewa kuishi kwa mazoea au kwa kutii mamlaka. Raia wasiohoji hawawezi kunusuru au kujenga taifa lao.

Raia wasiohoji huishi kwa kutii na kunyenyekea kila anayewekwa juu yao au mbele yao hata kama anawaonea au anawapotosha. Hali hii huzaa tabia ya kujipendekeza, hutufanya tuwe wanyonge na tupende kuwa upande wa “wenye nguvu” kama njia pekee ya kujinisuru. Hii ndiyo ya asili ya unafiki wa watu wetu wasemao wasichoamini, na waaminicho wasichosema. Na watawala wetu, kwa kujua tabia zetu hizi, wamekuwa wanadiriki kutudharau; wanathubutu kututumia, kutudanganya na kuingiza nchi katika ufisadi. Nchi inaendelea kuteketea, wananchi wapo kimya.

Si lazima, na haiwezekani, sote tuwe wasomi wa falsafa. Lakini tunaweza kushiriki kazi ya kifalsafa ya kutia shaka, kuhoji, na kuhoji, na kuhoji. Tuulizane maswali magumu; swali lizae jibu, na jibu lizae swali, ili tuweze kudhibiti mamlaka za nchi yetu ambazo zimejengewa misingi na utamaduni wa kusifiwa, kutukuzwa na kuogopwa, na sasa zimegeuka kichaka cha uovu na ufisadi wa watawala.

Woga wetu umezaa utii wa kijinga ambao, katika maeneo mengi, umetufanya tukubali kuchagua mbwembwe na hongo za wanasiasa badala ya hoja na sera makini. Ndivyo tulivyotumbukia katika ombwe la uongozi kitaifa. Ningependa andiko hili, pamoja na kuelimisha wasomaji, lisaidie kuchochea roho ya udadisi utakaoibua maswali magumu yanayohitaji majibu ya kuridhisha.

ITAENDELEA…

Like
21

Leave a Comment

Your email address will not be published.