Profesa Tibaijuka atunukiwa udaktari wa heshima

“I Change Nations International haimpi tuzo mtu kwa sababu ni rais wa nchi, inawapa watu wa aina mbalimbali kuanzia hao marais na watu wengine hadi mtaani. Tumefurahi tumepata na mtu mmoja ambaye ametunukiwa Shahada ya Heshima, hili ni jambo kubwa kwamba Tanzania tuna thamani kubwa duniani”

ALIYEKUWA Mtendaji wa Shirika la Makazi Duniani (UN-Habitat) Profesa Anna Tibaijuka ametunukiwa Cheti cha Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Utu na ubinadamu (Doctor of Philosophy in Humanities) kutoka Chuo Kikuu cha United Graduate College and Seminary International cha Marekani.

Mbali na hilo, Taasisi ya I Change Nations International (ICN) ya Marekani imempatia Profesa Tibaijuka tuzo ya kutambua mchango wake wa kupaza sauti na kuleta matokeo chanya duniani.

Hafla ya tuzo hizo ilifanyika Dar es Salaam mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza na vyombo vya habari kuhusu tukio hilo, Profesa Tibaijuka alisema anamshukuru Mungu kwa kupata heshima hiyo ambayo alisema inaongeza thamani ya watu kuendelea kujifunza pamoja na kuhamasisha vijana kwamba wako duniani kwenye hali bora.

Alisema jambo kubwa la kujiuliza na kujivunia sio tuzo au tunu alizozipata, bali ni jinsi gani tuzo hizo zinaisaidia jamii na kuongeza thamani kwa watu hasa vijana ambao wanategemewa kuwa chachu ya hali bora ya jamii.

Alisema licha ya kutunukiwa Shahada hiyo ya heshima, kwa umri na elimu aliyo nayo amewahi kupata tuzo nyingi, lakini tafsiri kubwa zaidi ya tuzo hizo za sasa ni kuboresha jamii aliyomo.

Profesa Tibaijuka ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Muleba Kusini na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alionya wanasiasa wanaowafanya vijana kuwa ‘chawa’ kwamba jambo hilo linawadumaza washindwe kujitambua na kujitegemea.

Alisema heshima aliyopewa ina maana kubwa, na zaidi ni kuhamasisha vijana kwamba wako hapa duniani kwenye hali bora, na huwezi kujiita mtu mwenye hali bora wakati hana mchango wowote kwenye jamii.

Alisema kizazi cha Mwalimu Nyerere ambacho yeye ni miongoni mwake, kilifundisha watu kufanyakazi na kujitegemea na si kuwa kama kupe, kunyonya damu bila kufanyakazi.

“Siku hizi kuna mambo ya uchawa, huwezi  kuchangia chochote kwenye jamii ukiwa kwenye uchawa. Chawa hatafuti cha kwake, kazi ya chawa anafyonza damu za wengine.

“Lakini vijana hawataki kuwa ‘machawa’, ila wabaya ni wale wanaowafanya vijana kuwa ‘machawa. Mimi nimelelewa na Mwalimu Nyerere, tuliambiwa usiwe kupe, ujitegemee, kwa hiyo kizazi changu sisi tunasimamia msimamo huo.

“Dawa ya chawa ni kuuawa tu kwenye kucha, sasa asubuhi unaua chawa mmoja unaanza mwingine, hii maana yake ni nini? Sisi kizazi cha Mwalimu Nyerere hatutaki mambo haya,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mratibu wa I Change Nations, Vennita Mwita, anayejulikana zaidi kwa jina la Veronika alisema wametimiza malengo yao kwa kupata washindi wa 12 wa tuzo hizo nchini Tanzania.

Alisema maana ya tuzo hizo ni kutambua na kuthamini mchango kwa mtu anayefanya mema katika jamii yake katika ngazi zote kuanzia za juu mpaka za chini kabisa mtaani wakiwamo wasiotumia mitandao ya kijamii lakini wanafanya vitu katika jamii zao.

“I Change Nations International haimpi tuzo mtu kwa sababu ni rais wa nchi, inawapa watu wa aina mbalimbali kuanzia hao marais na watu wengine hadi mtaani

“Tumefurahi tumepata na mtu mmoja ambaye ametunukiwa Shahada ya Heshima, hili ni jambo kubwa kwamba Tanzania tuna thamani kubwa duniani, ”alisema.

Wengine waliopata tuzo ya ICN ni Katibu wa Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Jokate Mwegelo, Mirad Ayo, mwanamuziki Selemani Msindi (Afande Sele) na wengine kutoka taasisi mbalimbali.

Mmoja wa wanzilishi wa tuzo hizo, Dkt Reuben West alisema Tanzania imekuwa nchi ya 156 duniani kutunukiwa tuzo hizo. Dk West ambaye ni Mmarekani Mweusi alisema ICN inahusika kuwatambua watu waliofanya mema katika jamii zao kupitia nyanja mbalimbali za kijamii.

Taasisi ya ICN ilianziashwa na Dr. Clyde Rivers ambaye pia ni mwanzilishi katika Jumuiya za Umoja wa Mataifa (UN).

Like