CHINA INADHIBITI KAMARI KWAO, HUKU IKIICHOCHEA TANZANIA

“Nimebahatika kutembelea miji mikubwa na midogo nchini China, ikiwemo Beijing, Shanghai, Xian, Tianjin, na Chongqing sijawahi kuona michezo ya kamari kwani inakatazwa kisheria…”

WASWAHILI husema: “Sumu haionjwi.” Usemi huu unaweza kutumika pia katika kujadili ukweli kwamba Wachina wanaitazama kamari kama sumu ambayo hawako tayari kuionja. Serikali ya China imepiga marufuku kamari.

Bahati mbaya ni kwamba Wachina hao hao wamekuwa tayari kueneza sumu hiyo kwa mataifa mengine, na sasa wamewekeza kwa wingi katika biashara ya kamari nchini Tanzania.

Taarifa mbalimbali zilizokusanywa na SAUTI KUBWA kupitia mitandao ya kijamii pamoja na watu mbalimbali waliowahi kusoma au kutembeleaa China kwa nyakati mbalimbali zinaonyesha kwamba China haliruhusu raia wake kushiriki michezo ya kamari nchini humo.

Kwa mujibu wa tovuti ya https://practiceguides.chambers.com/practice-guides/gaming-law-2022/china/trends-and-developments, watoto wanaruhusiwa kucheza michezo ya video mtandaoni kwa saa tatu tu kwa wiki.

Chanzo hicho cha habari kinaeleza kuwa kamari imekatazwa kabisa katika Jamhuri ya Watu wa China tangu mwaka 1935 isipokuwa Hong Kong, Macau, na Taiwan pekee ndizo zimeachwa.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, nchini China, shughuli zinazohusiana na kamari zinaweza kusababisha adhabu za utawala na hata kifungo cha jinai katika kesi kubwa.

Wizara ya Usalama wa Umma nchini China (Tanzania ni Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi) wameimarisha utekelezaji kuhusu aina mpya za kamari, zikiwamo za mtandaoni na kamari za mipaka huku aina yoyote ya michezo inayoweza kuwa kamari pia imezuiliwa kabisa.

James Mbalwe, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT)

Mariam Hussein mmiliki wa duka Kariakoo anayefuata biashara China, anasema michezo ya bahati nasibu hupewa leseni na serikali na uendeshaji wake unategemea mfumo wa ufikiaji ulio mkali; na uuzaji wa tiketi za bahati nasibu mtandaoni bila idhini unakatazwa kwa mujibu wa Sheria maalum za udhibiti.

Anasema bahati nasibu nchini China zinapewa leseni na serikali na uendeshaji wake unategemea mfumo mkali wa kutoa ruhusa. Ambapo uuzaji wa tiketi za bahati nasibu mtandaoni bila idhini unakatazwa, kulingana na hatua maalum za utawala kwa upatikanaji wa uwekezaji wa kigeni.

“Usimamizi wa bahati nasibu umekuwa ukisimamiwa kwa muda mrefu na kanuni za utawala na sheria za idara. Hadi sasa hakuna sheria  zilizopitishwa kuweka mfumo wa utoaji leseni za bahati nasibu,” anasema.

Mhadhili wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambaye ameishi China kwa miaka kadhaa masomoni, Edgar Bebwa anasema: “Nimebahatika kutembea miji mikubwa na midogo nchini China ikiwemo Beijing, Shanghai, Xian, Tianjin, na Chongqing sijawahi kuona michezo ya kamari kwani inakatazwa kisheria. Hakuna kabisa mchezo wa kucheza na sarafu za coin kama ilivyo hapa nchini kwetu, ijukanayo kama coin slot, machine ambayo inawekwa kwenye baa, grocery, maduka na kadhalika.

Anaongeza kuwa mamlaka za China zinasema watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kucheza tu kuanzia saa 12 jioni hadi saa 1 usiku, siku za Ijumaa na mwishoni mwa wiki huku kampuni za michezo zikilazimika kutekeleza sheria hizo.

UGANDA

Miongoni mwa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) zimeruhusu michezo ya kamari lakini kwa sheria tofauti kulingana na mazingira yake.

Nchini Uganda kamari imeshamiri zaidi katika Jiji la Kampala na miji mingine kama ilivyo jiji la Dar es Salaam Tanzania.

 Tofauti na Tanzania, ambapo Wachina ndiyo wamewekeza zaidi kwenye biashara hizo kuliko mataifa mengine, nchini Uganda biashara hiyo ya kamari inawahusisha Wachina na Wahindi.

Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya mwaka 2016 ya Uganda kimaudhui haina tofauti kubwa na Sheria ya Tanzania.

Ibara ya 64 ya sheria ya michezo ya kubahatisha nchini Uganda inatoa adhabu kwa mtu anayechezesha michezo hiyo bila leseni, kuwa anatenda jinai na akibainika anaweza kupata adhabu ya aidha faini au kifungo kisichozidi miaka minne, au vyote kwa pamoja.

RWANDA

Sheria ya Kusimamia Michezo ya kubahatisha ya mwaka 2011 nchini Rwanda inatofautiana na Tanzania.

Wakati Tanzania michezo hiyo ikisimamiwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), Rwanda Ibara ya 4 ya Sheria yao inatoa mamlaka ya usimamizi wa michezo hiyo kwa wizara yenye dhamana husika, ambapo Waziri Mkuu anaelekezwa kushiriki katika uundaji wa mamlaka nyingine za usimamizi.

Ibara ya 32 ya Rwanda, inaeleza sifa za watu wasioruhusiwa kushiriki michezo hiyo, ambao ni ndugu wa wamiliki wa leseni hizo, watu ambao bado ni tegemezi kiumri na kimajukumu, wenye matatizo ya akili na namna ya kuwashughulikia kupitia mahakama.

Hata hivyo, Ibara ya 33 ya sheria hiyo inazuia kabisa kurusha matangazo ya kuhamasisha michezo ya kubahatisha kwa namna itakayobainika ikiwa ni pamoja na kutangaza uongo wenye nia ya kuhamamsisha watu kushiriki michezo hiyo.

Habari hii ni mwendelezo wa makala maalum zilizoangazia uwekezaji wa biashara ya michezo ya kubahatisha nchini kiuchumi na kijamii.

Makala hizo ziliangazia tafiti za wataalam wa tiba na sayansi ambazo zimeonyesha kuwa uraibu wa kamari ni zaidi ya ule wa dawa za kulevya zikiwamo cocaine, heroin nakadhalika, huku Tanzania ikitajwa kuwa kinara wa waathirika wa michezo ya kamari kwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la sahara.

Kichumi uwekezaji huo wa kamari haujaonyesha ushahidi wa wazi kama umeongeza ajira kwa watazanaia, huku taasisi za utafiti zikionyesha ajira katika sekta binafsi zikiporomoka.

Like