MBOWE, LISSU WAAMSHA WATANGANYIKA KUHUSU TAIFA LAO

Wanadi Muungano wa Serikali Tatu
Wapongeza Wazanzibari kwa kulinda nchi yao
Wapigilia msumari madai ya Katiba Mpya

Na Edward Kinabo, Mwana wa Gombera

VIONGOZI wakuu wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, na Makamu wa chama hicho, Tundu Lissu, wakizungumza katika maeneo tofauti (leo Ijumaa tarehe 26 Aprili 2024) wameibua tena kero za Muungano, wakati wakijenga hoja na haja ya kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Tanzania.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Musoma mkoani Mara, ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mbowe amesema kwasababu ya mapungufu makubwa ya kikatiba, Tanganyika, nchi yenye watu milioni 64, hivi sasa inaongozwa na rais ambaye ametoka “nchi jirani.”

Akifafanua hoja hiyo Mbowe alisema:

Kwa hiyo leo Watanganyika milioni 64 tuna Rais ambaye ametoka nchi ya jirani, ambapo kwenye nchi yake ana rais wake, anakuja kutawala watu milioni 64…yaani sisi ni machizi,” alisema Mbowe na wananchi wakaangua vicheko.

Mbali na rais Samia Suluhu Hassan na Hayati, Ali Hassan Mwinyi, Watanzania wenye asili ya Zanzibar, historia inaonesha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewahi pia kuongozwa na Watanzania wengine wanne wenye asili ya Tanganyika, ambao ni Hayati Julius Kambarage Nyerere, Benjamin Wiliam Mkapa na Hayati John Pombe Magufuli, pamoja na rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete.

Akijenga hoja zaidi dhidi ya dosari za muundo wa Muungano, Mbowe alisema:

Mwaka 1964, tarehe 26, tuliingia kwenye Muungano, tukaua asili yetu, tukaua utaifa wetu, tukapewa utaifa ambao ni wa Muungano. Wenzetu upande wa Zanzibar wakabaki na nchi yao, wana serikali yao, wana Bunge lao, wana Rais wao, wana Baraza lao la mawaziri, wana mahakama yao, wana bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa. Sisi Watanganyika milioni 64 tuulizane, jina letu la asilia la Tanganyika na uhuru wa taifa la Tanganyika uko wapi?” alihoji Mbowe.

Aliwaomba wananchi waelewe kuwa Chadema inaukubali na inaupenda Muungano, lakini inataka kuandikwe Katiba Mpya, ambayo pamoja na mambo mengine, itatambua uwepo wa nchi ya Tanganyika, asili yake, historia yake, utaifa wake na dola yake, huku Zanzibar ikipata mamlaka zaidi ya kujiamulia mambo yake.

Mbowe amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kutetea utaifa wao na kwamba angalau Zanzibar ina serikali yake tofauti na Tanganyika.

Wenzetu wa Zanzibar ukiwagusa ni wakali. Mimi nawapongeza Wazanzibari, ni watu wachache, lakini wanajua namna ya kujitawala. Ni watu wachache wanajua kutetea utaifa wao. Sisi tuna watu milioni 64 tunashindwa kutetea utaifa wetu,” alisema Mbowe, na kuongeza:

Wazanzibari wana serikali yao na katiba yao. Kwa hiyo, wakikaa kwao ni nchi kamili, wakirudi kwenye Muungano wamo vile vile.”

Aliongeza kuwa maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba yalisema wazi kuwa Watanzania wanahitaji muundo wa Muungano wa Serikali Tatu, lakini Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeyapuuza maoni hayo na kuamua kuigeuza nchi kuwa koloni lake.

Mbowe ametoa wito kwa Watanzania wote kuzidi kuungana na Chadema katika kupigania katiba mpya itakayorejesha muundo wa Muungano wenye usawa, pamoja na haki na ustawi wa wananchi wote.

Kwa upande wake, Lissu, akihutubia maelfu ya wananchi wa Babati, mkoani Manyara, alisema Tanzania inaadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Maombolezo kwasababu ya Katiba mbovu iliyounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa sababu ya miaka 60 ya Katiba ya Muungano, mzanzibari akitaka kununua na kumiliki shamba hapa Babati anaweza. Wewe mtu wa Babati ukitaka kwenda kumiliki shamba kule Pemba….thubutuuu…huwez. Kwenye Bunge la Muungano kuna Wazanzibari zaidi ya 80, lakini mtu wa Tanganyika hawezi kwenda mjumbe wa Baraza la Wawakilishi,” alisema Lissu.

Akiendelea kuchambua mapungufu ya Katiba ya Muungano, Lissu alisema:

Leo Samia kutoka Zanzibar, kwasababu ya mamlaka makubwa aliyopewa na katiba ya Jamhuri ya Muungano ameweza kuwanyang’anya wamasai ardhi yao na kuwahamisha.

Kiongozi huyo pia amesisitiza haja ya kuandikwa kwa katiba mpya ambayo si tu itarejesha nchi ya Tanganyika bali pia itaipa Zanzibar mamlaka kamili ndani ya muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Alisema mbali na kuboresha muundo na kuondoa kero za Muungano kwa pande zote, Katiba mpya inahitajika sana ili kupunguza madaraka makubwa ya rais na kuondoa kinga ya rais kutoshitakiwa, hatua ambayo itaimarisha uwajibikaji kwa umma na kuondoa desturi ya kulindana katika utendaji wa serikali.

Like