WOGA na ujinga ni tabia mbili chafu na hatari. Anayofanya Paul Makonda – na matokeo yake – ni ushahidi wa hili.
Bwana mdogo huyu kapewa kazi ya uenezi wa chama chake – CCM ngazi ya taifa. Ni juzijuzi tu.
We! Ili uweze kujua unene, urefu na uzito wa mamlaka yake, tulia na sikiliza.
Anaamuru mkuu wa mkoa kuja anakimbia pale anapomwita. Anaamuru mawaziri kumpa taarifa za utekelezaji kazi zao; kila baada ya miezi mitatu. Anatoa amri kwa waziri kufanya hili na lile; na anaagiza hata waziri mkuu kutenda – ama kama anavyoona, anavyotaka au alivyoagizwa._
Yote haya, Makonda anayafanya mbele ya katibu mkuu wa chama chake; mbele ya makamu mwenyekiti wa chama chake; mbele ya mwenyekiti wa chama chake.
Mbele ya mawaziri. Naibu waziri mkuu, Waziri mkuu, Makamu wa Rais na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna anayeyuga. Wote kimya!
Si kwamba katika sekretarieti, kamati kuu na halmashauri kuu ya CCM hakuna vichwa (mbongo) vya kuona haya – kuyafuta, kuyakemea au kuyarekebisha. Zimo! Zimenywea. Zimestuka, kushangaa na kufa ganzi. Uuuuwi!
Ziko kimya, ama kwa woga kwamba aweza kuwa ametumwa na “ngazi za juu” ili kuandaa mchujo mpya; au ni ujinga tu – kwamba huyu kibweje ana madaraka yanayotanuka (nyumbufu mithili ya raba za kufungia noti katika benki) kuliko yeyote katika Jamhuri hii. Ziko kimya!
Zimeanza amri kwa viongozi na hata wakubwa zake kikazi. Kinachofuata, huenda kikawa amri kwa bunge; amri kwa mahakama; amri kwa viongozi wa vyama vingine nchini.
Ninahisi, hawa hawatakubali. Matokeo yake ni nini?
Hapa, Makonda amejituma au ametumwa kufanya kazi ya nyongeza; ile kazi ya jiwe lililotupwa kichakani; na aliyelitupa akisubiri kuona vilivyomo vikichomoka kwa taharuki: ndege wakiruka mshazari na wanyama wakitawanyika; wakigongana kutafuta pa kutokea na jinsi ya kujiokoa.
Lakini katika ngeli hii ya Makonda, walengwa wamekufa ganzi. Wamepofuka na kuziwika. Wamesimama kwa magoti badala ya miguu; sauti zao zimebaki migumio isiyoenda nusu-inchi mbele. Wapo, hawapo!
Na kama waliotarajiwa kuwa makini wamelowa; waliotarajiwa kujua hawajui; waliotarajiwa kuwa jasiri wamenywea, waliotarajiwa kusambaza nuru wenyewe wamepoteza mboni; na wale waliotarajiwa kuneemesha jamii kwa taarifa bulbul wamekwazwa kwa hongo rejareja; basi na hatimaye, tutatawaliwa na vimbweneleni.
Hii ni hatari na uchafu; uzao uleule wa woga na ujinga. Ni sumu. Kwanini usiseme, “HAPANA?”