Kesi ya Mbowe: Mabishano ya mawakili yaahirisha shauri kwa mara nyingine

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia BJ kutoka mahakamani leo Jumatano Novemba 10, 2021.

Saa 5:41 kwa saa za Afrika Mashariki Jaji ameshaingia mahakamani tayari kuanza kesi.

Kesi inatajwa leo Novemba 10, 2021. Ni kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe.

Wakili wa Serikali Robert Kidando anawatambulisha mawakili wa Serikali:

  1. Pius Hilla
  2. Abdallah Chavula
  3. Jenitreza Kitali
  4. Esther Martin
  5. Nasorro Katuga
  6. Tulimanywa Majige

Wakili Peter Kibatala anamtambulisha Wakili Paul Kaunda kuwa ni wakili mpya wa mshtakiwa wa pili. Pia anawatambulisha mawakili wengine wa upande wa utetezi:

  1. Jeremiah Mtobesya
  2. Fredrick Kihwelo
  3. Dickson Matata
  4. Alex Massaba
  5. Maria Mushi
  6. Hadija Aron

WAKILI WA SERIKALI: Tutakuwa na mashahidi sita na vielelezo vinne. Na leo tuna shahidi mmoja. Tunaomba kuendelea.

WAKILI WA SERIKALI: Lakini kabla ya kuendelea, leo tunaona kuna utambulisho wa wakili mpya Paul Kaunda. Je, instructions za yule wa mwanzo zimeisha tupate utaratibu wa Mahakama.

PETER KIBATALA: Kama wakili msomi mwenzangu amenielewa mwanzo nimesema kwamba wakili John Mallya ameanza kwenye mahakama nyingine na punde atakapofila nitamtambulisha. Huyu Paul Kaunda hakuwahi kuwa kwenye kesi hii hapo mwanzoni ila kuanzia sasa tutakuwa naye.

WAKILI WA SERIKALI: Kama ni hivyo imeeleweka.

JAJI: Kwa hiyo anajiuga na nyinyi kuanzia leo?

KIBATALA: Ndiyo.

JAJI: Utetezi mmesema mna vielelezo vingapi?

WAKILI WA SERIKALI: Vinne.

JAJI: Upande wa utetezi mpo tayari?

KIBATALA: Ndiyo.

JAJI: Shahidi jina lako?

SHAHIDI: Superitendent Jumanne Malangahe.

JAJI: Umri?

SHAHIDI: Miaka 46.

JAJI: Dini.

JAJI: (Kiapo)

SHAHIDI: Muislamu. Shahidi Wallah wabillah watallah. Nathibitisha ushahidi nitaotoa utakuwa ni kweli na ukweli mtupu, Eeeh Mwenyezi Mungu nisaidie.

WAKILI WA SERIKALI: Umesema wewe ni askari Polisi. Je, shughuli zako unazifanyia wapi kwa sasa?

SHAHIDI: Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

WAKILI WA SERIKALI: Una nafasi gani hapo Wilayani Arumeru?

SHAHIDI: Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru.

WAKILI WA SERIKALI: Majukumu yako ni yapi?

SHAHIDI: Kuzuia uhalifu. Kukamata watuhumiwa, kuwapekua watuhumiwa, kuwaongoza askari walio chini yangu kasika shughuli ya upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna mtu mmoja anaitwa Mohammed Abdilah Ling’wenya. Elezea Mahakamani kama unamfahamu mtu huyu.

SHAHIDI: Namfahamu.

WAKILI WA SERIKALI: Tangu lini?

SHAHIDI: Tarehe tano Agosti 2020.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwaje mpaka ukamfahamu?

SHAHIDI: Baada ya kumkamata pale Rau Madukani.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwaje ukamakamata?

SHAHIDI: Baada ya kuwapo kwa taarifa kwamba anajihusisha kula njama za kutenda vitendo vya kigaidi.

WAKILI WA SERIKALI: Vitendo gani vya kigaidi alivyokuwa anajihusisha navyo?

SHAHIDI: Kulipua vituo vya mafuta, kuchoma moto maeneo yenye mkusanyiko kama vile masoko , kukata miti na kuweka barabarani, ikwemo na kuwadhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ole Sabaya.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati unamkamata ni mazingira gani ambayo ulimkamata hapo Madukani?

SHAHIDI: Siku hiyo hapo Rau Madukani tulikuwa na askari wenzangu ambao jumla tulikuwa watano ambapo tuliongozwa na ACP Kingai ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha.

WAKILI WA SERIKALI: Na wewe ulikuwa wapi?

SHAHIDI: Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru. Shahidi alikuwapo pia Inspector Mahita, alikuwapo Detective Coplo Francis na Detective Constable Goodluck.

WAKILI WA SERIKALI: Hao ni askari wa wapi?

SHAHIDI: Hao ni askari alikuja na Afande Kingai alikuja nao Arumeru.

WAKILI WA SERIKALI: Ukamataji huo ulifanyikaje na eneo gani?

SHAHIDI: Ukamataji ulifanyika majira ya saa saba mchana katika maeneo ya RAU Madukani, ambapo tulifika wote sisi watano na tuligawanyika katika maeneo mawili ambapo eneo moja alikuwa akiongoza Afande Kingai, mimi mwenyewe na Detective Constable Goodluck. Na eneo lingine alikwenda Inspector Mahita na Detective Coplo Francis ambapo tulijigawa kwa upande wa kulia na kushoto

WAKILI WA SERIKALI: Kulia na kushoto mwa nini?

SHAHIDI: Mwa kibanda ambacho tulipata taarifa kwamba wapo pale ambapo Mohammed Ling’wenya alikuwa na wenzake wawili.

WAKILI WA SERIKALI: Wenzake wawili ni akina nani?

SHAHIDI: Ni Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo na Moses Lijenje alimaarufu kama Kakobe.

WAKILI WA SERIKALI: Sasa baada ya kuwa askari mmejigawa mara mbili kama mlivyosema nyinyi askari mlifanya nini?

SHAHIDI: Maeneo waliyokuwa watuhumiwa hao palikuwa na njia mbili.

JAJI: Naona kama anatoa ushahidi kwenye kesi kubwa na siyo kesi ndogo.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwa ulimkamata ulimpeleka wapi?

SHAHIDI: Baada ya kumkamata na kumfanyia upekuzi nilimpeleka katika Kituo cha Polisi Kati Moshi. Alikuwa pamoja na watuhumiwa wenzake ambao tuliwakamata wakati wote, Adam Hassan Kasekwa.

WAKILI WA SERIKALI: Sasa mlipofika hapo Kituo cha Polisi Kati Moshi ulimpeleka wapi mtuhumiwa huyu?

SHAHIDI: Mtuhumiwa huyu alibaki ndani ya gari, kwa kuwa tulikuwa bado tunaenda kumtafuta mtuhumiwa mwingine ambaye tulimkosa katika eneo lile. Na Mohamed Ling’wenya alituahidi kutusaidia kumpata mtuhumiwa huyo.

WAKILI WA SERIKALI: Sasa kwenye gari alibaki na nani?

SHAHIDI: Alibaki na ACP Kingai, Detective Constable Goodluck, na Coplo Francis wakati mimi na Inspector Mahita tulienda kituoni kukabidhi unga unadhaniwa kuwa madawa ya kukevya.

WAKILI WA SERIKALI: Nini kiliendelea baada ya kukamilisha shughuli zote pale kituoni Polisi?

SHAHIDI: Tuliondoka na Mohammed Ling’wenya kwenda maeneo mbalimbali ambapo tuliambiwa tungeweza kumpata Moses Lijenje.

WAKILI WA SERIKALI: Maeneo gani hayo?

SHAHIDI: Rau Madukani, Pasua, Aishi mpaka Boma.

SHAHIDI: Maeneo ambayo yeye Mohamed Ling’wenya alikuwa akiyataja.

WAKILI WA SERIKALI: Kitu gani hasa kilikuwa kinaendelea juu yake?

SHAHIDI: Ni yeye kutuongoza na kutushauri kwa hiari yake tupite maeneo mbalimbali mpaka ilipofika saa tatu kuelekea saa nne tulikula chakula maeneo ya Boma tukiwa na mtuhumiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya akiwa kwenye hali nzuri. Na baada ya hapo tulirudi Moshi kwani tulikuwa hatujafanikiwa kumpata Moses Lijenje.

WAKILI WA SERIKALI: Meneo hayo yote mliyopita mlikuwa nani na nani?

SHAHIDI: Ramadhan Kingai, mimi mwenyewe, Inspector Mahita, Detective Constable Goodluck, Coplo Francis na dereva wa gari hilo ambaye ni Detective Constable Azizi.

WAKILI WA SERIKALI: Mtuhumiwa Mohammed Ling’wenya alikuwa wapi?

SHAHIDI: Alikuwa mekaa katikati.

WAKILI WA SERIKALI: Na mtuhumiwa Adam Hassan Kasekwa alikuwa amekaa wapi?

SHAHIDI: Amekaa nyuma, baada ya siti za katikati.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kutokufanikiwa mlimpeleka wapi mtuhumiwa?

SHAHIDI: Tulirudi Kituo cha Polisi Kati Moshi, tukawakabidhi kwa askari wa chumba cha mashitaka.

WAKILI WA SERIKALI: Muda gani?

SHAHIDI: Saa nne kuelekea saa tano za usiku.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwakabidhi kwa askari wa chumba cha mashitaka nini kilitokea?

SHAHIDI: Baada ya kuhakikisha mtuhumiwa Mohamed Ling’wenya kupokelewa aliulizwa hali yake akasema nzuri.

WAKILI WA SERIKALI: Aliwekwa wapi?

SHAHIDI: Mahabusu.

WAKILI WA SERIKALI: Wewe na askari mliokuja kituoni mlifanya nini?

SHAHIDI: Tuliondoka kwenda kuendelea na shughuli zingine za kiupelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumkabidhi kituo cha Polisi Moshi alikaa kwa muda gani?

SHAHIDI: Alikaa mpaka asubuhi ya tarehe sita Agosti 2020.

WAKILI WA SERIKALI: Nini kilitokea?

SHAHIDI: Mimi na Afande Kingai tulifika pale, nikamchukua Mohammed Abdilah Ling’wenya na mwenzake kwenda kumtafuta Moses Lijenje.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumchukua Mohamed Abdilah Ling’wenya kwa shughuli za kiupelelezi?

KIBATALA: Objection! Mheshimiwa sijasikia mahali ambapo shahidi amesema alikwenda kwa shughuli za kiupelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Naomba nikumbushwe.

JAJI: Kumtafuta Moses Lijenje.

WAKILI WA SERIKALI: Asante. Ni maeneo gani sasa mlienda kumtafuta Moses Lijenje?

SHAHIDI: Moshi Mjini, KCMC, Rau Madukani, Pasua, Himo, Aishi Hotel, Boma na Arusha Sakina.

WAKILI WA SERIKALI: Mlimpata?

SHAHIDI: Hapana. Tulimkosa na kuamua kurudi kituoni. Na tulipofika kituoni pale Moshi Afande Kingai alisema amepokea maelekezo tuwapeleke watuhumiwa Dar es Salaam.

SHAHIDI: Saa moja jioni tulianza safari ya kuelekea Dar es Salaam. Lakini tulipofika Njia Panda ya Himo gari yetu ilipata matatizo ya kiufundi. Ndiyo Afande Kingai akapiga simu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro. Baada ya kukaa pale tuliagiza chakula tukiwa na Mohammed Ling’wenya akiwa na afya nzuri bila tatizo lolote.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kukaa pale muda gani safari iliendelea?

SHAHIDI: Ilifika gari ya aina ya FOTON Station Wagon ikiendeshwa na PC Wendo. Tukaanza safari.

WAKILI WA SERIKALI: Mpangilio wenu kwenye gari ulikuwaje?

SHAHIDI: Mbele alikaa afadhali Kingai na dereva wa gari hilo. Katikati nilikaa mimi, Mohamed Ling’wenya na Mahita upande wa kulia. Na nyuma alikaa Adam Kasekwa na Detective Constable Goodluck.

WAKILI WA SERIKALI: Safari yenu iliwafikisha wapi?

SHAHIDI: Safari ya takribani masaa manane ilitufikisha Dar es Salaam.

WAKILI WA SERIKALI: Lini?

SHAHIDI: Siku ya tarehe saba Agosti 2020.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa saa ngapi?

SHAHIDI: Saa 11 kuelekea saa 12.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kufika nini kiliendelea?

SHAHIDI: Alipokelewa na chumba cha mashitaka.

WAKILI WA SERIKALI: Nani aliwakabidhi?

SHAHIDI: Mimi mwenyewe na afande ACP Ramadhan Kingai.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuwafikisha Central Dar es Salaam akitokea Moshi hali yake ilikuwaje?

SHAHIDI: Alikuwa na hali nzuri kabisa. Kwa mujibu wa mafunzo yetu, mnapopokea mtu kuna mambo ya kuzingatia likiwemo suala la afya.

WAKILI WA SERIKALI: Nini kiliendelea kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam?

SHAHIDI: Walipokelewa na kuwekwa mahabusu na sisi tuliondoka.

WAKILI WA SERIKALI: Tarehe sita Agosti 2020 wakati mnamchukua alfajiri Mohammed Abdilah Ling’wenya alikuwa na hali gani?

SHAHIDI: Siku hiyo wakati namchukua Mohammed Abdilah Ling’wenya alikuwa mzima na hakuwa na tatizo lolote.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna madai kwamba mtuhumiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya aliteswa akiwa mikononi mwa polisi baada ya wewe kumkamata.

SHAHIDI: Mtuhumiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya hakuwa akiteswa hata kidogo muda wote tulipokuwa naye. Alikuwa vizuri kuanzia kituo cha Polisi Moshi na kama angekuwa na tatizo asingepokelewa.

WAKILI WA SERIKALI: Vipi kuhusiana na ukaaji wake hapo Moshi kati ya muda wa tarehe tano na tarehe sita Agosti 2020 ulipomchukua Kituo cha Polisi Kati Moshi?

SHAHIDI: Alikuwa vizuri kabisa.

Kibatala” Objection! Yeye alisema aliondoka, sasa kusema mambo ambayo amesema kwamba amemkabidhi na kuondoka ni ‘hearsay’.

JAJI: Bila shaka kwa kumbukumbu za Mahakama alisema aliondoka baada ya kumkabidhi.

WAKILI WA SERIKALI: Siku ile ya tarehe tano Agosti baada ya kumkabidhi Kituo cha Polisi Kati Moshi, kitu gani kiliendelea?

SHAHIDI: Baada ya kufika siku hiyo ya tarehe tano Agosti 2020 hatukuendelea na chochote pale.

WAKILI WA SERIKALI: Mtuhumiwa Mohammed Abdilah Ling’wenya mlimuacha akiwa eneo gani pale polisi?

SHAHIDI: Aliwekwq lock-up pamoja na wenzake.

WAKILI WA SERIKALI: Turudi sasa tarehe saba Agosti 2020. Baada ya kumkabidhi kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam nini kiliendelea?

SHAHIDI: Tuliondoka kwa muda sisi na kiongozi wetu ACP Ramadhan Kingai. Tukarudi baadaye na baada ya kufika Afande Kingai alinipa maelekezo nimhoji Mohammed Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa saa ngapi wakati anakupa maelekezo?

SHAHIDI: Majira ya saa moja.

WAKILI WA SERIKALI: Ikawaje?

SHAHIDI: Nilianza kutafuta chumba cha kuweza kumhoji.

WAKILI WA SERIKALI: Ilikuwa ni eneo gani?

SHAHIDI: Ni chumba katika eneo la Polisi Mjini Kati Dar es Salaam.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kutafuta chumba nini kiliendelea?

SHAHIDI: Kwenye saa mbili nilifanikiwa kupata chumba saa mbili na saa mbili na nusu nilimfuata mtuhumiwa kutoka chumba cha mashitaka.

WAKILI WA SERIKALI: Ulimtoa kutoka sehemu gani na ulienda kumhoji sehemu gani?

SHAHIDI: Nilimtoa chumba cha mashitaka katika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam na kwenda kwenye chumba jirani palepale.

WAKILI WA SERIKALI: Taratibu gani ukitumia kumchukua.

SHAHIDI: Nilisaini kwa kitabu cha Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Ulisaini kwa kitu gani?

SHAHIDI: Kusaini kuonyesha kwamba mtuhumiwa huyo sasa yupo mikononi mwamgu.

WAKILI WA SERIKALI: Detention Register ulipata wapi?

SHAHIDI: Kwenye chumba cha mashitaka. Nikasaini ndipo wakanipatia mtuhumiwa huyo.

WAKILI WA SERIKALI: Leo hii ukiiona hiyo Detention Register unaweza kuitambuaje?

SHAHIDI: Nitaitambua kwa kuona sahihi yangu.

SHAHIDI: Naweza kutambua kwa kuona sahihi yangu ambapo nilimtoa mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa tunaomba kupatiwa Exhibit P1 ambayo tuliitumia siku ya tarehe 20 mwezi Septemba ambayo tuliitumia kwemye kesi ndogo.

MTOBESYA: Awe specific kwa anachoomba kwa sababu hiyo nyaraka siyo kwa ajili ya kesi hii.

MTOBESYA: Kama anataka kuomba aombe kwa maombi rasmi.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, statement yangu haiko hivyo. Lakini naomba nikumbushwe nilichokiongea.

JAJI: Kwa sasa tumpatie kwanza halafu tutaona anataka kusema nini mbeleni.

WAKILI WA SERIKALI: Leo hii ukionyeshwa Detention Register hiyo, kitu gani kitakufanya ukumbuke kwamba ulimtoa Mohamed Ling’wenya?

SHAHIDI: Uwepo wa sahihi yangu.

WAKILI WA SERIKALI: Vitu hivyo vinapatika wapi kwenye hiyo register?

SHAHIDI: Kwenye sehemu imeandikwa “OUT”. Hapo ndipo utakapoona saini yangu.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji naomba tumpatie kielelezo shahidi kwa utambuzi wa alichokisema.

(Shahidi anapatiwa kielelezo. Anakagua na kusoma).

(Baada ya shahidi kupekua na kusoma, huku akiweka miwani yake sawasawa anasema…)

SHAHIDI: Nimeiona.

WAKILI WA SERIKALI: Elezea kitu gani umeona.

SHAHIDI: Uwepo ma majina ya Mohamed Abdilah Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Ulichokiona ni nini na nini?

SHAHIDI: Sahihi yangu na sahihi yake.

WAKILI WA SERIKALI: Lipo eneo gani haswa la Detention Register?

SHAHIDI: Majina ya mtuhumiwa yapo kushoto na…

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji, hakusema mambo ya kushoto na kulia.

JAJI: Sawasawa.

WAKILI WA SERIKALI: Ungependa Mahakama ifanye nini hiyo Detention Register.

SHAHIDI: Naomba Mahakama ipokee kwa utambuzi.

JAJI: Kwa utambuzi?

WAKILI WA SERIKALI: Yes.

MTOBESYA: Tuna objection kwenye kupokelewa kwa hii nyaraka. Kwanza, shahidi hajasema tangu aiache hii nyaraka alionana nayo lini.

MTOBESYA: Kwa sababu nyaraka inataka kupokelewa, basi ni ‘admission’, na kwamba nyaraka inatakakiwa kutolewa shahidi awe ‘competence’ na inaenda pale ambapo shahidi ana )authentication). Kesi ya DPP dhidi ya Sharif Mohammed Mahakama ilisema shahidi anapoomba kupokelewa kwa nyaraka Mahakamani, shahidi aonyeshe kwamba anatambua nyaraka anayotaka kupokelewa Mahakamani, MOJA, ni ‘unique’ na ya PILI ni chain of custody. Hapa kwenye chain of custody inaenda kwa shahidi kuna foundation ambapo Shahidi anatakiwa kufanya kwenye witness box.

MTOBESYA: Na kwamba unique features ambayo shahidi kafanya siyo ENTRY. Kwa mfano kitabu hiki ni kweli kinatumika kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam? Hajafanya wala hajaonyesha kwamba kitabu hiki kinatoka Central na features zake ni hizi na hizi. Kwa hiyo ni wasilisho letu kwamba shahidi haja- lay foundation. Kwa hiyo hajafanya authentication. Na PILI, kwamba shahidi hajasema tangu aachane na hiki kitabu tarehe saba Agosti 2020 kimemfikiaje leo hapa Mahakamani. Kwa hiyo shahidi hajafanya chain of custody.

Paul KAUNDA: Kwa niaba ya mshitakiwa wa pili nakubalina na yote yaliyowasilishwa na wakili Msomi Mtobesya.

FREDRICK KIHWELO: Kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu napinga pia kupokelewa kwa nyaraka hiyo na naunga mkono hoja iliyotolewa na Wakili Mtobesya.

KIBATALA: Na sisi pia tunapinga kwa shahidi kutoa D. R hata kama kwa ajili ya utambuzi kwa sababu kutoa nyaraka ya utambuzi ni suala la kisheria kunapaswa kuwa na ‘legal’ na ‘factual’. Ni wazi kwenye kumbukumbu zako kwamba nyaraka hii ilitolewa katika shauri dogo la Adam Hassan Kasekwa. Shauri lile lina hadhi ya peke yake. Katika hili tunatatizo na ‘nexus’ kwa shahidi kutoa nyaraka kutoka kwenye store ya Mahakama. Wenzetu walitakiwa kuandika barua au hatua zingine nyaraka hii iwarudie mikononi mwao kwa sababu Mahakama na wao ni taasisi mbili tofauti. Wamezua wasiwasi kama walivyoiomba na kumpatia shahidi hapa Mahakamani. Shahidi hakuongozwa kwa namna yoyote ile kuhusianisha kuwepo Kwa nyaraka hii Mahakamani na yeye kuja kufanyia utambuzi. Nyaraka ilikabidhiwa na mtu mwingine kabisa. Hajazungumza chochote kati yake na shahidi Msemwa. Angekuwa yeye tungefumba macho kisheria. Kwa hili hajaonyesha uhusiano wowote kati yao.

KIBATALA: Nyaraka inapotolewa kama ID ni prerequisite ya baadae kwenda kutolewa kuwa kielelezo. Kwa hiyo tunapinga kupokelewa kwa nyaraka hii kama alivyosema Mtobesya na wenzangu wote.

(Jaji anainama na kuandika kidogo).

WAKILI WA SERIKALI: Tunaomba muda mfupi wa ahirisho ili kuweza kutoa hoja zetu. Zipo kwemye soft copy lakini tutahitaji muda wa kuzi- print na kuziwasilisha.

JAJI: Upande wa utetezi mnasemaje?

KIBATALA: Hatuna pingamizi na ahirisho lakini tunaomba lisizidi nusu saa kwa sababu leo tumechelewa kuanza na ni kwa sababu ya ombi lao hao hao.

(Kibatala anakaa halafu anateta na mawakili wenzake).

JAJI: Dakika 30 zinawatosha?

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Zinatosha.

JAJI: Basi tunaahirisha kwa dakika 30. Mpaka saa ngapi?

KIBATALA: Saa nane kamili. Iwe dakika 35.

JAJI: Saa nane kamili. Basi saa nane kamili tutarudi tena kuendelea na kesi.

Jaji anaondoka katika chumba cha mahakama.

Jaji ameshaingia mahakamani.

Kesi imeshatajwa tena, ni kesi namba 16 ya mwaka 2021, Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe.

Wakili wa Serikali anasema column yao ni ile ile na kwamba wako tayari kuendelea.

KIBATALA: Kama nilivyokuwa nimetoa taarifa awali, kwamba wakili John Mallya atakapofika nitamwombea ruhusa. Naomba sasa ikukupendeza tumuingize Wakili John Malya ambaye atakuwa na Paul Kaunda kwenye jopo letu.

JAJI: Anaanza nani?

WAKILI WA SERIKALI: Ataanza wakili wa Serikali Abdallah Chavula na Baadae Pius Hilla.

WAKILI WA SERIKALI: (Abdallah Chavula) Baada ya kusikiliza hoja za mapingamizi kutoka kwa wenzetu upande wa utetezi, sisi upande wa Jamhuri hatukubaliani nao.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji kwenye pingamizi la wenzetu, hoja yao ya kwanza iliyoletewa na Mtobesya kwamba shahidi ameshindwa kuweka misingi na kwamba hajaieleza Mahakama mara ya mwisho alipiona nyaraka leo hii imefikafika vipi kwenye mikono yake, na akaieleza Mahakama kwamba ushahidi unaendelea mpaka pale shahidi atakapo- authenticate ile nyaraka. Na akailekeza Mahakama kwenye shauri la DPP Vs Sharif Mohammed au jina lingine la Athuman na wenzake sita, Shauri la Rufaa ya Jinai la 64 mwaka 2016. Naomba na sisi tujibu kuanzia hapo.

WAKILI WA SERIKALI: Shauri hilo kuanzia ukurasa wa saba mpaka ukurasa wa nane, naomba kunukuu kilichozungumzwa.

JAJI: Haraka haraka.

(Wakili wa Serikali anasoma).

WAKILI WA SERIKALI: Huwezi kuzi- apply test hizi kwenye kielelezo ambacho ni nyaraka. Sifa hizi zilikuwa kwenye kielelezo ambacho ni gari. Mheshimiwa Jaji, kwa a ufupi tu niseme hoja za mwenzetu ambazo amekuwa akisheresha na kesi hii haziendani. Tulichonacho Mahakamani ni nyaraka. Mheshimiwa Jaji haya aliyokuwa anayasema haya akionyesha uniqueness kwenye shauri letu hayahusiani. Hoja nyingine wenzetu ni amejikita sana ni competence.

WAKILI WA SERIKALI: Naomba nielekeze Mahakama yako katika shauri la Jamhuri vs Charles Gazilabo na Wenzake Watatu. Lilikuwa ni shauri la Jinai la Rufaa Namba 354 la mwaka 2019. Mahakama ilikutana na mazingira kama haya isipokuwa wenzetu walikuwa wanatoa kama kielelezo sisi kama utambuzi, lakini inafahamika kwamba kanuni ni zile ile, iwe unatoa kwa utambuzi au kielelezo. Wenzetu wanasema shahidi siyo competent, lakini kwenye ukurasa wa 12 wa Shauri la Jamhuri vs Charles Gazilabo na Wenzake Watatu ukurasa wa 12 paragraph ya kwanza …..

(Anasoma…)

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye hilo hilo naomba nirejeshe Mahakama kwenye shauri la DPP Vs Mohammed Sharif ukurasa wa tisa paragraph ya tatu.

(Anasoma…..).

WAKILI WA SERIKALI: Hapa pia Mahakama ya Rufaa imesisitiza knowledge kwamba knowledge ni suala la msingi sana.

WAKILI WA SERIKALI: ,,,Na subject matter yetu leo Mahakamani ni ENTRY ya utambuzi Agosti 7, 2020 saa mbili na dakika kumi asubuhi. Shahidi ameileza Mahakama kwamba majira hayo alifika kwenye charge room (CRO) ya Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam kwa malengo ya kupatiwa mtuhumiwa. Na shahidi huyu anasema alipopatiwa mtuhumiwa aliweka sahihi katika kielelezo ambacho tunataka akitokea na baada ya sahihi akaondoka na mtuhumiwa. Shahidi akahojiwa “Utatambua vipi hicho kitabu ulichoweka sahihi zako? Kipi kitakufanya utambue?” Shahidi kasema nitaitambua kwa sahihi yangu. Shahidi akasema majina ya mtuhumiwa, kumbukumbu ya shauri ambalo lipo hapo kituoni. Mwisho akamaliza kwa kusema hayo yote utayakuta kwenye entry ya Agosti 7, 2020.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, kipi kingine atafanya? Hayo ndiyo ya kipekee. Hakuna zaidi ya hayo kwenye hii nyaraka tulizotaka kutoa. Nikionanisha yalisomwa na shahidi katika haya mashauri mawili tuliyoyarejea hakuna shaka shahidi wetu ana information ya subject matter ambayo ni entry ya Agosti 7, 2020. Mheshimiwa Jaji, wenzetu wakaenda mbali zaidi kwa kueleza habari ya Chain of Custody.

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye hilo walau mwenzetu akikubali kwamba hana ubishi kwamba kwenye kanuni ya Chain of Custody inakujakufanyia maamuzi baada ya kuisha kwa shauri na siyo katikati ya shauri. Lakini kasema kwa lililopo hapa tulipaswa ku- establish Chain of Custody. Hakuielekeza Mahakama kwa kanuni gani, kwa kifungu gani cha sheria wala kwa maamuzi ya Mahakama. Hakufanya.

WAKILI WA SERIKALI: Alichofanya ni kutoa hoja isiyo kuwa na msaada na sheria. Mheshimiwa Jaji, naomba nikurejeshe kwenye shauri la Jamhuri vs Charles Gazilabo katika ukurasa wa 17. Kwa ruhusa yako naomba ninukuu kuanzia aya ya tatu.

(Wakili wa Serikali anasoma….)

WAKILI WA SERIKALI: Katika shauri hili kilichokuwa kinabishaniwa ni nyaraka na Mahakama ikasema kwamba hoja ya Chain of Custody inapaswa kuwa established mwisho wa shauri na siyo katikati ya shauri. Mheshimiwa Jaji naomba niishie hapa nimkaribishe mwenzangu Pius Hilla naye aendelee.

Anakuja Wakili wa Serikali Pius Hilla

Kuna kamjadala hapa kwa mawakili wa Serikali. Jaji anawasubiri.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, nianze kwa kusema kwamba nayaunga mkono yote ambayo Mr. Chavula ameya- establish. Na mimi naomba niseme machache kuhusiana na foundation. Wakili Mtobesya alielekeza Mahakama kwamba shahidi hakuieleza Mahakama kwamba hicho kitabu ni cha jinsi gani. Wakili mwenzangu amelisemea hilo namimi nitaongezea kidogo.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, shahidi aliyopo kizimbani alishaeleza kwamba alimfikisha Mohammed Ling’wenya Kituo cha Kati Dar es Salaam, na kwamba watu wale waliingizwa mahabusu. Mheshimiwa hatuna Dar es Salaam nyingine. Hatuna Kituo Kikuu cha mjini kati Dar es Salaam kingine.

(Anakaa kimya kidogo)

WAKILI WA SERIKALI: Hakuna kituo kingine cha Kati Dar es Salaam ambacho Mahakama inaweza kukifikiria zaidi ya kilichopo. Na kingine shahidi alisema kwamba siku ya tarehe saba Agosti 2020 alikwenda Kituo cha Kati ambapo aliweka sahihi yake katika nyaraka Iliyopo mbele yetu. Ushahidi huo ni foundation tosha kwamba shahidi anazungumzia nyaraka ya kitu gani. Mheshimiwa Jaji nihame kwenye foundation nizungumzie alichokisema Kibatala kwamba hakuna nexus na kwamba kielelezo kilipaswa kitoke kwenye Exhibit Store ya Mahakama na siyo kuomba kama tulivyofanya. Mheshimiwa Jaji hoja yetu kwenye hili ni kwamba wenzetu hawapo sawasawa. Hawapo sawa kwa sababu Mheshimiwa Mahakama yako tukufu haijaelezwa ni procedure ipi imekiukwa. Mahakama yako tukufu haijaelezwa sheria ipi imekuwa violated. Mheshimiwa Mahakama yako haijaelezwa kwa namna yoyote ile washitakiwa wamekuwa treated vipi. Mheshimiwa Kibatala anasema kwamba Trial Within Trial ya Adamoo ilishaisha kule na exhibit ilipaswa iwe store. Tunakubaliana na hilo ni separate case Mheshimiwa Jaji lakini kiuhalisia huwezi kulitenganisha shauri lile na shauri la msingi lililopo Mahakamani, na uzuri hapajawahi kuwa na disposal order y a vielelezo.

WAKILI WA SERIKALI: Tupo sahihi kuomba vitu vya Mahakama na kuendelea kuvitumia na wala hatuja- violate yoyote ile. Mheshimiwa Jaji ukizipima hizi hoja zilizotolewa na wenzetu ni hoja yangu kwamba haziwezi kuzuia nyaraka isipolelewe. Haina uzito wa kuzia nyaraka tunayoomba ipokelewe. Mheshimiwa pasipo kuichosha Mahakama yako tukufu tunaomba mapingamizi yao yatupiliwe mbali. Nyaraka ambayo shahidi ameitambua na wenzetu hawapingi hilo. Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

(Wakili wa Serikali Pius Hilla anakaa)

(Jaji anaandika kidogo na Mahakama ipo kimya.

JAJI: Utetezi?

Mtobesya anasimama sasa.

MTOBESYA: Mheshimiwa nimesikia mawasilisho ya wasomi wenzetu mawakili wa Serikali. Mheshimiwa Jaji nimesikia kaka yangu anasema kwamba shauri la DPP na Sharif Mohammed ukurasa wa saba. Amesoma mwenyewe. Naomba na mimi nisome.

(Mtobesya anasoma)

MTOBESYA: Nashukuru kusoma kwake kumeleta msisitizo hapa Mahakamani kwa wasilisho lake kwamba kesi hii haihusiki na shauri hili amejielekeza vibaya. Kuna sehemu pia amesema pia kwamba hoja yetu ya competence kwa shahidi kuliko ushahidi wenyewe. Ni kwamba ushahidi hauwezi kujithibitisha wenyewe. Katika kesi hiyo hiyo ya DPP vs Sharif Mohammed ukurasa wa nane, paragraph ya tatu, ni kwamba anayepaswa kukieleza kielelezo ni shahidi mwenyewe. Na ni hoja yetu wakati anasoma nyaraka hajafanya ionekane anakijua. Nimesikia wakili wa Serikali kwamba kinachotakiwa kuwa authenticated ni ENTRY siyo document.

MTOBESYA: Sisi tunasema shahidi anafanya kwa lolote lile authenticate lile analosema. Ipo pia kwenye kesi ya Sharif Mohammed ukurasa wa nane aya ya pili.

(Mtobesya anasoma….)

MTOBESYA: Na pia alikuwa anasema kesi ya Sharif kuwa haijazungumzia Chain of Custody. Sasa hapo nimekusomea, na hayo ni maagizo ambayo Mahakama ya chini inapaswa kuyafuata. Na bado tunasisitiza kwamba shahidi hajafanya hayo.

MTOBESYA: Nimesikia kaka yangu anasema kwamba nimesema Chain of Custody ni jambo la mwisho. Sijasema hivyo. Nimesema kwamba kuna baadhi ya Mahakama zinasemaje Chain of Custody ni jambo la mwisho. Lakini tofauti na kilichopo Mhakamani ni suala la prerequisite. Chain of Custody ni kuangalia ushahidi wote kama palikuwa na proper paper trade. Lakini tofauti na kilichozungumzia hapa ni kwamba hajasema mara ya mwisho aliona wapi nyaraka mpaka leo anaitoa hapa Mahakamani. Wenzangu pia walitupitisha kwenye kesi ya Charles Gazilabo. Kwenye hiyo kesi walirejea kwenye hiyo hapo sasa ni submission yetu kwamba knowledge ni suala msingi lakini kwenye kesi hii ni tofauti.

MTOBESYA: Hii ya Gazilabo unakubalina na mimi kwamba kwenye kesi hii shahidi alikuwa na knowledge mpaka kwenye hukumu majaji wanasema shahidi yule akuitambua mpaka Unique Features. Sasa shahidi hajafanya chochote kwenye suala la ENTRY na kwamba kama tunakubaliana na kanuni za GAZILABO, lakini tunatofautisha mazingira ya GAZILABO na mazingira haya. Nimalizie kwenye wasilisho la kaka yangu Wakili wa Serikali Pius Hilla, kwamba shahidi alifanyia kazi nyaraka ambayo ilikuwa Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam. Hakuna kinachoifanya hiyo nyaraka ifanye iwe ya pekee. Na sisi hatukatai kwamba kuna Kituo kikuu cha Polisi Kati Dar es Salaam, lakini hakuna lolote kwenye nyaraka kinachoifanya ionekane ni nyaraka ya pale Central. Mheshimiwa Jaji sisi tunahitimisha kwamba kanuni ni zile zile zinatumika iwe kwa utambuzi au kielelezo.

MTOBESYA: Kanuni zipo wazi kabisa. Na sisi tunasisitiza kabisa kwamba nyaraka hii isipolelewe. Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

(Mtobesya anakaa)

(Paul Kaunda anakubaliana na mawasilisho yite yaliyifanywa na wakili Mtobesya na anasema anayo machache ya kuongezea).

KAUNDA: Mheshimiwa Jaji nianze kwa kurejea Provision na Jurisprudence ya kumbukumbu za Mahakama, kwamba muda sahihi wa kupinga nyaraka inayowasilishwa kwa maombi, iwe kwa utambuzi au kielelezo, ni pale inapotolewa tu, na siyo wakati wa cross examination, na siyo wakati wa re examination. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo. Shahidi aliyepo kizimbani hajaimbia Mahakama kwamba nini kilitokea kuanzia tarehe saba Agosti 2020 mpaka sasa kuhusiana na D. R. Na hiyo ndiyo kanuni kuu ya Chain of Custody juu ya nyaraka. Alipaswa asiache ombwe. Kwenye kesi ya SHARIF ilisema kwamba kushindwa kufanya hivyo Chain of Custody inakataaa.

KAUNDA: Mheshimiwa kwenye kesi hiyo hiyo ukurasa wa nane paragraph ya pili, Mheshimiwa Jaji Masati wakati huo na mnukuu ifuatavyo:

(Wakili Kaunda anasoma).

KAUNDA: Na hii ndiyo hoja yetu, na hayo ndiyo hajayasema Bwana Jumanne. Na hoja ya kusema tusubiri mpaka mwisho wa trial ndiyo Mahakama ndiyo iangalie siyo sahihi. Inapaswa ingaliwe tangu tarehe saba Agosti 2020 mpaka leo nyaraka ilikuwa wapi. Kwa kifupi Mahakama isifanye kinyume na hayo. Mheshimiwa Jaji mwaka jana mwezi Septemba Mahakama iliandaa mwongozo.

(Mawakili wa Serikali wamesimama wote)

JAJI: Tuaiache hiyo.

KAUNDA: Siyo new fact. Ni sheria tu nasoma.

JAJI: Hawatapata nafasi kuzungumzia hiyo.

KAUNDA: Sawa.

KAUNDA: Ni mahitaji ya msingi katika Mahakama inapotoa sifa za ushahidi.

JAJI: Unatuletea mambo mapya.

KAUNDA: Sawa Mheshimiwa Jaji.

FREDRICK KIHWELO: Wakili wa Serikali Pius Hilla amesema kwamba Trial Within Trial ni sehemu ya kesi hii.

JAJI: Umesikia hivyo?

Fredrick: Ndiyo.

JAJI: Hakusema hivyo. Nilisikia anasema Trial Within Trial ya Adam Kasekwa ni sehemu ya kesi ya msingi. We ishia alipoishia kusema.

FREDRICK KIHWELO: Basi nilitaka kusema kwamba Trial Within Trial ya Adam Kasekwa ni vitu viwili tofauti na Trial Within Trial ya Mohammed Abdilah Ling’wenya. Ndiyo maana wameomba tena kuingiza nyaraka.

JAJI: Kwa hiyo hoja yako kama kingekuwa ni kitu kimoja wasingeomba upya kupokelewa kwa nyaraka.

FREDRICK KIHWELO: Ndiyo hivyo.

KIBATALA: Nimemsiliza kwa makini hoja zake Bwana Pius Hilla lakini hajajibu hoja moja, kwamba nyaraka anayoiomba kupokelewa leo ipo kwenye Exhibit Room kwa sababu ilitolewa kwenye shauri lingine, na sijasikia akipinga hilo. Kwa hiyo ni ghafla sana tumekuta nyaraka ya ushahidi imetoka Exhibit Room imejikuta ipo hapa mahakamani kwa afisa wa mahakama. Tunakubali kwamba shauri dogo ni sehemu ya shauri mama, lakini leo hatupo katika shauri mama. Ndiyo maana leo shahidi PW1 ameapishwa na leo amepewa jina la PW1 wakati shauri mama ni PW8. Hairithi chochote na shauri lililopita.

KIBATALA: Hajapinga kwamba kuna Permission Rule kwamba kuna sheria Iliyomruhusu kwamba anaruhusiwa kutoa Exhibit Store. Kwa hiyo kuna mazoezi fulani ya kisheria walitakiwa kuyafanya yaweze kuwapa exhibit hapa Mahakamani. Pia hawajasema kuhusu ku- lay foundation kwamba kesi hii inahusiana vipi na kesi ya Adam Kasekwa, Siyo Jukumu la Mahakama kutoa kielelezo kwenye kaunta kwenda kwa shahidi, labda iwe kwamba ilishapokelewa. Wenzangu wanasema Sijaonyesha Procedural Violation, sasa kama sijafanya hivyo nilichofanya hapa ni nini? Wakati Mahakama inafanya uamuzi wake, je, kielelezo alichokitumia kwenye kesi ya Adamoo kingeruhusiwa tu kuingia kwenye kesi mama. Jibu ni HAPANA, lazima yangekuja maombi rasmi, kwamba siyo jukumu la mahakama. Hapo hoja shahidi haijamfikia makusudi. Jambo la PI:I ni kwamba wenzetu wanacheza na vichaka kuhusu kesi ya jana. Ndiyo maana wanasema “hawajasema hawajasema”. They are very clever. Nawasifu kwa hilo. Ila wajue kwamba Mahakama kuvuruga taratibu za kisheria tu ndiyo madhara yenyewe. Bunge limitunga sheria halafu Mahakama ikakiuka kwa umma hayo tu ni madhara kwa kuwa mkataba wa wananchi kupitia Bunge umekiukwa. Na hiyo ndiyo Adversarial System. Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Nimesikia hoja zenu kama namna ambavyo mmeziwasilisha na nitahitaji muda wa kuzipitia. Itanibidi kuahirisha ili niweze kupitia na kesho nifanye maamuzi.

JAJI: Kwa namna ambayo mmesalisha kwa muda mrefu na mimi nitahitaji muda mrefu kupitia na kutoa maamuzi. Kwa hiyo tukutane kesho saa tano asubuhi. Basi naahirisha shauri hili mpaka kesho saa tano. Shahidi utapaswa urudi ili uamuzi ukisomwa uweze kuendelea na ushahidi wako. Muwe na jioni njema.

Jaji anatoka mahakamani.

Like
3