Magufuli aanza kusahau kauli yake juu ya “umahiri” wa wabunge wa CCM

RAIS John Magufuli ameanza kusahau kauli yake juu ya “umahiri” wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao alisema wanafaa kuwa mawaziri. Sasa anateua mawaziri na manaibu wao nje ya wabunge wa majimbo ambao wiki chache zilizopita aliwasifu.

Akizindua rasmi Bunge la 12, jijini Dodoma, Rais Magufuli alisema kutokana na wingi wa wabunge wa chama chake, hatapata shida kuchagua mawaziri, kwa kuwa walioingia bungeni wana sifa nyingi na kubwa kushika nafasi za uwaziri.

“Sitapata  shida kupata mawaziri wangu humu, wengi mna sifa sahihi,” alisema.

Katika hotuba yake hiyo ya Novemba 13, mwaka huu, Rais Magufuli alisema haoni sababu ya kuanza “kuokoteza” watu wengine kujaza nafasi za uwaziri ili kumsaidia kuwatumikia Watanzania. 

Hata hivyo, kabla mwangwi wa maneno yake haujakatika masikioni mwa watu, Rais Magufuli wakati ikitangaza baraza la mawaziri, alipinga msimamo wake wa “kutoteua wengine” kwenye uwaziri, alipotaja majina ya watu wawili wasiokuwa miongoni mwa wabunge 270 wa majimbo wa CCM aliokuwa akitamba kwamba ni hazina katika kuteua wasaidizi wake.

Mbali na wabunge hao wa majimbo, CCM CCM wabunge 94 wa viti maalum ambao jumla yao wanatengeneza wabunge 364 wa chama hicho. Vyama vya upinzani vina wabunge sita wa majimbo na 19 wa viti maalum, wote wakitoka chama kikuu cha upinzani, Chadema.

Wabunge walioteuliwa katika nafasi 2 za “upendeleo wa rais” na hatimaye kuwa mawaziri ni Dk. Dorothy Gwajima ambaye amekuwa waziri wa afya, huku Dk. Leonard Chamuhiro akiwa waziri wa ujenzi na uchukuzi. Mwingine aliyeukwaa unaibu waziri wa madini baada ya kupata ubunge wa rais, ni Prof. Shukrani Manya. 

Viongozi wawili waliopita ubunge wa Rais Magufuli ni;  Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na Riziki Lulinda, mwanachama wa CCM aliyehamia kwenye chama hicho karibuni akitokea chama cha upinzani, CUF.

Mwenyekiti wa Chauma ambaye alichuana na Rais Magufuli na wagombea wengine, kuwania urais wa Tanzania, Hashimu Rungwe anasema hatua ya kiongozi wa nchi kushindwa kusimamia kauli zake ni ishara ya kushindwa katika utendaji. 

“Ukisikia kiongozi ana ahidi jambo moja na kesho anafanya jingine, tambua kuna shida, haiwezekani rais   mwenye uwanja mpana wa kuchagua wabunge wake zaidi ya 350, kupata mawaziri, anawakosa humo na kulazimika kutafuta kwingine, na kibaya zaidi alituambia kwamba anao wengi wa kuchagua, sasa yako wapi? Anahoji na kuongeza – “tuna shida sana.”

Mwanasheria Rajab Magembe wa Dar es Salaam, anasema kwamba anashangaa kuona Rais aliyetangaza kwa tambo kuwa ana nafasi kubwa ya kuchagua mawaziri kutoka ndani ya wabunge wake, amekengeuka na “kuwaacha solemba.”

Msomi huyo wa sheria aliyehitimu masomo hayo Chuo Kikuu cha Witswaterstrand, Afrika Kusini, anasema inastaajabisha kwa wasomi na wataalamu wengi walioshinda ubunge kupitia CCM, hakuna wanaoweza kuteuliwa kuwa mawaziri.

Kwa uteuzi wa wabunge hao watano, Rais Magufuli amebakiza nafasi zingine tano ili kufikia wabunge wa upendeleo wa rais 10 kama inavyoainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa TanzaniaReplyForward
Like