Tovuti za serikali zalaumiwa kwa “kuficha” taarifa muhimu

Haya ndiyo majina na sura pekee za mawaziri zilizopo kwenye tovuti rasmi ya rais hadi leo wakati tunachapisha habari hii.

TOVUTI rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hadi leo Jumamosi Desemba 12, 2020 inaonyesha kuwa serikali ina mawaziri watano tu.

Mawaziri wengine hawajawekwa katika orodha hiyo ya tovuti rasmi ya rais.

Hadi saa 7.00 ya leo, mawaziri wanaoonekana katika tovuti ya Ikulu ni Dotto Biteko (Waziri wa Madini), Dk. Philip Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango),  Dk. Faustine Ndugulile (Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Luhaga Mpina (Waziri wa Mifugo na Uvuvi) na Elias Kuandikwa (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).

Hatua hii inaweza kuelezwa kuwa ni uzembe na kuonyesha namna baadhi ya watendaji wasivyoweza kwenda na kasi ya teknolojia.

Mtaalamu wa teknolojia ya habari ambaye anahudumu katika kampuni ya Aidank Technologies, iliyoko Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, Aidan Nkimanyi, anasema kushindwa kuiweka tovuti hiyo ni uzembe.

“Haiwezekani tovuti rasmi ya Rais wa Tanzania ikashindwa kuhuisha taarifa zake, tena zenye kubeba Baraza jipya ambalo kila mmoja anafuatilia kufahamu watendaji wapya, ni uzembe tu,” anaongeza.

SAUTI KUBWA imebaini pia kuwa miongoni mwa tovuti muhimu zenye watendaji wanaolipwa lakini zipo nyuma ya wakati ni pamoja na tovuti ya serikali kuu  ambayo hadi leo saa 07.00 mchana haijaweka taarifa wala picha za mawaziri wapya.

Nyingine ni tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo licha ya kutangaza washindi tangu mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, bao haijachaoisha taarifa za matokeo hayo.

Wakosoaji wa uzembe huu wanasema imekuwa kawaida kwa NEC kutoweka matokeo ya wabunge jimbo kwa jimbo. Habari pekee kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu iliyopo ni ya matokeo ya urais.

Mmoja wa wakosoaji ambaye hakutaka kutajwa jina anasema: “Tatizo ni kwamba wana matokeo bandia. Hesabu ya kura waliyoweka si ile ya kura zilizopigwa. Walichakachua, na sasa wamekosa muda wa kufanya uchambuzi wa jimbo kwa jimbo.”

Ofisi ya NEC haijapatikana kueleza sababu za kushindwa kuweka matokeo katika tovuti kama wanavyoweka ya taarifa nyingine za kazi zao.

Mwalimu wa kujitegemea wa teknolojia ya habari anayefunza vyuo mbalimbali nchini, Ismail Mahebood, anasema kushindwa kuhuisha taarifa za tovuti rasmi za serikali ni “jambo la kusikitisha.”

Waziri wa mawasiliano na teknolojia ya habari, Dk. Faustine Ndugulile anasema anasononeshwa na hatua hiyo ya kuchelewesha kuhuisha taarifa. Ameahidi kuwa atahakikisha kila eneo la serikali linalotakiwa kutoa taarifa linafanya hivyo kwa wakati vema ili umma upate taarifa rasmi zisizokuwa na chembe ya uzushi.

Waziri huyo amewataka watu wote wanaotumia mitandao ya kijamii, kujiepusha na habari za uongo, uzushi na kutowatia wananchi hofu.

Like
1