Serikali imeleta bajeti hewa – upinzani

KAMBI rasmi ya upinzani inaamini kwamba iwapo Bunge llitapitisha bajeti ya serikali mwaka huu, litakuwa limepitisha bajeti hewa. Yafuatayo ni maoni kambi hiyo kama yalivyowasilishwa bungeni wiki iliyopita: 

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ni wajibu wa Bunge kupanga na kuidhinisha mapato na matumizi ya serikali kila mwaka wa fedha .Hii ni kwa mujibu wa ibara ya 137(1)’Rais atatoa maagizo kwa watu wanaohusika kwamba watengeneze na kuwasilisha kwenye Bunge katika kila mwaka wa fedha wa Serikali, makadirio ya ‘Mapato na Matumizi’ ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kipindi cha mwaka wa fedha unaofuata’Mheshimiwa Spika, nasikitika kusema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2016/17 serikali imewasilisha bajeti hewa hapa Bungeni.Mheshimiwa Spika, ninasema kuwa serikali hii imeleta bajeti hewa hapa Bungeni na nitathibitisha maoni yangu haya kama ifuatavyo;

  1. Kwa mujibu wa Kitabu cha Mapato ya serikali katika mwaka huu wa fedha volume 1 ‘Financial Statements and Revenue estimates’ for the year 1st July ,2016 to 30th June 2017 kilicholetwa hapa Bungeni kinaonyesha kuwa mapato yote ya serikali yaani mapato ya kodi , yasiyokuwa ya kodi ,mikopo na misaada ya kibajeti itakuwa jumla ya shilingi Trilioni 22.063.  Mheshimiwa Spika, upatikananji wa mapato hayo ni kama ifuatavyo;

    i.        Mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali ni shilingi Trilioni 17.797

    ii.        Mapato yasiyokuwa ya kodi ni shilingi Bilioni 665.664

    iii.        Mikopo na misaada ya kibajeti ni shilingi Trilioni 3.600Mheshimiwa Spika, ni muhimu Waheshimiwa Wabunge wakatambua kwamba Serikali hii haijaonyesha chanzo kingine kipya cha mapato ambacho hakijathibitishwa na au kupitishwa na Bunge hili kwa mujibu wa katiba na ijulikane pia kuwa Bunge halipitishi kitabu cha hotuba ya waziri bali hupitisha mafungu yaliyopo kwenye vitabu vya bajeti ya serikali.

  2. Kwa mujibu wa kitabu cha matumizi ya kawaida ,volume II Estimates of Public Expenditure Consolidated Fund Services for the year 1st July ,2016 to 30th June, 2017 na kitabu cha Maendeleo, Volume IV Public Expenditure Estimates Development Votes (part A) kama vilivyowasilishwa Bungeni , tayari bunge limeshaidhinisha matumizi ya jumla ya shilingi Trilioni 23.847 Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa fedha hizo ni kama ifuatavyo:

    i.     Fedha za Matumizi ya Kawaida (Volume II) shilingi 13,336,042,030,510

    ii.     Fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo (Volume IV) shilingi 10,511,945,288,575

  3. Ukichukua kitabu cha Mapato ya Serikali (Revenue Book Volume I) utaona kuwa jumla ya mapato yote ya serikali ni shilingi Trilioni 22.063 , ila serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Trilioni 23.847 ambacho ni kiasi tofauti na Mapato ambayo serikali imepanga kukusanya na tofauti yake ni kuwa kuna nakisi ya shilingi Trilioni 1.783 jambo ambalo linaifanya bajeti hii kukosa uhalali kwani nakisi hii ni kubwa sana.
  4. Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa fedha ‘Mapendekezo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17 kwenye mkutano wa wabunge wote katika ukumbi wa JNICC’ mnamo tarehe 06 Aprili, 2016 pamoja na maelezo ya hotuba yake aliyoyatoa hapa Bungeni uk. 91 ameendelea kulidanganya Bunge na Dunia kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali ina bajeti ya kiasi cha shilingi Trilioni 29.539.
  5. Hotuba ya waziri wa fedha katika ukurasa wa 92 ‘Mfumo wa Bajeti wa Mwaka 2016/17’ inaonyesha kuwa kiasi cha shilingi trilioni 7.475 ni mikopo ya ndani yenye masharti ya kibiashara. Fedha hizi kwenye kitabu cha mapato hazipo na pia hazionekani zitakopwa kutoka Benki gani kama ambavyo mikopo ya nje yote imeonyeshwa kwenye kitabu cha mapato na hata kwenye kitabu cha miradi ya maendeleo hazionekani kwenye kutekeleza mradi wowote ule na hivyo ni sahihi kusema kuwa ni fedha hewa , maana hazina hata kasma yake na Bunge hili tunapitisha kasma .
  6. Hotuba ya waziri wa fedha uk.58 anasema kuwa moja ya chanzo chake cha mapato ni pamoja na kurekebisha sheria ya Kodi ya Mapato SURA 332 (i)’kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye malipo ya kiinua mgongo kinacholipwa kwa wabunge kila mwisho wa muhula wa miaka mitano.’

Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kupata majibu ya kina kuhusu mambo yafuatayo;

  1. Bunge linapitisha takwimu zipi hasa? Ni kitabu cha hotuba ya waziri au ni vitabu vya mapato na matumizi pamoja na kile cha Miradi ya maendeleo?
  2. Fedha ambazo waziri kwenye hotuba yake anasema kuwa ni mikopo ya ndani ya masharti ya kibiashara, zinakopwa ili kugharimia miradi ipi? Kwani tayari kitabu cha miradi ya maendeleo VOLUME IV kimeshataja miradi yote na kiasi cha fedha ambazo kila mradi utatumia.Hii miradi inayosemwa kuwa fedha itakopwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni miradi ipi hiyo? Mbona haijapitishwa na bunge au ni miradi hewa?
  3. Waziri wa fedha anaposema kuwa fedha za matumizi ya kawaida ni shilingi Trilioni 17.719 na hapo hapo anasema kuwa tunakwenda kulipa deni la taifa kiasi cha shilingi trillion 8, mbona hizi fedha hazipo kwenye kitabu ambacho kinapitishwa na Bunge? Kitabu cha matumizi ya kawaida VOLUME IV?
  4. Kwa kuwa CAG anakagua kasma zilizopo kwenye vitabu yaani VOLUME IV na VOLUME II, katika bajeti hii atakagua kasma ipi?maana fedha za kulipia deni la taifa hazipo kwenye kitabu cha VOLUME II na hata mikopo yenye masharti ya kibiashara inayosemwa itakopwa haipo kwenye Revenue Book
  5. Huu mkanganyiko wa vitabu vya serikali moja imesababishwa na nini au kuna mikopo na miradi hewa? Ni kwanini kitabu cha mapato (revenue book) kinaonyesha mapato madogo kuliko kiwango cha matumizi?
  6. Kuingiza malipo ya kiinua mgongo cha wabunge ambacho kinatakiwa kulipwa mwaka 2020 kwa mujibu wa sheria na kuwa chanzo cha mapato katika mwaka huu wa fedha 2016/17 hiki si chanzo hewa? Nasema hivi kwa kuwa, kila mwaka tutakuwa tukipitisha bajeti na hiki kilipaswa kuwa chanzo ifikapo mwaka 2020 ambapo ndio kiinua mgongo hiki kinalipwa na ndio kingekuwa chanzo cha mapato au serikali imepanga kulipa kiinua mgongo hicho kila mwaka wa fedha?

Mwisho Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, tunaitaka serikali iwasilishe Vitabu vyenye kumbukumbu na takwimu sahihi kabla ya kulitaka Bunge hili kujadili bajeti hii na kuamua kuipitisha au kuikataa, la sivyo Bunge litakuwa halitimizi wajibu wake kikamilifu kwa mujibu wa katiba ya Nchi yetu.

Like

Leave a Comment

Your email address will not be published.