Mashirika ya ndege: usipochanjwa hupandi, sahau kusafiri

KAMPUNI kubwa za ndege duniani zinapanga kuanzisha utaratibu wa kila abiria kuonyesha kuwa na kadi ya chanjo ya ugonjwa wa Corona – akiwa hana maambukizi – kabla hajapanda ndege.

Ikiwa hatua hii itaanza kutekelezwa, Tanzania itaathirika zaidi kwa wananchi wake kuzuiwa safiri nje ya nchi hiyo, kwa kuwa Rais John Magufuli na serikali yake wamekataa kupokea chanjo. Wanaidhihaki kwamba chanjo ya “mzungu” haifai.

Taarifa zinaeleza kuwa kampuni hizo zimeanza kuhimiza kampuni za kikanda au nchi kujipanga kuanza zoezi hilo baada ya kupata “baraka” kutoka mamlaka stahiki.

Inaelezwa kwamba Corona imeathiri zaidi biashara ya usafiri wa anga, kiasi cha kuwepo baadhi ya kampuni kufunga biashara kutokana na kukosa abiria.

SAUTI KUBWA iliripoti kampuni ya usafiri wa anga ya Precision Air ya Tanzania, ilipunguza wafanyakazi wake na kuamuru wengine kupunguzwa mishahara ili kunusuru kufungwa kabisa kutokana na athari za Corona. Hata hivyo kampuni hiyo ilikanusha taarifa hizo kwa kujikanganya, ikionyesha kuikiri.

Tangu mwanzoni mwa mwaka jana, mara baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa Corona na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutangaza kuwa ni janga la dunia, nchi nyingi zilifunga viwanja vya ndege na kuzuia wasafiri kuingia na kutoka ikiwa njia ya kudhibiti ugonjwa huo.

Leo kampuni za ndege na mashirika yanayohusika na usafiri wa anga nchini Marekani yameandika barua kwa Rais Joe Biden kuruhusu kuanza kutumika kwa kadi zinazoonyesha wasafiri wamechanjwa dhidi ya Corona.

Like