Maridhiano Zanzibar: Kuna siri nzito tusiyoijua

Rais Hussein Mwinyi akimwapisha Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. PICHA YA MAKTABA

HATUA ya chama kikuu cha upinzani Zanzibar kuridhia kuingia katika serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Dk. Hussein Mwinyi imeibua maswali na maoni yanayokinzana kutoka kwa wadadisi na wafuatiliaji wa masuala ya siasa kwa wiki kadhaa sasa.

Wakati watu wakiendelea kudadisi na kufuatilia maridhiano hayo, SAUTI KUBWA imekuwa kwa takriban wiki kadhaa sasa ikifuatilia kile kilichomo nyuma ya pazia ya hatua hiyo ambayo baadhi ya watu wanaiona kuwa inayoweza kuonekana kubariki mwenendo uliojaa hila, kasoro na hujuma za dhahiri katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28.

Habari kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya vyama vikuu viwili, Chama Cha Mapinduzi na kile cha ACT-Wazalendo zinaonyesha kwamba maridhiano hayo kwa kiwango kikubwa yamefanywa kama hatua ya mwanzo ya kuhitimisha safari ndefu ya historia ya siasa za visiwani ambazo hata kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964 zimekuwa zikitawaliwa na chuki, uhasama, ubaguzi, uunguja na upemba. 

Watu walio karibu na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo ambaye kwa sasa ndiye Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, wameieleza SAUTI KUBWA kwamba maridhiano hayo yamekuja baada ya kuwapo kwa vikao kadhaa vya faragha ndani ya kila chama na miongoni mwa vyama husika kwa pamoja.

Mmoja wa viongozi wa juu wa kisiasa Zanzibar aliyezungumza na SAUTI KUBWA anasema kabla ya chama ACT-Wazalendo kutangaza kupitia katika Kamati Kuu yake uamuzi wa kuridhia kuingia katika serikali ya Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kulikuwa kumefanyika vikao takriban sita vya faragha kati ya Rais huyo na Maalim Seif.

Mbali ya vikao hivyo, taarifa kutoka ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) zinaeleza kuwa kabla maridhiano hayo kila upande ulipata fursa pia ya kufanya mashauriano na wawakilishi kadhaa wa jumuiya ya kimataifa na wanadiplomasia ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa mambio kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Chanzo kimoja cha uhakika kutoka katika ubalozi wa moja ya mataifa makubwa uliopo Dar es Salaam kimeieleza SK kwamba haiba binafsi ya Rais Mwinyi na dhamira yake ya dhati iliyokuwa ikionyesha nia ya dhahiri ya kutafuta maridhiano ndiyo kiini kikubwa ambacho hatimaye kiliwapa imani ACT-Wazalendo, wana diplomasia na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa.

Katika hotuba yake jana mbele ya viongozi na makada wa CCM Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi alisema amedhamiria kufanya uamuzi mgumu ili kunusuru Zanzibar isiingie katika hali ngumu hapo baadaye.

Kwa mujibu wa chanzo hicho kingine cha habari, hata kabla ya uamuzi wa ACT-Wazalendo kutangaza kuingia katika serikali ya umoja wa kitaifa, tayari chama hicho kilikuwa kimeshapata baraka kutoka mamia ya wanachama wake wenye ushawishi Zanzibar na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa ambao walikuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa mambo Zanzibar.

Dalili za awali za kufikiwa kwa maridhiano hayo zilianza kuonekana mapema hata kabla ya tangazo rasmi kutokana na kauli za mara kwa mara za Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye mara kadhaa alikaririwa akiwaeleza watu waliokuwa karibu yake kwamba chama hicho kilikuwa katika hatua za mwisho za kutoa uamuzi mzito kwa maslahi mapana ya chama chao na wapenda amani na mshikamano wa kitaifa Zanzibar.

Kila wakati Zitto alipokuwa akitoa kauli hizo alikuwa akifanya rejea ya kile ambacho alikuwa akikisema chini chini kuwa ni mvutano wa ndani katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) uliosababisha hatua ya wanawake 19 kuapishwa kuwa wabunge na viti maalum kwa tiketi ya chama hicho na mgogoro uliolazimisha chama kuwafukuza uanachama.

“Sisi hatutafanya makosa ya Chadema. Tuko hatua za mwisho kabla ya kueleza msimamo wetu juu ya Zanzibar. Subirini!” Hayo ni maneno ya Zitto kwa mmoja wa marafiki zake aliyotoa zaidi ya wiki moja.

Habari zaidi zinaeleza kwamba mazungumzo na mashauriano kuhusu maridhiano yalianza kwa hoja ya ACT-Wazalendo kuweka sharti la kuachiwa kwanza huru kwa Naibu Katibu Mkuu wa wao, Nassor Mazrui, ambaye alikuwa kizuizini katika eneo ambalo lilikuwa halijulikani huku kukiwa na taarifa kwamba alikuwa akiandaliwa mashitaka ambayo hayakuwekwa bayana.

Taarifa hizo zilikwenda sambamba na kueleza kwamba viongozi wa ACT-Wazalendo katika kuhakikisha kwamba Mazrui anaachiwa, walianza kutaja jina lake kuwa miongoni mwa wanachama wao waliokuwa wakiwafikiria kupeleka jina lake kwa ajili ya uteuzi wa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Kwa mujibu wa habari hizo, serikali ya Mwinyi ambayo inatajwa kuwa yenye ushawishi mkubwa visiwani na Tanzania Bara kwa hivi sasa, iliridhia sharti la kumwachia Mazrui bila ya masharti yoyote ikiwa ni pamoja na kuachana na mpango wa kumfungulia mashitaka.

Mbali ya hilo inaelezwa kwamba, pande hizo mbili chini wa uratibu wa Rais mmoja mstaafu kutoka katika ukanda wa SADC ambaye aliteuliwa kuwa msuluhishi zilikubaliana kuanza kuchukuliwa kwa hatua mahususi za kutibu majeraha yaliyotokana na vitendo vya ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.

Katika mazungumzo hayo ya faragha, ilibainika kwamba baadhi ya matendo ya ukatili dhidi ya binadamu yalifanywa na watu binafsi ndani ya vikosi vya ulinzi na usalama ambao wamekuwa na uhasama na chuki binafsi dhidi ya wafuasi wa ACT-Wazalendo na Maalim Seif binafsi.

Inaelezwa kwamba, miongoni mwa mambo ambayo yako katika azimio la pamoja la maridhiano hayo ni kuundwa kwa tume maalum ya Rais ambayo pamoja na mambo mengine itachunguza juu ya matendo hayo na hatua kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika katika matendo ya namna hiyo.

Mbali ya hayo, inaelezwa kwamba pande hizo mbili zimepeana muda maalum wa utekelezaji wa maazimio yote kwa kila upande ambao unaendelea kuratibiwa na msuluhishi huyo aliyeteuliwa na taasisi moja ya kimataifa ambayo Tanzania ni mwanachama wake. 

 
Like
4