Magufuli na kichwa cha chui ndani ya kopo

Magufuli akigawa mapapai sokoni. Leo amesema maabara ya taifa imepima mapapai ma kukuta yana Korona. - Picha ya maktaba

KATIKA hotuba yake kwa taifa leo baada ya kumwapisha Waziri wa Sheria na Katiba, Rais John Magufuli amezungumza mambo mengi ambayo yanaweza kuchambuliwa kwa namna mbalimbali, lakini mimi nitayachambua kwa lugha nyepesi.

Ameachia mishale mingi kila upande. Mishale hii inaweza kuwa na matokeo hasi au chanya, au yote mawili. 

Amewasema viongozi wa dini, hata kubeza baadhi yao kuwa wamejengewa nyumba za ibada. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Magufuli, akiwa waziri, alijenga “kanisa” huko kwao Chato, akaliweka kwa ajii ya madhehebu yote ya Kikristo, lakini Wakatoliki na Walutheri hawakukubali kulitumia kwa sababu za kiliturjia. Kwa ujumbe  huu, alilenga kumweleza askofu wake kuwa “kanisa lile si la askofu bali ni la waliolijenga.” 

Huu ni mwendelezo wa mchuano mkali ambao Magufuli amekuwa nao dhidi ya viongozi wa dini, hasa wale wasiompigia makofi au magoti. Katika mzozo wa mwaka juzi kati ya serikali na makanisa, baada ya maaskofu kutoa nyaraka za Pasaka na Krismasi zilizokemea dhuluma na kutetea haki, Magufuli alieleza baadhi ya watu wake wa karibu kuwa anataka maaskofu watambue kuwa nchi ina “rais mmoja tu.” 

Ujumbe huo ulimlenga zaidi Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Iringa aliyekuwa Rais wa Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania, ambaye alisimama kidete dhidi ya vitisho vya serikali kupitia msajili wa vyama katika wizara ya mambo ya ndani. 

Katika mzozo huo, serikali ilimnyang’anya pasipoti Padri Raymond Saba aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, ikikerwa na jinsi alivyosimamiwa mawasiliano kati ya serikali na wizara. Ilimtuhumu kuwa si raia wa Tanzania. Baadaye kanisa lilimwondoa katika wadhifa huo na kumteua Padri Charles Kitima

Tangu wakati huo, uongozi wa Askofu Ngalalekumtwa ulipofikia mwisho wa ngwe yake na kuondoka, wakateuliwa wengine, Kanisa Katoliki limekuwa “laini” mbele ya serikali na kupoteza taswira ya kinabii iliyozoeleka kwa miaka mingi. 

Mbali na Padri Saba, serikali ya Magufuli pia ilichukua pasipoti ya Askofu Severin Niwemugizi mwaka 2016, ikimtuhumu kuwa si raia, baada ya askofu huyo kusisitiza umuhimu wa katiba mpya.

Hata hivyo, SAUTI KUBWA ina taarifa kuwa askofu alirejeshewa pasipoti yake mwaka mmoja uliopita kimya kimya, baada ya kelele kuwa nyingi mitandaoni na katika duru za kidiplomasi na kanisa. 

Askofu Niwemugizi ndiye anaongoza Jimbo la Rulenge-Ngara ambalo pia linajumisha Parokia ya Chato, nyumbani kwa Rais Magufuli. Katika kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Korona, Askofu Niwemugizi amefuta mikusanyiko ya kiibada ya waamini jimboni mwake kwa mwezi mzima.

Rais Magufuli alikerwa na uamuzi wa askofu huyo, na alitumia hotuba ya jana kukejeli na kusakama viongozi wa dini waliofunga makanisa kwa muda katika kipindi hiki.

Baadhi ya wachambuzi wanasema hasira za Magufuli zinatokana na ukweli kuwa amekuwa akitumia fursa ya ibada Jumapili kufanya siasa kanisani. Ana mazoea ya kutuma maofisa wake kuomba kwa kiongozi wa mahali anapokusudia kusali ili wampe nafasi ya kuongea na waamini baada ya misa.

Amekuwa anatumia fursa hiyo kuwahutubia, jambo ambao limelalamikiwa kimya kimya na waamini wanaojali liturjia – kwamba anatumia mwanya huo kupenyeza ajenda zake ambazo husambazwa pia kwenye vyombo vya habari; na ndizo hubebwa na waamini kuelekea makwao badala ya mahubiri ya siku hiyo.

Katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Korona, Magufuli amekuwa anatumia mimbari za makanisa kueneza ajenda zake akitumia maneno ya dini, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wanadai ni  siasa za kuelekea Oktoba 2020. Anazungumza lugha ya waamini kwa shabaha ya kisiasa. Kufungwa kwa makanisa kumemnyima Rais Magufuli fursa hiyo, ambayo inakera baadhi ya viongozi wa dini na waamini lakini wanasita kumweleza.

Rais amewasema pia wataalam wa maabara, na amewasema madaktari. Amewasema pia maofisa wa Hazina waliotoa hela ya kununua mashine na kupokea nyingine za msaada.

Amesakama pia “kitengo kikuu cha usalama.” Inavyoonekana, yeye ana kitengo kidogo cha watu wachache anaowaamini. Matokeo ya utendaji wa aina hii, sasa huko ndani maofisa wamegawanyika, na wanapishana bila indiketa.

Lakini kibaya zaidi ni kwamba rais ameingilia utaalamu. Siku kadhaa zilizopita, alianza kupinga takwimu za serikali yake kuhusu idadi ya wagojwa wanaopona. Alitaka ipande.

Asubuhi yake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, walitangaza kuwa waliopona walikuwa 11. Jioni yeye akawapinga akisema takwimu zao ni za uwongo, na kwamba waliopona ni 100.

Akambadili katibu mkuu wa wizara. Matokeo yake, idadi ya wanaopona ikaanza “kupaa” kuliko hata wanaougua. Ni wazi, bosi mpya alipewa maelekezo, akayatekeleza, ndiyo maana amesifiwa katika hotuba ya leo. 

Leo ametumia mapapai, mbuzi, mafenesi na kondoo kushambulia maabara ya taifa inayopima wagonjwa wa Korona.  Kitakachofuata sasa, tutarajie wataalamu kuleta vipimo vingi vilivyo “negative” ili kumfurahisha rais kama walivyofanya katika kupandisha idadi ya wanaopona. Siasa zimekalia utaalamu.

Rais Magufuli bado anapingana na hali halisi kuhusu kusambaa kwa ugonjwa na jitihada za kujihadhari zinazopaswa kuchukuliwa. Anazungumza kana kwamba huu ni ugonjwa ulioenezwa na maadui wa Tanzania, kiasi cha kutuhumu mataifa mengine kwa ubeberu dhidi ya nchi yake.

Kama hayati Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alivyowahi kutumia chuki dhidi ya wazungu kama kete ya kujitetea kuhusu poromoko la uchumi wa nchi yake, Magufuli naye anatumia kisingizio cha “ubeberu” kujitetea, kusaka huruma, kulinda udhaifu wa serikali yake au kushambulia wakosaji wake.

Ukweli ni kuwa watu wanaendelea kufa kwa mamia, na wengi wamekuwa wanazikwa usiku kwa kificho. Kama ni presha, visukari, magonjwa ya moyo na mengine walikuwa nayo siku zote; hawakufa kwa wingi kama wanavyokufa sasa.

Wapo wanaosema sasa chui ameingiza kichwa ndani ya kopo kikagomea humo. Tufanyeje?

Like
10

Leave a Comment

Your email address will not be published.