Zitto aichanachana sera ya viwanda ya Magufuli

KATIKA andiko hili, Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Maendeleo), anachambua ajenda ya serikali ya CCM kuhusu viwanda, akisema ni safari isiyo na kituo, isiyo na mwendelezo. Endelea.

Nimeona nitafakari nanyi kuhusu ndoto yetu ya kuwa na Tanzania ya Viwanda. Nimetazama maeneo 4 muhimu Sana ambayo yangeweza kutusaidia kupiga hatua kubwa kuelekea Tanzania yenye FUNGAMANISHO la Sekta za uzalishaji nchini na hivyo kuongeza uzalishaji, kutengeneza ajira nyingi na kuongeza mauzo yetu nje. Hata hivyo miaka mitatu ya utawala wa Awamu ya 5 ni miaka ya kukatisha tamaa kutokana na Serikali kukosa Kituo kwenye mipango yake ya Maendeleo ya Viwanda, kukosa mwendelezo ( sequencing) na kukosa MAARIFA ya kuendesha Uchumi wa Viwanda.

Tutafakari pamoja hapa:

1. 2016/17 ilileta Bungeni ‘mikakati ya kukabiliana na uhaba wa Sukari nchini’. Ilieleza kwa kina changamoto nzima ya bidhaa ya Sukari na miradi inayopaswa kutekelezwa ili kumaliza kabisa suala la uhaba na kupanda kwa bei ya Sukari nchini. Miradi kutoka kila kona ya nchi, ililenga takribani Hekta 300,000 za kulima Miwa. Miradi ingetekelezwa Tanzania ingeweza kuzalisha Tani 1.5 milioni za Sukari.

Miradi ingeweza kuliingizia Taifa Fedha za Kigeni, USD 500 milioni, sawa na 30% ya malengo ya Mpango wa Maendeleo kwa sekta ya Viwanda, wa kupata mapato ya Fedha za kigeni, kiasi cha USD 3 bilioni. Hapo ni bila kutazama kiwango cha Ajira zitakazozalishwa, ukuaji wa biashara kwenye sekta nyengine, Umeme nk (Multiplier effect ).

Leo mwaka 2018 hakuna Taarifa ya utekelezaji wa Mkakati huu na nakisi ya mahitaji ya sukari imekua zaidi, bei ya sukari iko juu zaidi ya 1,800/- ilikuwepo mwaka 2016 kabla ya Serikali kuweka zuio la kuagiza nje sukari bila kwanza kuwa na mpango wa kuondoa nakisi iliyopo, sasa bei ikiwa ni wastani wa 3,000/- nchi nzima.

Vibali vya uagizaji wa Sukari vinaendelea kutolewa, mgogoro wa Sukari umekua Siasa za Maagizo yasiyotekelezwa na Nchi inaendelea kuchoma Fedha za Kigeni kuagiza Sukari, ajira kwa Vijana kutotengenezwa na FUNGAMANISHO la Sekta ya Kilimo na Sekta ya Viwanda kutokuwepo. Tumekuwa na Hali mbaya zaidi kuliko mwaka 2016.

2. Mwaka 2016/17 Serikali ilikubali kuandaa mkakati wa uzalishaji wa bidhaa za Mbegu za mafuta nchini ili kuzalisha Mafuta ya Kula kwa matumizi ya ndani na kwa mauzo nje. Mikoa ya Singida, Dodoma na Manyara ikaanishwa kwa Kilimo cha Alizeti na Mkoa wa Kigoma ukaanishwa kwa Kilimo cha Michikichi. Mkoa wa Kigoma kupitia Kikao chake cha RCC ( Kamati ya Ushauri ya Mkoa- Bunge la Mkoa ) ilipitisha Mkakati wa kulima Hekta 200,000 za Michikichi ili kuzalisha Tani 800,000 za Mawese Ghafi, Tani 200,000 za Mafuta ya Mise na Viwanda 8 vya usindikaji wa Mazao ya Mawese.

Kupitia TPSF, Serikali iliidhinisha Mkakati wa Kilimo cha Alizeti na Viwanda vya kusindika Alizeti. Mwaka jana, uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ulikuwa ni tani 180,000 tu, wakati mahitaji yalikadiriwa kuwa ni tani 400,000 mpaka tani 520,000 kwa mwaka. Uwezo wa kuzalishaji ndani ukiwa ni 30% ya mahitaji, na uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ukiwa ni 70%. Pia 55% ya mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni mafuta ya mawese (palm oil) yanayoagizwa kutoka nje ya nchi ( Malaysia na Indonesia).

Inakadiriwa kuwa mafuta ya alizeti yanayozalishwa yanatosheleza mahitaji ya ndani kwa 40% tu. Serikali ilipaswa kutumia mfumo wa Kodi kuwezesha Wazalishaji wa ndani kuongeza uwezo, kutumia Dirisha la Fedha la Benki ya Maendeleo ya Afrika ( AfDB ) kupata fedha za kuwekeza kwenye Kilimo na Viwanda vya mazao ya Kilimo kuzalisha Mafuta ya Kula na kuweka vivutio kwa Wakulima na Wazalishaji wa ndani. Mipango hii ingeokoa $240m ( TZS 500bn ) tunazotumia kuagiza mawese kutoka nje, kuongeza Mapato ya Fedha za kigeni kwa kuuza nje Mafuta ya Kula kwa kiwango cha $630m ( TZS 1.3T ) na kuzalisha maelfu ya ajira kwa Vijana wanaoingia soko la Ajira kila Mwaka.

Serikali imeamua kufanya maamuzi ya kibabe na kushindwa kufungamanisha kilimo chetu na viwanda tunavyotaka kujenga, hasa vya bidhaa tunazozitumia zaidi, kama mafuta ya kula, bidhaa ambayo ina mahitaji makubwa. Leo Mwaka 2018 bei ya mafuta ya kula imepanda toka 55,000/- mpaka 70,000/- kwa ndoo ya lita 20 kutokana na masuala yanayohusu uingizwaji wake kutoka Nje ya Nchi. Tumekuwa na hali mbaya zaidi kuliko mwaka 2016.

3. Mwaka 2016/17 Serikali ilikuja Bungeni na Mkakati wa kuzalisha nguo ( C2C ) yaani kutoka Pamba mpaka Nguo. Lengo ni kuongeza thamani ya Pamba nchini kwa kuhamasisha ujenzi wa Viwanda vya Nguo ili kuuza ndani ya nchi na nje ya nchi Nguo badala ya Pamba Ghafi. Tanzania inazalisha marobota ya Pamba 700,000 kwa mwaka Lakini inaagiza Nguo kutoka nje sawasawa na marobota zaidi ya 2,000,000 kwa mwaka.

Uwezo wa Tanzania ni kuzalisha mpaka marobota 7,000,000 kwa mwaka na hivyo kukidhi mahitaji ya Nguo ya ndani na nje ya nchi kwa kuuza na kupata Fedha za Kigeni. Mwaka 2018 Serikali imeshindwa hata kuleta Bungeni Taarifa ya Mkakati huo ambao ungewezesha kuwa na Fedha nyingi za Kigeni, ajira kwa Watanzania na kuongeza tija kwa Wakulima wa Pamba na bidhaa za Pamba. Leo Mwaka 2018 Bado Tanzania inaagiza Nguo kutoka nje na Mkakati wa C2C umetupwa na waliouanzisha.

4. Serikali imekuwa na mkakati wa muda mrefu wa Viwanda vya Msingi kama vile uzalishaji wa Chuma. Mradi wa Chuma na Makaa ya Mawe wa Mchuchuma na Liganga ni moja ya Miradi Mikubwa iliyobuniwa ili kuwezesha nchi yetu kuzalisha bidhaa za Chuma. Wakati huo Serikali imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, kama vile reli, barabara, ndege, madaraja, mabomba ya gesi na mafuta nk. Fedha nyingi za ndani na za wafadhili zimetengwa Kwa ajili ya kuendeleza miradi hii.

Mradi wa reli ya kati kwa kiwango cha SGR unahitaji chuma kingi sana. Kwenye mradi huu wastani wa shilingi 17 trilioni zinahitajika kukamilisha ujenzi wake kati ya Dar es salaam na Mwanza (1200km). Ujenzi wa 1km ya Reli unahitaji chuma cha pua (steel) chenye ubora wa hali ya juu kiasi cha tani 40 mpaka 60. Tanzania tunajenga 1200km za reli kwa sasa hivi na baadaye zitaongezeka Kwa vipande vya Tabora – Kigoma, Kaliua – Mpanda – Karema, Uvinza – Musongati na miradi mingine kama Mtwara – Mbamba Bay, Ruvu – Tanga, Tanga – Musoma – Kigali nk.

Hivyo Tanzania itahitaji sio chini ya tani 500,000 za chuma cha pua (steel) katika kipindi cha miaka michache ijayo. Kwa mipango iliyopo sasa ni kwamba mataruma ya reli yataagizwa kutoka nje na kuletwa nchini na hivyo kuzalisha ajira huko kwenye nchi za nje (ambazo mataruma hayo yatazalishiwa). Fedha za miradi hii zitakwenda nje ya nchi, kama ilivyo kwenye fedha za mafuta ya kula na sukari, watanzania hawatafaidika kabisa.

Mkandarasi Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki na kampuni ya Construcao Africa SA ya Ureno ulioshinda zabuni kipande cha reli kati ya Dar – Morogoro- Makutupora ( Dodoma) ) wataagiza chuma kutoka nje. Nchi yetu ina chuma kingi sana kule Mchuchuma na Liganga, na pia tuna makaa ya mawe ya kuchenjua chuma hiki ili kupata chuma cha pua (steel). Mradi huu wa reli peke yake ungeweza kuchochea maendeleo makubwa kwenye sekta ndogo ya migodi na viwanda vya Chuma.

Tungekuwa na mipango thabiti, sisi Tanzania tungekuwa ndio wazalishaji wakubwa wa Chuma nchini na hata uzalishaji wa chuma cha kujengea reli kwenye eneo la Mashariki mwa Afrika na Maziwa Makuu. Leo Mwaka 2018 ndio kwanza Serikali inazungumzia kulipa fidia watu wa Ludewa ili Mwekezaji aanze mradi. Mpaka mradi unakwisha reli itakuwa imeshajengwa na soko kupeperuka. Sasa Hivi Tanzania inaagiza Chuma tani 200,000 kutoka nje kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendelea na kulisha viwanda vya nondo nchini.

Mifano hii 4 tu inaonyesha kuwa Serikali ya CCM ya Awamu ya 5 hutangaza mikakati yake kama kufurahisha genge Lakini haina dhamira ya kuleta Maendeleo ya Viwanda nchini kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Serikali imekuwa ikifanya ‘ hit and run ‘ kwa maana kwamba inatangaza kuwa Ina mkakati fulani Lakini hawautekelezi wala hauna mwendelezo. Matokeo yake tumekuwa Taifa la kuzungumza yale yale mwaka hadi mwaka bila kufanikiwa chochote. Hapa sijagusia kabisa namna tunapoteza Biashara ya kimataifa kwenye masoko yetu kama India, China na hata Jumuiya ya Afrika Mashariki ( EAC ) ambapo Kwa ujumla tumepoteza jumla ya $1bn ( TZS 2.2trn ) Katika kipindi cha miaka 2 iliyopita.

Leo huko Dodoma tunapitisha Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara Kwa mara ya 3 mfululizo, mwaka kesho mwezi kama huu tutajadili Bajeti ya 4 ya Wizara hiyo hiyo kwa maneno haya haya bila Taarifa ya utekelezaji wa mwaka uliopita. Kama unabisha maneno yangu tazama mijadala ya wabunge mwaka 2016 na mwaka 2017 na mwaka huu 2018 kwenye Wizara hii. Serikali inasema maneno yale yale na Wabunge kama Kasuku tunarudia maneno yale yale. Tusipobadilika nchi yetu itakuwa kichekesho.

Tunahitaji Mapinduzi

Like
16

Leave a Comment

Your email address will not be published.