Nguvu ya umma yang’oa chama tawala kilichokaa madarakani miaka 60 Malaysia

NGUVU ya umma imeshinda hila na mabavu ya watawala nchini Malaysia, na kuangusha muungano wa chama tawala, National Front, ambacho kimetawala nchi hiyo kwa miaka 60 mfululizo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1957. Kwa anguko la watawala hao, Mahathir Mohamad (92), aliyeongoza muungano wa upinzani ujulikanao kama Alliance of Hope, amekuwa waziri mkuu mpya, akiwa kiongozi mpya mzee kuliko wote katika kumbukumbu zilizopo.

Mahathir amemwangusha Waziri Mkuu Najib Razak ambaye alichafuka kwa ufisadi wa dola za Kimarekani bilioni 4.5 kutoka kwenye mfuko wa uwekezaji wa serikali ambazo alizichota kwa kushirikiana na maswahiba wake kati ya mwaka 2009 na 2014, wakaziingiza katika akaunti binafsi ya Najib. Ufisadi huu na kodi ya manyanyaso walizowekewa wananchi vilisababisha chuki na hasira ambayo licha ya ujanja ujanja, vitisho na njama za watawala, wapinzani wamefanikiwa kupata kura za kutosha.

Mahathir, ambaye anatarajiwa kuapishwa kesho na kuunda serikali, aliwahi kuongoza nchi hiyo kwa miaka 22 hadi 2003. Akiwa mstaafu, baada ya kuona mambo yameharibika, aliibuka na kujiunga na upinzani kupinga na kumwondoa madarakani swahiba wake wa zamani, Najib.

Wachambuzi wanasema ushindi wa upinzani ni kielelezo cha hasira za wananchi dhidi ya mfumo mkongwe wa kisiasa katika nchi hiyo ambao ulifanya watawala kulewa madaraka, kudharau na kunyanyasa wananchi. Serikali, baada ya kuzidiwa, ilijaribu mbinu nyingi za kuwawekea vigingi wapinzani na kudhibiti habari na taarifa, hata kwa kutunga sheria ya “habari feki” kama njia ya kuzuia mijadala huru katika jamii na kulinda serikali dhidi ya wakosoaji. Mbinu zote hizi hazikufua dafu mbele ya nguvu ya umma na hasira za wananchi.

Mbali na njama hizo, serikali ilibadili pia mipaka ya majimbo ili kugawa maeneo yenye upinzani mkubwa kama njia ya kuongeza viti vya chama tawala bungeni.

Like
1

Leave a Comment

Your email address will not be published.