KWA kawaida, mtu anapofariki dunia, wanaobaki hai hupokea msiba kwa namna tofauti kwa kutegemea jinsi marehemu alivyogusa maisha yao.
Wapo watakaoguswa zaidi na tukio la kufariki kwa mtu wa karibu kwao na kupokea msiba kwa vilio na wapo; walioumizwa – kwa njia yoyote na marehemu, hawa hawatarajiwi kulia, watafurahi na pengine kushangilia.
Kifo cha Rais John Magufuli kilichotangazwa kutokea Jumatano- Machi 17, 2021, kimegusa watu kwa njia hizo mbili. Wapo wanaolia na wapo wasiojali – wala kuumizwa kwa kuwa “walitendwa” ama kuumizwa na mfumo aliouongoza.
Watu hususan makao makuu ya mikoa, majiji miji na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa ya watu walianza kusherehekea saa chache baada ya kupata uhakika kupitia tangazo la aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu kifo hicho saa 5 usiku.
Jana wakati wa kuaga mwili wa Magufuli katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimwaga chozi, ikiwa ni ishara ya kuguswa zaidi na kifo cha kiongozi huyo wa Tanzania.
Majaliwa akiwa mbele ya jeneza lililowekwa mwili wa Magufuli, alionekana kufuta chozi mara kwa mara kwa kutumia kitambaa kidogo cheupe cha mkononi. Alikuwa ameongozana na mkewe, Mary.
Mbali na Majaliwa, idadi kubwa ya watu uwanjani hapo walionekana kuishiwa nguvu wakati wanapotoa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Magufuli. Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Skauti, kikosi cha ‘Red Cross” na wanausalama wengine walikuwa na kazi kubwa ya kusaidia wananchi waliokuwa wakilia na kuishiwa nguvu.
Baada ya ibada ya kuaga mwili iliyofanyika Kanisa Katoliki la St Peters, msafara wa magari kuelekea Uwanja wa Uhuru ulipita barabara mbalimbali ambapo wananchi alionekana wamejipanga pembezoni na katika kuonyesha mapenzi yao kwa Magufuli, baadhi yao waliingia katikati ya barabara na kutandika vitenge na kanga hizo huku wakinekana kulia.
Wakati vilio vikitawala kila barabara ambayo msafara wenye mwili wake ulipita; kuanzia eneo la Morocco, Kinondoni, Magomeni, Ilala na Chang’ombe, baadhi ya wananchi walikuwa na mabango hayo ambayo baadhi yalisomeka – “Kwaheri Jemedari wetu,” “R.I.P chuma mtetezi wa wanyonge,” “R.I.P JPM chuma cha Afrika.”
Hata hivyo, katika mitandao ya kijamii, hasa Twitter na Instagram, baadhi ya watu waliweka maandishi katika kurasa zao wakithibitika kushangilia kifo hicho cha kiongozi wa Tanzania aliyeongoza tangu mwaka 2015 hadi kifo chake.
Taarifa zilizofika kwa SAUTI KUBWA kupitia waandshi wake maeneo mbalimbali zinaeleza kuwa wapo watu walionekana maeneo ya starehe, hasa baa na klabu wakinywa vinywaji vyenye kileo na kusikika “wakifurahia kifo cha Magufuli.”
“Huyu mtu ameumiza sana watu, wapo waliopoeza nyumba zao, kuuawa, kuonewa na kufungwa kwa kuwa tu Magufuli alikuwa rais mwenye roho mbaya, acha tulewe, ametuonea sana,” alisikika kijana mmoja wa makamu akipayuka kwenye duka moja lialouza vinywaji eneo la KImara Bucha.
Yamekuwepo madai kwamba Magufuli wakati wa uongozi wake, aliamuru kuteswa na kuonea kwa baadhi ya watu, hasa wapinzani wake, wakiwamo wanasiasa, waandishi wa habari na wafanyabiashara wakubwa, ambao wengi, ili kuepuka mkono wa chuma wa mateso ya Magufuli, walikimbia nje ya nchi, uhamishoni.
Katika baadhi ya maeneo jijini Dar e Salaam, wakazi kadhaa wa maeneo ya Kimara, Mbezi kwa Musuguri baada ya kupata taarifa za kifo walikusanyika ghafla kwenye ya starehe na kufurahia hadi usiku wa manane kabla ya maofisa wa Polisi kuwavamia na kuwasambaratisha.
Ikumbukwe kuwa wakazi wa Mbezi na Kimara ni wahanga wakubwa wa utawala wa Rais Magufuli kwani siku chache baada ya kuingia madarakani- 2015, aliamuru kubomolewa kwa baadhi ya nyumba bila fidia, jambo ambalo liliwaumiza na kuwepo kwa taarifa za wengine kufariki kutokana na mshituko.
Taarifa zinaeleza kuwa”furaha” hiyo iliendelea hadi jana ambapo watu wengi waliamua kukamilisha furaha yao kujipatia kitoweo kwa kuchinja kuku na mbuzi.
Katika hatua hiyo, imegndulika kuwa soko maarufu la mbuzi la Vingunguti lililopo Ilala, Dar es Salaam jana limeshuhudia wateja wengi tofauti na mazoea.
Mmoja wa wauza mbuzi katika soko hilo, Chiteta Shaaban alisema alipata mshangao wa kuongezeka kwa mauzo ya mbuzi. Kwamba aliuza 50 tofauti na siku zingine ambapo huuza mbuzi kati ya 10-15 kwa siku, isipokuwa siku za sikukuu; Pasaka, Idd na Krismas.
“Hata sisi wauzaji wa mbuzi hapa tumeshangazwa, watu wengi wamenunua mbuzi wakati hakuna sikukuu yoyote kubwa, hata wateja wetu wa mtaani wamerudi mara mbilimbili kuchukua mbuzi jambo ambalo ni nadra sana kutokea,” alisema Chiteta.
Baadhi ya wakazi wa Dodoma wameshuhudiwa wakikusanyika katika maeneo ya starehe, na kusikika wakisema – “hakika Mungu amejibu maombi yetu.” Mmoja wa watu hao, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema, “Mungu ameonyesha namna roho mbaya isivyolipa” na kumtaja Magufuli kwamba alikuwa na “roho mbaya.”
Kutoka maeneo kadhaa ya Jiji la Mwanza, baadhi ya wafanyabiashara eneo la Mkolani walionekana wakichangishana fedha kwa ajili ya kuandaa sherehe ya kujipongeza huku wengine wakisikika walisema ” tumekuwa huru tena.”
Taarifa kutoka Mkoa wa Manyara, ambazo zimethibitishwa na Jeshi la Polisi leo, zinaeleza kuwa wakazi wanane Mji Mdogo wa Mererani, Wilaya Simanjiro wanashikiliwa na Polisi kwa madai ya kukejeli na kushangilia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli. Haijafahamika lini watafikishwa mahakamani na kwa kosa gani.
Rais Magufuli amekuwa akilaumiwa na baadhi ya watu kwa kuongoza nchi kiimla, kuzuia mikutano ya siasa na kubana uhuru wa vyombo vya habari. Pia analaumiwa kwa kugeuza matamko yake kuwa ni sheria. Kwamba hakujali kufanya kazi kwa kzingatia Katiba ya Tanzania.
Yapo madai ambayo baadaye yamethibitishwa kwamba wasaidizi wa Rais Magufuli walikuwa wakikamata na kutesa baadhi ya wananchi wenye mawazo na misimamo tofati na kiongozi huyo wa Tanzania.
Mbali na hilo, takwimu zinaonyesha kuwa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifunga shughuli zao baada ya kuvamiwa na maofisa wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA) kuwataka kulipa kiasi kikubwa cha fedha za kodi zaidi ya mitaji yao.
Taarifa zinaeleza kuwa wapo wafanyabiashara waliofungwa ama kuendelea kuwa mahabusu kutokana na visingizo vya hujumu uchumi. Hawa, kama walivyokuwa baadhi ya wanasiasa waliotofautiana naye, kamwe hawawezi kusikitishwa na kifo cha Rais Magufuli.