Wanahabari Tanzania bado tupo utumwani

Hongereni na poleni wahariri, waandishi, wasomaji na wananchi wote wa Tanzania kwa kuadhimisha siku ya uhuru wa habari katika mazingira yasiyofanana na uhuru. Na kinyume cha uhuru tunakijua. Ni utumwa.
Hata hivyo, tusife moyo. Tusiache kutafuta na kupigania uhuru wetu. Siku moja tutakuwa huru. Kazi ya maadui wa uhuru ni kuweka mipaka, na kutulazimisha tukariri na kukubaliana nao kwamba “hakuna uhuru usio na mipaka.”
Sisi hatupiganii mipaka. Tunapigania uhuru. Wao wanakesha wakiwaza jinsi ya kuweka mipaka, na aina ya mipaka ya kutuwekea. Sisi tuendelee kukaa upande wetu. Wao wasimame kwao.
Tujihadhari na kishawishi cha kusimama nao wanapokuwa wanatutaka tukubali baadhi ya mipaka. Hiyo ni kazi yao. Yetu ni kupigania uhuru, si mipaka.
Mwandishi mwenzetu, Ndimara Tegambwage, ana kauli mbiu – sijui aliitoa wapi – inasema: “Uhuru hauna mipaka; mipaka huwekwa na maadui wa uhuru.” Naona MwanahalisiOnline walikubaliana na kauli hiyo, wakaitumia. Nami nakubaliana nao.
Kwa mujibu wa utafiti wa Reporters without Borders kuhusu uhuru wa habari kimataifa, ndani ya mwaka mmoja tu, Tanzania tumeshuka nafasi 25 kutoka 93 (2018) hadi 118 (2019). Kwa miaka mitano tangu 2014, tumeshuka nafasi 49, kutoka namba 69.
Kwa kifupi, hatupo huru. Tuna kila sababu ya kuendelea kupigania uhuru wetu, maana leo Mei 3, 2019 imetukuta utumwani.
Like
4

Leave a Comment

Your email address will not be published.