INASEMEKANA kuwa moja ya vichocheo vya ukuaji wa uchumi wa bluu kwa mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwemo Taifa la Tanzania, ni uvuvi wenye kina kirefu (bahari kuu) katika Bahari ya Hindi.
Katika miaka ya hivi karibuni, miongoni mwa kampuni zilizopatiwa leseni za kufanya uvuvi huo ni za China, ambayo imewekeza kwa wingi katika sekta ya uvuvi nchini Tanzania.
Ushawishi wa China kwa Tanzania una miaka mingi, huku kukiwemo ushirikiano kati ya chama Cha Mapinduzi CCM na Chama cha Kikomunisti cha China yaani China Communist Party (CCP).
Kwa takwimu zilizopo, China ni mwekezaji mkubwa wa kigeni kuliko wote nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Tanzania Investment Center (TIC), uwekezaji wa China umefikia dola za kimarekani bilioni 9.
Miongoni mwa sekta ambazo kampuni nyingi za China zimewekeza nchini Tanzania ni Uvuvi wa bahari kuu. Kampuni kadhaa kutoka China zimemekuwa zikipata leseni ya kuendesha shughuli za uvuvi wa Jodari katika bahari kuu ya Tanzania na nchi jirani. Katika makala hii tutamulika uwekezaji wa China katika sekta ya Uvuvi nchini Tanzania na kile kinachofanyika katika bahari ya Hindi.
Rejea kubwa ya andiko hili ni ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa mwezi uliopita na shirika la mazingira la Environmental Justice Foundation (EJF) la nchini Uingereza.
Ripoti ya EJF iliyochapishwa mwezi wa Aprili, inaonesha kuwa meli za China za uvuvi wa kina kirefu hasa zile za uvuvi wa Jodari zinahusika katika Uvuvi haramu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika Ukanda wa Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi. Ukanda huu umeonesha kuwa na utajiri wa rasilimali adimu za bahari hivyo kuwa kivutio kwa meli za kigeni za kibiashara.
Eneo hili linalotajwa katika ripoti ya shirika la EJF linahusisha nchi za Tanzania, Kenya,Msumbiji, Maadagascar, Ushelisheli, Mauritius na Comoro. Ukanda huu hujulikana kama South West Indian Ocean au kwa kifupi SWIO. Tutatumia kifupi SWIO katika andiko hili.
Matokeo ya utafiti katika bahari ya Tanzania
Matokeo ya ripoti hii ni kuwa wafanyakazi wa zamani waliofanya kazi katika meli za China wapatao 35 kati ya 44 ambao ni asilimia 79 walisema walishuhudia ukataji wa mapezi ya papa katika meli za China katika Ukanda wa SWIO.
Baada ya kukata mapezi, samaki hao huachiwa tena baharini ambapo huteseka na baadaye kufa. Kwa mujibu wa matokeo haya huu ni ukiukwaji wa mikataba na makubaliano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo sheria za Tanzania.
Kwa upande mwingine wafanyakazi wa meli za China wapatao 26 kati ya 48 waliohojiwa walisema walishuhudia meli za China katika ukanda huu zikijihusisha na uvuaji au utesaji wa jamii za samaki pamoja na wanyama wa baharini. Shuhuda hizi zinaacha doa kwa mara nyingine juu ya usalama wa rasilimali za baharini nchini Tanzania licha ya China kuonekana kushiriki pamoja na Tanzania katika baadhi ya tafiti katika sekta ya Uvuvi.
Mmoja wa watu walioshuhudia anasema: “Walikuwa wamekata mapezi ya papa karibu kilo 40 katika eneo la Tanzania na wakiwa baharini waliona Polisi wa Tanzania wakielekea kwenye chombo chao. Msimamizi wao aliwaambia watupe mapezi hayo ya samaki na walifanya hivyo.”
Kifungu cha 6 cha kanuni za Uvuvi wa kina kirefu nchini Tanzania yaani Deep Seas Fisheries Management and Development Regulations 2021 inasema kuwa Chombo chochote cha Uvuvi katika eneo la EEZ hakitatakiwa (a) kujihusisha na uvuvi wa kibiashara wa papa; (b) kujihusisha na ukatajai wa mapezi ya papa……
Ukataji wa mapezi ya samaki aina ya papa pia ni kinyume cha azimio la Kamisheni ya Jodari Bahari ya Hindi yaani Indian Ocaen Tuna Commssion (IOTC). Licha ya kanuni zetu na makubaliano ya kimataifa kuwa kinyume na ukataji wa mapezi ya samaki aina ya papa, inaonekana bado mamlaka zetu hazijawa imara katika utekelezaji kanuni hizi na usimamizi wa rasilimali za bahari kwa ujumla
Meli za China kutoroka bila kukaguliwa
Ripoti ya EJF inaonesha meli za China zikitoroka katika Bahari ya Hindi bila kufanyiwa ukaguzi na mamlaka za Tanzania jambo ambalo ni kinyume na kanuni za Uvuvi wa kina kirefu nchini Tanzania yaani Deep Sea Fishing Management and Regulations 2021.
Ripoti hii inieleza: “Mwaka 2018, wakati wa Operesheni Jodari, ambayo ilikuwa ya pamoja kati ya serikali ya Tanzania na Sea Shepherd, vyombo 20, ambapo 13 vilitoka katika kampuni ya Shandong Zhonglu vilikwepa ukaguzi katika maji ya Tanzania. Sheria ya inavitaka vyombo vyenye leseni ya kuvua katika eneo la EEZ lililopo Tanzania kukaguliwa kabla ya kuondoka eneo hilo ili kuhakikisha kama vilifuata masharti yaliyopo katika leseni hizo”
Kitendo cha meli za China kuondoka bila kufanyiwa ukaguzi zinaibua maswali juu ya uwezo wa mamalaka zetu katika ulinzi wa rasilimali za bahari pamoja na uthibiti wa Uvuvi haramu.
Meli 20 zinazotajwa katika ripoti ya EJF, zinatajwa pia katika ripoti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyotolewa bungeni mwaka 2020 na Luhaga Mpina. Meli hizi zinamilikiwa na kampuni tatu kutoka China ambazo ni Shadong Zhonglu Haiyan Ocean Fisheries Company Ltd, Zhongyu Global Seafood Corp, na Zhejiang Ocean Family, Co. Ltd.
“Matokeo yake, kila chombo kilipigwa faini ya bilioni moja za Kitanzania (dola 386,500) na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya Tanzania. Hata hivyo, mpaka sasa haijulikani kama Shandong Zhonglu ililipa faini hiyo. Kulingana na mtandao wa Shandong Zhonglu, mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa kwanza wa ujio wake mpya katika maji ya Tanzania baada ya miaka 4. Licha ya ukweli kuwa vyombo vyote vya Shandong Zhonglu vinavyofanya shughuli zake katika maji ya Tanzania vina historia ya uvuvi haramu na ukiukwaji wa haki za binadamu, viliweza kurejea katika uvuvi nchini Tanzania mwaka 2022, vikiwezeshwa na majadiliano ya MARA katika serikali ya Tanzania.” Inaeleza ripoti ya EJF.
Katika kile kinachonesha utitiri wa meli za China katika eneo la Bahari Kuu ya Tanzania, mwaka 2020, kampuni ya China Overseas Fisheries Association ilipewa leseni za uvuvi 30. Hapa wasiwasi mkubwa siyo kuhusu ongezeko la uwekezaji, la hasha.
Wasiwasi ni kuhusu ufuatiliaji na utekelezwaji wa matakwa ya sheria na kanuni za Uvuvi kwa meli zinazopewa leseni katika eneo la bahari yetu. Ni wazi kuwa ni kusudi la kila mtanzania kuona rasilimali hizi zikinufaisha kizazi cha sasa na cha baadaye kwa kuwa na usimamizi mzuri.
Katika kinachoibua wasiwasi ni kitendo cha Wizara kuruhusu baadhi ya meli za Uvuvi wa Jodari kuondoka na samaki wasioruhusiwa (bycatch) bila kufanyiwa ukaguzi. Novemba 2023 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdalah Ulega alipokea tani 50 za samaki wasioruhusiwa kuchukuliwa na meli za uvuvi wa Jodari kutoka meli ya Pacific Star inayomilikiwa na kampuni ya Albacore ya nchini Hispania.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega Meli ya Pacific Star iliyopewa leseni ya uvuvi wa Jodari iliondoka Tanzania na baadaye kuamua kurudisha samaki wasiolengwa.
Kitendo hiki ni kiyume cha kanuni zinazotakiwa kusimamiwa na wizara ambazo zinataka ukaguzi kufanyika kabla ya meli hizo kuondoka. Kwa mujibu wa Kanuni za Uvuvi wa Bahari Kuu ya 10(1)(a) na (10)(1)(c) ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2016, meli za kigeni zinatakiwa kuhakikiwa mavuno (catch verification) na kushushwa samaki wasiolengwa yaani bycatch.
Licha ya kanuni hizi kuwa wazi, Waziri Ulega aliita vyombo vya habari ili kushuhudia samaki waliorudishwa na Albacore. Maswali yanayoibuka ni kwanini kanuni za uvuvi zinakiukwa?
Je, serikali ya Tanzania ina uhakika gani kuwa kiwango cha samaki wasiolengwa yaani bycatch waliorudishwa na Albacore ndiyo kiwango sahihi? Je, siyo hatari kwa rasilimali za bahari kuvunwa bila usimamizi unaofuata sheria zetu ili kulinda rasilimali zetu?
Wakati haya yanajiri watanzania wanatakiwa kuelewa kuwa mwaka 2020, serikali ya Tanzania ilikabidhi leseni 15 za uvuvi wa bahari kuu kwa kampuni hii ya Albacore. Kwahiyo ieweleweke wazi kuwa kama kuna ukiukaji wa kanuni kwa chombo kimoja kinachomilikiwa na Albacore, huenda hali ni hivyohivyo kwa vyombo vingine vya meli zake.
Uvunaji wa rasilimali za bahari uliopita kiwango
Katika ripoti ya EJF yameorodheshwa masuala kadhaa yanayoandama uvuvi katika ukanda wa SWIO ikiwemo suala la kuvuna rasilimali za bahari kupita kiwango. Ripoti inaeleza
“Mwaka 2020, jodari wa manjano waliovuliwa katika Bahari ta Hindi walivuka kiwango, mwaka 2018 na 2019, uvuvi wa jodari weusi katika Bahari ya Hindi pia ulivuka kiwango kilichoidhinishwa na sheria za uvunaji wa samaki hao…”
Uvunaji wa rasilimali za majini katika ukanda huu ikiwemo eneo la Bahari Kuu ya Tanzania unahitaji kuangaliwa upya na kuwa wazi kwa Wananchi.
China ambayo ndiyo taifa linalomiliki meli kubwa za uvuvi duniani inaweza kuhatarisha uendelevu wa rasilimali hizi kama mamlaka katika mataifa yetu hayatafungua macho na kusogelea kwa karibu uvuvi huu. Ni muhimu kuelewa meli hizi zinavua nini, wakati gani, wapi na kwa kufuata taratibu zipi
Katika ripoti iliyochapishwa na EJF, shirika la chakula duniani FAO lilishaonya kuhusu uvuvi wa samaki wasiokomaa katika eneo hili. “Idadi ya samaki wanaotakiwa katika eneo hili imeonesha dalili ya kuvuka kiwango cha uvuvi kilichowekwa, ambapo mwaka 2019 tathmini ya FAO ilikadiria kuwa 37.5% ya idadi ya samaki waliopo katika eneo la SWIO walivuliwa wakiwa hawajafikia kiwango cha kukomaa”, Ilieleza ripoti ya EJF.
Kitisho cha kiwango cha juu cha uvunaji wa rasilimali unaikabili nchi mbalimbali duniani kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu hivyo mahitaji kuongezeka. Namna pekee ya kukabiliana na kitisho hiki ni kuwa na njia mbadala za uzalishaji endelevu wa rasilimali, usimamizi mzuri na kuongeza ulinzi katika rasimali adimu. Tanzania haiwezi kukwepa jukumu la kusimamia ipasavyo rasilimali zake ili kuleta manufaa ya kiuchumi ya sasa na ya baadaye.
Misaada na Uwekezaji wa China katika sekta ya Uvuvi
China inaonekana kuwa na ushawishi katika sekta ya Uvuvi nchini Tanzania licha ya meli zake kuwa na historia ya kujihusisha na Uvuvi haramu na kutoroka bila ukaguzi. Miaka ya hivi karibuni taifa la china limetoa misaada inayolenga sekta ya Uvuvi kwa Tanzania huku kukiwa na ushirikiano katika kufanya tafiti mablimbali.
Kwa mfano Taasisi ya Tanzania Fisheries Research Institute yaani TAFIRI ilianza ushirikiano wa kufanya tafiti na taasisi ya Nanjing Institute of Geography and Limnology (NIGLAS) kutoka China tangu mwaka 2008. Mwaka 2023, NIGLAS iliwakilisha serikali ya China katika kutoa msaada ya thamani ya dola za kimarekani laki 2 kwa TAFIRI msaada uliopokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe.
Mwaka 2021, China iliisaidia sekta ya Uvuvi nchini Tanzania vifaa vya Uchakataji wa Samaki vyenye thamani ya milioni 350 za kitanzania. Vifaa hivi viliwasilishwa na balozi wa China hapa nchini Wang Ken na kupokelewa na Waziri wa Elimu nchini Tanzania kwa muda huo, Profesa Joyce Ndalichako.
Mwaka jana, Shirika la Uwakala wa meli Tanzania yaani TASAC ilikuwa mwenyeji wa Jacob Chan kutoka China aliwakilisha China Classification Society (CCS) ambayo ilitaka kuruhusiwa ili kufanya kazi ya Uwakala hapa nchini. Ikumbukwe kuwa TASAC ndiyo wenye mamlaka ya kuvikagua vyombo vyote vya maji na kutoa leseni kwa vile vilivyokidhi matakwa ya kisheria. Je, CCS walelenga nini hasa katika uwakala wao?
Serikali ya Tanzania ambayo imekuwa katika ushirikiano na China hasa katika miradi mingine ya kiuchumi, imekuwa ikiuita uwekezaji wa China kama wenye faida kwa pande zote mbili. Lakini ripoti za hivi karibuni zinatia mashaka lengo hasa la uwekezaji wa China katika nchi za Afrika. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaona China kama taifa linalochungulia rasilimali zilizolala katika bara la Afrika na kuichukua kwa ajili ya manufaa yake.
Nje ya sekta ya Uvuvi, China inawekeza katika ujenzi wa bandari mbalimbali nchini Tanzania. Kwanza ni uwekezaji wake katika bandari ya Dar es salaam na Kilwa. Pili, ni uwekezaji ambao ulisimama kwa muda katika bandari ya Bagamoyo. Uwekezaji wa China unaonesha ushawishi wake kwa serikali ya Tanzania na jinsi ambavyo huenda inakuwa ngumu kwa mamlaka za Tanzania kuthibiti meli za China katika eneo lake la bahari ya Hindi.
Kwingineko, kampuni za China zinaendelea kushinda zabuni za ujenzi wa barabara na miundombinu mbalimbali katika nchi za Ukanda wa SWIO hasa Tanzania na Msumbiji. Ujenzi wa barabara, njia za reli, madaraja na baadhi ya majengo ya Umma kunaibua maswali zaidi iwapo nchi hizi zinaweza kusimama kidete mbele ya China na kueleza kinagaubaga makosa ya kampuni kadhaa za Uvuvi za China zinazovunja sheria za nchi husika na kukiuka kanuni za Uvuvi katika bahari ya Hindi.
Msimamo wa serikali ya China baada ya ripoti ya EJF
Siku moja baada ya ripoti ya EJF kutolewa serikali ya China ilitoa msimamo wake tarehe 12 mwezi wa nne kupitia Msemaji wa Wizara ya mambo ya kigeni Mao Ning ikipinga vikali matokeo ya ripoti hiyo.
“Sisi tunafuata msingi wa uvumilivu sifuri katika masuala ya ukiukwaji wa sheria na kanuni na kuhakikisha kuwa wafanyakazi (wa meli) wanapokea malimbikizo yao kama sheria inavyotaka. Tunapinga tuhuma za uongo ambazo hazina ukweli wowote,” alisema Mao Ning katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Licha ya serikali ya China kupinga matokeo ya ripoti hii, EJF ilifanya mahojiano zaidi ya 318 na wafanyakazi wa meli za China katika ukanda wa SWIO ambao nje ya kushuhudia Uharamia wa meli hizo walifanikiwa kupiga picha na kurekodi baadhi ya matukio kwa kutumia simu zao. Tofauti na ripoti hii, mara kadhaa meli za China katika ukanda huu zimekuwa zikikamatwa na serikali za nchi husika na kutuhumiwa kukiuka sheria na kanuni za uvuvi ikiwemo leseni zao.
Kwa mujibu wa ripoti ya EJF, kwa sasa, kati ya meli 95 zinazoruhusiwa kufanya kazi katika eneo la SWIO kwa lengo la kuvua jodari, meli 45 (47.3%) zinaunganishwa na kesi za uvuvi haramu na/au unyanyasaji wa haki za binadamu (kesi 62, makosa 125), haswa kwa makosa ya kukata mapezi ya papa, unyanyasaji wa haki za binadamu, na kukwepa ukaguzi.
Ni wakati muafaka wa serikali ya Tanzania kuangalia upya usimamizi wa rasilimali zake na kuchukua hatua kabla hakujatokea madhara ya uvunaji wa rasilimali usiokuwa na usimamizi katika eneo la Bahari kuu ya Tanzania.