IBARA ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ndiyo inazungumzia uwepo wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na majukumu yake. Moja ya majukumu ya CAG ni kuhakikisha kwamba matumizi ya fedha zozote zinazokusudiwa kutolewa kutoka mfuko mkuu wa hazina ya serikali yameidhinishwa, na kwamba fedha hizo hizo zitatolewa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 136 ya katiba. Iwapo atatosheka kwamba masharti hayo yatatekelezwa ipasavyo, basi ataidhinisha fedha hizo zitolewe.
Ibara 143 2(b) inamtaka CAG, “kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo matumizi yake yameidhinishwa yatokane na fedha zilizomo katika mfuko mkuu wa hazina ya serikali au fedha ambazo matumizi yake yameidhinishwa na sheria iliyotungwa na Bunge; na ambazo zimetumika, zimetumiwa kwa ajili ya shughuli zilizohusika na matumizi ya fedha hizo, na kwamba matumizi hayo yamefanywa kwa kufuata idhini iliyotolewa kuhusu matumizi hayo.”
Ibara ya 143 2(c) inamtaka CAG, “angalau mara moja kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa taarifa juu ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya Jamhuri ya Muungano, hesabu zinazosimamiwa na watumishi wote wa serikali ya Jamhuri ya Muungano na hesabu za mahakama zote za Jamhuri ya Muungano na hesabu zinazosimamiwa na katibu wa Bunge.”
Nimelazimika kuanza na nukuu hizi za katiba kuhusu mamlaka ya kikatiba aliyonayo CAG ili kuleta uelewa wa pamoja katika mjadala ya nafasi ya ofisi hii muhimu kutokana na sintofahamu ya kihistoria iliyojitokeza sasa kuhusu “kupotea” kwa fedha za umma zaidi ya trilioni 1.5, kwa mujibu wa ripoti ya CAG za serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Ukurasa wa 34 katika ripoti ya CAG kwa ripoti kuku ya Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 unasomeka hivi: “Kati ya shilingi bilioni 25,307.48 zilizokusanywa, shilingi bilioni 23,792.30 zilitolewa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengine, matumizi ya maendeleo na fedha kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na amana za Serikali pamoja na riba.”
CAG anatuambia kuwa serikali ya Magufuli, inayojinasibu siku zote kuwa ni serikali ya wanyonge, ilikusanya bilioni 25,307.48 kutoka vyanzo vyote vya mapato, misaada, mikopo na kutumia bilioni 23,792.30 katika matumizi yake kwa bajeti ya mwaka 2016/2017.
Maana yake, na kwa hesabu rahisi, ni kuwa katika pesa zote zilizokusanywa na kutimiwa (25,307.48-23,792.30 = 1,515.18) zaidi ya shilingi za Kitanzania trilioni 1.5 haikutumika na haileweki sehemu ilipo mpaka ukaguzi unamalizika na ripoti kutolewa kwa umma.
Ukaguzi wa CAG hufanyika kwa matumizi halisi na si makisio, kama baadhi ya watumishi wa serikali na makada wa CCM wanavyojaribu kupotosha umma. Ukaguzi hutegemea ushahidi sahihi, wa uhakika, ushahidi wa kutosha na kwa wakati.
Kwa mfano bajeti ya mwaka 2017/2018 unaoisha tarehe 30/6/2018 mwaka huu, CAG anapoanza ukaguzi wake mwezi wa saba mwaka 2018, anakagua hesabu za bajeti iliyotumika kwa mwaka wa 2017/2018. Maana yake ni kwamba anafanya ukaguzi wa matumizi halisi ambayo yameshafanyika na si makisio au matajio.
Ukaguzi wa hesabu hupitia hatua mbalimbali na mpaka unafikia hatua ya kundika hoja ya ukaguzi kuwa sehemu ya ripoti ya ukaguzi na kutolewa kwa ajili umma, maana yake ni wakaguliwa kushindwa kuwa na majibu sahihi ya kuridhisha na kwa wakati kwa wakaguzi zinazotosha kufunga hoja iliyoibuliwa wakati wa ukaguzi.
Wakaguzi wa ofisi ya CAG, kabla ya kuandika hoja za ukaguzi, hutoa muda wa kutosha kwa mkaguliwa, yaani serikali, kutoa vielelezo, maelezo na ushahidi wa kutosha wakati wa ukaguzi. Wakaguliwa wakishindwa kutoa majibu wakati ukaguzi unaendelea, ofisi ya CAG hutoa nafasi ya pili ya kujibu hoja za ukaguzi kwa kutoa ripoti yenye hoja za ukaguzi kwa uongozi wa taasisi iliyokaguliwa na kupewa siku 21 ya kujibu hoja zilizoibuliwa wakati wa ukaguzi.
Baada ya uongozi wa taasisi iliyokaguliwa (Serikali) kutoa majibu kulingana na hoja zilizoibuliwa na wakaguzi kwenye ripoti ya uongozi, Wakaguzi kutoka ofisi ya taifa ya ukaguzi wanaenda kuhakiki majibu kulingana na ushahidi uliowasilishwa na wakaguliwa na kama kuna ushahidi wa kutosha na kuridhisha, hoja ya ukaguzi hufungwa kwa kutolewa na baada ya hapo wakaguzi hufanya kikao cha kuaga wakaguliwa (Exit meeting) kwa kuwajulisha wakaguliwa hoja za ukaguzi ambazo hazikujibiwa mpaka wakati huo, na ambazo zitukuwa sehemu ya ripoti ya mwisho ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Kulingana na hatua zote hizo za ukaguzi, serikali ya Magufuli ilikuwa na muda wa kutosha wa kutoa majibu ya zilipo kiasi cha trilioni 1.5 ambazo hazionekani kulingana na ripoti ya CAG. Ni wazi kuwa kuna ufisadi wa kihistoria katika pesa za umma nchini Tanzania, na mpaka sasa serikali ya Magufuli imeshindwa kutoa majibu. Badala yake, imegeuka kutisha walioibua hoja na wanahoji zilipo pesa za umma.
Ili kuondoa wingu nzito na harufu ya ufisadi ya zaidi ya trilioni 1.5 lililotanda kwa sasa, serikali kupitia Bunge iunde tume huru ya kiuchunguzi ili ijulikane zilikopelekwa hizi pesa za Watanzania. Kama serikali inajinasabu kuwa pesa hazikuibwa na wahawahusiki na ufisadi huu, iruhusu uchunguzi huru na wa haki.
Ni muda muafaka na wakati sahihi kwa Bunge la Tanzania kuchukua jukumu lake la kikatiba la kusimamia na kushauri serikali kwa kuunda kamati teule ya Bunge kufanya kazi ya uwakilishi kwa Watanzania kwa kuchunguza upotevu wa zaidi ya trilioni 1.5 kupitia ripoti ya CAG. Matokeo ya utafiti huu yanaweza kuwa mwisho wa ufisadi huu wa kihistoria kwa nchi yetu – nchi inayotegemea misaada ya wahisani huku Watanzania wakiendelea kuishi katika umaskini uliotopea.
Wakati tukiendelea kudai uchunguzi huru kupitia kamati teule ya Bunge letu la Tanzania, tukutane wiki ijayo kwenye ukurasa huu kujadili upotevu wa kutisha wa kodi na mapato ya Watanzania kupitia maneo mengine, na serikali kushidwa kuchukua hatua ndani ya ripoti ya CAG.