Tume ya Taifa ya Uchaguzi yalaumiwa kwa ushabiki, ubaguzi

TUME ta Taifa ya Uchaguzi imejiingiza katika kashfa, na umma wa Watanzania sasa unaiona kuwa inashabikia na kusaidia mgombea mmoja wa urais, badala kuwa mwamuzi na msimamzi wa haki kwa wagombea wote.

Hatua hii inathibitishwa na kauli na vitendo vya tume yenyewe kwa kutaka kuadhibu chama na mgombea mmoja wa urais, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukiuka taratibu na ratiba ya mikutano ya kampeni.

Habari zisizothibitishwa zinasema kuwa tayari tume hiyo imeandaa adhabu dhidi kali dhidi ya mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Inadai kuwa amekiuka kanuni kwa kufanya baadhi ya mikutano katika maeneo ambayo hakupangiwa, jambo ambalo pia linafanywa zaidi na mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli.

Vile vile, tume inamtuhumu Lissu kwa “kusema uwongo” dhidi ya Magufuli, lakini kabla haijampatia fursa ya kujieleza kwa mujibu wa kanuni na maadili ya uchaguzi, tayari tume ilitangazia vyombo vya habari – kupitia Mkurugenzi wa Tume, Dk Charles Mahera, kuwa Lissu ameitwa kukutana na kamati ya maadili leo tarehe 29 Septemba mjini Dodoma.

Lissu naye amejibu kupitia vyombo vya habari kuwa iwapo tume inataka kumwita kwenye kikao lazima ifuate utaratibu wa kikanuni, si kumtumia matamko kwenye vyombo vya habari.

Wakati Lissu akisumbuliwa, mgombea wa CCM, Magufuli, hajaandikiwa barua wala kuitwa. Chama chake, kupitia kwa Katibu Mwenezi, Humphrey Polepole, wiki iliyopita kiliituhumu tume na kuitaka ichukue hatua dhidi ya mgombea wa upinzani ambaye, kwa mujibu wa CCM, anamchafua Magufuli majukwaani kwa kutaja kashfa zake.

Mara kadhaa, Magufuli amekuwa akihutubia mikutano nje ya maeneo aliyopangiwa. Katika tukio moja siku chache zilizopita, Magufuli alihutubia mkutano usio wake katika eneo la Kazuramimba, mkoani Kigoma, mahali ambapo Lissu alipaswa kuhutubia.

Katika mikutano yake, Magufuli amekuwa anadhalilisha wapinzani na akinamama kwa maneno ambayo ya chuki na dhihaka. Chama chake hakijaandikiwa barua ya kuonywa na yeye hajaitwa kujieleza kwa kufanya mikutano kila anakopita, nje ya ratiba ya kampeni na kusema yanayopandikiza chuki na ubaguzi katika jamii.

Lissu, ameeleza umma – kwenye mikutano yake ya kampeni, kuwa hadi jana alikuwa hajapokea barua ya wito kutoka kwa tume, zaidi ya kuambiwa na watu wasiohusika na tume kwamba anaitajika kufika Dodoma kujileleza.

Mhadhiri mstaafu wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azavery Lwaitama, anasema baadhi ya kauli za tume zinaonekana kupendelea CCM, hatua ambayo ni mbaya na inaweza kusababisha vurugu.

“Haihitaji kuwa msomi wala mtafiti kubaini kwamba tume inaipendelea CCM. Ni kama inapokea maagizo kutoka kwa mgombea wa chama tawala, kama inaelekezwa kufanya hili, kuacha lile, ili tu chama hicho na mgombea wake wapate upenyo wa kushinda nafasi ya urais na wagombea wake wengine wa ubunge na udiwani. Hii si sawa hata kidogo. Waache wananchi wachague wanaowapenda kuwaongoza,” amesema Dk. Lwairama.

Mtaaalamu wa fani siasa uchumi, Dk. Lenny Kasoga, ameilaumu tume kwa kuonyesha dalili za kupendelea CCM katika uchaguzi huu. Ameitaka iache uwanja sawa wa “mapambano ya kisiasa.”

Anasema CCM na serikali yake imeleta maendeleo makubwa kwa Watanzania yanayoonekana, hivyo ushindi wake siyo tena wa “kushikia manati” au kubebwa na tume.

“Tume ndiyo inaweza kuwa chanzo cha vurugu, iache watu waamue, na kwa kuwa CCM imefanya mengi, wala haina wasiwasi na ushindi, lakini huenda tume imeamua tu kujipendekeza kwa Rais Magufuli ili waubwa wake waonekane wanafanya kazi kumbeba,” ameongeza Dk. Kasoga aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Vyanzo vyetu vinaeleza kuwa Tume ye Taifa ya Uchaguzi inashinikizwa na Magufuli mwenyewe. Katika vikao kadhaa vya ndani, Magufuli amekuwa analaumuna viongozi wenzake wa CCM kuwa wamemwachia kampeni imwelemee, na kwamba wanapaswa wajibu mapigo ya Lissu. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, mapigo ya kisiasa anayorushiwa na Lissu, ni makali na hayajibiki kirahisi kwa kuwa ni kasoro zitokanazo na ama utendaji au amri zake Magufuli mwenyewe.

Hata hivyo, yeye anadai kwamba hayo ni matusi dhidi yake, na kuwa yanapaswa yajibiwe na wana CCM. Katika kutafuta nafuu ya kampeni, Magufuli ameamua kutumia vyombo vya dola, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi dhidi ya Lissu.

Tayari kuna taarifa kuwa tume imeshapanga kumwadhibu Lissu kwa kumtaka asitishe kampeni zake kwa siku 14 kuanzia Oktoba Mosi.

Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa hizi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Dk. Mahera, alijibu harakaharaka; “sisi ni tume huru, hatufanyi kazi kwa maelekezo ya yeyote na hatuna mgombea tunayemuogopa, wote wako sawa.”

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nayo imeiandikia barua Chadema ikiitaka kujieleza kwanini isichukuliwe hatua kwa mgombea wake wa urais kueleza mara wa mara kwamba hawatakubali kushindwa na kwamba watahakikisha kura zao zinalindwa.

Ofisi hiyo imeeleza kwamba kauli hizo zinaashiria kuchochea uvunjifu wa amani na kwamba ni kosa kisheria. Tayari Chadema wamejibu barua hiyo iliyokuwa na ukomo wa kujibiwa siku la leo mchana.

Like