KIFAFA ni ugonjwa sugu unaohusisha mtu kupata mshituko katika ubongo na kusababisha degedege au kuanguka. Hali hii hutofautiana kulingana na ukubwa wa mshituko.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kifafa ni moja ya hali kongwe zaidi duniani inayotambulika, ikiwa na rekodi zilizoandikwa tangu 4000 Kabla ya Kristo.
Vipindi vya mshtuko kwa mtu mwenye kifafa ni matokeo ya kuzalishwa kwa umeme kupita kiasi katika kundi la seli za ubongo.
Tafiti za kisayansi zinaeleza kuwa sehemu mbalimbali za ubongo zinaweza kuwa chanzo cha utoaji umeme huo wa mwili usiokuwa wa kawaida.
Mshituko hutofautiana kutoka muda mfupi zaidi au mshtuko wa misuli hadi degedege kali ya muda mrefu. Mshtuko unaweza kutofautiana mzunguko kutoka chini ya mshituko mmoja kwa mwaka hadi mara kadhaa kwa siku.
Hata hivyo, mtu kupata degedege mara moja haimaanishi kuwa ana kifafa, kwani asilimia 10 ya watu ulimwenguni wamewahi kupata degedege mara moja katika maisha yao.
Kama ilivyo kwa mataifa mengine, Tanzania pia ni miongoni mwa nchi zenye watu wanaougua ugonjwa huo wa kifafa.
Baadhi ya wajumbe wa Chama cha wazazi wa watoto wanaoishi na kifafa (UWAKITA) pamoja na wadau wengine walikutana jijini Dar es Salaam kuweka mkakati wa pamoja juu ya ugonjwa huo.
Katika mjadala huo mambo kadhaa yalijitokeza, lakini unyanyapaa ulielezwa kuwa ni hatari na kikwazo kwenye suala zima la matibabu ya watu wanaoishi na ukifafa.
Daktari bingwa Afya na magonjwa ya akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili -Upanga Dar es Salaa, Nurueri Kitomary anasema zaidi ya watu milioni 50 Duniani wanaishi na hali ya ukifafa ambapo asilimia 80 wanaishi kwenye nchi zenye hali duni.
Miongoni mwake nhi hizo zinatoka barani Afrika na Tanzania ikiwemo.
Anasema watu milioni 10 wanaishi Afrika wanaishi na hali ya ukifafa na takwimu hizo zikiwa ni zamani kidogo hivyo kuna uwezekano idadi hiyo ikawa zaidi ya hapo.
Dkt Kitomari anasema mwaka 2022, WHO iligundua kuwa watu 45,000 nchini Tanzania wanaishi na hali ya kifafa. Na kwamba idadi hiyo nikwa wale tu wenye usajiri rasmi wa matibabu hospitalini; lakini kuna kundi kubwa nje ya hao wanaoendelea kufichwa majumbani na wengine kutibiwa kwa waganga wa kienyeji na maeneo mengine kama kuombewa makanisani na kadhalika.
“Unaweza kuona kuna idadi kubwa ya hawa ambao hatuwajui. Yaani ni asilimia 3.7 tu ndio wapo kwenye matibabu, hivyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili watu zaidi ya asilimia 96 waingie kwenye mfumo.
“Ni vizuri jamii ifahamu kuwa magonjwa haya yanaongoza kwa kuleta ulemavu, kwa sababu wengi wanafungiwa ndani wanashindwa kujishughulisha na shughuli za kijamii na kuzalisha kipato kwa sababu ya unyanyapaa, dhana potofu na mazingira ambayo wanapitia kila siku,” anasema Dkt Kitomari na kuongeza:
“Unyanyapaa ni moja ya vizuizi vikubwa vya jitihada zote za kumtibu mtu anayeishi na hali ya kifafa. Mwingine anajinyanyapaa mwenyewe kwa sababu ya malezi na makuzi kwenye jamii yake inayomuona mgonjwa wa kifafa kuwa ni mtu mwenye mapepo, bahati mbaya, mkosi, na majina mengine mabaya.”
Naye Mratibu wa Afya ya akili Manispaa ya Kinondoni, Dkt Mwendo Peter anasema mapambano dhidi ya maradhi hayo yanakabiliwa na changamoto kubwa ya unyanyapaa kwa watu wanaougua ugonjwa huo, jambo ambalo anasema linahitaji kampeni kubwa ya utoaji elimu kwa jamii.
Anasema unyanyapaa huo mkubwa umechangiwa na masuala mtambuka zikiwamo mila, desturi na tamaduni tangu zamani ambapo familia zilizokuwa na mtu anayeishi na kifafa zilikuwa zinatengwa.
“Hili jambo lina historia toka kwa mababu zetu kwamba mtu hawezi kuoa kwenye familia ambayo ina watu au mtu anayeugua kifafa; vitu hivyo vimeendelea hadi sasa na hivyo kupoteza watu na wataalam wenye uwezo mzuri kutumikia jamii kama watu wengine,” anasema na kuongeza:
“Kutokana na unyanyapaa huo, baadhi ya wagonjwa wanaamua kujinyanyapaa wenyewe kwa kutokwenda hospitali na ndugu zao; mwingine anakuja kituo cha afya kwa kujificha ili watu wasimuone; mtu wa aina hii hawezi kusikiliza sawa sawa ushauri na maelekezo ya daktari au mshauri wa ustawi wa jamii kuhusiana na maradhi yake.”
Kutokana na hali hiyo; mratibu huyo anasema kuwa mgonjwa wa namna hiyo, hata akipewa dawa, haiwezi kumsaidia kwani anaweza kufika nyumbani asizitumie kwa usahihi na hivyo kushindwa kutatua tatizo.
Anashauri watumishi wanaowahudumia wagonjwa wanaoishi na kifafa wapatiwe elimu ya ziada ili kuendana na mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia inayokwenda kwa kasi sana duniani.
Anasema asilimia kubwa ya watumishi katika vituo vya afya na hospitali wanatumia mbinu na elimu waliyoisoma darasani tu ambayo kwa sasa haitoshi, hivyo wanahitaji kuongezewa ujuzi wa mara kwa mara ili waweze kuendana na wakati wa sasa.
“Utaalam wetu umepitwa na wakati, kile tulichojifunza darasani ni kile kile, hatuna cha ziada. Hivyo litakuwa jambo la msingi watalaam wetu wakaongezewa ujuzi kupitia mafunzo mbalimbali, ”anasisitiza.
Kuhusu upatikanaji wa dawa kwa watu wanaoishi na kifafa, Dkt Peter anasema ni changamoto nyingine inayopaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee.
Anatolea mfano jiji la Dar es Salaam kwamba dawa kwa ajili ya watu wenye kifafa zipo, lakini upatikanaji wake ni changamoto kwa sababu zinalipiwa.
“Kama mnavyojua asilimia kubwa ya watu wenye changamoto ya ugonjwa huo uwezo wao kiuchumi ni mdogo, hivyo hulazimika kutumia dawa zilizopo ambazo wakati mwingine; daktari unatamani umwandikie mgonjwa dawa ambayo ingemsaidia zaidi, lakini wengi hawana uwezo wa kumudu gharama hizo,” anasema.
Mmoja wa wazazi mwenye mtoto anayeishi na changamoto ya kifafa, Jovina Josephati Hamis asema unyanyapaa unarudisha nyuma juhudi za matibabu ya ugonjwa huo nchini.
Anataja hospitali (jina tunalo) alikompeleka mtoto wake, wakampima na kugundua tatizo kwa mara ya kwanza, lakini kwa mujibu wake, daktari wake alitaka kumsababishia hatari zaidi yeye mzazi.
“Daktari alikuja moja kwa moja ananiambia mtoto wangu ana ugonjwa wa kifafa. Nilimwomba anielezee vizuri, lakini hakujali, aliniacha kwenye benchi la hosptali. Nilipoteza mwelekeo na kusahau mlango wa kurudi nilipotoka. Alipaswa kuniandaa kisaikolojia, kunielimisha ili nipokee hayo majibu kwa utulivu. Je tunao madaktari wangapi wa aina hiyo? Je wameandaliwaje kuelimisha wateja wao amba oni wazazi au wagonjwa wenyewe? Anahoji.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya Afya ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa Amana Dar es Salaam, Dkt Wanda Rwiza, anasema ili kupunguza unyanyapaa kwa watu wenye magonjwa ya kifafa, ni bora kutenganisha magonjwa hayo na yale ya akili.
Anasema mtu anayeishi na kifafa akienda hospitali akatibiwa eneo moja na wenye changamoto ya afya ya akili anapoteza matumaini.
“Jambo hili linawatisha, hivyo nashauri ugonjwa wa kifafa usichanganywe na wenye changamoto ya afya ya akili. Hata watumishi wa afya kwa sababu ya kutokuwa na elimu ya kutosha wakiona mgonjwa wa kifafa wanasema ni ‘mapepo’’ anasema Dkt Rwiza.