SEPA ZAKO 2.0.1.8

UTENZI HUU WA KUAGA MWAKA NA KUKARIBISHA MWINGINE UMEANDIKWA NA Dk. Christopher Cyrilo

Umetuchosha kwakweli, mwaka wa mauzauza. 

Bora tuseme kwa heri, bila ya kujiuliza.

Mabaya tumenakili, mazuri tumejifunza.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mwanzoni mwa Januari, Tuliufungua Mwaka.

Tukazisoma habari, Kipanya Wamemteka.

Eti alizua shari, vikatuni kuandika.

Nenda zako nenda zako, mbili ziro moja nane.

Januari haikwisha, taarifa zikatoka.

LISSU amesafirishwa, Belgiji amefika.

Wengi tukafurahishwa, Kamanda kaimarika

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mara ukaja mpango, Tanesko kuliangusha.

Tukalitetea jengo, hadi wakahairisha.

Leo napita ubungo, jengo wameling’arisha.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Habari za Nabi Tito, nazo zilitamba sana.

Yule Afande Muloto, alimkamia Mwana.

Akamuwashia moto, jamaa akajikana.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Februari ikafika, Misiba tukaipata.

Kingunge akatutoka, Tambwe Hiza akafuata.

Daima twawakumbuka, sisi sote tunapita.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Aquilina na Aleni, walikufa Februari.

Kaskazi na kusini, vilio vilikithiri.

Polisi mahayawani, waliuwaua dhahiri.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Laana za Sheikh mkuu, kwa dada Mange Kimambi.

Aliahidi makuu, Mwaka huu rambirambi.

Watu kumjia juu, kufichua zake dhambi.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mwezi Machi harakati. Nondo katekwa Iringa.

Mbowe na yake kamati, Mahakamani kutinga.

Hazijafika tamati, kesi za kuungaunga.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane

Nyaraka za makanisa, zilimchefua Anko.

Akatengeneza visa, na kuzua chokochoko.

Wenzake wakamuasa, kuepuka machafuko.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Aprili kapiga hodi, Wadau kuandamana.

Wakaweka na ahadi, Dikteta kumkana.

Ilipofika miadi, jeshi likaandamana.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Trilioni pointi tano, Magufuli kachafuka.

Kaitisha mkutano, akaishia kufoka.

Hakuna maelewano, majibu hayakutoka.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mwezi mei nawo shida, nusuru elimu yetu. Ni vitabu vya kiada, kukosewa vingi vitu.

Tukaweka jitihada, kupaza sauti zetu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Sirro kapiga mkwara, Tukamwambia tulia.

Ndalichako akafura, tukazidi vumilia.

Zilipoisha hasira, ndipo wakafatilia.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane

Ya Juni hayasomeki, changamoto kwelikweli.

Kupima rula samaki, kabla kula ugali.

Ilizua taharuki, watu hawakukubali.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Sugu kuachiwa huru, na songi akaachia.

Tarime zikaja duru, Kuvamiwa Zakaria.

Kataka kujinusuru, risasi kawamiminia.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

JF kifungoni, Melo katuharifia.

Kuuliza kulikoni, mitandao na sheria.

Tukapamisi jamvini, baadaye tukarejea.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Julai kitimutimu, Mwigulu kadi nyekundu.

Akaachia hatamu, ziara ikawa gundu.

Hakutaka kulaumu, kisiasa ni mtundu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Kangi kapewa nafasi, zikaanza sarakasi.

Kapiga ‘biti’ polisi, waiheshimu ofisi.  

Mbele ya kadamnasi, akamtimua bosi.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mbwa bandari hayupo, Kangi Lugola kawaka.

Akatafutwe alipo, la! hapatakalika.

Hakuijua michapo, tulibakia kucheka.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Julai ikaishia, na teuzi wilayani.

Jokate akapatia, aliwekeza zamani.  

Mitandao kujazia, picha zake za sirini.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Agosti naikumbuka, kwa samani za Makonda.

Bandari hazikuvuka, Mipango alijipinda.

Habari wakafunika, mashuleni hazikwenda.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Ubalozi Marekani, waliandika waraka.

Hawakuwa na imani, siasa zenye mashaka.

Serikali bila soni, ikajitia kuwaka.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Ajali ya Kigwangala, Mungu wake kamuona.

Pamoja na zetu sala, amejaliwa kupona.

Kikokotoo kambwela, alikuwa hajapona.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Ya septemba mazito, kule ziwa Victoria.

Roho zao na watoto, kwa Mola zimerejea.

Walizidisha uzito, Mizigo na abiria.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Kivuko kile kizuri, tatizo waendeshaji.

Lazima kutafakari, pamwe na uwajibikaji.

Serikali sisubiri, wengine wafe na maji.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Tafakuri Oktoba, Mengi sana yalijiri.

Wajinga walimkaba, wakamteka tajiri.

Maombi kwa Mungu Baba, MO karudi vizuri.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Picha za CCTV, zikatuumiza mbavu.

Walijiona wajuvi, kutufanya wapumbavu.

Hawajui ‘cheza ‘muvi’, tukawachana makavu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Amba Ruth naye vipi?, Hatumsikii tena.

Alituonesha chupi, hadharani tukaona.

Sasa hivi yupo wapi, Oktoba alifana.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Benki kuu ya dunia, ikatufundisha kitu.

Viongozi Tanzania, kumbe hawana utu.

Msaada kuzuia, wasome mabinti zetu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Novemba nayo shughuli, ilikuwa nginjanginja.

Waandishi mashughuli, walivamiwa kininja.

Walikutwa kwa hoteli, wakazidiwa ujanja.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Kongamano la siasa, la pale chuo kikuu.

Lengo kusifia hasa, kujikomba kwa mkuu.

Wengine Maprofesa, siwezi kuwanukuu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Makonda naye kabipu, mashoga awatishia.

Kumbe kichwani mtupu, moto anajiwashia.

Nusura aliwe supu, kanisani kaishia.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Ubalozi wa Ulaya, ukatoa matamko.

Serikali hii mbaya, ubinadamu hauko.

Iache mambo mabaya, kuepuka machafuko.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Membe akawaamsha, walolala usingizi.

Urais kakumbusha, aliyepo hauwezi.

Wakaanza kumtisha, kwa maneno ya ki’ndezi’.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Desemba nayo ni ‘kwere’, rangi za bendera tabu.

Watu na viherehere, Njano waita dhahabu.

Tukajua ni ‘biere’, vichwani zawapa tabu.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Magufuli kamaliza, na kikokotoo chake.

Ndiye aliyeagiza, wakaandaa wenzake.

Leo amekikataza, akombe masifa yake.

Nenda zako nenda zako, Mbili Ziro Moja Nane.

Mbili Ziro Moja Tisa, karibia kwa uzuri.

Mwenzako ametutesa, tunamuaga kwa shari.

Ukituletea visa, sisi tutakukabiri.

Mbili Ziro Moja Tisa, Karibia kwa Uzuri.

Usituletee zako, akili zimeshadata.

Baki nayo mambo yako, pesa tutazitafuta.

Ukileta chokochoko, cha moto utakipata.

Hapa kazi sera yako! SISI NI KAZI NA BATA.

Like
3

Leave a Comment

Your email address will not be published.