MAKAMU wa Rais Samia Suluhu ameongeza neno kuhusu uvumi unaoendelea juu ya hali ya afya ya Rais John Magufuli, akidokeza kuwa kuumwa umwa ni jambo la kawaida.
Samia ametoa kauli hiyo akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Tanga. Akihutubia wananchi katika eneo la Mkata, makamu wa rais alisema: “Ni kawaida binadamu kukaguliwa; mara mafua, mara homa, mara chochote kile… tupo salama… huu ni wakati muhimu kwa Watanzania kushikamana…”
Mara baada ya kauli ya makamu wa rais, msomi mmoja ameiambia SAUTI KUBWA: “Kauli yake imebeba ujumbe mzito. Inathibitisha kuwa rais anaumwa, na anaumwa (mafua ya) Corona. Anaposema tupo salama anamaanisha kuwa nchi ipo salama mikononi mwake (Samia), na anamaanisha tushikamane kujenga umoja wa nchi katika mtikisiko huu kwenye jukumu kubwa alilonalo.”
Kauli hii ya Samia imekuja wakati kuna uvumi kuwa Rais John Magufuli amelazwa tangu tarehe 3 Machi na anatibiwa maradhi ya Corona ambayo yameingilia changamoto za moyo wake. Rais Magufuli hajaonekana hadharani kwa wiki tatu sasa, na matukio kadhaa ambayo alipaswa kushiriki yameahirishwa.
Upo pia uvumi, kwa siku tatu mfululizo sasa, kwamba ameshafariki dunia, na kwamba kinachofanywa na dola ni kusogeza muda ili kuweka mambo sawa.
Vyanzo vingine vinasema hata ziara hii ya Samia ni mbinu ya kiintelijensia ya kutuliza umma kisaikolojia kuhusu hali ya afya ya rais. Kwa kumbukumbu tulizonazo, hii ni ziara ya kwanza ya Samia kutangazwa mubashara tangu 2015. Mara zote, ziara zinazotangazwa mubashara na TBc ni za Rais Magufuli.
Kauli hii ya Samia inapingana na ile ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyotoa wiki iliyopita akisema, “rais yupo salama salimini anachapa kazi.” Majaliwa, ambaye alikuwa ameanza ziara ya mikoa ya Kusini, alilazimika kuahirisha ziara hiyo na kurejea Dar es Salaam kwa dharura.
Taarifa zinasema mawaziri na viongozi wengi wa serikali wamefichwa suala hili ambalo linadhibitiwa na kikosi maalumu cha Idara ya Usalama wa Taifa.
Chanzo kimoja kimesema serikali itakuwa tayari kutoa taarifa kwa umma katikati au mwishoni mwa wiki hii. Zipo taarifa pia kuwa kinachochelewesha serikali kutoa kauli ni kwa kuwa wenye uhakika na kinachoendelea ni watu wachache sana, na kuna mtifuano wa nani atapata nini baada ya Magufuli.
Wakati hayo yakiendelea, wapika propaganda wa serikali wamekuwa wakizusha taarifa feki kuhusu hali ya Magufuli, huku wengine wakisambaza video na picha zinazoonyesha akiwa kwenye matukio ya zamani, na wengine wakidai yupo kwenye mfungo wa Kwaresima.
Chanzo kimoja kimeiambia SAUTI KUBWA: “Sahau. Hajiwezi, na hataamka tena, labda uwe muujiza kama wa Lazaro.”
Kauli ya Samia ndiyo ya kwanza kutoka kwa viongozi wakuu inayodokeza kuwa rais si mzima wa afya tofauti na ilivyodaiwa awali na waziri mkuu.