RAIS Samia Suluhu aliwahi kusema kuwa yeye na hayati John Magufuli ni kitu kimoja. Wapo walioyabeba maneno hayo kama yalivyo. Wapo walioyatafakari na kuyachambua.
Ukitazama baadhi ya mambo mazuri aliyotenda Samia ndani ya siku 100 za kwanza, waweza kusema yeye na Magufuli si kitu kimoja.
Ukimhukumu kwa yanayotokea sasa, ambayo yanafanana na ya Magufuli au yanaendeleza kile alichokuwa anafanya mtangulizi wake, jumuisho la haraka litakuwa “yeye na Magufuli ni kitu kimoja”
Wapo pia ambao sasa wanaamini kuwa Samia ni mbaya kuliko Magufuli. Wanatoa sababu zao.
Hebu tumfuatilie huyu mmoja ambaye amesema hivi:
Madai kuwa Samia na Magufuli ni kitu kimoja hayana ukweli wowote. Alicho nacho na Magufuli ni ukweli kuwa alishuhudia, na wakati mwingine alilazimika kushiriki, uovu wa Magufuli. Kwa haiba na utendaji kazi hawa ni watu wawili tofauti.
Eneo moja kuu linalowatofautisha ni uwezo wa kufanya uamuzi. Magufuli alifanya uamuzi wa mambo mengi mabaya kwa sababu ya hulka yake. Alifanya mambo mazuri machache kwa bahati mbaya – kwa sababu si hulka ya mtu mwovu kutenda mambo mema kwa dhamiri njema.
Yote alihakikisha anawatumia na kuwasimamia wateule wake kuyatekeleza hata kama walikuwa hawataki.
Kwa upande wake Samia, hana “maamuzi.” Mara nyingi anafika kwenye “briefings” za wateule wake akiwa hana kitu huku akitegemea wamsaidie kujua na kuamua.
Wateule wanamuongoza kufikia uamuzi au kumlisha uamuzi na kwenda kuutekeleza. Yeye huishia kuwaambia “haya ndugu zanguni nendeni mtekeleze hayo mlosema.”
Mmoja wa wateule wa Magufuli aliyekataa mashinikizo ya rais (JPM) na kuomba ajiuzulu lakini akakataliwa na badala yake akatumbuliwa, amesema mahali fulani: “JPM alijua namna nzuri ya kutumia vyombo na wateule wake.”
Akitoa mfano alisema, baada ya Uchaguzi wa 2015 aliamua kumteua Mbunge fulani (jina kapuni kwa sasa) lakini watu wa usalama wakaleta ripoti kuwa si raia bali ni Mnyarwanda. Walimpa ripoti iliyoandikwa na ushahidi wote. Walileta hata picha za kijijini kwao Rwanda.
JPM kwa siri alimuita Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na kumwagiza afanye awezavyo kuhakikisha Mbunge huyo anapata uraia na afanye hivyo bila wasaidizi wake kujua. Kamishna Jenerali alijifungia akafanya kazi ile na mbunge akatangazwa kuwa waziri. Wana usalama waliona aibu na wakawa na hasira.
JPM alifanya hivyo hivyo kwa Bashiru Ally Kakurwa na kumpa uraia pale wana usalama walipoleta pingamizi la uteuzi wake.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara naye alipewa uraia wa haraka baada ya kuwekewa mizengwe kuwa ni Mkenya.
JPM alijua namna ya kutumia vyombo na wateule wake kutekeleza hata mambo magumu na maovu kama mauaji ya Ben Saanane ambaye aliuawa katika “mahali patakatifu” na akatumbukizwa majini asiweze kuonekana tena. Uovu huu ulifanyika kwa siri kubwa kwa sababu JPM alikuwa anaelekeza mwenyewe.
Suala la kesi ya Freeman Mbowe lilianzia kwa JPM. Wanausalama walimpelekea JPM mapendekezo ya kumbambikia Mbowe kesi ya ugaidi.
JPM aliwagombeza na kuwadharau kuwa hawajafikiri sawasawa. Alifikia kuwaambia bora wapendekeze kumpiga risasi kama Lissu kuliko kumbambikizia kesi ya ugaidi, akidai kuwa majaji wengi na mahakimu wanamchukia yeye (JPM). Wana usalama walirudisha ripoti kabatini.
Mtoa habari wangu anasema, “cha ajabu ripoti ile ile iliyofukuzwa na JPM kuhusu Mbowe, alipoletewa mama akashangilia na kuagiza itekelezwe; vyombo vimetekeleza na kuongeza mengine zaidi ili kumkomoa mama.”
Afisa mmoja Mtanzania aliye katika ubalozi wa Marekani nchini Tanzania amesema kuwa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rais Samia aliagiza vyombo vimuandalie ripoti ya uchunguzi wa kesi ya Mbowe kwa hofu kuwa mgeni yule angeuliza.
Vyombo vilimletea Rais Samia orodha ya kesi alizowahi kushtakiwa Mbowe. Rais Samia alilalamika na kudai aletewe ripoti yenye maelezo lakini mpaka anakutana na mgeni, vyombo vilishindwa kumpatia.
Ili kuhakikisha rais hapokei ushauri wowote kutoka kwa watu wasiotakiwa na vyombo, amebadilishiwa namba ya simu ili asifikike. Hali kadhalika makamu wa rais na waziri mkuu wamebadilishiwa namba za simu ili wasitumiwe kumbadilisha rais mawazo.
Kimsingi, rais yuko chini ya udhibiti mkali ili kuhakikisha anawasikiliza wanausalama hao tu.
Rais amedanganywa mno kuhusu suala la Mbowe hadi akasema uwongo wazi kwenye mahojiano na BBC – uwongo unaodhalilisha polisi na mamlaka ya rais mwenyewe.
Na hii inatokana na minyukano ya kisiasa ndani ya chama chake, makundi ya wanaomkubali na wasiomkubali, mashabiki wa JPM ambao walikerwa mno na hatua alizochukua ndani ya siku 100 za kwanza, wanaotaka urais na waliodhamiria awe rais wa muhula mmoja, na wale wenye ukakasi na rais mwanamke wanaotaka ashindwe mapema kwa kurudia makosa yale yale yaliyomfanya JPM “anuke.”
Ndio hawa wanaompatia Samia ushauri wa “kijinsia” wakimtaka achukue hatua kali ili kuonyesha anaweza, na kwamba wanaomkosoa wanafanya hivyo kwa kuwa yeye “ni mwanamke.” Naye bila kujua dhamira zao anajimaliza mwenyewe.
Na hapo ndipo swali linapozidi kukolea – ni kitu kimoja au vitu viwili?
Uchambuzi unaendelea. TAZAMA VIDEO YAKE HAPA.