SASA ni dhahiri kuwa zama za rais John Pombe Magufuli zimezikwa rasmi na Tanzania imeingia katika “mwanzo mpya” chini ya rais Samia Suluhu Hassan, Sauti Kubwa linaweza kuthibitisha.
Ikiwa ni siku ya mwisho ya maombolezo ya siku 21 ya Hayati Magufuli, Rais Samia ameendelea kuifumua kwa kasi serikali aliyoachiwa na kuipa mwelekeo na maagizo yaliyo kinyume na sera na mtindo wa utendaji wa serikali ya Magufuli.
Kwanza, ameonesha kutoridhishwa kwake na hatua zisizo za kisayansi za kupambana na janga la COVID-19 zilizoanzishwa na mtangulizi wake, wakati huo yeye akiwa makamu wake.
Akizungumza leo Ikulu Dar es Salaam katika hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, Rais Samia ametangaza nia ya kuunda timu maalum ya wataalam itakayokuwa na jukumu utafiti, kushauri na kuiongoza serikali katika mapambano dhidi ya Covid-19 kwa kutumia njia za kisayansi zaidi.
Akizungumza kama vile ni mtu mpya kabisa na ambaye hajawahi kuhudumu katika utawala wa Magufuli, rais Samia amesema haiwezekani nchi nyingine zinatangaza takwimu za maambukizi ya Corona halafu Tanzania hakuna kitu.
“Nchi nyingine tunaona takwimu za Corona lakini hapa kwetu ni dash dash tu. …hatuwezi kujitenga na ulimwengu,” alisema rais Samia.
Hatua na kauli hizo, zinaashiria wazi kuwa sasa Tanzania itaanza kufuata kikamilifu miongozo ya Shirika la Afya duniani (WHO) dhidi ya Covid-19, tofauti na ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wake.
Magufuli alihimiza zaidi wananchi kujikinga kwa mvuke wa mitishamba (kupiga nyungu), huku mara kadhaa akitilia shaka matumizi ya njia za kisayansi hususan barakoa na chanjo.
Wakati rais Samia akielekea kuruhusu takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona ziwe zikitangazwa wazi, Magufuli alidai kupitia watafiti wake kuwa vipimo vya Corona havikuwa vikitoa majibu sahihi. Baada ya hapo utaratibu wa kutangaza takwimu za hali ya maambukizi na vifo haukuendelea tena. Ulizuiwa tangu mwezi Aprili mwaka jana.
Pili, katika hatua nyingine mpya, rais Samia ameagiza kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na utawala wa Magufuli kwa madai mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria na maadili ya habari.
Uamuzi huo umepokewa kwa shangwe kubwa nchi nzima. Na umeweka alama kubwa ya utofauti uliopo baina yake na mtangulizi wake.
Magufuli alilalamikiwa sana kwa kuminya sana uhuru wa vyombo vya habari, haki za binadamu, haki za kiraia na kisiasa na kubana demokrasia kwa ujumla.
Tatu, rais Samia pia amechukua mwelekeo mpya kabisa wa namna ya kutekeleza sera za kodi, akinukuliwa kuitaka wizara ya fedha na mamlaka ya mapato nchini (TRA) watumie akili na njia rafiki zaidi katika kudai kodi kuliko kutumia nguvu. Rais ameonesha kuyafahamu madhila yaliyowafika wafanyabiashara wengi waliofungiwa au waliolazimika kufunga biashara zao kwasababu ya sera mbaya za makusanyo ya kodi zilizotekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Nataka kodi ndiyo lakini kodi ya dhuluma hapana”, amesisitiza rais Samia. Kwa kauli hii ametangaza kupinga waziwazi vitendo vya kubambikia wafanyabiashara kodi kubwa na kuwafungulia kesi za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi vilivyoshamiri sana wakati wa utawala wa Magufuli.
Nne, sambamba na hilo rais Samia amechukua mwelekeo tofauti pia katika masuala yahusuyo mahusiano ya kimataifa, diplomasia na uwekezaji.
Wakati Magufuli aliwaita watu wa magharibi majizi na mabeberu yanayopora utajiri wetu, huku akikwepa hata kuhudhuria karibu mikutano yote muhimu ya kimataifa iliyokutanisha wakuu wa nchi isipokuwa tu ile mikutano ya wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika (SADCC) na Jumuiya ya Afrika Masharika (EAC).
Rais Samia yeye amechukua hatua kuu mbili tofauti. Mosi, amemuondoa Profesa Palamaganda Kabudi, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kikanda na kumuhamishia wizara ya katiba na sheria na kisha kumteua mwanadiplomasia mzoefu Liberata Mulamula kuwa mbunge na waziri wa mambo ya nje. Kisha, leo ametoa maelekezo ya kutaka wizara na watendaji wote wanaohusika wavutie wawekezaji kwa kuondoa vikwazo vyote vilivyopo. Hii ndiyo kusema kuwa rais Samia anachukua mwelekeo mpya wa kuhimiza matumizi ya diplomasia ya uchumi zaidi tofauti na mtangulizi wake.
Tano, rais Samia ameanza kuchukua hatua dhidi ya rushwa na ufisadi katika namna inayoheshimu na kuzingatia tahadhari za utawala wa sheria zaidi tofauti na mtangulizi wake.
Wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hivi karibuni, rais Samia alichukua uamuzi wa kumsimamisha kazi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Huduma za Bandari Tanzania, Bwana Kakoko, ili kupisha uchunguzi zaidi wa wahusika wa ufisadi wa Shilingi bilioni 3 uliofanyika katika mamlaka hiyo.
Wachambuzi wa mambo wanasema angekuwepo Magufuli kwanza bwana Kakoko asingechukuliwa hatua kwasababu alikuwa ni swahiba wa karibu wa rais. Ilishazoeleka kwa rais kuwashughulikia mafisadi wengine na kuwalinda wale alio na urafiki, undugu au maslahi nao.
Lakini kwa upande mwingine, hata kama Kakoko angekuwa wa kuchukuliwa hatua na Magufuli basi asingemsimamisha kupisha uchunguzi kama sheria, kanuni na taratibu za kikazi zinavyotaka bali yeye angemtumbua papo hapo bila kujali taratibu za kisheria zinatakaje.
Uamuzi wa rais Samia umeonesha jinsi anavyoweza kuwa kiongozi mtulivu, msikivu na makini katika kufuata sheria na taratibu, sifa ambazo hazikuonekana kabisa wa Magufuli.
Sita, kwa ujumla, mabadiliko mbalimbali ya viongozi na watendaji aliyoyafanya katika serikali yake, yakiwemo ya kumuondoa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Bashiru Ally Kakurwa na kumteua kuwa mbunge, yanaonesha jinsi rais Samia alivyodhamiria kuendesha serikali ya namna yake kinyume na ilivyodhaniwa kuwa pengine angeendeleza mambo yote ya Magufuli kwa mtindo wa kimagufulimagufuli.