TUREJEE HISTORIA
ADOLF Hitler alipotawala Ujerumani kwa ukatili, mambo yake yalienda vizuri katika miaka ya mwanzo.
Alipojaribiwa na akaagiza viongozi wa dini waweke kiapo cha ziada cha kumtii yeye kila wanapoingizwa kazini, mambo yalianza kuporomoka.
Alipoishiwa woga akawakamata na kuwatesa wachungaji wa Kanisa lililokataa kula kiapo cha ziada. Mmoja wao aliitwa Dietrich Bonhoeffer. Mambo ya Hitler yaliporomoka mpaka akajiua kabla ya kukamatwa. Damu ya viongozi wa dini ina nuksi.
Idd Amin alipindua serikali ya Uganda 1971. Aliua na kutesa watu wengi bila kutikiswa. Mwaka 1977 akamuua Askofu Janan Luwum na kulazimisha kumzika haraka.
Tangu hapo alianza kuporomoka kwa kasi ya ajabu. Mwaka 1978 akaichokoza Tanzania, mwaka 1979 akaondolewa madarakani. Damu ya viongozi wa dini ni nuksi.
John Magufuli aliongoza serikali ya awamu ya tano Tanzania kwa mkono wa chuma. Mwaka 2017 akamnyanganya uraia na pasipoti Askofu Severin Niwemugizi. Mwaka 2018 akampokonya uraia Padre Raymond Saba aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), lakini akampa uraia Samweli Kiboye Mwenyekiti wa CCM Mkoa Mara.
Mwaka 2018 TEC na KKKT wakatoa nyaraka za kichungaji zilizokemea unyanyaswaji wa raia. Magufuli akachukia.
Akampigia simu Askofu Tarcisius Ngalelikumtwa aliyekuwa Rais wa TEC; akamtisha na kumtukana. Akafunga baadhi ya vyuo vikuu vya makanisa na kutumia “watu wasiojulikana” kutisha baadhi ya maaskofu.
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akamwonya mara tatu aache kugombana na viongozi wa dini. Magufuli hakusikia.
Akamkamata Shehe Issa Ponda, akatuma watu wakampiga risasi mkononi. Akamkamata Askofu Emmaus Mwamakula akanyea debe siku kadhaa. Akawanunua mashehe, maaskofu na wachungaji ili wamwabudu yeye kuliko Mungu.
Akashauriwa na watu wengi awaachie mashehe wa uamsho akagoma na kuwatukana kwenye hotuba mbalimbali.
Wiki mbili kabla ya kifo chake, mwishoni mwa mwezi Februari 2021, Magufuli alipanda madhabauni Katika Kanisa la Mt. Petro, Dar es Sakaam, akamkebehi Askofu Mkuu Yuda Tadei Ruwa’ichi , akawabeza mapadre na masista. Akathubutu kumchonganisha paroko na askofu na kuchochea uasi ndani ya Kanisa. Akajitwalia utukufu katika madhabahu ya Mungu.
Ndiyo ilikuwa siku yake ya mwisho kuonekana kanisani, kwani Jumapili ya Machi 7 ambayo akikuwa aende kusali katika Kanisa la KKKT Azania Front, ilimkuta akiwa na hali mbaya kiafya. Hakuinuka tena.
Baadhi ya waliokuwa karibu naye wanasema ndani ya wiki tatu “alibadilika kuwa kichaa mpaka mauti yalipomkuta.” Mafuta ya wapakwa mafuta yana nuksi, ukiyadharau.
Sasa mambo yanaanza kuwa magumu kwa Rais Samia Suluhu. Hazina haina kitu, mafuta yamepanda, miamala imepanda, mafuta ya kula yamepanda, Ajira hakuna na rushwa inapaa.
Askari wake wameanza kukamata watu hovyo, na jana walimkamata Askofu Emmaus Mwamakula huko Mwanza.
Askofu Mwamakula anateseka kwa “kosa la kumtetea Samia” ili awe rais wa kukumbukwa.
Katika mazingira haya, Samia ataponaje nuksi ya damu na mateso ya maaskofu? Ataponaje nuksi ya mafuta ya maaskofu anayoikanyaga kwa kutumia simu kuagiza polisi wamkamate askofu?
Je, Dk Philip Mpango, makamu wa rais, yupo tayari?