JE, katika mazingira ya uandishi wa habari; yale ya ukusanyaji taarifa kwa ajili ya kuandaa habari au andiko la kuwasilisha katika chombo cha mawasiliano; bado kuna sababu au haja kwa Serikali kuendelea kutoa kitambulisho kwa mwandishi wa habari?
Kati ya mwaka 1985 na 1995 nilisimamia na kushiriki kuchagiza, pamoja na mambo mengine – ndani ya Tanzania na katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika – hoja muhimu ya Uhuru wa Mwandishi wa Habari, Uhuru wa Vyombo vya Habari na Uhuru wa kutoa maoni.
Kipengele mojawapo na muhimu katika eneo hili kilihusu kitambulisho au leseni kwa mwandishi wa habari – Press Card.
Tuliulizana. Tulijibizana. Tulisemezana. Tulikubaliana. Tulitofautiana. Tulilaza hoja. Tukairejea asubuhi: Je, kuna sababu kwa serikali kutoa leseni au kitambulisho kwa kila mwandishi wa habari?
Wakati huo, nikiongoza semina, warsha, mikutano ya waandishi wa habari, wamiliki wa vyombo vya habari na utetezi wa waandishi walio katika mazingira magumu; washiriki wapatao asilimia 75, kwa kila kusanyiko (45 hadi 60), walikuwa wanakubaliana: Hakuna haja wala sababu, kwa serikali kutoa kitambulisho kwa kila mwandishi wa habari nchini.
Wachangiaji wengi walitoa hoja kwamba, kama ni lazima serikali kutoa Press Card, basi impe yule mwandishi wa habari ambaye inamwajiri, ili kumtambulisha kokote kule anakotumwa, anakokuwa au anakokutwa.
Turudi kwenye shina. Mwandishi wa habari asiyemwajiriwa wa Serikali, anapewa Press Card ya Serikali kwa msingi gani na shabaha ipi?
Bali serikali yoyote yaweza kuwa na sababu zozote za kutoa kitambulisho kwa kila mwandishi wa habari. Kuna sababu kuu tatu ambazo tulikubaliana kuwa ni chanzo cha serikali kusajili waandishi wa habari. Hizi hapa:
Sababu ya kwanza kwa serikali kutoa Press Card ni udhibiti. Kuna ushahidi wa tawala zilizowapa leseni waandishi wa habari, na baadaye kuwanyang`anya leseni hizo pale walipoandika kile ambacho watawala waliita “habari mbaya.”
Watawala wana Kamusi zao. Ndani ya Kamusi hizo, maneno “habari mbaya” huwa yana maana ya taarifa au habari ambazo zinafichua ubadhilifu, wizi, uzembe, ufisadi ndani ya serikali na washirika wake; au zinazoanika ushiriki wa serikali au watendaji wake, katika vitendo vya ukatili unayanyasaji, ubaguzi, utovu wa uwajibikaji, ukiukaji Katiba za nchi zao na kutokuwa na utawala wa sheria.
Kwahiyo, katika nchi hizo, kama wewe ni mwandishi wa habari mchunguzi, mfukuaji, mchokonozi, mfichuaji na mwanikaji wa taarifa zinazodaiwa na watawala kuwa zinawafedhehesha na kuwaumbua; au “zinaiacha uchi” serikali; basi hutapata leseni ya kazi.
Gundua basi, kwamba kusajiliwa na kupewa leseni – katika mazingira kama hayo; ni kukuandaa kunyang`anywa leseni hata kabla tabasamu lako halijanyauka.
Vinginevyo, utende watakavyo: uimbe nyimbo zao za wasifu; uwafichie siri zao na wakati wote ujitokeze haraka kuwatetea kwa “mshiko” wa faragha au fadhila.
Sababu ya tatu ni mapato. Serikali huuza Press Card kwa waandishi wa habari. Kwa mfano kama nchi ina vyombo 500 vinavyojihusisha na uzalishaji na usambazaji “maudhui,” ingizo hilo, kwa kiwango chochote kile, siyo haba hasa ikichukuliwa wanahitajika waandishi angalao wanne (4) kwa chombo makini kuanza kazi. Aidha, kuna vyombo vyenye waandishi wa habari zaidi ya 20 – kila kimoja kutegemea ukubwa wa shughuli zake.
Si hilo tu. Idadi pekee ya waandishi wa habari ni fedha. Inatosha kuandikia mradi. Serikali yaweza kuitumia kuomba mikopo (au hata misaada) ya kifedha kutoka kokote kule kwa maelezo kuwa inakwenda “kuelimisha” waandishi wa habari. Fedha hizi zaweza pia kutumika kuzalisha miradi mingine. Mavuno.
Sababu hizi kuu tatu na nyingine za uzito tofauti, zilitosha kuwa utangulizi tu kwenye hoja ya msingi iliyoelekeza katika kuchukua msimamo kuwa; kama kitambulisho chochote kinahitajika kwa mwandishi wa habari – kikiitwa jina lolote lile – basi kitolewe na Mwajiri wa mwandishi wa habari; na siyo Serikali.
Ni hivi: Kama Serikali inataka kutoa vitambulisho kwa waandishi wa habari; ifanye hivyo kwa wale tu ambao inawaajiri. Kwanini? Kwasababu, mwajiri ndiye mwenye wajibu wa kutambulisha mwajiriwa wake – kokote anakokwenda, anakotumwa na anakokutwa.
Ni mwajiri anayejua sababu za kuajiri mfanyakazi – mwandishi huyu na siyo yule – na anayejua thamani yake. Mwajiri ndiye anasimamia, anastahili na kuwajibika kulinda mwajiriwa wakati wote wa ajira yake.
Katika hili, Serikali ishauriwe, kwa nia njema, kujiondoa katika mradi hatari wa uchuuzi, usajili na utoaji leseni kwa waandishi wa habari ambao haiwaajiri.
Kila mwajiri wa mwandishi wa habari atambulishe, kwa njia ya Kitambulisho Maalumu, yule tu ambaye anamwajiri. Kila mwenye nia njema anakubaliana na hili; na linawezekana.
Serikali iking`ang`ania kutoa Press Card kwa waandishi wote; kwa sababu au hata bila sababu zozote; itakuwa inalenga kuendelea kutishia uhuru wa waandishi wa habari na kuweka wazi kwamba inawamiliki au inataka kuwamiliki.
Kumiliki waandishi wa habari, kwa shuruti ya sheria, kwa ujanjaujanja au kwa waandishi wenyewe “kujidogodesha” na kuhiari kupakatwa na watawala; kunaweza kufinyaza uhuru na upeo wao na hatimaye kunyakua uhuru wa wananchi wa kupata taarifa na habari. Tusemezane.