Polisi Dar wamsaka mume anayetaka kuua mkewe

JESHI la Polisi Tanzania linamsaka Ramadhan Baraka kwa tuhuma za kutishia maisha ya aliyekuwa mkewe, Anne Maleya.

Mkewe huyo yupo ughaibuni, na kwa sababu kadhaa, mamlaka za nchi aliko, Ufini, zimemwamuru arejee Tanzania.

Lakini, kwa mujibu wa vyanzo vya kipolisi mkoani Dar es Salaam, Baraka alipopata taarifa za mpango wa kurejea nchini kwa mkewe wa zamani, alijiapiza kuondoa uhai wake mara atakapowasili.

Alisema hataki kamwe kumwona Anne akiwa hai, na kwa sababu hiyo atahakikisha anaondoa uhai wake kwa njia yoyote ile.

Haijajulikana mara moja kwanini Baraka anataka kumuua Anne, lakini vyanzo vya kipolisi Jijini Dar es Salaam vinasema Anne alimtoroka mumewe sababu ya ukatili wa kijinsia aliokuwa akimfanyia kwa miaka kadhaa.

Raia wema waliomsikia mwanaume huyo akipanga njama hizo na kutoa vitisho kwa maneno, walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.

SAUTI KUBWA haikuweza kufahamu iwapo Anne amesharejea Tanzania au la, lakini iliweza kupata taarifa hiyo ya kipolisi iliyosajiliwa kwa namba rejea OST/RB/2347/2020 mbele ya Koplo Yohane katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay.

Matukio ya wanaume kuua wake zao au wapenzi wao yamekuwa yakiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Polisi wamesema kwa sababu hiyo, kitisho hiki si cha kupuuza kwani kinaweza kusababisha kifo cha mwanamke mwingine asiye na hatia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, ukatili wa kijinsia umekuwa moja ya changamoto za kifamilia ambazo lazima zitazamwe kwa jicho kali la sheria ili kuukomesha.

Katika mwaka 2020, tayari kuna matukio kama haya ambayo yanaacha doa katika jamii kwa wapenzi wa kiume kuua wapenzi wao wa kike kama vile wanachinja kuku.

Januari mwaka huu 2020, Mkazi wa Yombo Dar es Salaam Saidi Ali alimuua mkewe Amina Salmin mbele ya watoto wao. Bofya hapa upate habari hiyo kwa undani.

Katika tukio jingine, mwanamke aitwaye Mercy aliuawa na mumewe kikatili na kusababisha taharuki kubwa katika jamii. Habari hiyo inapatikana kwa kubofya hapa.

Tukio jingine la mwaka huu linahusu Isabo Joseph aliyemuua mkewe kwa kumkata shingo. Bofya hapa kusikiliza kisa hiki cha kusikitisha.

Polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo kama yalivyoropotiwa kwenye vyombo vya habari.

Polisi wanasema matukio ya wanaume kuua wake zao au wapenzi wao yameongezeka katika jamii, hivyo walipopata taarifa za vitisho dhidi ya Anne, walizipa uzito mkubwa, na ndiyo maana wanamsaka Bakari ili sheria ichukue mkondo wake.

SAUTI KUBWA haina taarifa za mahali alipo Anne, ndiyo maana haijawezeka kumhoji ili aeleze sababu ya vitisho hivi na hatua ambazo angeweza kuchukua au atachukua.

Like