NDUGAI AMENG’OLEWA NA “WATU WASIOJULIKANA”

BAADA ya yote yaliyotokea, napenda kusema kuwa Job Ndugai, aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano tangu mwaka 2015 hadi tarehe 6 Januari 2022, amefukuzwa kihuni. Hajajiuzulu. Vielelezo vipo wazi.

Kwanza, ni barua ya yenyewe ya “kujiuzulu.” Imeandikwa kwa herufi kubwa mwanzo hadi mwisho kwa mwandiko tunaokutana nao mara kwa mara katika vituo vya polisi. 

Binafsi, sina kumbukumbu yoyote kutoka Ofisi ya Spika inayoonyesha kuwa kumewahi kuwa na barua iliyoandikwa kwa herufi kubwa. Hii ya Ndugai “kujiuzulu” ndiyo pekee iliyoandikwa kwa mtindo huo. 

Kisaikolojia, kuandika kwa herufi kubwa pekee ni ishara ya ugomvi na kupiga kelele. Ndugai wa “nimekosa mimi, nimekosa mimi” hakuwa na nguvu tena wala sababu ya kupiga kelele katika hatua hii, kama angeamua kuandika barua ya kujiuzulu. 

Pili, aliyeandikiwa barua ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya Katibu wa Bunge. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara ya 149 (1.c) inaelekeza kuwa: “Spika wa Bunge anaweza kujiuzulu kwa kutoa taarifa iliyoandikwa na kutiwa sahihi kwa mkono wake, na taarifa hiyo ya kujiuzulu ataiwasilisha kwenye Bunge.” 

Kwa mantiki hiyo, kama asingekuwa anaogopa mamlaka zilizoagiza jambo hili, Ndugai angeweza kusema ukweli kuwa hajaandika barua hiyo, na hata kama angekuwa ameiandika, kisheria ni dhahiri kuwa hajajiuzulu – kwa kuwa utaratibu haukuzingatiwa. Lakini hana jinsi. Atake, asitake, anaondoka tu!

Tatu, ninazo taarifa kuwa barua ya kujiuzulu iliandikwa siku moja  kabla ya Spika mwenyewe kukutana na wenyeviti wa kamati za Bunge katika kikao maalumu kilichopaswa kufanyikia Unguja. Hadi kikao kinasitishwa ghafla, wajumbe walikuwa wameshawasili Dar es Salaam. Ndugai naye alikutana na barua yake ya “kujiuzulu” mitandaoni wakati anajiandaa kwenda Zanzibar! Asingeandaa kikao huku akijua anajiuzulu wakati huo huo.

Nne, Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Fasili ya 158.6 inasema: “Spika anaweza kujiuzulu nafasi yake kwa kutoa maelezo ya kujiuzulu kwake Bungeni kabla ya uamuzi juu ya hoja ya kumwondoa madarakani.

Ndugai ni mbabe lakini si mjinga wa kutojua apeleke wapi barua ya kujiuzulu. Barua ya Ndugai kujiuzulu, yenye makosa lukuki, imeandikwa na “watu wasiojulikana.” Amekumbana na uovu aliowahi kushiriki kuwafanyia wengine alipokuwa “mtoto mpendwa wa Ikulu.”

Walioghushi barua yake ni wale wale waliokuwa wanaghushi barua za kujiuzulu za viongozi wa upinzani, hasa wabunge na madiwani, kwa maelezo kwamba “wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli” – barua ambazo zilifanana kiuandishi, maneno na mpangilio wake. Ni barua zilizoghushiwa.

Kwa kishindo cha mashambulizi ambacho kiliratibiwa na CCM dhidi ya Ndugai kwa wiki nzima, huku wengine wakimtaka ajiuzulu, ni wazi kuwa hawakutaka kumpa fursa ya kuamua hatima yake. Walimuamulia, wakamwandikia barua na kubandika saini yake na kuisambaza mitandaoni.

Kwa kuwa utaratibu wa kikatiba wa kumwondoa Spika hakuzingatiwa, Katibu wa Bunge angeweza kusema hajapokea barua ya Ndugai – kwa kuwa yeye hapaswi kupewa nakala bali barua halisi. Lakini kwa kuwa kila hatua ni ya shinikizo, naye anajua kuwa hana ubavu wa kuwagomea “watu wasiojulikana.” Kumbukeni kuwa “watu wasiojulikana” hawazingatii sheria wala katiba.

Kwa hiyo, mhimili wa dola, kwa mikono ya “watu wasiojulikana,” ndiyo umemng’oa Ndugai kwenye uspika; atake, asitake!    

Jambo hili ni la kihuni na la hatari. Lina maana yake na madhara yake, na halitaishia kwa Ndugai,  lakini hayo tutayajadili siku nyingine. 

Kutokana na tukio hili, rafiki yangu mmoja ameniandikia ujumbe mfupi wenye maana nzito: “Ndugai katudhihirishia kwamba ile mihimili mitatu ni kwa ajili ya kujibia mitihani ya somo la Uraia. Mhimili ni mmoja. Hayo mengine ni matawi.”

Hii ni hatari kwa taifa!

Like
5