Nadharia za asili ya mtikisiko na “uasi” wa Bawacha katika Chadema

Chadema's 19 women MPs in a group photo with House Speaker Job Ndugai and Parliament Clerk Stephen Kagaigai

UAMUZI wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwavua uanachama makada wake mashuhuri 19 kutokana na mzozo wa Viti Maalum vya ubunge, umefungua ukurasa mpya wa siasa za Tanzania. Ufuatao ni uchambuzi na tafakuri juu ya sababu za msingi za mzozo uliozaa “uasi” wa akina mama hawa ndani ya chama hicho.

Mzozo huo ulipamba moto Jumanne ya wiki hii baada ya hatua ya kundi la viongozi 19 wanawake wa Chadema wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho, Halima Mdee, kufika bungeni na kula kiapo mbele ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Hatua ya wabunge hao kuapa pasipo kupata baraka za Kamati Kuu ya chama hicho iliibua mvutano mkali mitandaoni kuhusu uhalali wa tukio hilo.

Kwa mfano wa kidonda kilichotiwa chumvi, hali ilikuwa ni tete baada ya Katibu Mkuu wa Chadema kuandika mtandaoni kwamba si yeye binafsi wala Kamati Kuu ya chama hicho iliyokuwa inajua lolote kuhusu uamuzi wa wanawake hao.

Mnyika ahusishwa, akana

John Mnyika, kwa mamlaka yake kama Katibu Mkuu Chadema, ndiye aliyepaswa, kisheria, kuwasilisha majina ya wanawake ambao chama cha siasa kinawateua kujaza nafasi hizo.

Wakati Mnyika akisema kuwa ofisi yake haikupeleka majina kwenye Tume, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Wilson Mahera, anadai kuwa ofisi yake ilipokea barua iliyosainiwa na Mnyika ikiambatana na orodha ya majina ya wabunge hao.

Jumatano wiki hii, Mnyika aliitisha mkutano wa waandishi wa habari akasema kwa ukali kuwa wanachama walioapa wamesaliti chama, na kwamba wameitwa wajieleze katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana Ijumaa.

Wabunge hao hawakuhudhuria kikao hicho wakidai kuwa kauli ya Mnyika ilionyesha kuwa walikuwa wameshahukumiwa kufukuzwa, na kwamba kuhudhuria kwao kikao hicho kungetumika tu kuhalalisha jambo ambalo Mnyika alishatangazia umma. 

Hata hivyo, katika mawasiliano yao na Mnyika kwa maandishi, waliomba udhuru wakiomba kamati kuu iahirishwe ili wajipange kwa utetezi siku nyingine.

Msingi wa mvutano huo, ambao fukuto lake limekuwa kali chini kwa chini kwa muda mrefu sasa, unatokana na uamuzi wa Chadema kutangazia umma kuwa hakitapeleka wabunge wa viti maalumu kwa kuwa hakitambui matokeo ya Uchaguzi Mkuu ya Oktoba 28 mwaka huu ambayo yalitawaliwa na hujuma zilizokiacha chama hicho kikuu cha upinzani kikipata kiti kimoja tu cha ubunge.

Kumekuwa na vuta-nikuvute ndani na nje ya Chadema, tangu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilipokitaka chama hicho  kupeleka majina ya wanawake 19 wa viti maalum wiki kadhaa zilizopita.

Athari ya msimamo, matamko ya viongozi wakuu

Kimsingi, hali ya mvutano ilisababisha kusigana kwa kichini chini kati  ya uongozi wa chama taifa na Bawacha ambayo inatuhumiwa kupeleka majina ya wabunge hao ilhali kukiwa na msimamo ambao ulishawekwa bayana katika siku za awali kwanza na aliyekuwa mgombea urais, Tundu Lissu, akiungwa mkono na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema Freeman Mbowe, kwamba chama hicho kilikuwa kimejitenga kabisa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28. Lakini Bawacha wanadai kuwa majina yalipelekwa na mamlaka.

Taarifa zinasema kuwa awali Bawacha walidai kwamba msimamo wa Lissu, ambao uliungwa mkono na Mbowe, haukuwa umepitishwa na kikao chochote kabla ya kutangazwa kwa umma. Taarifa zinasema pia kuwa katika kikao cha kamati kuu iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba, wajumbe waligawanyika, huku wengi wakitaka chama kipeleke wabunge.

Wingi wa wajumbe kikaoni waliounga mkono chama kiridhie kupeleka wabunge, ulimfanya Lissu akabadili msimamo, akasema iwapo chama kitaridhia waende bungeni, basi wasainishwe makubaliano muhimu ya kuchangia chama nusu ya kipato chao. 

Hata hivyo, Mbowe aligomea hoja hiyo, kikao hicho kikaahirishwa baada ya Mbowe kutishia kujiuzulu iwapo kamati kuu ingeridhia kupeleka wabunge, kwa malezo kuwa msingi wa hoja yao si kipato.

Mzozo ulianzia hapo, huku Bawacha wakisisitiza kuwa kwenda bungeni hakumaanishi kutambua matokeo bali kutumia fursa chache ambazo waliibiwa zikabaki, kama daraja la kupigania demokrasia na kupaza sauti rasmi za kilio chao dhidi ya kile wanachokiona kuwa ni ubabe wa watawala.

Baadaye, Bawacha na viongozi wakuu walikutana na kujadiliana jinsi ya kumaliza mvutano huo, huku viongozi wakuu wakipendekeza kuwa chama kivute subira hadi mwakani kuhusu suala la viti maalumu kabla ya kutoa kauli ya mwisho.

Hata hivyo, sekretarieti ya chama iliomba Bawacha iwapatie majina ya akina mama waliopendkezwa na Baraza kwa ajili ya uteuzi.

Tetesi za NEC kughushi majina

Joto lilizidi kupanda ndani ya Chadema baada ya taarifa kuanza kusikika kwamba NEC ilikuwa imeshaanza kuendesha mchakato wa chini chini wa kughushi majina, huku wanawake kadhaa, hasa waliohisi kuwa wasingekuwa kwenye orodha ya Bawacha, wakihamasishana kukubali uteuzi wa NEC bila ridhaa ya chama.

Taarifa ambazo SAUTI KUBWA inazo zinasema kuwa ofisi ya Tume ilipokea nakala zaidi ya 50 kutoka kwa makundi mbalimbali ndani na nje ya Chadema yaliyokuwa yakishawishi tume iyateue kuziba nafasi zilizokataliwa na Chadema. 

Miongoni mwa barua zilizowasilishwa ofisini mwa Mahera, zipo zilizopelekewa na wabunge wa zamani ambao walihisi kuwa Bawacha isingeweza kuwaweka katika orodha yao kwa kuwa walipata alama ndogo katika mchakato wa mapendekezo yaliyoletwa na mikoa yao.

Taarifa zilipovuja kuwa NEC ilikuwa inapanga kughushi majina, Mnyika aliionya, akiitaka kutokihusisha kabisa Chadema katika jambo hilo..

Wakati Mnyika akitangaza msimamo huo, uongozi wa Bawacha ulishashtukia mazingira yaliyokuwa yamejengwa Dodoma ambako wanawake wenzao wengi walikuwa wamepiga kambi kushawishi NEC na Ofisi ya Spika. Bawacha pia walihisi kuwa viongozi wakuu wa chama walikuwa wanawachezea akili, wakionyesha kupiga danadana suala hili ili muda upite, nalo liishe kimya kimya.

Hofu ya mgawanyiko ndani ya Bawacha

Lakini hofu ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama ilikuwa kwamba iwapo chama kingepeleka wabunge, kwa uchache huo, na kwa aina ya majina yaliyopendekezwa na Bawacha, baraza hilo lingegubikwa na mgogoro mkubwa. Hata viongozi wenyewe hawakuwa na kauli moja. Wapo waliotaka chama kipeleke wabunge Dodoma.

Kutoka ndani ya Bawacha na uongozi wa Chadema inaelezwa kuwa kutokana na uchache wa nafasi 19 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya chama hicho, Bawacha waliainisha vigezo vya wanawake ambao mikoa ilikuwa iwapendekeze kwa ajili hiyo kwa nchi nzima.

SAUTI KUBWA inatambua kuwa mchakato wa kura za siri za mapendekezo ya wanawake hao ulikamilika kabla ya uchaguzi, lakini chama kiliomba tume ikiongezee muda wa kuwasilisha majina baada ya uchaguzi. Kutokana na mazingira ya uchaguzi kubadilika na kuleta matokeo yasiyotarajiwa, sekretarieti ya Bawacha iliratibu upya mchakato wa kupata wanawake 19 wa nafasi zilizopatikana.

Mchakato huo ulipokamilika, majina yaliwasilishwa kwa uongozi wa Bawacha ambao nao ulikabidhi majina hayo kwa sekretarieti ya Chadema kwa ajili ya kuwasilishwa katika Kamati Kuu.

SAUTI KUBWA ilithibitishiwa juu ya kauli ya Mbowe kukataa kata kata orodha hiyo hata kufikia hatua ya kuwaambia viongozi wenzake kuwa alikuwa tayari kuachia ngazi kuliko kupeleka wabunge wa viti maalumu bungeni.

Msimamo huo wa Mbowe uliokuwa ukiungwa mkono pia na Lissu na Mnyika, ulipingwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ambao walisimama upande mmoja na uongozi wa juu wa Bawacha. 

Zipo taarifa kuwa wakati mzozo ukiendelea, Bawacha walibaini kwamba NEC ilikuwa imepelekewa orodha yenye majina 34 tofauti na yale ya Bawacha, orodha ambayo inadaiwa kusainiwa na Mnyika, wiki iliyopita. Bawacha hawajathibitisha suala hili hadi sasa.

Hata hivyo, Mnyika amekana kuhusika na orodha inayotajwa na NEC, huku baadhi ya watu wakidai anaikana kwa sababu mbili. Kwanza, alikuwa hajaipitisha katika kamati kuu, bali alitanguliza majina ili kuwahi muda aliokuwa amepewa na tume, na kwamba angeirasimisha iwapo hatimaye kamati kuu ingeridhia waende – sana sana katika kikao cha Februari mwakani.

Pili, kuna vyanzo vinasema kama Bawacha walishiriki kupangua orodha ya majina tofauti na ile waliyoonyeshwa na NEC kwamba ilitoka kwa Mnyika, na hatimaye orodha mpya ilikuwa na majina ya baadhi ya wabunge ambao Mnyika hakuwa anataka wawemo. Hivyo, basi, alipokataa kuwa siye aliyewateua, alikuwa sahihi.

Mnyika amekana tuhuma hizi. Msimamo wa chama ni kwamba iwapo kuna sahihi ya Mnyika katika ofisi za NEC, basi kuna mtu aliighushi. Taarifa kutoka NEC zinasema barua inayodaiwia kutoka kwa Mnyika ilipelekwa kwa dispath. Jaji Semistocles Kaijage alikuwa amegoma kuidhinisha uteuzi hadi alipoonyeshwa na kuhakiki saini ya Mnyika.

Katika hatua hii ndipo maofisa wa NEC waliwasiliana na viongozi wa Bunge na kurasimisha orodha iliyoonekana rasmi.

Kwa kuwa NEC na Bunge wana maslahi katika uteuzi wa viti maalumu, kwa sababu za kisiasa, kuonekana kwa orodha yenye majina ya viongozi wa Bawacha kulionekana kuwa jambo jema ambalo lingesababisha mpasuko mkubwa Chadema, ambao ndiyo umekifikisha chama hicho hapa kilipo leo.

Katika Kikao cha Kamati Kuu kilichokaa Ijumaa kujadili hatima ya akina mama hawa, kutokana na upepo uliokuwa unavuma baada ya kauli ya Mnyika, huku wanachama na viongozi wakituhumiana na kutajana kwamba miongoni mwao yupo kiongozi aliyesaini barua na kuipelea NEC, hata wajumbe waliokuwa na dhamira ya kutetea akina mama hao waliogopa macho ya wenzao, wakashiriki kupiga kura ya kuwaadhibu kwa kuwavua uanachama.

Sababu saba za sintofahamu hii

Wafuatiliaji wa siasa za ndani ya Chadema wanadai kuwa kilichotokea ni sintofahamu iliyosababishwa na mambo kadhaa.

Kwanza, msimamo wa chama kutopeleka wabunge haukuwa umepitishwa rasmi na kikao chochote kabla ya kutamkwa na mgombea urais na kukubaliwa na mwenyekiti. Ndiyo sababu ya mzozo ulioibuka katika kamati kuu.

Pili, hata kama mgombea urais na mwenyekiti walikuwa na msimamo mkali, na hata kama kauli yao ingetarajiwa ikubaliwe na wenzao, kwa kuwa wajumbe walionyesha kutaka wabunge wa viti maalumu waende bungeni, viongozi hao wakuu walistahili kulegeza msimamo na kuridhia.

Tatu, wakati mgombea urais alikuwa amebadili msimamo katika kikao cha kamati kuu, alipohojiwa na waandishi wa habari baada ya kuwasili Ulaya aligeuka tena akarudi kwenye msimamo wa awali, akisema “haramu haizai halali.”

Nne, kwa kuwa tayari kulikuwa na hisia za viongozi wakuu kubadili maoni baada ya kikao cha kamati kuu, hata kuwataka Bawacha wawasilishe orodha ya majina ya wateule wao, msingi haukuwa tena kwamba “hatupeleki” bali “tutapeleka lini, na tutapeleka akina nani.”

Tano, kuliibuka hisia, hata vikaoni, kuwa wanaume walikuwa wanazuia wanawake kwenda Bungeni kwa kuwa wao hawakuwa wamepata bahati ya kuwa wabunge.

Sita, katika jitihada za makundi kujaribu kuzidiana kete, ni dhahiri kwamba mwanachama yeyote wa Bawacha ambaye angetangazwa na NEC au kuitwa na spika angekubali kuapa. SAUTI KUBWA ina majina ya baadhi ya wanawake waandamizi wa Chadema ambao walikuwa tayari Dodoma wanavizia kuapishwa, wakakosa. Baadhi yao sasa ndiyo wanatoa kauli za kulaani walioapishwa.

Saba, kwa kuwa watawala wana maslahi na viti maalumu hivi, walitumia mwanya huu kuchochea mnyukano ili kuongeza ufa ndani ya Chadema, na wamefanikiwa baada ya kuwatia kiwewe wanawake na kuwachonganisha na viongozi wao, hasa wanaume.

Kwa jinsi hali ilivyokuwa, iwapo wanachama hawa 19 wasingeapa, wangeapishwa wengine ambao tayari walishawasili Dodoma na kuwasiliana na mamlaka za Bunge na NEC wakidhani Bawacha ilikuwa imesusa viti hivyo. Bawacha ilikuwa inawahi kuwapiku ili “wasiipokonye viti vyake vya ubunge.”

Kwa usahihi kabisa, hili ni kundi la pili, la “waasi watarajiwa,” na baadhi yao wana vyeo ndani ya chama.

Baadhi ya wachambuzi wanabainisha kuwa, vyovyote vile iwavyo, mvutano huu, licha ya kufukuzisha wanawake wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama, umejenga mazingira mapya ya uimara wa Chadema iwapo viongozi watatafakari kiini halisi cha mnyukano huu uliozaa uasi huu.

Kama hili lisingetokea,chama kingekuwa kimevimba kwa mgogoro wa ndani usiolipuka nje. Kwa hatua hii, chama kimepumua, na makundi yaliyokuwa yanaviziana yameungana dhidi ya “Bawacha iliyokwenda Bungeni.”

Moja ya matokeo mema yanayotajwa kwa sura hasi ni kuondolewa jela kwa Nusrat Hanje, binti aliyeswekwa ndani akiwa na wenzake kadhaa halafu wakanyimwa dhamana na kulazimika kukaa jela kwa miezi minne mfululizo. Kosa lao lilikuwa kuongeza ubeti usio rasmi katika wimbo wa taifa.

“Hawakuwa na hatia yoyote. Walifungwa kisiasa kwa maagizo ya kisiasa, na wameondolewa kwa maagizo ya kisiasa. Kimsingi, kulikuwa na dhamira mbaya ya kuwafunga kabisa. Hakuna wakili angeweza kuwatoa kwa kuwa hawakuwa na shauri lolote kisheria. Ni ubabe tu ulitumika dhidi yao. Aliyewanusuru ni yule aliyewaza kumwingiza binti huyu katika orodha ya viti maalumu. Hili ni moja ya matendo ya kishujaa ya akina dada na mama zake hawa,” chanzo chetu kimesisitiza, kikiombwa kisitajwe jina kwa sababu binafsi.

Wanawake 19 waliofukuzwa hawajatoa kauli yoyote kwa umma tangu mzozo huu ulipoanza. Taarifa zinasema kuwa wakati wowote wiki ijayo watatoa ufafanuzi wa kilichowatokea.

Kwa jicho la uchambuzi, kufukuzwa kwa wanawake hawa kunaweza kukawa moja ya majeraha makubwa kabisa ya kisiasa na kiuongozi kwa Chadema tangu alipoondoka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, takriban miaka sita iliyopita.

Like
1